Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon. Deodatus Philip Mwanyika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Njombe Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hoja iliyo mbele yetu ya kilimo. Nianze kumpongeza sana mdogo wangu Mheshimiwa Bashe na Naibu Waziri na Watendaji wote katika Wizara hii. Kwa kweli wameonyesha njia, tunaona mambo yanakwenda vizuri, wamefanya ushawishi mkubwa, wamekuwa wasikivu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile namshukuru Mheshimiwa Rais toka mwanzo kabisa kwa kuonesha nia ya dhati kabisa na kutekeleza nia hiyo ya dhati kwa vitendo. Tulilalamika sana hapa Bunge lililopita kuhusiana na mbolea tukamwona Mheshimiwa Rais kwa nafasi mbalimbali kupitia Waziri Mkuu akatuambia asingeweza kulitekeleza jambo lile kwa sababu muda ulikuwa ni mfupi na fedha zilikuwa hakuna. Akatuahidi, analishughulikia. Tunamshukuru sana kwamba ameweza kulishughulikia hili jambo kwa wakati. Tumetoa ahadi majimboni kwamba linashughulikiwa na kwa kweli limeshughulikiwa. Ahsante sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sasa kuongelea mambo mawili; moja, ni kilimo cha biashara au ushindani ambacho ndiyo dira ambayo ndiyo inaonekana tunakwenda kwenye mazao ya kimkakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kusema, kilimo cha ushindani au cha kibiashara tunapokiongelea tunaangalia ni namna gani tunafika kwenye soko. Vile vile tunaangalia vitu viwili; tunaangalia ubora na gharama. Ubora huo tunaupata kwa gharama gani? Sasa kuna mambo ambayo tumshukuru sana Mheshimiwa Bashe pamoja na Naibu Waziri na Wizara nzima, kuna mambo ambayo yapo ndani ya uwezo wao wameanza kuyafanya na tumeyashuhudia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulizungumzia ubora kwamba lazima uanze kwenye miche, kwenye kitalu. Tulisema sana mwaka 2021 kwenye bajeti iliyopita na kweli wamelitekeleza, tumeona wazi kabisa wameanza mafunzo, wameanza kuwatambua wazalishaji wa miche na wengine wengi wamekuwa hapa kwenye training na wengine tumewaona hapa walikuja Bungeni kwa ajili ya kuangalia kinachoendelea hapa. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kutekeleza hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna mambo mengine ambayo nadhani pamoja na kuangalia ubora, bado tulikuwa tunamwomba Mheshimiwa Waziri ajaribu kuona ni kwa namna gani; kwa sababu kwa kweli kwenye mazao ya mbogamboga na parachichi lazima tukubali kwamba ubora ndiyo utakaotutoa. Hizo Shilingi bilioni mbili anazoziongelea Mheshimiwa Waziri au Wizara hatutaweza kuzipata kama hatutakuwa na ubora kwenye soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuna mambo ambayo ni ya muhimu sana kuyaangalia kwenye soko ikiwa ni pamoja na kuangalia uthibiti wa ubora. Tulikuwa tumeongea hapa ni vizuri tukawa na agency au tukawa na chombo kitakachosaidia kwenye kuthibiti ubora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua na ninafurahi kwamba hata hilo nalo Mheshimiwa Waziri ametuonesha wazi kwamba lipo katika mchakato. Tunaomba likamilishwe mapema. Hatutaki chombo hiki kiwekwe kwa ajili ya kuingilia biashara, lakini tuna uhakika chombo hiki ni muhimu kwa ajili ya kuhakikisha kwamba hakutakuwa na mazao ambayo yatakwenda sokoni bila kuwa na ubora. Tuna uhakika chombo hiki kitapewa mandate zaidi ya kuhakikisha kwamba hili zao lenyewe linakuwa promoted. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kusema, kuna mambo ambayo Mheshimiwa Bashe na Wizara yake hawana uwezo na ni mambo ya muhimu sana ya kutelepeka kwenye soko. Zao hili la parachichi na mazao ya mbogamboga yanalimwa kwenye mashamba, lakini yanachukuliwa na wachukuzi, yanasafirishwa na wasafarishaji mpaka yanafika kwenye masoko, lakini ni mazao ambayo yapo sensitive, yanataka ubora wa hali ya juu, pia ni mazao ambayo yanapoteza ubora kwa haraka sana. Kwa hiyo, ni dhahiri kwamba yapo mambo lazima tuyafanye kwa umakini na kimkakati na hasa yale yanayohusiana na miundombinu kwa ujumla. Wengine wanasema kwa jina rahisi logistics. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli napenda kusema, tukianza na barabara, tuna vizuizi bado vinasumbua wasafirishaji wa mazao ya mbogamboga na mazao ya parachichi. Ukienda ma-gate fulani fulani, na kuna gate moja lipo pale Iringa, wana maswali mengi sana ambayo yanaonesha bado hawatambui kwamba maswali hayo hayasaidii sana kwa sababu mchukuaji amechukua perishable goods na maswali yanayoulizwa hayapo relevant. Kwa hiyo, naomba Wizara zinazohusika ziweze kutusaidia kwenye hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo makubwa sana yapo kwenye maeneo ya Mamlaka zetu za Usafirishaji za Anga na Mamlaka ya Bandari. Kwa kweli kama tupo kwenye ushindani tutambue kwamba tunatakiwa kufanya kazi kubwa sana katika Mamlaka ya Bandari. Nafahamu kuna kazi kubwa inafanyika, lakini bado wana mambo mengi ya kufanya tukilinganisha na wenzetu, bado tupo nyuma sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, ukiangalia kwenye maeneo yetu ya Airport bado cold rooms facility hazina uhakika. Ukienda Songwe ambako kuna uzalishaji mkubwa wa parachichi Southern Highlands kwa mtu ambaye atataka kusafirisha kwa haraka, atapeleka Songwe Airport. Hatuna cold room facility pale au kama zipo, bado zinatengenezwa na zinakwenda pole pole sana. Ipo haja ya kuharakisha zoezi hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye Bandari yetu ya Dar es Salaam, hakuna dedicated berth, ipo ya export kwa ujumla, lakini kwa vitu ambavyo ni perishable hakuna dedicated berth. Ukienda kwa wenzetu ambao tunashindana nao wana berth zaidi ya tatu, nne, mpaka saba ambazo zipo dedicated kwa perishable. Wafanyakazi kwenye hizo berth akili yao yote kila wakati inafikiria ni namna gani wa-facilitate mzigo uondoke ili uweze ku-maintain ubora wake. Kwa hiyo, haya ni mambo ambayo Wizara ya Kilimo wanatakiwa wasaidiwe kimkakati kama nchi tuhakikishe kwamba tunafikia hilo lengo linaloongelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusiangalie soko la nje tu kwenye mazao ya mbogamboga na parachichi, tuangalie na soko la ndani. Ipo haja ya kuwa na mkakati wa kuhakikisha zao la parachichi hata hapa ndani linapewa elimu ya kutosha, watu wafahamu, siyo kulima na kusafirisha tu, tunaweza tuka-process zao la parachichi hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeongolea gap la laki nne, mafuta hatuna ya kutosha, tunahitaji mafuta. Parachichi inawezekana. Kuna watu duniani wana technology ya kuzalisha parachichi kwa wazalishaji wadogo. Njombe sasa hivi tuna viwanda tisa vya packing na exporting ya parachichi. Viwanda vyote hivyo vinamilikiwa na watu toka nje, ukiacha kimoja tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge na Mheshimiwa Waziri, tuliangalie hili kwa makini sana. Nafahamu nchi ina mkakati wa kuwa na packing facility lakini tuelewe kwamba tupo kwenye ushindani. Hawa wenzetu wenye viwanda wakiwa na mazao kule kwao, mazao ya wakulima huku hawatayachukua kwa muda, watayaacha, wata- process, wata-export mazao yao. Kwa hiyo, ni vizuri tukahakikisha kwamba na sisi tunafanya hiyo shughuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwenye umwagiliaji; parachichi inahitaji maji kama vile chai. Tulipokuwa tunaongea mwaka 2021 hapa, namshukuru Mheshimiwa Waziri na timu yake wameweza kuwa na mkakati mzuri wa kufanya umwagiliaji. Sina uhakika ni kwa kiasi gani mkakati huo wa umwagiliaji unakwenda vile vile kwenye maeneo. Imeongelewa Njombe kwa ujumla, Mheshimiwa Waziri atakapohitimisha hapa naomba nielewe anaongelea maeneo gani huko Njombe? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake kuna maeneo ambayo ni ya flat, lakini maeneo mengi ya uzalishaji ya parachichi ni maeneo ya milima ambayo unaweza ukafanya umwagiliaji kwa urahisi sana. Ni kutafuta bonde la asili linazibwa, unapata maji mengi yanatawanywa, yanakwenda mbali, yanakamata wakulima wengi kwa pamoja. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile muda hautoshi, niongelee chai kwa haraka haraka…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwanyika muda wako umekwisha.

