Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kishapu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu kabisa Wizara ya Kilimo ambayo hotuba yake kimsingi ni hotuba nzuri na unaweza ukaona bajeti hii ni kubwa, ni takribani mara tatu zaidi ya bajeti katika kipindi kilichopita ambayo ina jumla Shilingi Bilioni 751. Kwa kweli naomba nitumie fursa hii kukupongeza sana Mheshimiwa Waziri Bashe, Naibu Waziri Mavunde, Katibu Mkuu, Naibu Makatibu Wakuu, Mrajisi wa Vyama vya Ushirika na Ndugu zetu Watendaji Wakuu, Bodi ya Pamba, Bodi ya Korosho, Wakurugenzi ambao kwa kweli mmekuwa mkitekeleza wajibu wenu pakubwa sana pamoja na watumishi wote wa Wizara hii ya Kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kwa kweli kumshukuru sana na kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano, Mama yetu mpendwa Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo anaipa kipaumbele sana Wizara hii ya Kilimo ili mradi kuona kwamba Watanzania sasa wanapata ukombozi kupitia shughuli kubwa kwa sababu Watanzania zaidi ya asilimia 70 ni wakulima, tuna matumaini watanzania Mama atatufikisha pale ambapo sote tunatarajia tutakwenda kufika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumza hayo kimsingi nataka nianzie katika eneo zima la Wizara ambayo imefanya kazi kubwa ya kuhakikisha kwamba wanatoa vitendea kazi hususan pikipiki kwa maana pia vifaa kwa ajili ya kupima udongo na vifaa vingine ambavyo kwa kweli vitasaidia sana kusukuma jitihada za mafanikio katika sekta ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili Mheshimiwa Bashe pamoja na Naibu Waziri pamoja na Watendaji wote Wizara hii, ninawapongeza sana kwa ubunifu mkubwa na mawazo chanya ambayo nchi yetu ya Tanzania tunao uhakika kwa Watendaji kama hawa na Viongozi kama hawa tutafika mbali sana. Hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala jingine muhimu sana ni kuhusiana na suala la pembejeo. Tumeshuhudia na hasa katika eneo ambalo ni la ukanda wa Ziwa Viktoria na hasa Mkoa wa Shinyanga na sisi tunalima zao la pamba. Tumepata pembejeo kwa maana ya viuatilifu pamoja na mbegu kwa wakati. Hili ni jambo kubwa sana kwa sababu kwa miaka mingi tumekuwa tukipiga kelele kuhusiana na suala zima la kuchelewesha mbegu na kuchelewesha dawa. Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mama Samia Suluhu Hassan na chini ya Mheshimiwa Hussein Bashe ukweli umeupiga mwingi na tumepata dawa kwa wakati na mbegu kwa wakati na wakulima wamelima kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa iliyopo ni suala la mvua. Wenzangu wamezungumza hapa, tuna mvua za wastani na kwa kipindi hiki hasa cha mwaka wa kilimo msimu huu, kwa kweli tunatarajia mapato yetu ya uzalishaji kupungua kutoka asilimia tuliyokuwa tunatarajia hadi asilimia 50. Kwa hiyo, tunaona kwamba kuna uwezekano wa zao la pamba kutokupatikana katika matarajio tuliyokuwa tumejiwekea kwa sababu ya hali halisi ya hewa na kutokana na suala la mvua kutokuwepo ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba jitihada hizi ziendelee katika msimu unaokuja ili changamoto hii isije ikajirudia kwa mara nyingine kabisa kuhusu suala la pembejeo na mbegu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka nizungumzie jambo jingine ni suala zima la Kitengo cha Ushirika. Kuna changamoto kubwa katika eneo hili. Kwanza ni upungufu wa watumishi katika eneo hili. Kama tunavyofahamu Maafisa Ushirika hawa ndiyo Wakaguzi wa Ndani (Internal Auditor) katika Vyama vya Msingi katika maeneo yetu yote. Tatizo hili ni kubwa, unaweza ukaangalia katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu tuna Maafisa Ushirika Wanne, lakini Kishapu ina vijiji zaidi ya 128. Hili ni tatizo kubwa, Tarafa Tatu ukubwa zaidi ya kilomita za mraba karibu 4,300, ni eneo kubwa sana. Sasa Maafisa Ushirika Wanne, Vyama vya Msingi zaidi ya 98 watafanyaje kazi? Kwa hiyo, eneo hili tunaomba sana Mheshimiwa Waziri lifanyiwe kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine ni suala zima la ku-over stay kwa watumishi. Maafisa Ushirika wapo ambao wanao umri wa miaka 15 mpaka zaidi ya miaka 15. Serikali na Wizara ifanye kazi ya ziada kuhakikisha kwamba watumishi hawa wawe wanahamishwa ili tuweze kuleta watumishi ambao wanaweza wakaleta chachu na mafanikio ya haraka katika maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala jingine ni suala la sekta ya umwagiliaji. Tunashukuru kwamba Serikali katika mwaka huu wa fedha wametenga fedha za kutosha. Naomba skimu ya kwangu ya Itilima, skimu ya kwangu ya Nyenze, Idukilo hizi zipewe kipaumbele na hasa ile ya Itilima ina zaidi ya hekari 2,000. Eneo hilo ni kubwa na ni zuri. Serikali ya Awamu ya Nne iliwahi kuleta Shilingi Milioni 200 na baadhi ya miundombinu iko sawasawa. Naomba Mheshimiwa Waziri utakapokuwa una-wind up eneo hili uzungumzie ni kwa namna gani utaenda kutusaidia ili hizi skimu ziweze kukaa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine ni Vyama vya Ushirika. Tuna Chama Kikuu cha Ushirika – SHIRECU. SHIRECU hii ndiyo imezaa Chama Kikuu cha Mkoa wa Simiyu, lakini Bukombe na Ushirombo pia KACU. Chama hiki ni kama tumekitupa. Zaidi ya awamu tatu au miaka mitatu ama minne tumekuwa tukiomba ukomo wa bajeti kwa ajili ya kuhakikisha tunafufua viwanda vyetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ginery ya Munze, wewe mwenyewe umefika Mheshimiwa Waziri Bashe na unaifahamu vizuri. Ginery ile ni nzima inahitaji matengenezo ya kawaida. Ginery ya Uzogole lakini tunayo Oil Milling Manispaa ya Shinyanga. Hizi asset tunazitupa, naomba Mheshimiwa Waziri, wameomba Shilingi Bilioni Sita. Shilingi Bilioni 4.4 ni kwa ajili ya ununuzi wa pamba pamoja na marekebisho ya magari, Shilingi Bilioni 1.3 kwa ajili ya kulipa madeni na vitu vingine, kwa nini katika Shilingi zaidi ya Bilioni Mia Saba hii tusije tukawafikiria SHIRECU? kwa sababu wakati mwingine tunakatisha tamaa Viongozi wa Ushirika na watu wa Ushirika. Naomba wakati una-wind up uzungumze kuhusu ginery ya Munze, ginery ya Uzogole na suala zima la ukomo wa madeni hizi Shilingi Bilioni Sita tuweze kuwasaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nina imani na wewe kwa sababu utakwenda kusaidia, lakini nikupongeze kwa sababu baadhi ya Vyama vya Ushirika ambavyo vimesajiliwa…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Butondo kengele yako ya pili imeshalia tayari.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naunga mkono. (Makofi)