Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon. Njalu Daudi Silanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Itilima

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kukushukuru kwa kunipa nafasi. Nimshukuru Mheshimiwa Rais na kumshukuru Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu na Makatibu Wakuu, pamoja na waratibu wa taasisi zote zinazoshiriki kwenye mazao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza kutoa pongezi zangu kwa Mheshimiwa Waziri kwa muda mchache ameleta matumaini makubwa ndani ya Sekta ya Kilimo. Na hii nikwasababu Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake wamekuwa vijana wakizunguka nchi hii kusikiliza kero za wananchi, kero za wakulima na kuhakikisha yakuwa wanakuja kuzifanyia kazi niwapongeze sana kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninayo machache. Kwanza la kwanza Mheshimwa Waziri tukupongeze sana kwa hatu ya kwanza ambayo umefanya kutoa pembejeo bure kwa wakulima hususani kwenye zao la pamba. Mimi nisipoizungumzia pamba sitapata usingizi kwasababu ndio mkoa mkubwa unaozalisha pamba ya Tanzania hii. Na ndiyo inayowapatia wananchi wangu kipato kikubwa ambacho tunakitegemea na mwaka huu wa fedha ulioisha tulipata tena zao la alizeti. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri tunakupongeza kwenye maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa iliyopo ni suala zima la viuatilifu vinavyopatikana. Kwamba vinakuja ndani ya muda, lakini kulingana na elimu ya watumiaji wetu ile dawa haiui wale wadudu. Sasa, kwa kutokuua kule kunasababisha madhara makubwa sana. Jambo muhimu ambalo umelizungumzia leo kwenye suala zima la utafiti mimi nadhani wadudu waliopo sasa ni tofauti na mazoea tuliyonayo. Mwaka huu tungetarajia kupata takribani tani laki 400, lakini naamini tunaweza tukapata 200 au 300. Madhara makubwa yametokana na viuatilifu ambavyo vimepatikana tukavisambaza vijijini bila kuwa na elimu nzuri kwa watumiaji wa hivyo viwatirifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana, kupitia Bodi ya Pamba usimamizi uongezeke. Wamefanyakazi kubwa sana na zao lilikuwa limepotea lakini tunaona matumaini makubwa sana ambayo sasa yanaweza yakatuletea fedha za kigeni nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwenye suala la mafuta, kwa sababu unapoizungumzia pamba unazungumza mbegu na unapata na mafuta. Kwa hiyo, naamini kabisa tukiwa madhubuti na tukiwa na usimamizi uliobora imani yangu kubwa kwamba tutapiga hatua kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, leo Mkoa wa Simiyu Kamati ya Siasa ya Mkoa ilikuwepo hapa, imekuja kushuhudia jambo kubwa Mheshimiwa Waziri alilolisema, la kufanya majaribio katika maeneo haya ya ushirika. Mimi sina tatizo na ushirika, ninachokuomba Mheshimiwa Waziri hakikisha unatafuta fedha tuwape washirika wa Mkoa wa Simiyu na mikoa mingine kama Kaku, kama Uchato na kama kule Bukombe ili waingie kwenye soko watengeneze ushindani wa kwenda kufanyabiashara na sekta
binafsi. Ukifanya hivyo utatengeneza ushindani mkubwa na imani kubwa…

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumtaarifu mchangiaji kaka yangu Njalu kwamba wananchi wa Mkoa wa Simiyu wanampongeza sana Mheshimiwa Rais pamoja na Waziri kwa kukubali mwaka huu kuwa na soko huria la zao letu la pamba kwenye Mkoa wa Simiyu, ambapo inapunguza sasa unyanyasaji ulikuwepo kwenye AMCOS zetu kwa kuwadhulumu fedha zao wakulima. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Njalu unapokea taarifa.

MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naye alitakiwa apate muda wa kuchangia, naipokea. Ni kweli jambo hili ni muhimu sana. N aamini Mheshimiwa Bashe kwa kufika mpaka kutoa maamuzi hayo alipoteuliwa kuwa Naibu Waziri mwaka 2019 madudu yaliyokuwepo kwenye Mkoa wetu wa Simiyu na kwa Tanzania kwa ujumla anajua na bosi wake siku moja aliomba kusema ushirika ufutwe. Kwa hiyo, ni jambo ambalo ameliona yeye kwa kulishuhudia nawala hajafuta na wala hatuzungumzi kufuta ushirika tunahitaji ni kuboresha wasiwe wagaragaja kama neno lake alivyokuwa akilitumia wakati akiwa hajawa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuwe na sera ambazo haziwezi kuyumbisha Taasisi za Fedha. Sera zilizo imara zilisimama zitatusaidia sana sisi kama nchi kuhakikisha uzalishaji wa mazao yetu tunayafanya yanapata tija na tunapata fedha nyingi za kigeni kupitia mazao hayo. Kwa hiyo naamini, kwa haya ambayo tunaendelea kuyazungumza na tunaendelea kuishauri Serikali wakiyasimamia vizuri tutakuwa na uzalishaji ulio na tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tumeona kuna watu wa makombati walikuwepo hapa, basi yale makombati yaende yakafanye kazi, ikibidi Mheshimiwa Waziri awafungie hata GPS ili tuwe tunawaona wakiwa mashambani kabisa kazi wanazokuwa wanazitekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pikipiki nazo ziende vijijini, kuna hatari ya kuja kupasuka matairi tena, zikikaa zinapigwa jua muda mrefu tunakuta zinaharibika. Kwa hiyo, niendelee tu kusema kwamba kazi hii nzuri ambayo Waziri anaifanya, naamini kabisa kwamba tutafanya mazuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilianzisha Benki ya TADB na Benki ya TIB Commercial Bank, hizi zote zilikuwa na madhumuni yake. Mheshimiwa Waziri ameizungumzia Benki ya TADB, jukumu lake kubwa ni kuhakikisha inasimamia kilimo. Sasa leo tunazungumzia allegation na vitu vingi na vingi. Kwa hiyo ningeomba Wizara husika hii Benki tuiangalie kwenye jicho la pekee ili itoe huduma kwenye jamii hii ambayo tunayoitarajia. Tukifanya hivyo, kwa sababu yenyewe haifanyi biashara kazi yake ni kuhakikisha inavyoelekezwa na Serikali inapeleka kusaidia pembejeo, umwagiliaji na vitu vingine vyote kadha wa kadha ambavyo vinawezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukitumia fursa hiyo na fedha tunazozitenga kwa Wizara zikienda, aliyokuwa anayasema Mheshimiwa Mwijage asubuhi yatatimilika, nchi hii ni tajiri, ina vitu vingi kila kona kuna uzalishaji wa kutosha. Miaka hii miwili bei za mazao yetu zimeendelea kukua kwa kasi ni kwa sababu uzalishaji tunao na watu wetu wanajituma. Nchi za wenzetu kuchuma ile pamba wanatumia mashine, lakini sisi wakulima wetu wanavuna pamba iliyo nzuri na iliyo bora zaidi, lakini nchi zingine kila kitu ni remote, remote. Kwa hiyo utaona bado tuna nguvu ya kutumia, kwa hiyo kama Taifa tuna jukumu, nguvu hii kuitumia hivi sasa ili kizazi kinachokuja kiweze kufaidika na haya tunayoyatarajia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya haya machache, naunga mkono hoja na nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Pia nawatakia kila la kheri wenye Wizara, mambo yaendelee vizuri. (Makofi)