Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon. Charles John Mwijage

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mimi ni Mjumbe wa Kamati lakini ni muumini wa sekta za kiuzalishaji. Naogopa nisije nikasahau, naomba kuunga mkono taarifa ya Kamati pia ninaunga mkono yote taarifa ya mtumishi, mimi naiita bajeti ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitazungumza mambo matatu kwa sababu tumezungumza sana suala hili mwaka jana na tumelichakata kwenye Kamati. Moja nitazungumza kuhusu umuhimu wa kilimo. Suala la pili nitazungumza mtazamo wa Serikali ya Awamu ya Sita kwenye sekta ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilipokuwa mdogo, nilipoacha ziwa la Mama nilikwenda kulelewa na Bibi yangu aliitwa Zuhura Teshasha. Mama yangu alinipenda sana na watu wengine walikuwa wananiletea zawadi. Pamoja na udogo wangu nilikuwa na uwezo wa kutambua zawadi ya Mama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zawadi ya Mama ingekuja ningesema hiyo zawadi ya mama. Napenda niwaambie, kitendo cha kutoa bajeti shilingi bilioni 294 kwenda kwenye shilingi bilioni 751 hiyo ni zawadi ya Mama. Nimemsikia mtumishi na wewe mtumishi hii siyo ya kwako umetumwa. Hii ni zawadi ya Mama, anasema atawatafuta vijana, atawapa heka tano au heka 10 hiyo siyo ya kwako, wewe ni mtumishi hiyo ni zawadi ya Mama. Wale ambao siyo watumishi wa Mama anachukua watu 10 anawapa heka mbili, huyo siyo mtumishi wa Mama. Mtumishi wa Mama ni kama wewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumza kitu kingine. Hii ni bajeti ya Taifa, ile ya TAMISEMI ilikuwa ni bajeti ya wananchi, hii ni bajeti ya Taifa. Nizungumze suala jingine nikipata muda nitawaambia change of mind, working by targets. Nimemsikia mtumishi kwamba sisi tubadilishe malengo, sikiliza bajeti yake na ninyi Watanzania mnasikiliza, anaweka malengo kwamba ifikapo mwaka fulani sisi tuuze kiasi fulani. Kiburi cha Ukraine anauza nje Dola Bilioni 64, ndiyo kiburi cha Ukraine na angalia anauza nini Ukraine, anauza mazao ambayo na sisi tunaweza kulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine nitakalozungumzia ni suala la uchumi jumuishi. Ziko block farming 110 anasema mtumishi na hii umetumwa na mama nina taarifa. Anasema yeye mtumishi, block farming 110 atatengeneza block farming 10,000 kufikia 2025. Angalizo, hakikisha na Mkuu wa Mkoa wa Kagera unamwambia akutengee hekta 50,000 na vijana wa Kagera waweze kupata ardhi na mimi nitapambana na uongozi wa Kagera kuanzia Kijiji, iwe Wilaya lazima watoe ardhi vijana walime. Siwezi kukubali, siwezi kukubali wananchi wangu kutengewa heka mbili, lazima watengewe heka tano, heka 10, heka 20. Naanza kuchangia. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma gazeti la Business Insider, Business Insider wanasema sababu tano, nazungumza umuhimu wa kilimo. Wanasema umasikini wa Afrika unatokana na sababu tano na sababu mbili ziko kilimo, lakini sababu mbili za kilimo zinaweza kuondoa umasikini kwa asilimia 70 tukizi-address. Mheshimiwa Waziri amezungumza anaweza kuondoa umaskini kwa asilimia 50 kama Mama atampa zawadi na sina wasiwasi. Sina wasiwasi zawadi itakuja, Shilingi Trilioni Mbili zitakuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mojawapo ya sababu inayotajwa ni tariff berrier na non-tariff berrier. Wale wenye ukwasi mkubwa, mazao yetu tunayolima wanayawekea kodi kubwa na wanayawekea masharti yasiyokuwa ya kikodi. Lakini watu wale wenye ukwasi mkubwa, kitu ambacho wanacho kingine wana ruzuku sana mazao yao yanayoshindana na kwetu hapo ndipo naungana na mtumishi anasema litoke jua inyeshe mvua atatoa ruzuku kwa mbolea. Naomba mumuunge mkono ili kusudi aweze kutoa ruzuku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala jingine Business Insider wanasema inadequate infrastructure and inadequate expertise. Kwamba hatuna miundombinu na hatuna utaalam. Nimewaona jeshi la kilimo limeshajengwa uniform, usiwavike uniform, usiwaruhusu kurudi nyumbani wapige wiki kama mbili hapa uwapige shule na mimi uje uniite mtumishi mwenzako niwape maneno. Kwa hiyo, inadequate expertise is very important. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala jingine ni miundombinu. Nitumie fursa hii kuiunga mkono Serikali, mwaka 1970 Muadhama Raulian Rugambwa na Baba Askofu Kibila na Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Kagera waliamua kuanzisha mradi wa Mto Ngono tangia siku hiyo tulijua kwamba tunakwenda kwenye neema, baadae Mzee Byabato wakaanzisha Kagera Basin Organization. Nimesoma kwenye bajeti kwamba Serikali inakwenda kufanya assessment ya irrigation Mkoa mzima wa Kagera.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie kama kuna kitu kilisahaulika na sasa hivi wakati wa Mama hakikufufuka, hakitafufuka tena. Wananchi wa Kagera, Kagera Basin inakwenda kurudi halafu niwaambie Ngono Project inakwenda kurudi halafu basin yote ya Victoria inakwenda kulimwa, tunakwenda kuzalisha chakula. Maana yake ni nini? Tunakwenda kuwa exporter wa mazao. Kiburi cha Ukraine ni uwezo wa kuuza nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimewaambia target lazima mambo yote Wabunge tuyalenge kwenye malengo, unauza nini? Natofautiana na Mtumishi. Hatuwezi kusubiri mpaka 2030 kuweza kuuza nje mazao yenye thamani ya Dola Bilioni Sita no! Lazima kabla ya 2025 tutumie pesa hizi na Mama atakuongeza nyingine ili kusudi uweze kuzalisha zaidi. Kuzalisha zaidi ndiyo kutatuwezesha sisi kuwezakuwa na kiburi. Hatutampiga jirani yetu lakini tutakuwa na kiburi ili hata wale vijana wenye jambo lao kwa sababu tutakuwa na kipato kikubwa tunaweza kubadilisha ile jezi Namba 23 ikawa Namba 46, ni kiasi cha kubadilisha tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ngoja niwaambie. Kiasi cha mafuta tunachotumia nchini lita Bilioni Saba ndiyo mafuta ya alizeti ambayo Ukraine anazalisha. Lakini arable land ya Ukraine ni ndogo tunamzidi mara tatu kwa arable land ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina imani sana, nina imani lakini kuna mazao yenye mashaka, mojawapo ya mazao yenye mashaka ni haya yanayojitokeza. Kwetu sisi tunalima vanila, Serikali itusaidie ku-address suala la vanilla, lakini kwetu sisi tunalima chai, chai ya Kagera irudi kwenye nafasi yake.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwijage, Mheshimiwa Mwijage.

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo.

MWENYEKITI: Ninakuongeza dakika moja uhitimishe hoja yako Mheshimiwa. (Makofi)

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja. Lakini jambo la Mama, zawadi ya Mama ukiiangalia utaiona na watumishi wa Mama wanakuja na heka tano kwa mtu siyo heka mbili kwa watu 10.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)