Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Namtumbo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na mimi kunipa fursa hii. Kwanza naomba kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake aliyoitoa iliyosheheni mambo mengi sana. Katika hotuba yake Mheshimiwa alizungumzia uchumi wa dunia umeendelea kuyumba kama alivyoainisha katika ukurasa wa 15 aya ya 20 mpaka aya ya 25 ukurasa wa 18. Hata hivyo Tanzania chini ya uongozi wa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuchukua hatua madhubuti kabisa na wote tunazijua zimefanya uchumi wetu usiendelee kuyumba. Ukuaji wa uchumi Duniani umeonesha umeshuka kutoka 6.2 asilimia mwaka 2021 mpaka 6.4 mwaka 2022. Lakini pamoja na kuteteleka kwa uchumi duniani, sisi Tanzania tumeweza kujiimarisha kutekeleza mambo ya msingi kwa ajili ya jamii yetu kama kutengeneza mazingira ya shule, infrastructure za shule, zahanati, vituo vya afya, miradi ya maji, barabara, miradi ya umeme na treni ya mwendokasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali imeweza kutoa ruzuku katika maeneo ya makubwa ya mafuta na mbolea ili kuhimili mfumuko wa bei ambao tuliweza kufanikiwa kwani mwaka 2022 ilifikia wastani wa asilimia 4.3 kutoka kwenye asilimia 3.7 ya mfumuko wa bei kwa mwaka 2021. Kwa hiyo, hatua hizi zote zilizochukuliwa si kazi rahisi na watu wengine wanaweza kuwa hawayaoni haya au hawayafahamu, lakini wenzetu wa nje huko waliofanya tafiti kama hawa Numbeo Business Inside Africa imeripoti kuwa katika tafiti yao Tanzania kati ya nchi kumi Afrika ni nchi ya nane miongoni mwa nchi zenye gharama nafuu na ambayo imevutia wawekezaji kuja kuwekeza katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hii si kazi ndogo, ni kazi ambayo Rais Samia ameifanya. Tunaposema anaupiga mwingi, ameifungua Tanzania ndio tunazungumzia mambo haya. Kwa hiyo, ili tuweze kuendelea kuimarisha uchumi wetu na kukuza uchumi wetu hatuna budi kuendelea kuhakikisha kwamba gharama za maisha tunaendelea kuzidhibiti, ndio kazi inayofanywa na Serikali yetu mpaka tumefikia hapo tulipofika. Wote tunafahamu wawekezaji wowote katika nchi zetu hizi wanakuja kuona nchi ambayo ina gharama nafuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kutokana na taarifa mbalimbali pia za Business Insider inasema kwamba Tanzania is one of the first becoming the best investment destination in the world. Hii ndio ripoti ya wenzetu na hii ni kwa sababu ya hali inayofanywa na imejidhihirisha katika miradi iliyoandikishwa na TAC katika mwaka 2023 Februari, imeongezeka by hundred and twenty eight percent.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inaonesha significant potential growth ya uchumi wetu nchini. Kwa hiyo, TIC imeorodhesha miradi hii gharama yake ni million dollars 339 sawa na zaidi ya Shilingi Bilioni 780 na itaenda kuajiri watu 7,370. Kwa hiyo ni kazi kubwa sana hii ambayo inafanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirudi nyumbani Namtumbo. Kwanza tunaomba tuishukuru sana Serikali, katika kipindi hiki Serikali imeweza kutusaidia sisi zaidi ya shilingi 15,820,000,000 kutekeleza miradi mbalimbali. Katika afya tuliweza kupata shilingi 5,318,000,000 ambayo tumejenga majengo ya upasuaji katika hospitali ya Wilaya, wodi na tumejenga majengo ya Mama ngojea, katika kipindi hiki tumejenga mortuary na jengo la mama na mtoto zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni tano tulizozipokea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumejenga vituo vya afya katika Kata ya Magazini, Kata ya Ligela na miundombinu ya uboreshaji wa maji katika vituo vyetu vya afya. Vile vile tumeweza ukamilishaji wa zahanati na tumemaliza kuzijenga Ukiwayuyu, Misufini, Songambele, Naholo, Mhangazi, Luhangano na tunaendelea na zahanati zingine kama Namanguli, Nhamali, Ulamboni na Chengena katika kipindi hiki chote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi hiki tumepata vifaa tiba vya thamani ya shilingi 758,848,000. Vilevile tumeweza kupata katika elimu, Serikali imetuletea shilingi 7,564,000,000 katika kuendeleza ujenzi. tumejenga shule ya sekondari ya wasichana kati ya shule kumi zilizojengwa nchini Tanzania, moja iko Namtumbo tumejenga kwa shilingi bilioni nne na shule hiyo iko mwishoni kukamilika. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuja kuitembelea na kuweka jiwe la msingi katika shule ambayo tumeiita Dr. Samia Suluhu Hassan Secondary School.