Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Shamsia Aziz Mtamba

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Mtwara Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ili nami niweze kuchangia hotuba hii ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya nzuri na leo hii nikaweza kusimama katika Bunge hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nitaanza kwa kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuhakikisha Watanzania wa mijini na vijijini wanapata maendeleo. Kwa hakika wanawake tunaweza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze kwa dhati Waziri Mkuu kwa kuguswa katika Jimbo la Mtwara Vijijini, tulipopata maafa makubwa kweli ya mafuriko. Tunamshukuru sana kwa kuchukua hatua ya haraka kuwafikia wahanga wa mafuriko na kutupatia misaada ya kibinadamu. Kwa kweli Mheshimiwa Waziri Mkuu wananchi wa Jimbo langu hasa wa Kata ya Kivava, Kata Mahurunga, Kijiji cha Kivava wanakushukuru sana. Misaada imewafikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza Mkuu wangu wa Mkoa wa Mtwara, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, na vyombo vya ulinzi na usalama vyote, kwa kweli wamefanya kazi kubwa ya kuhakikisha wahanga wa mafuriko wapo katika sehemu nzuri na wanapata huduma nzuri. Ninawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu nitazungumzia sehemu tatu. Kwanza, nitaanza kuzungumzia kuhusu Wizara ya Uchukuzi. Tokea nimekuwa Mbunge katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nimekuwa nikizungumzia sana suala la barabara; barabara ya ulinzi na pia barabara ya uchumi inayotoka Mtwara Mjini kuelekea Msimbati ambako kuna mitambo na visima vya gesi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna barabara yetu ya ulinzi, ina umuhimu mkubwa sana. Barabara hii ni muhimu Serikali iiangalie kwa macho mawili kwa sababu itaweza kulinda usalama wa watu wetu na kutoa urahisi kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kufika katika maeneo kwa uharaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tumekwenda kule kwa wahanga wa mafuriko, barabara hii ni mbovu na haipitiki kabisa. Sehemu ambayo tulitakiwa tutumie muda wa saa moja, tumetumia karibu masaa manne kutokana na ubovu wa barabara. Ninyi mnafahamu hali halisi iliyopo katika maeneo yetu kule mipakani, kwa hiyo, barabara hii ina umuhimu mkubwa sana wa kututengenezea kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye barabara ya uchumi ambayo inatoka Mtwara Mjini kuelekea Msimbati, ambako kuna mitambo na visima vya gesi kule. Ninaongea kwa masikitiko makubwa sana, ni aibu, sehemu ambayo tumewekeza uwekezaji mkubwa, barabara ni mbovu; sehemu ambayo kuna mitambo kule ya gesi, kuna visima vya gesi, barabara ni mbovu. Ninaiomba sana Serikali mwiangalie barabara hii kwa macho mawili na kwa umuhimu wake, mtujengee kwa kiwango cha lami kwa uharaka kutokana na umuhimu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kuzungumzia kwenye suala la maji. Katika majimbo sugu yenye changamoto ya maji, ni Jimbo la Mtwara Vijijini. Bajeti iliyopita nilizungumza hapa katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa vizuri kwenye huduma hii muhimu ya maji safi na salama, ni Jimbo langu la Mtwara Vijiji. Kuna maeneo mengi yana changamoto ya maji. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali, na Mheshimiwa Aweso nimekufuata mara nyingi, nakuomba kaka yangu utuone kwa macho mawili katika Jimbo langu Mtwara Vijijini, bado tuna changamoto kubwa ya maji katika maeneo mengi. Maeneo mengine toka tumepata uhuru wa nchi hii, hawajawahi kabisa kufuruhia huduma hii muhimu ya maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna mradi wa maji wa Mto Ruvuma. Kuna bomba limepita katika maeneo yale, na kuna wananchi walishafanyiwa uthamini tokea mwaka 2015, takribani miaka nane, mpaka leo hii wananchi wale hawajapewa fidia karibu vijiji 25; Kijiji cha Mayembe, Mitambo, Madimba, Kitaya, Kihamba, Kivava, Mahurunga, Kitunguli, Kihimika, Litembe mpaka Mtwara Vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo haya wananchi wanashindwa kuendeleza maeneo yao kutokana na kutolipwa fidia. Kwa hiyo, naiomba Serikali iangalie maeneo haya, wananchi wanashindwa kufanya maendeleo kutokana na kulipwa fidia yao. Kama wameshindwa kuendeleza, Serikali naomba mtueleze ili maeneo haya wananchi waweze kufanya shughuli zao za maendeleo, waweze kufanya shughuli zao za kilimo, waweze kufanya shughuli zao za ujenzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia suala la afya. Tunaishukuru sana Serikali kwa kutujengea majengo mengi katika vijiji vyetu; zahanati na vituo vya afya, lakini kuna uhaba mkubwa wa watumishi katika maeneo yetu, hasa katika maeneo ya vijijini. Tunaiomba Serikali watuletee watumishi wa kutosha. Utakuta zahanati nyingi muuguzi yupo mmoja; mgawa dawa ni huyo huyo, mchoma sindano ni huyo huyo, mzalishaji ni huyo huyo. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali iangalie maeneo mengi ya vijijini, kuna uhaba mkubwa sana wa watumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa nitazungumzia kuhusu suala la kilimo. Sisi wananchi wa Mkoa wa Mtwara, kilimo chetu kikubwa ni zao la korosho, uchumi wetu mkubwa ni zao la korosho. Tunaomba msimu wa mwaka huu usiyumbishwe yumbishwe. Tunaiomba sana Serikali watuletee viuatilifu kwa wakati. Pia nilizungumza kwenye bajeti ya mwaka jana 2022, tunaiomba Serikali ifanye takwimu kwa kila mkulima wa korosho kwa ajili ya ugawaji wa viuatilifu ili kuondoa mikanganyiko inayojitokeza mara kwa mara katika ugawaji wa viuatilifu hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumza hayo, nakushukuru sana. (Makofi)