Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon Lucy John Sabu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. LUCY J. SABU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa fursa hii ili niweze kuchangia Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya katika kuwaletea maendeleo wananchi. Kiupekee nimpongeze kwa kutoa pikipiki 7,000 na vitendea kazi kwa Maafisa Ugani, nina imani itawezesha kufanya kazi kwa weledi mkubwa na kuweza kuwafikia wakulima na kutatua changamoto zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020 imeahidi ajira zisizopungua 8,000,000 na tunatambua sote changamoto ya ajira iliyopo kwa vijana. Nimepitia Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Kilimo, nimefarijika zaidi nilipoona vijana tumeguswa kupitia bajeti hii. Nichukue nafasi hii kuwapongeza Wizara ya Kilimo, kiupekee kabisa nampongeza Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Hussein Bashe; Naibu Waziri pamoja na watendaji wote wa Wizara. Nina imani kupitia mradi huu ambao unaenda kuanzishwa hususan kwa vijana tutaweza kunufaika vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze, kupitia bajeti tumeona kuna mradi unaenda kuanzishwa unaitwa Jenga Kesho Bora (Building a Better Tomorrow) Mradi mahususi kwa ajili ya vijana ambao wanaenda ku-fund, watatoa mtaji, watatota ardhi, watatoa mbegu, mafunzo, lakini pia watatafuta masoko kwa ajili ya bidhaa za mradi watakaouanzisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia mradi huu, Mheshimiwa Waziri atakuwa shahidi wakati anautangaza kwenye mitandao ya kijamii, aliona namna gani vijana wengi wamevutiwa nao na wapo tayari kushiriki katika mradi huo. Nimefarijirika zaidi nimeona fedha imetengwa kiasi cha bilioni nne ambayo itakwenda kuwasaidia vijana hawa ili waweze kufanya mradi huu kwa ubunifu wa hali ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kutoa ushauri wangu katika maeneo mawili hususan kwenye huu mradi. Nimeona mradi huu kwa majaribio utaanza Dodoma. Ningependa kushauri, Mheshimiwa Waziri tunaomba mradi huu usambae kwa nchi nzima ili vijana wengi waweze kunufaika. Pia tungependa kushauri hususan namna na utaratibu ambao utawekwa kwa ajili ya vijana au walengwa waweze kushiriki mradi huu, ningeshauri uwekwe utaratibu mzuri ambao vijana wengi waweze kuchaguliwa wale walengwa ambao kweli wanayo interest ya kufanya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii hususan kwa Mkoa wetu wa Simiyu nimpongeze Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa yeye ameshatoa mashamba na mwaka jana kuna vijana ambao walipewa mashamba na wameshaanza ninaomba tu Mheshimiwa Waziri ikikupendeza basi kwenye hiyo Bilioni Nne na Mkoa wa Simiyu uweze kutuona ili tuweze kunufaika na mradi huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue nafasi hii kuwaomba, niliona mwaka huu kwa mara ya kwanza kuna vijana walipelekwa kwenye maonesho ya Dubai na Uturuki, ninawaomba Wizara waendelee na utaratibu huu wa kuwajengea uwezo lakini vijana wengi waweze kujifunza wenzetu huko nje wanafanya kilimo cha aina gani ili tuweze kunufaika lakini pia vijana wengi waweze kujiajiri katika sekta hii ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)