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejenga pia Shule ya Sekondari katika Kata ya Mzizima, lakini vilevile tumejenga madarasa 86 yenye thamani ya zaidi ya shilingi 1,720,000,000. Vile vile tumeweza kujenga maabara katika shule zetu za sekondari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye sekta ya maji; tumeweza kupata zaidi ya shilingi bilioni mbili na milioni mia tisa katika miradi mbalimbali ambayo tumeweza kukamilisha Mradi wa Maji Namtumbo Mjini, tumeweka line mpya na leo imepunguza adha waliyokuwa wanapata wananchi, walikuwa wanapata maji siku saba mara moja kwenye mgao, lakini leo angalau imepunguza adha hii. Kuna maji Litola-Kumbala tumeweza kufanikisha kupata maji lakini Luhimbalilo na Ikesi nayo kazi inaendelea. Vilevile maji Masugulu nayo shilingi milioni 578 kazi imekamilika na maji watu wanakunywa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika barabara; tulipata zaidi ya shilingi bilioni mbili na milioni mia tano, tumeweza kujenga daraja kubwa Mto Luwegu. Mto Luwegu unatokea Namtumbo, kwa hiyo tumejenga pale daraja kubwa ambalo sasa hivi linawasaidia wananchi kuvuka. Vile vile tumejenga barabara za vijijini, fedha hizi tulizipata za TARURA ila tunaweza kuiomba Serikali tuna changamoto, tunaomba kwenye barabara, tuna barabara yetu ya Mtwara Pachani kupita Mkongo – Lusewa – Magazini mpaka Tunduru, hii barabara ni ya kiusalama, lakini vile vile ina eneo ambalo wanakaa watu wengi sana. Kwa hiyo, tunaomba sana Serikali ifikirie kuitekeleza Ilani ya Uchaguzi, ipo katika ukurasa wa 73, ahadi ya Ilani wa Uchaguzi wa 2020 - 2025. Kwa hiyo, tunaomba sana Serikali ifanye ifanyavyo iweze kutekeleza ahadi yake ya kujenga kwa kiwango cha Lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru barabara ya kutoka Lumecha – Kitanda mpaka Malinyi iko katika hatua nzuri ambayo tuko katika hatua za manunuzi, tunaamini kabisa tutaweza kufanikiwa kufanya kazi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia changamoto tuliyonayo ni Kilimo. Kilimo tunashukuru sana mwaka 2022 tumepata mbolea za ruzuku, lakini mbolea hizi hazikufika katika maeneo ya vijiji vyetu. Tunaomba kama alivyosema leo Naibu Waziri asubuhi kwenye swali aliloliuliza Mama Anne Kilango, tunaomba utaratibu wa mwaka huu uende kama ulivyopangwa. Mbolea ziwafikie wakulima mapema. Tunashauri taratibu za manunuzi ya mbolea zianze mwezi huu Aprili ili mpaka mwezi wa Julai au Agosti mbolea ziwe zimeshafika nchini, ziwe zimesambazwa ili kama kuna changamoto tuweze kuzitatua changamoto hizo kabla ya wakati wa msimu kuanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, naomba sana pia Serikali yetu isaidie, sisi tuna changamoto ya Kituo cha Mabasi katika Wilaya ya Namtumbo, tunaomba sana itufikirie. Hatuna kituo chenye hadhi ya Wilaya, vile vile hatuna soko. Sisi ni wakulima tuna mazao mengi lakini hatuna soko la mazao Namtumbo. Tunaomba Serikali itufikirie katika eneo hili. Hii ni changamoto mojawapo kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tuna changamoto ya ukarabati wa Vituo vya Afya kongwe vitatu ambavyo vilijengwa miaka ya 1970; Mkongo, Lusewa na Mputa. Vituo hivi nasema ni kama zahanati, kwa hiyo vilijengwa miaka ile na vina upungufu wa majengo na vimechoka sana. Kwa hiyo, tunaiomba sana Serikali iweze kutusaidia katika eneo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwingiliano kati ya wakulima na wafugaji ni changamoto kubwa sana kwenye eneo letu. Sisi ni wakulima na nchi hii inategemea sana kilimo. Kwa hiyo tunaomba sana Serikali izingatie hili ije, haijawahi kuja toka nimeanza kuzungumza changamoto hizi hadi watu wamekufa hajawahi kuja Waziri wa Mifugo. Tunaomba Waziri wa Mifugo aje aone changamoto tuliyokuwa nayo. Mifugo inatusumbua sana sisi wakulima na sisi katika maeneo yetu nchini kuna maeneo sasa hivi yana uhaba wa mvua lakini kwetu sisi tuna mvua nzuri na sisi ndio ghala la chakula kule. Kwa hiyo, kukiwa na mwingiliano wa wakulima na wafugaji tutashindwa kulima na tutashindwa kuzalisha nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naomba kuishauri Serikali, ili kuendeleza uchumi wa nchi yetu na kuulinda lazima tu-focus zaidi kwenye export oriented industrialization ili tuweze ku-concetrate kuzalisha mazao tutakayokuwa tunauza nje ya nchi. Tukiwa na mazao na viwanda vinavyozalisha mazao ya kuuza nje ya nchi itatusaidia kuuza nje kwa sana na kutoa foreign exchange. Kutoa mifano ya nchi wenzetu walioendelea ambao tuliuwa nao katika miaka ya 1960 nchi za Asia pale Tiger ambao wao miaka ile walianza ku-concentrate kwenye hivi viwanda vya kuzalisha vitu vya kuuza nje, leo wanauza nje sana na uchumi wao wa Tiger kule umekuwa mkubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu huo ulikuwa ni huo. Naomba sana kukushukuru ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. (Makofi)