Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tabora Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nakushukuru sana kuniruhusu nichangie hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ambayo imetandawaa kwenye bajeti yote, lakini pia imekuwa mtambuka kwa maoteo ya bajeti yote ya Serikali kwa mwaka huu unaokuja.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo niko hapa kuipongeza Serikali. Pamoja na upungufu ambao umetajwa na CAG, nimeweka kiporo kwa sababu kwa kweli siyo muda wa kujadili hotuba ile, hotuba ile itakuja baadaye baada ya kuangaliwa vizuri kwenye Kamati yetu ya PAC. Najua taarifa ile imeonesha uchafu, lakini kuifua nguo inaruhusiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kuipongeza Serikali kwa mambo makubwa; miradi mikubwa ya kiuchumi ambayo imefanya hata ikasababisha uchumi wa nchi hii kubaki kama ulivyo na pia bila kukua kwa bei za vitu. Japo bei zimepanda, lakini kiujumla, nitamke wazi wazi kwamba, sisi hapa tumefanya huu mfumuko wa bei ubakie chini kuliko nchi zote za Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi mikubwa ambayo imejengwa na Serikali ambayo inajengwa sasa hatuioni kwamba muhimu, lakini ni muhimu sana. Nikiitaja kwa mfano Bwawa la Umeme la Rufiji, Reli ya SGR, ujenzi wa madaraja, ujenzi wa meli kadhaa maziwani, ujenzi wa barabara za kisasa, ununuzi wa ndege, miradi ya afya, miradi ya maji, miradi ya elimu, na kadhalika, mambo haya yakikamilika, nchi hii itapaa na watu wengi watakuja kushangaa kwa nini tulifanya hali ngumu hii na tukamwona Mheshimiwa Mama Samia anahangaika, lakini badaye watu watafaidi na watafaidika sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika jimbo langu tumefanyiwa miradi mingi sana. Alama ambazo ziko kwenye jimbo langu ni mfano wa kazi nzuri aliyoifanya Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan. Kwanza elimu; bado wanafunzi wanasoma bure, vile vile tumejenga madarasa, nyumba za walimu na kituo kikubwa kabisa cha VETA. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu maji, jimboni kwangu kuna mwamba chini ukichimba visima maji yanakauka. Leo tumetandaza maji ya Ziwa Viktoria, tunafungua maji kwenye mashamba na chini ya miti. Leo kuna vijiji 64 vina maji ya bomba kutoka Ziwa Viktoria. Hili siyo jambo dogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu umeme, tulipoanza hapakuwa hata na Kijiji kimoja chanye umeme. Leo kuna vijiji 51 vina umeme katika jimbo langu. Hili siyo jambo rahisi. Pia barabara za ndani, tumekuwa na barabara kila mahali ambako kulikuwa hakuna barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi ya afya. Sisi jimbo lile ni jipya na Wilaya yetu ni mpya, ilikuwa haina hospitali ya Wilaya. Tumejengewa hospitali ya Wilaya nzuri kabisa, lakini vituo vya afya katika jimbo langu, vinne vinajengwa, vilevile tumejenga zahanati katika jimbo langu na kule kulikokuwa hakuna huduma ya afya, sasa inapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utawala bora. Serikali ya Awamu ya Sita haikutusahau. Halmashauri ya Uyui haikuwa na majengo kabisa. Naipongeza sana Serikali, sasa tuna majengo mapya ya Halmashauri. Hili limetufanya sisi wana-Uyui tujisikie kwamba ni sehemu ya utawala bora. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina mambo mawili ambayo ninadhani ni muhimu sana niyachangie leo. Katika Jimbo langu na Wilaya yangu ya Uyui tunaishi na ahadi za Marais watatu kuhusu kujenga Kituo cha Afya. Huu ni mwaka karibu wa tatu, wa nne, au wa tano umepita, lakini Marais wote; Marehemu Benjamin Mkapa, Marehemu John Pombe Magufuli na Rais wa sasa waliahidi kujenga kituo. Ilitokea historia ya kituo hiki kujengwa na Marehemu Benjamin Mkapa. Alikwenda kufungua kituo kidogo cha afya, lakini alipokwenda akasema kituo hiki ni kidogo, mimi nina miaka 97, naahidi kwamba, nitajenga hospitali kubwa hapa. Akamaliza muda wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilipoingia madarakani tumeenda kuanzisha mradi wa kituo kile, alipokuja marehemu Magufuli, Rais wangu aliyetangulia, nikamwambia kuna ahadi ya Mheshimiwa Benjamin Mkapa, akasema anzeni, nami nakuja kuchangia, tutamaliza, na nitakuja kufungua mimi. Bahati mbaya amefariki.