Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi ili niweze kuchangia. Niunganie na Wabunge wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa uwezo wake binafsi kwa namna ambavyo ameandaa Hotuba yake vizuri sana na mipango mizuri sana kwenye hotuba yake. Pia nimpongeze pia Naibu Waziri, tumeona namna ambavyo wanawajibika kwa muda mfupi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo machache, leo nitakwenda kwenye angle ya tofauti, miaka yote sita nilikuwa najikita sana kwenye utafiti, nimeona wameongeza fedha kidogo. Naamini hakuna maendeleo ya kilimo bila kuwekeza kwenye utafiti, leo wamewekeza hiyo fedha, lakini kuwekeza ni jambo moja na kupewa fedha ni jambo lingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia namna ambavyo Waziri ameisoma hotuba yake na mipango yao ni mizuri sana, unaona kweli kwamba wameanza kusikiliza mawazo ya Wabunge. Leo nitajikita zaidi kwenye Wizara ya Fedha na Serikali ni vizuri wakatuelewa. Wakati tunazungumza bajeti hii ambayo imesomwa leo, bajeti iliyopita mpaka Februari tukiwa tunakuja kwenye lile Bunge la Mwezi Februari, walikuwa wametekeza kwa asilimia 35 tu ya fedha iliyoidhinishwa na Bunge. Hili jambo kama Wabunge hatuwezi kulifurahia, tukiidhinisha fedha ni vizuri ziende kama tulivyoidhinisha kama Bunge. Sasa kwa kuwa mipango ya Mheshimiwa Waziri ni mizuri na figure imepanda kidogo, sasa kupanda kwa figure ni jambo moja, lakini tunataka fedha hiyo iende kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitajikita katika mkulima wa kawaida kabisa anayetumia jembe la mkono. Nataka kuja kujenga hoja yangu kwa nini ruzuku ni lazima na siyo ombi kwenye mbolea. Mkulima wa kawaida kabisa kwa eka moja anakodi kwa Sh.50,000, mkulima huyo anaandaa hilo shamba kwa Sh.50,000 inakuwa Sh.100,000. Mkulima huyo kwenye ekari hiyo hiyo inabidi anunue mbegu mifuko mitano ambayo thamani yake ni Sh.62,500, mkulima huyo inabidi anunue mbolea mifuko mitatu kwa bei ambayo imepita sasa hivi ni Sh.360,000 kwenye eka moja, mkulima huyo huyo atafanya palizi mara mbili kwa Sh.100,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, kuna kuvuna, kupiga na kusafirisha kutoka shambani mpaka nyumbani jumla yake nimepiga kwa ekari moja peke yake anaweza kupata gunia 20, huyo wa Nkasi kwa gharama zote nilizosema hapa. Gunia 20 bei hiyo ambayo atakwenda kuuza kwa wakati huo ni Sh.35,000. Jumla ya mapato yake yote kwenye eka nzima ni 700,000; akiuza hayo mahindi gunia 20 wakati gharama zote alizotumia ni 742,000 hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namuuliza Mheshimiwa Bashe, hii bajeti tunayotenga tunaenda kumlenga mkulima gani? Ni kweli tunataka kuwainua wakulima wadogo leo, waliokuwa wanalima kwa mkono, watoke wakanunue trekta? Bado najiuliza pamoja na figure yote hiyo bado hatumkomboi mkulima wa kawaida. Hivyo, nataka nishauri mambo yafuatayo: - (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kwanza, pamoja na kwamba Mheshimiwa Waziri amesema ruzuku, sisi Wabunge tunasema ruzuku ni lazima na Wizara ya Fedha itoe fedha kumpatia Waziri wa Kilimo ili akatekeleze. Kumekuwa na utaratibu ambao siyo mzuri sana, yaani Waziri anakuja hapa anaeleza mipango yake, mwisho wa siku Wizara ya Fedha ndiyo inakuwa kikwazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huo muda ambao mkulima anautumia kwanza anapoteza muda wake wa kutosha zaidi ya miezi mitatu kuandaa eneo lake, lakini kinachokwenda kumkwamisha ni hiyo mbolea, hivi nani anaweza