Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE ZITTO Z. R. KABWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuchangia mapendekezo yangu kuhusu Mpango wa Maendeleo kwa ajili ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2016/2017. Nina maeneo machache sana ambayo naomba yafanyiwe improvement katika Mpango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza linahusiana na ujenzi wa uwezo wa watu kwa ajili ya kuwaandaa kwenye uchumi wa viwanda. Katika ukurasa wa 25 wa Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa 2016/2017, kifungu cha 3.2.2; miradi mikubwa ya kielelezo, Serikali imezungumzia kusomesha vijana wengi kwa mkupuo katika fani za mafuta na gesi, wahandisi kemikali, viwanda vya kioo na afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza kwamba, hatuwezi tu kuwa na watu ambao wamesomeshwa katika ngazi ya Vyuo Vikuu na hatuna watu ambao wako kwenye ngazi za chini. Kwa hiyo, mapendekezo yangu ni kwamba, tuongeze katika vipaumbele vya miradi mikubwa ya kielelezo (flagship projects) uwepo kwa VETA na Vyuo vya Ufundi vya Kati, kwa maana ya Technical Colleges.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji mafundi wa kuwasaidia Wahandisi na bila kuwa na VETA za kutosha nchini, hatutakuwa na mafundi wa ngazi za chini na bila kuwa na Technical Schools za kutosha nchini, hatutakuwa na mafundi mchundo wa katikati, ambapo kila Mhandisi mmoja, anahitaji zaidi ya mafundi mchundo 25 ili kuwezesha kazi kufanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yangu ni kwamba, kwa sasa hivi, kuna low-hanging fruits. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge tukubaliane kwamba kuanzia sasa, kila Kambi ya JKT, iwe ni Chuo cha VETA, iwe designated kuwa chuo cha VETA na wale vijana ambao wanakwenda JKT kwa hiari, wale wa miaka miwili wale, watoke na ujuzi badala ya kuwafundisha tu masuala ya kijeshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili, wapate mafunzo ya kuweza kwenda mtaani na kuweza kufanya kazi, itatusaidia kupunguza tatizo la ajira na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili, naomba tupate support Kigoma kule kuanzisha Chuo cha Ufundi wa Kati. Pendekezo langu ni kwamba angalau kila mkoa uwe na Technical School moja, maana yake sasa hivi vyuo ambavyo vipo, kama Dar Tech. imekuwa Dar es Salaam Institute of Technology, Mbeya Technology sasa hivi imekuwa ni Chuo Kikuu, vimegeuzwa kuwa Vyuo Vikuu. Kuna haja ya kurejea kila mkoa kuwa na Technical School moja na kila Wilaya iwe na VETA kwa maana ya Halmashauri ya Wilaya na kwa kuanzia tuanze na Kambi za JKT kuweza kuwa VETA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pendekezo langu la pili ni suala la reli. Tunahitaji kupata tafsiri ya reli ya kati na baadhi ya Wabunge wamezungumza jana hapa na naomba niongezee nguvu tu, kwamba tunapaswa kuwa makini sana kwenye siasa za kikanda. Tusikubali maslahi ya nchi zingine yafunike maslahi ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni lazima tuanze kwanza kuhakikisha mtandao wa reli ambao utaisaidia nchi yetu ndiyo ambao unakwenda sawasawa. Juzi nilisikia kwamba, tuna tatizo la fedha. Mwaka jana Bunge lilipitisha Sheria ya Railways Development Levy, kodi ya maendeleo ya reli ambayo kila mzigo unaoingia nchini, unatozwa asilimia 1.5 kama niko sahihi; naweza nikarekebishwa, kwa ajili ya reli. Kwa hiyo, ina maana kwamba tunacho chanzo cha uhakika cha fedha, tunachokihitaji ni kuhakikisha kwamba chanzo hiki kinatumika kwa madhumuni yale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba tupate tafsiri ya reli ya kati na kwetu sisi, reli ya kati ni inayotoka Dar es Salaam mpaka Tabora, mpaka Uvinza kwenda Msongati Burundi, kutoka Kaliua kwenda Mpanda mpaka Kalema kwa ajili ya ujenzi wa Bandari ya Kalema na kutoka Isaka kwenda Keza, Ngara