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia alikuja Tabora Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wangu mpendwa, mama mwenye maono makubwa, nikasimama tena nikamwambia, kuna ahadi ya Marais wawili. Akasema hili jambo litafanyika mara moja. Wakati huo Mheshimiwa Silinde alikuwa Naibu Waziri, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Akamwambia hili tafuteni hela mara moja, hili limeisha. Sasa kumekuwa na kuhamishwa Mawaziri huku na huku, suala lile la hospitali ile ya ahadi ya viongozi watatu, limekuwa mwiba kwa wananchi, hawaelewi kwa nini hospitali ile haijengwi,
tumejenga sasa mpaka imefikia wodi ya mama na watoto, lakini bado ahadi hiyo haijatekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia liko suala la pili ambalo linanisumbua mimi. Tumekuwa tunashauri humu ndani kwamba ni muhimu sana kupanua wigo wa kodi. Mimi nimetoka katika sekta ya ulinzi binafsi na kule kuna hali nzuri sana ya kukusanya kodi, lakini kampuni zile karibu 1,200 sasa hakuna GN wala sheria ya kuiziongoza. Kwa hiyo, zinajiendea tu. Tumejaribu kuzikusanya huku na huku sisi wenyewe tumekusanyana na kuanzisha sekta ya ulinzi binafsi. Chama chetu kinaitwa Tanzania Security Association lakini ni vigumu sana kusema wanalipaje kodi?
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa tunagombania kodi. Nilileta Muswada Binafsi hapa mwaka 2017, na Muswada ule ulinigharimu sana kwenda nchi za nje kutafuta input za Muswada ule. Nilipouleta hapa, Muswada ulipelekwa Bungeni kwa Katibu wa Bunge, lakini Mheshimiwa Spika na wataalamu wote wa Bunge wakapitia Muswada ule wakasema unafaa, Serikali ikauchukua ikasema itauleta hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutumia Kanuni ya 94 ambayo inaruhusu Mbunge kuleta Muswada Binafsi Bungeni, na kanuni hizi ndiyo zinatulinda sisi hapa tuweze kufanya kazi kama Wabunge, mpaka leo Serikali haijaleta Muswada huu. Licha ya kuahidi na kuuliza maswali ya kibunge, lakini Muswada huu utasaidia kodi, utasaidia mapato ya Serikali, utaanzisha mamlaka kama vile EWURA, mamlaka kama vile ya kusimamia sekta hii ya ulinzi binafsi ifanye vizuri. Tangu mwaka 1980 zikiwa kampuni mbili, zimekua mpaka kuwa kampuni 1,200, lakini hakuna sheria, hakuna kanuni, wala miongozo ya kampuni hizi. Serikali inapoteza.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulisema juzi juzi hapa, tozo, tozo! Leo tozo tunafaidika, tunajenga barabara, tunajenga shule na kadhalika. Tozo au kodi itakayotokana na uendeshaji bora wa kampuni za ulinzi zitafaidisha wananchi na zitafaidisha Serikali. Kwa hiyo, nilikuwa naomba, ili kuweza kupanua wigo wa kodi, basi Serikali ilete ule Muswada wa Sheria ya Sekta ya Ulinzi Binafsi hapa Bungeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu waajiri; kumekuwa na matatizo sana huko kwa waajiri, lakini mjue waajiri tumefanya kazi kubwa sana ya kuzuia migomo hapa nchini, kwa kuongea vizuri na wenzetu wa TUCTA na wafanyakazi wenzetu. Sisi tunalalamika; nina maana waajiri wanalalamika, sheria ile ya Na. 6 ya Mwaka 2004 imepitwa na wakati, inatakiwa ifanyiwe mabadiliko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna baraza linasaidia kutunga sheria za kaziā¦
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Maige, kengele ya pili.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)