leo kutumia 842,000 halafu kwenye eka moja hiyo akapata 700,000, ni mkulima gani ataenda shambani? Safari hii hali si nzuri sana, hali si nzuri sana na kwa sababu hali si nzuri, mwaka jana tumepiga kelele hapa, tunamshukuru Mheshimiwa Rais alitoa fedha ikaenda kwa ajili ya ununuzi wa mahindi, lakini ule muda Serikali iliotoa fedha haikwenda kumlenga mkulima wa chini, ilikwenda kupeleka fedha ikaenda kununua kwa wale waliolangua kwa wakulima wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka fedha iende mapema, lakini na mbolea iende mapema na si kwenda tu, lazima Mheshimiwa Bashe, abadilishe utaratibu na achunguze kwa kina nini huwa kinatokea kwenye mbolea. Waziri asipojua tatizo hata akiweka ruzuku bado mkulima wa kawaida hawezi kufaidika na hii ruzuku ambayo itakuwa imewekwa kwenye mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira haya ambayo tunayazungumza leo nataka nishauri. Jambo la kwanza kwa kuwa lazima tuwe na mbegu zetu sisi kwa sababu tunaingia kwenye ushindani wa masoko, lazima Wizara wapeleke fedha za kutosha kwa Wakala wa Mbegu. Hata hivyo, sisi tuna Taasisi za Serikali zikiwemo Magereza, Magereza wana maeneo makubwa tofauti na maeneo wanayoyatumia. Leo tunazungumzia uhaba wa mafuta. Mheshimiwa Waziri katika hili hatuhitaji muujiza, narudia tena kwa siku nyingine leo hatuhitaji muujiza, tunahitaji waliopo kwenye nafasi leo, waweze kuonyesha dhamira zao za dhati kwamba fedha, hata wakiamua leo kuwekeza kwenye Magereza tano tu, tunapozungumza uhaba wa mafuta leo hatutazungumza tena. Tutakuwa namna gani tuuze nje kwa sababu hizi taasisi nguvu kazi wanayo, ni wao kuwawezesha nyenzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Magereza kama ya Namanyele pale Kitete wako tayari kufanya kazi, ile ardhi imepimwa na hapa Waziri ametuambia vizuri, huwezi kuboresha kilimo kama hujawekeza kwenye kupima udongo. Tumeona ametueleza hapo kwamba kuna fedha imeenda kidogo, tuone kwenye kupima udongo, wakipima udongo, watajua ni mbegu gani inafaa kuweza kuzalisha kwenye hilo eneo na hiyo hatutafanya kama sasa hivi ambavyo tunavyofanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo mengi wakiona kwamba Singida wamelima vizuri alizeti, leo wamepata sisi tulipata shida ya mahindi, anaona ngoja nilime alizeti. Kama Wizara imefanya utafiti watamwambia eneo lako linafaa kwa ngano na sisi tunakutafutia soko, ndiyo wajibu wa Serikali kuwasaidia wakulima. Leo mtu akiingia kwenye kilimo inakuwa kama adhabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri akipewa fedha hii tunaamini mkulima yule wa chini ndiyo ambaye sisi Wabunge tunataka akafanikiwe. Kama ni ununuzi uanze leo, huu ni msimu wa mavuno, Nkasi tunataka tujue soko la uhakika la wakulima wa Mkoa wa Rukwa katika zao la mahindi, ile ndiyo siasa yetu, ile ndiyo pamba yetu, ile ndiyo madini yetu kwa Mkoa wa Rukwa. Hatutaki itokee kama mwaka jana na lazima utaratibu uwekwe, isiwe kwamba ikitokea balaa sasa ndiyo tunaanza kusema tunamwomba Mheshimiwa Rais, hapana. Lazima tupate mpango wa Serikali, unapofika msimu wa mavuno Serikali wamejipangaje, soko liko wapi, kama hawawezi kununua, lazima mtafute soko nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wameenda kujenga kule Bandari, ukiziona zile Bandari Kabwe, Kalema hazionekani faida yake. tunataka tutumie zile bandari tupeleke mahindi yetu Congo na Burundi ili iwasaidie Watanzania wa Mkoa wa Rukwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi. (Makofi)