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, basi naomba ni-windup.

MWENYEKITI: Sasa naona umegusia chai hapo. Mheshimiwa dakika moja basi, angalau. (Makofi)

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye chai tumeona matunda mazuri na tumeona mikakati mizuri, lakini bado napenda kusema, tuna Bodi ya Chai, tuna Wakala wa Chai. Kwa kweli pamoja na kazi wanazozifanya zinaonekana ni nzuri, lakini bado mandate zao hawazitumii vizuri. Kwa mfano, wakulima wa chai bado mpaka sasa wananyonywa sana kwa maana ya kwamba hawalipwi kwa wakati na wanadai madeni. Bodi ya Chai tuna uhakika inatakiwa iwasaidie hawa wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi ni hawa watu Tea Agency. Hawa watu wa Tea Agency wanatakiwa waelewe kwamba zao la chai siyo lazima lilimwe na watu wakubwa. Unaweza ukawa na wakulima wadogo ambao wanaweza wakazilisha chai ikapelekwa na maisha yao yakawa mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kusema, hawa watu wa Tea Agency wamepata muda, walikwenda…

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwakagenda taarifa. Unataka kumuongezea taarifa kwenye dakika yake moja ya nyongeza siyo! Maana muda wake ulishaisha.

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampa taarifa.

T A A R I F A

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampa taarifa mzungumzaji, anasema Bodi ipo vizuri, wakati huohuo anasema hawafanyi vizuri. Bodi haisimamii chai vizuri, aseme wazi. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwanyika, unapokea taarifa.

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa kwa maana ya kwamba wana kazi nyingi ambazo wamezifanya na ni nzuri, lakini wana maeneo bado wako very weak hawa watu wa Bodi, na mojawapo ndilo nililolisema hilo la kwamba hawasimamii wakulima kupata fedha zao wanazozidai. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kuongelea suala la wakala kidogo tu. Nipende kusema…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwanyika nakushukuru sana kwa mchango wako, muda wako umekwisha.

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)