Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon. Deus Clement Sangu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa fursa hii ili niweze kuchangia kwenye Sekta muhimu sana ya Kilimo. Kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri Bashe na Naibu wake kwa kazi nzuri wanazofanya pale Wizarani. Katika Wizara hii nitakuwa na mambo muhimu matatu: Kwanza nitaongelea kampuni yetu ya mbolea ya Taifa kwa maana ya Tanzania Fertilizer Company; muda ukiniruhusu nitaongelea Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko; na mwisho kabisa nitamkumbushia Mheshimiwa Bashe ahadi zake alizotupa wakati alipofanya ziara Mkoani Rukwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na Kampuni yetu ya Mbolea, Mheshimiwa Bashe anajua wazi na kwenye bajeti yake leo hii amesema kwamba wanaenda kuiongezea uwezo Kampuni yetu ya Mbolea ya Taifa kwa maana Tanzania Fertilizer Company bilioni 6.0. Hata hivyo, nimkumbushe, kampuni yetu hii bilioni 6.0 aliyotaja hapa leo, ni token tu, tuna tatizo kubwa na ndiyo instrument kubwa ya nchi hii ambayo itatusaidia katika ku-stabilize bei za mbolea nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu mwaka 2008 tulipoiacha hii kampuni ikafa kwa sababu ya mbolea ya ruzuku isiyolipika, tukaitwisha mzigo wa madeni mengi, hii kampuni ya mbolea ikafa, tumewaacha private operator wana-operate soko la mbolea, tatizo lake ni nini? Wanaweza wakafanya curtail, wakafanya inflation na ndiyo maana unaona bei ya mbolea nchini imekuwa haitabiriki. Kama kampuni yetu ingeweza kuwa na fedha, kama kampuni yetu ingekuwa ina uwezo, tungeweza angalau kama Serikali tukasimama, wakati wa migogoro na shida ya mbolea kama leo, kampuni hii wangeweza wakafanya kazi hiyo pasipo tatizo lolote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ninavyoongea Waziri ametaja bajeti yake bilioni 6.0, wakati huo hii kampuni inawadai watu, Serikali bilioni 3.0, vyama vya ushirika bilioni 2.0, watu private zaidi ya bilioni 10 na na kitu. Kwa hiyo jumla ya bilioni 19 ziko kwa watu. Mheshimiwa Waziri anahangaika tumpitishie bilioni 6.0 hizi, lakini kuna bilioni 19 watu wapo, hawajafa, wapo na wanaendelea kuwepo. Mheshimiwa Waziri atumie Serikali ina mkono mrefu, watu warudishe bilioni 19 tufufue kampuni yetu ya mbolea kwa sababu bila hivyo tatizo la mbolea litatusumbua sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wamesema kwamba hatuna hata stock ya mbolea, lazima tuwe na buffer stock ya mbolea kwa sababu bila hivyo ukitegemea private operator wao wanafanya kwa kufuata theory ya just in time. Akileta mbolea anauza, hawezi kuweka stock ya miaka miwili au mitatu kwa sababu yeye siyo shughuli yake, yeye anataka apate faida kwa wakati huo, akishapata faida anaachana na mambo hayo. Hivyo, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri aende kufanya shughuli hii ya kuwafuatilia wale waliochukua bilioni 19 kwenye kampuni yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nimshukuru pia Mheshimiwa Rais kwa mara ya kwanza ameonyesha nia njema na kampuni hii. Amelipa madeni bilioni 9.0 kwenye Benki ya Exim, lakini bado tunadaiwa bilioni 15 kwenye mabenki mengine. Mheshimiwa Waziri aende kupambana kwa namna yoyote, tutakapoenda kupeleka ruzuku ya bilioni 250 alizotaja hapa, kampuni yetu iwe imefufuka nayo ishiriki ili isaidie ku-regulate suala la mbolea. Wananchi wangu kwa mfano Mkoa wa Rukwa tumehangaika, tumeshindwa hata kulima mahindi kwa sababu mbolea ilikuwa juu. DAP tulikuwa tunanunua mpaka mfuko mmoja Sh.150,000; UREA imeenda Sh.85,000, bei ni kubwa, wananchi waliamua waachane na mahindi. Hivyo, Nimwombe sana Mheshimiwa Bashe, nataka nijue atakapokuwa anahitimisha atupe strategy, aachane na hiyo bilioni 6.0, ni namna gani anafufua Kampuni yetu ya Mbolea ya Tanzania. Hilo ni jambo la kwanza nilisema nitalisemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni Bodi yetu ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko. Inatusaidia sana kutafuta masoko, tumepata masoko ya mazao kule Sudan ya Kusini, Rwanda, Zimbabwe, Comoro na DRC. Sasa suala la DRC kwa kwetu Mkoa wa Rukwa ndiyo soko letu la Jirani, lakini linakumbwa na vikwazo vingi sana kwa sababu lazima tupite Zambia na pale Zambia nao ni competitor wetu kwenye zao la mahindi wanatuwekea trade embargoes ambazo zinafanya biashara ile iwe ngumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshauri Mheshimiwa Bashe