kwa ajili ya madini ya nickel ambayo yamegundulika kule Ngara ili yaweze kusafirishwa kupelekwa Bandari ya Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba jambo hili liweze kutazamwa, ni muhimu sana na ni priority. Naungana na wote walioongea jana kuhusiana na reli, ya kwamba bila reli na tafsiri hii, hakuna kitakachoendelea katika mfumo mzima wa bajeti ambao unakuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kulipendekeza ni ukurasa wa 29, usafiri wa anga. Namba tatu pale ununuzi wa ndege mpya mbili za Shirika la Ndege la Tanzania. Watu wamezungumzia sana hili, lakini kuna haja, Serikali haiwezi kuwa kila wakati inanunua ndege za ATCL, lazima kulifanyia marekebisho Shirika na tunajua na tumewahi kuzungumza huko nyuma, Mheshimiwa Mwakyembe atakuwa anakumbuka maana yake alilianza kidogo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu ambao wanafaidika na kuwepo kwa Shirika la Ndege. Hawa ni Taasisi zinazohusu utalii, lazima tuzihusishe hizi taasisi ziweze kuhakikisha kwamba zinashiriki katika kuwepo na national carrier. Hapa nazungumzia Ngorongoro, TANAPA, hawa kutokana na wingi wa watalii wanaoingia nchini wao wanapata mapato. Turuhusu mashirika haya yawe na hisa ndani ya ATCL ili kuweza kupata fedha shirika liweze kujiendesha kibiashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo siyo kama tunalianza upya, lilishaanza Mheshimiwa Mwakyembe anakumbuka, kuna maelekezo yalitoka, ni kiasi cha Waziri Ndugu Mbarawa kukaa na Msajili wa Hazina, wakubaliane utaratibu ambao unapaswa kuwa ili mashirika yenye ukwasi yaweze kusaidia mashirika ambayo bado yako chini ili tuweze kwenda mbele katika nchi yetu, kwa sababu hatuwezi kuwa tunapanga bajeti ya kununua ndege kila siku. Hizi mbili sawa zitanunuliwa, lakini kuna haja kubwa sana ya kuweza kuangalia huko mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, maana yake kengele imegonga ambalo ningependa nilichangie ni ukurasa wa 30. Ukurasa wa 30 huduma za fedha namba nne, Serikali inasema inataka kuanzisha Mfuko wa Mzunguko (Revolving Fund). Wakati wa kampeni tulisikia, kulikuwa kuna ahadi ya shilingi milioni 50 kila kijiji, naamini kila kijiji na mtaa na leo asubuhi Profesa Muhongo ametupa takwimu ya idadi ya vijiji nchini, 15,209 ndiyo vilivyoko nchini. Ukichukua 50,000,000 times idadi ya vijiji unapata zaidi ya shilingi bilioni 750 kwa mwaka ndiyo itakayokuwa ya 50,000,000 ya kila kijiji.
Waheshimiwa Wabunge naomba niwakumbushe, tulikuwa na mabilioni ya JK, mnakumbuka namna ambavyo yalitumika vibaya, kwa sababu hapakuwa na mfumo mzuri wa namna gani fedha hizi zitatumika. Naomba nishauri, moja ya kipaumbele ambacho Waziri wa Fedha jana amezungumza hapa ni Hifadhi ya Jamii. Naomba niwashauri kwamba, tutumie fedha hizi kama incentive ya watu kuwekeza kwa ajili ya social security, kwa kufanyaje? Tuweke incentive kwamba, raia wetu mmoja akichangia shilingi 20,000/= kuingia kwenye Mfuko wowote ule wa Hifadhi ya Jamii, Serikali imwekee shilingi 10,000/= zinakuwa ni shilingi 30,000/=.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa idadi ya fedha ambazo zitapatikana, mwanzoni nilikuwa napiga hesabu ya vijiji elfu kumi na mbili, maana yake ni kwamba ndani ya mwaka mmoja, tutakuwa na one point eight trillion ambayo iko kwenye saving ya social security ambayo Serikali mnaweza mkaitumia kwa miradi yoyote mikubwa mnayoitaka. Kwa sababu social security liability yake ni long term, kwa hiyo mnao uwezo wa kujenga madaraja, mnao uwezo wa kujenga irrigation schemes kwa sababu mtu akiingia kwenye mfumo wa social security now anakuja kupata yale mafao ya muda mrefu baada ya miaka 15, baada ya miaka 20. Kwa hiyo, naomba jambo hili liangaliwe na nitaliandika vizuri, tuweze kuona ni namna gani ya kwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. (Makofi)