Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Iramba Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika bajeti ya Wizara ambayo tumezoea kusema uti wa mgongo lakini leo Mwijage ameongeza ni Bajeti ya Taifa, kwa sababu tunagusa wananchi wa Tanzania kwa asilimia kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niwape pongezi Mawaziri, Waziri wa Wizara hii na Naibu Waziri wake, hawa vijana mimi nawafahamu akili ya Mheshimiwa Bashe naijua vizuri, mimi nilikuwa bosi wake nikiwa Katibu Mkuu wa Vijana, ana akili nyingi sana hapa ametumia robo tu. Kwa hiyo, nina hakika kama bajeti yake hii itatekelezwa yote tutafika mahali tutaongeza fedha nyingi zaidi kwa jinsi ambavyo wanaupiga mwingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mwanasheria Antony pia namfahamu, kwa kweli Mama amechagua vijana hawa ili baadaye tuwe na model, kwamba vijana wakipewa nchi au wakipewa kazi wanaweza kuifanya. Nami sina wasiwasi kabisa na ninyi vijana wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitagusa kwenye jambo ambalo linagusa sana Jimbo langu pia linagusa nchi kwa maana ya mbegu za mafuta ya kula na hususan alizeti. Tunalo tatizo kubwa la mafuta, tunalo ombwe kubwa la mafuta na tunaagiza nje ya nchi wakati sisi ni nchi ya wakulima. Katika kulima mbegu hizi Mkoa wa Singida na hususan Jimbo la Mkalama ndiyo uti wa mgongo haswa wa kulima zao la alizeti. Kwa hivyo, ninakuomba Waziri jambo ambalo ulilianza mwaka jana la kutoa mbegu kwa mkopo lilikuwa ni jambo zuri, katika bajeti yako umesema tena kwamba utatoa mbegu lakini ningeomba sasa niseme machache ambayo yalikuwa ni kasoro kidogo kwenye ugawaji wa mbegu zilizopita ili mbegu hizi utakazogawa sasa ifanyike kwa ufanisi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni aina ya mbegu, wananchi walitegemea sana wapate Highsun, tunajua kwamba Highsun ni mbegu inayotoka nje ya nchi, umesema kwamba ASA watatutengenezea mbegu zetu wenyewe lakini ni process ambayo mbegu zitachukua muda kidogo, kama itakuwa bado katika msimu huu, ninaomba mbegu utakazoleta highsun iwepo kwa sababu wananchi wanahitaji highsun ili waweze kuzalisha mafuta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbegu iliyokuja pia wameitoa kasoro kidogo, inatoa matawi mengi kwenye mti mmoja wa alizeti na vichwa vinakuwa vidogo, kwa hiyo, wananchi wangu hasa wa Mkalama ambao ni wakulima wakubwa wa alizeti wamelalamika na hii mbegu. Kwa hiyo, ninakuomba sana katika zoezi linalofuata hili tulirekebishe mapema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ugawaji wa hizi mbegu, ulitoa mbegu vizuri ukatupeleka Mkoani lakini hamkutoa waraka mzuri jinsi gani mbegu hii igawiwe. Sehemu nyingine Maafisa Ugani wakawa wanasema lazima ulipie kwanza, sehemu nyingine wanasema ukopeshwe, kwa hiyo kukawa na mchanganyiko hapa, hii imesababisha mbegu nyingi imebaki kwa sababu hakukuwa na waraka mzuri ulioeleza jinsi gani mbegu hii igawiwe au ikopeshwe. Kwa hiyo, nikuombe katika mbegu zinazofuata sasa jambo hili uliangalie kwa umakini sana ndugu yangu Mheshimiwa Waziri wa Kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni miundombinu. Umesema hapa kutakuwa na miundombinu ya kutosha, ruzuku na kila kitu, lakini ndugu zangu kutegemea mvua, mbegu hii ambayo imegawiwa pamoja na kasoro zake lakini nyingi imepelea mvua. Kwa hivyo, kilimo cha kutegemea mvua hakitufai kwa sasa katika nchi yetu hii ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna ardhi ya kutosha, mabonde ya kutosha, mfano mimi katika Jimbo langu la Mkalama ukienda Kata ya Mwangeza - Dominic pale kuna eneo wanalima vitunguu, wakipata bwawa wakichimbiwa visima pale wanaweza kuzalisha muda wote wa mwaka. Pia kuna scheme ya umwagiliaji pale Mwangeza imekufa muda mrefu ikifufuliwa ila katika hizo scheme ambazo umesema utaziweka naomba kabisa Mwangeza katika ufufuaji wa scheme usije ukaicha katika Jimbo langu la Mkalama. Hii itatusaidia sana kuhakikisha tunapata mbegu za kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri block farming ulikuwa muumini wa hili jambo, ulipokuwa backbencher ndugu yangu Bashe, nikiwa mtaani kila ukisimama nilikuwa najua aidha utaongelea block farming ama utamuandama Makamu wa Rais sasa kuhusu kwenye mambo ya fedha akiwa Waziri wa Fedha, hizo zilikuwa ajenda zako. Sasa Mungu ni fundi kweli kweli alivyojua unasema sana mambo block farming akakupa Unaibu, lakini ukawa unasingizia huingii Baraza la Mawaziri, Mungu alivyofundi akakuongezea Uwaziri. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa usipoe Mheshimiwa Bashe ndugu yangu, block farming ndiyo itakuwa ukombozi. Umesema tu pale kutakuwa na block farming lakini kwenye alizeti hujasema vizuri. Mimi nikushauri kwamba angalau kila Kata katika nchi hii hasa kwenye Jimbo langu la Mkalama, kule kuna block farm ambayo wale Maafisa Ugani uliowapa nyenzo, uliowashonea na jezi na kila kitu anakuwa ofisi yake ni block farm iliyopo kwenye Kata. Wanaomiliki ile block farm wanakuwa vijana wa kike na kiume ndani ya Kata. Kwa hiyo, uta-solve mambo matatu hapa, kwanza utatengeneza ajira kwa vijana, pili utazalisha mbegu za uhakika na tatu utawapima vizuri Maafisa Ugani wako kwa sababu watakuwa na ofisi ndani ya Kata ambalo ni shamba kubwa la block farm. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, ninakuomba katika hizi block farm peleka kwenye Kata hasa hizi za alizeti hapo utakuwa umetusaidia sana katika jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile viwanda vyetu vya mafuta, viwanda vikubwa kama Mount Meru na viwanda vingine, hawana mashamba makubwa ya kulima wanategemea wakulima wadogo wadogo. Naomba ufanye kama yalivyo mashamba ya miwa kwenye viwanda vya sukari. Kiwanda kinakuwa kina shamba outgrowers wanajazia tu. Kwa hiyo, viwanda vikubwa wapewe hekta za kutosha hata 10,000, wapewe na waambiwe walime, kwa hiyo anakuwa na mbegu za kiwanda lakini wananchi wanakuja kujazia kwa hiyo viwanda vyetu vitafanya kazi throughout the year na hii itatusababisha sisi tuweze kupata mafuta ya kutosha na tuokoe fedha zetu hizi ambazo tunazipoteza nyingi sana fedha za kigeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingineā¦
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa.
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru naomba niunge mkono hoja lakini nitakuona kuhusu suala la masoko Mheshimiwa Waziri ili tuliweke vizuri, ahsante sana. (Makofi)