Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ushetu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nikuombe radhi sauti yangu sio rafiki kulingana na hali ya hewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa nafasi hii ya pekee ya upendeleo ya kuweza kujadili kwa mara ya kwanza Wizara ya Kilimo. Nimpongeze sana pia Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wetu Samia Suluhu Hassan, kwa upande wa kilimo ametusaidia sana sisi wakulima. Kwa mara ya kwanza katika nchi ya Tanzania tumeweza wakulima wa pamba kupewa mbegu zenye thamani ya bilioni 16 bure bila kukatwa chochote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwenye upande huohuo wa pamba Mheshimiwa Rais ametoa dawa zenye thamani ya za zaidi ya bilioni 36 kwa nchi nzima, mikoa yote, ya zao la pamba bure, haijawahi kutokea. Kwa hiyo, niendelee kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, lakini nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Kilimo na Naibu Waziri wa Kilimo, pamoja na Makatibu Wakuu na watumishi wote kwa kazi nzuri wanayoitendea nchi yao, wanayowatendea wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimshukuru sana Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Tanzania, Dkt. Benson Ndiege. Kwa mara ya kwanza mwaka jana alipeleka magari saba kwa warajisi wasaidizi wa mikoa, amepeleka pikipiki 135 kwa Maafisa Ushirika. Hii yote ni kwaajili ya kuboresha wakulima, kwaajili ya kuboresha sekta za wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nataka niende moja kwa moja kwenye mchango wangu. Cha kwanza kabisa pamoja na mazuri yote wanayoyafanya Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri na viongozi wote, bado tuna changamoto kwenye Sheria ya Ushirika. Sheria ya Ushirika bado inahitaji marekebisho makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia bajeti ya Mheshimiwa Waziri yote sijaona mahali ambapo anaweza akaileta Sheria ya Ushirika Bungeni iweze kujadiliwa, iweze kupitiwa pamoja na Sera ya Ushirika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunajivunia Mheshimiwa Bashe kuwepo pale na umahiri wake wa kazi, lakini bado uwezo wa utendaji wake wa kazi unaweza ukapotea kwa sababu, bado sheria ya ushirika si pana. Tunaomba sana hili suala la ushirika na Sheria ya Ushirika iletwe Bungeni ili tuifanyie marekebisho na tuweze kuiboresha ili iwe na makucha kwa ajili ya kushughulikia wabadhirifu wa fedha na mali za wakulima wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ugawaji wa pembejeo kama kwenye bajeti ilivyoandikwa; nataka nijikite kwenye mfumo mzima wa usajili wa wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, Serikali inajitahidi sana kupeleka mbegu pamoja na dawa, lakini tuna changamoto ya kutowatambua tunaowahudumia. Tunatumia makisio ya tunaowahudumia lakini bado hatujawatambua tunaowahudumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Wizara imetoa pikipiki 6,000 kwaajili ya kwenda kwa wakulima wetu, lakini leo hii ukitaka uwaulize hata maafisa ugani wanahudumia wakulima wangapi hawawezi kukwambia. Mimi nilikuwa nashauri, na hata kwenye bajeti sijaiona; tupate mkakati mzuri wa kuwatambua wakulima, wa kuwajua wakulima mahali walipo na kuhakikisha kwamba mkulima wa Imala Makoye anayelima pamba yuko maeneo gani? Analima eka ngapi? Anazalisha kiasi gani? Pamoja na kwamba, tunapima udongo, lakini suala la kujua na kutambua mahitaji yake ni suala la msingi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoa mfano hata sisi kwenye zao la tumbaku, kwenye zao la tumbaku mkulima huwezi kumpelekea bidhaa kama haumtambui. Pembejeo zote zinazotoka kwenye sekta ya tubaku zinakuja zinamlenga mkulima moja kwa moja kwa sababu tayari yuko kwenye usajili; ana namba yake, ana kitambulisho chake na anajua anacholima leo analima nini na anazalisha kiasi gani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tukirudi kwenye zao la pamba ndio maana hata pembejeo zinazoenda kwenye zao la pamba matokeo yake tunakutananazo sokoni kwenye magulio kwa sababu, tunawapelekea watu tusiowafahamu. Tumeangalia kwenye bajeti