kupitia Wizara ya Mambo ya Nje, yeye mwenyewe na Ubalozi wetu wa Zambia, waende wakaongee na Serikali ya Zambia watupunguzie hivi vikwazo kwenye mazao, yaani mfanyabiashara akitoka na mazao kwa mfano Songwe, Rukwa akifika tu Zambia wanaweza wakamweka hata wiki mbili au wiki tatu. Mambo mengine kama samaki na mazao mengine hawana shida, ila zao moja tu la mahindi ndiyo kikwazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe na Waziri analijua vizuri jambo hili, kupitia ubalozi wetu, Wizara ya Mambo ya Nje, tukafanye kupitia diplomasia yetu na nchi jirani ya Zambia wasitunyanyase kwenye zao la mahindi, kwa sababu wamekuwa wakitoa visingizio kwamba mahindi yetu yana sumu, wafanyabiashara wanapata hasara wakiwa hapo hapo na mwishowe wanakata tamaa, kwa hiyo mazao yetu hayapati fursa ya kwenda huko DRC pale Lubumbashi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili kwenye hii Bodi ya Mazao Mchanganyiko, nimefanya utafiti na mpaka tukafanya mazungumzo na Jimbo jirani la Out Katanga, wametushauri jambo moja hii habari ya kupita nchi za jirani ndiyo maana tunapata mateso, tukae na Wizara ya Fedha, tutafute mwekezaji, tutengeneze zile kilometa 720 ambazo zitatupeleka Lubumbashi, ambayo itatupa fursa sasa ya kufunguka kwa Bandari ya Kasanga, Bandari ya Kalema na Bandari ya Kabwe, tutaenda kwa urahisi kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukipata mwekezaji atawekewa fee ya barabara ambayo return yake haifiki hata miaka mitano, yule mwekezaji pesa itarudi na barabara ile itafungua Mkoa wa Rukwa, Katavi na Kigoma. Nimwombe sana Mheshimiwa Bashe, haya manyanyaso ninayomwambia ya kupitia nchi za jirani sasa tukafungue. Tumewekeza bandari nilisema hata kwenye hotuba ya Waziri Mkuu, bandari zile zinabaki kuwa idle. Twende tukamalize tu kilomita 720 tuunganishe pale Bandari ya Moba, upande wa pili wa Zambia, tukafike Lubumbashi ili ghala lile linalotunza zaidi ya tani 2000 kule Lubumbashi liwe na impact na Bodi ya Mazao Mchanganyiko waone tija kwamba kweli tumeenda kusaidia kutafuta masoko kwa ajili ya wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo nataka niongelee pia ni kwamba, hii bodi tumeipa majukumu mazito ya kuchukua viwanda vilivyokuwa chini ya NMC. Ili viwanda hivi viweze kuongeza thamani ya mazao ya wakulima wetu na nimwombe Waziri, mikoa mingine imeweka vinu vya kusindika mpunga, mahindi, lakini Mkoa wa Rukwa sijaona. Nimwombe sana Mheshimiwa Bashe na amekuja pale, tupate na sisi kiwanda walau cha kusindika mpunga, tupate viwanda vya kusindika mahindi ili tuongeze thamani ya mazao yetu ambayo yatafanya wananchi wetu wapate urahisi wa kupata masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna shida moja na naomba hii Waziri wa Fedha popote alipo anisikie. Bodi ya Mazao Mchanganyiko wameandika proposal kuomba kuendeleza hivi viwanda na ile proposal inataka tu approval kutoka Wizara ya Fedha. Approval ile imekuwa na vikwazo na ile siyo government guarantee ni just a government concept, wana-approve tu, wanatupa fedha na ile fedha haina impact yoyote kwenye deni la Taifa, yenyewe inaenda kufanya jambo moja kwamba mnakuwa na partnership na Benki, CPB na Benki wana-operate kiwanda, Benki ikipata revenue yake wanawaachia kiwanda kinakuwa cha kwenu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwomba sana Mheshimiwa Bashe, watakapokuwa hata kwenye Baraza la Mawaziri amweleweshe vizuri najua ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu Nchemba ni Economist anajua, hili jambo halina impact yoyote kwenye deni la Taifa, ni jambo tu la ku-approve, wachukue hizo fedha, wajenge viwanda vya kuongeza thamani za mazao kwa mwananchi ili tuweze ku-compete. Mwezi Machi Mheshimiwa Waziri alikuwa yuko kwenye maonyesho ya Dubai expo, sasa masoko yatakuja mengi, baadaye hatutaweza ku-compete kwa sababu hatuna value addition ya mazao yetu. Nimwombe sana Waziri, hili jambo ni muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu na la mwisho sasa, nimkumbushie ahadi alizokuwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha, malizia kwa dakika chache malizia.

MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi zote za Mheshimiwa Bashe nitampelekea kwa maandishi na nitataka kujua status ya hizi ahadi alizoahidi zitaishaje, maana ana ahadi kama 10, naona ametekeleza mbili tu, ahadi nane bado namdai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. (Makofi)