Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Amiri Jeshi Mkuu wa Nchi yetu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekerekwa na ubadhilifu, mimi ni nani Ester Bulaya niuchekee? Kama Waziri Mkuu wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesikia kwenye ziara zake mbalimbali akikemea ubadhilifu mimi Ester Bulaya mwakilishi wa wananchi ni nani niuchekee na hasa jicho likiwa limefanya kazi yake? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumsaidia hivyo hivyo Rais kwa kuisaidia Serikali iweze kuchukua hatua lazima tuonyeshe kwenye mapungufu hatua zichukuliwe nchi yetu isonge, maendeleo ya Taifa yaonekane kwa wananchi wake.
Mheshimwa Mwenyekiti, kwa utangulizi naanza. Kikokotoo Wafanyakazi bado wanalia, tusitengeneze mgomo baridi, hawa ndiyo wanaoenda kutekeleza miradi ya maendeleo, najua mnasikia, najua mmeona na najua mkiamua kulifanyia jambo mnaweza, bado asilimia 33 si haki yao, maisha magumu Wafanyakazi wanalia wanafanya kazi kwa kinyongo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukurasa wa 14 wa Waziri Mkuu, hotuba yake ameisoma vizuri tu hapa, kuzungumzia miradi ya kimkakati na anazungumzia mradi wa Mkulazi ambao amesema upo asilimia 75, tunataka majibu ya kina hapa kuna fedha za Mifuko zimewekezwa. Je tathmini ya kina ilifanyika? Maana ripoti mbalimbali za CAG zimeonesha hapa pametengeneza hasara ya bilioni 11 sawa na asilimia 21 ya mtaji uliowekezwa, Mkulazi hapa. Moja ya sababu inasemekana kulikuwa kuna ucheleweshaji wa mashine. Sasa ukienda ya mwaka huu inasema hiyo mashine aliyepewa tenda ya kununua mtambo wa kutengenezea Kiwanda cha Sukari ni Wakala wa Barabara TANROADS, wapi na wapi! Kwa nini haikuwa TEMESA, kwanini haikuwa wakala wa kuagiza vifaa Serikalini, TANROADS, barabara wa sukari wapi na wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kuna fedha za Kimarekani takribani milioni 50.8 na inasemekana mbali ya kwamba na huu mkataba ambao Mkulazi hawajashiriki hata kuweka Saini, kila kitu walifanya TANROADS. Kuna nyongeza ya bilioni 11 na hatujui kwamba Mwanasheria Mkuu alithibitisha kwa mujibu wa Kanuni ya 59(1) cha manunuzi. Tunataka majibu ya kina, haya tunayasema kwa sababu tunataka hatua zichukuliwe, watu wasiichukulie Serikali poa, watu watimize wajibu wao, hizi ni fedha za wastaafu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni Mkulazi bado kiwanda cha Ngozi cha Kilimanjaro hasara Bilioni Nne, fedha za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii shilingi bilioni nne. Katika malengo yao hicho kiwanda kipya cha Kilimanjaro kilikuwa kimepanga kuzalisha jozi za viatu 1,200,000 wakazalisha 11,354, kilikuwa kimepanga kuzalisha jozi za sori za viatu 900,000 kikazalisha sifuri. Kilikuwa kimepanga kuzalisha bidhaa za ngozi 48,000 kikazalisha 224, kilikuwa kimepanga kuzalisha ajira 300 kikazalisha 79. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, malengo hayajafikiwa usimamizi mbovu kwenye pesa za wastaafu zinazoenda kuwekezwa kwenye viwanda. Wakati haya yanafanyika bado mifuko iko hohehahe PSSF tena ripoti mpya ambayo tutaenda kushughulika nayo huko mwezi wa Agosti, PSSF imesema Mfuko ukwasi upo asilimia 22 kinyume na sheria cha asilimia 40. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana nimesema na leo narudia, wakati hizi pesa zinaendelea Trilioni 1.5 pesa za muda mrefu hamjalipa kwenye Mifuko tuliahidiwa na Waziri wa Fedha akalipa kwa Hati Fungani nyingine hamjatoa, wakati haya wanaendelea Mfuko wa PSSF umelipa bilioni 767 pesa za Wastaafu, kiinua mgongo chao zaidi ya mapato waliyonayo kuna mwaka walienda kukopa kwenye maeneo mengine, kiasi walicholipa ni kingi kulingana na mapato ya michango. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati haya yanaendelea kuna mashirika manne hayajapeleka michango takribani bilioni 129 kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, wakati haya yanaendelea kuna Mamlaka ya Serikali za Mitaa 133 hazijapeleka takribani bilioni 119 maslahi ya mishahara na posho za wafanyakazi hazijalipwa. Wakati haya yanaendelea kuna mashirika nane hayajalipa malimbikizo ya mishahara ya watumishi na madeni mbalimbali takribani bilioni 5.8, bilioni 2.2 ni malimbikizo ya mishahara. Wakati haya yanaendelea kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuna Mamlaka 76 hazilijalipa milioni 309 za mizigo za wastaafu 223. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayasema haya kwa sababu tunataka nchi yetu iende, haya mambo Bunge tumekuwa tukiyaongea mara kwa mara na Serikali haifuati maagizo ya Bunge. Niwaambie tu kwenye maagizo ya Bunge 892 ya Kamati ya LAAC yaliyofanyiwa kazi ni asilimia 26 tu, yamefanyiwa kazi maagizo 228. Kwa nini Hoja za Ukaguzi zisijirudierudie? Hapo kuna maagizo 159 ya Bunge lako Tukufu hayajafanyiwa kazi takribani miaka 10. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge lazima tutimize wajibu wetu, tuibane Serikali itimize wajibu wake, tumsaidie Mheshimiwa Rais ameonesha makasiriko yake ya kukerwa, lazima kama Wabunge, kama Taifa tusimame imara, hatumtafuti mtu hapa, tunataka tuwatendee haki Watanzania fedha zao ziende kwenye miradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haya Maagizo ya Bunge hayafanyiwi kazi, kwa nini Wakurugezi kule wasifanye mambo wanayojitakia kwenye Halmashauri? Kwa nini pesa za vikundi zisipigwe takribani shilingi bilioni 88? Kwa nini asilimia 40 za kisheria zinazopaswa zikusanywe na Halmashauri hazikusanywi? Kwa sababu Bunge tunatoa maagizo, hamsikilizi. Tunaomba haya maagizo yakafanyiwe kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua Mheshimiwa Waziri Mkuu ni mnyenyekevu, tunaomba watumishi watimize wajibu wao. Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, madeni yalipwe. Watumishi pesa zao kwa mujibu ya sheria, michango ipelekwe. Kwenye uwekezaji kuwe na tija. Ifanyike tathmini ya kina ili hizi pesa za hawa watumishi wa umma ambao ni wastaafu watarajiwa, huku wanapigana na stress za kikokotoo, huku pesa zao hawajui huko zilikoenda zitarudi kiasi gani? Please! Naomba sana tuwatendee haki Watanzania, tuwatendee haki watumishi wa Taifa hili. Haya tunayopanga, wao ndio wanaenda kutekeleza, hawataenda kutekeleza wakiwa na stress, hawajui hatima yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)