sijaona kitengo ambacho kimeandaa kuwahudumia na kuwezesha bodi za mazao ziweze kuwa na nguvu. Tumeangalia bodi za mazao hazijatengewa fedha, tunaomba suala hili liangaliwe vizuri. Tuna Bodi ya Pamba; Bodi za Pamba, Tumbaku pamoja na Korosho zinafanya kazi nzuri sana, lakini hatuoni fedha gani zinapelekwa kushughulikia kuwezesha hizi bodi za mazao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mfano tosha sisi kwenye upande wa masoko ya tumbaku. Masoko ya tumbaku ili tuweze kupata madaraja classifier ni Mteuzi Mfawidhi wa Bodi ya Tumbaku. Na Mteuzi Mfawidhi wa Bodi ya Tumbaku wakati mwingine hana usafiri wa kwenda sokoni, usafiri anaotumia anabebwa na gari la mnunuzi ambaye wanaenda kushindana kwenye bei ya mkulima, nai atatendewa haki? Sidhani kama mkulima anaweza akapata haki wakati mwenye kutenda haki amepewa lifti na mnunuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba hili suala la fedha na bajeti kwa upande wa bodi zetu za mazao liweze kuimarishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa upande wa Jimbo la Ushetu. Nilitaka nimuombe Mheshimiwa Waziri, upande wa Ushetu tunazalisha sana mazao ya tumbaku, pamba, mahindi, tmpunga, karanga pamoja na dengu. Ningeomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha bajeti yake, kwa sababu Halmashauri ya Ushetu hatuna maghala na hivyo tunapoteza mazao mengi sana kwa sababu ya kukosa maghala na tumeshatenga eneo la zaidi ya ekari 600 kwa ajili ya kujenga maghala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kwa sababu tunazalisha mpunga na tunalisha nchi za mazaiwa makuu, Mkoa mzima wa Shinyanga pia unalishwa na Halmashauri ya Ushetu. Nchi za Kongo zinanunua mazao yao Ushetu, nchi ya Rwanda inanunua mazao yake Ushetu na wenzetu wa Burundi na Uganda wananunua mazao Ushetu. Tunaomba Mheshimiwa Waziri tuletewe maghala katika Halmashauri ya Ushetu, lakini pia tunahitaji eneo la umwagiliaji. Tumetenga zaidi ya ekari 3,500 kwa ajili ya umwagiliaji kwa kilimo cha mpunga. Tunaomba hili Mheshimiwa Waziri atakapokuja aje nalo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nijikite pia kwenye suala la utafiti. Tuna taasisi ya utafiti wa zao la tumbaku inayoitwa TORITA, sijaona fedha zinazopelekwa kwenye utafiti hasa kwenye upande wa TORITA, inatafiti sana suala la mbegu. Tuna changamoto kubwa sana ya mbegu za zao la tumbaku. Mbegu tunazozitumia kwenye zao la tumbaku wanao-supply ni wanunuzi wenyewe. Sasa tunaomba, kwa sababu tuna taasisi ya utafiti ambayo inasimamia zao la tumbaku, tunaomba fedha ziweze kuelekezwa kwenye taasisi ili mbegu za tumbaku zizalishwe hapa nchini, wakulima wengi wazalishwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa kuingiza kampuni nyingine ya ununuzi wa tumbaku na kuwasha kiwanda cha TLTC. Hili tumpongeze sana Mheshimiwa Waziri, wakulima wetu walikuwa na hali ngumu sana ya wapi wauze tumbaku. Na mwaka huu ameahidi kununua zaidi ya kilo milioni 10, na msimu unaukuja ataongeza kilo milioni 30. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe tu, nchi za wenzetu, kwa mfano Malawi wanazalisha zaidi ya kilo milioni 230 kwa mwaka na bei yao ni kuanzia dola tatu mpaka dola nane. Zimbabwe wanazalisha zaidi ya milioni 200 mpaka milioni 300 na bei yao ni kuanzia dola tatu mpaka dola nane, iweje sisi Tanzania tumekuwa kisiwa? Wastani wetu wa bei ni dola 1.4, umezipanga sana ni dola 2.2. Niombe kwamba, Waziri kupitia Wizara yake ya Kilimo ateuwe wataalamu na Bodi ya Tumbaku waende kwenye nchi za wenzetu hizi ili kuona wanatumia mfumo gani kupanda kutoka dola tatu mpaka dola nane ilhali sisi tunahangaika na wastani wa dola moja? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiendani na gharama za uzalishaji. Gharama za uzalishaji na bei ya pembejeo imepanda kwa kiasi kikubwa sana lakini bei ya tumbaku inazidi kuporomoka. Ningeomba sana hili Mheshimiwa Waziri aliangalie sana kwa sababu bodi zipo na viongozi wa ushirika wapo, waweze kutembelea kwenye nchi jirani waweze kuona wenzetu wanatumia mfumo gani kuweza kupata bei nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)