Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalambo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na mimi kunipa nafasi jioni ya leo niwe miongozni mwa wachangiaji wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niungane na wenzangu ambao kwa dhati kabisa wamepongeza kazi iliyotukuka inayofanywa na Mheshimiwa Rais katika kuhakikisha kwamba Taifa hili linasonga mbele. Sisi wananchi wa Kalambo hatuna la kumlipa zaidi ya kumwombea kwa Mwenyezi Mungu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika maeneo machache ambayo nitataja, mimi leo nawiwa kutaja kwenye upande wa barabara. Kwa sisi wananchi wa Kalambo tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais tumeweza kupata jumla ya shilingi bilioni 37 kwa ajili ya kujenga barabara kutoka Matai kwenda Kasesha Border kilometa 25 na kilometa zingine 25 ziko kwenye mchakato wa manunuzi. Ni imani yetu kubwa kwamba akipata fursa ya kuja Mkoani Rukwa atapita Kalambo na kutuwekea jiwe la Msingi kama sio kufungua barabara hii. Barabara hii ni kiunganisho kikubwa sana kutoka nchi ya Zambia lakini pia itapunguza umbali mrefu ambao wasafiri wanalazimika kusafiri kutoka maeneo ya Mwanza, Uganda, Kenya kuzunguka kwenda Tunduma kwa kuwa sasa watapunguza zaidi ya kilometa 600, hivyo tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama hiyo haitoshi kuna daraja letu ambalo kwa muda mrefu tulilipigia kelele. Safari hii tumeweza kupata jumla ya Shilingi isiyopungua bilioni tano, sasa litajengwa. Daraja hili ni kiungo kikubwa sana kwa barabara ya zamani inayojulikana kama Barabara ya Mjerumani ambayo inaenda Bismark Kasanga.
Mheshimiwa Spika, baada ya kupongeza hayo naomba pia nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu na niunge mkono hoja ambayo imewasilishwa. Pia niweze kumkumbusha Mheshimiwa Waziri Mkuu, alipokuwa amekuja Kalambo mwaka 2020, akiwa Kasanga pale aliwaahidi wananchi wa Kasanga na Tarafa ya Kasanga ujenzi wa kituo cha afya. Wamenituma nije nimkumbushe kwa sababu kwa muungwana ahadi huwa ni deni. Naamini katika majumuisho atalisema na hilo ili tuweze kujua lini ujenzi unaanza maana eneo la kujenga tayari tumeshaliandaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kueleza maneno hayo naomba nichangie katika maeneo yafuatayo. Muda ukiruhusu nitachangia kuhusiana na mfuko wa dharula kwa maana ya contingency fund.
Mheshimiwa Spika, nitachangia kuhusiana na mgawanyo wa rasilimali watu kwa watumishi wa umma, utaratibu wa shughuli za Serikali na kodi ya majengo kwa maana ya property tax na usimamizi wa mifumo ndani ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na mfuko wa dharula (Contingency Fund). Uanzishwaji wa mfuko wa dharula kwa Taifa ni takwa la kikatiba ibara ya 140(i)a. Na kama hiyo haitoshi inaenda kukaziwa na Sheria ya bajeti ya mwaka 2015 kifungu cha 22.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Taifa, sheria ya bajeti inataka asilimia moja ya bajeti kila mwaka itengwe kwa ajili ya kupelekwa kwenye mfuko wa dharura.
Mheshimiwa Naibu Spika, utakubaliana, kama Taifa tumekuwa tukiona nchi majirani, hivi juzi ilitokea nchi ya Malawi, wakapatwa na ile dhoruba, sisi kama Taifa tunawajibu wa kuhakikisha kwamba mfuko huu unaanzishwa; na bahati nzuri unatakiwa kusimamiwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Tumekuwa tukishuhudia yakitokea maafa, fungu linalotumika ni Fungu 21 hazina ambapo kwa mujibu wa Sheria ambayo ipo kwa mujibu wa Katiba na Sheria ya Bajeti sio sahihi kuendelea kutumia Fungu 21. Ni wakati mwafaka kama Taifa tuhakikishe kwamba mfuko wa dharura unakuwepo na unafanya kazi iliyokusudiwa kwa mujibu wa Katiba. Katika hali ya kawaida hakuna familia yoyote ambayo inaweza ikajidai pale ambapo hawana hata akiba likitokea lolote la kutokea unaanza kukimbilia kwenda kwa majirani. Ni wakati mwafaka tutekeleze takwa la katiba na takwa la kisheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini eneo lingine ambalo naomba nichangie ni ukusanyaji wa kodi ya majengo (property tax).
Mheshimiwa Naibu Spika, na wewe ni shuhuda ukirejea siku za nyuma halmashauri na hasa hata halmshauri yako ya Ilala ilikuwa inaonekana inakusanya vizuri zaidi kulikoni utaratibu uliokuja kuanzishwa ambao mpaka leo tunashindwa kupata uhakika hayo makusanyo ili tulinganishe na vile ambavyo halmashauri zetu zilikuwa zikikusanya. Umekuja utaratibu wa kutumia Luku lakini nayo imekuwa ni changamoto. Ni wakati mwafaka Serikali, na hasa baada ya kuendesha zoezi zuri la sensa tuna uhakika kwamba kila mwenye mali kama ni nyumba anajulikana kwa mujibu wa sensa iliyofanyika. Sasa, ni wakati mwafaka kwa Serikali kuhakikisha kwamba sensa na takwimu zake zitusaidie ili kuwezesha kukusanya mapato yake halali kuhusiana na property tax.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili ni eneo ambalo lina fedha nyingi sana. Tukilisimamia hakika maendeleo ambayo Mheshimiwa Rais anapigana nayo kila siku tutamrahisishia kazi kwa sababu eneo hili ni eneo oevu. Linachukua muda mrefu, ukiuliza TANESCO hawana interest na makusanyo hayo kwa sababu si fedha ambayo inaingia kwao; lakini hata halmashauri nazo wanajiweka nyuma kwa sababu hawaoni manufaa yake; halikadhalika na Serikali kuu. Mfumo ambao ni rasmi wa kuhakikisha kwamba property tax inakusanywa na ikagawanywa kwa ajili ya maendeleo haifanyiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni imani yangu kubwa kwamba wakati Mheshimiwa Waziri Mkuu anakuja kuhitimisha atatuambia wamefikia wapi ili tuwe na mfumo mahsusi wa kuhakikisha kwamba kodi hii inaenda kukusanywa ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala zima la mgawanyo wa rasilimali watu kwa watumishi wa umma; amelisema vizuri sana Profesa Kitila. Hata hivyo, ukitafuta idadi ya wafanyakazi wa Serikali au wa umma hutashangaa kukuta baadhi ya halmashauri wapo wengi lakini ukienda maeneo mengine hawapo. Sasa Dar Es Salaam Kinondoni unamweka Afisa Kilimo wa kazi gani badala ya kumpeleka Kalambo ambapo wakulima wanamuitaji? Ni wakati mwafaka wa Serikali kufanya human resource audit ili kujua kabla ya kuanza kuajili tunao watumishi wangapi ndani ya Serikali na tunawatumiaje ili effect yake iweze kuwepo.
Mheshimiwa Naibu Spika, na ni ukweli usiopingika, unakuta maeneo ambayo wapo watumishi wengi wazuri hata maandiko yao wakiandika wakati wa kupitisha project wanafanikiwa; lakini maeneo mengine wanakuwepo wachache hata namna ya kuweza kuandika hata project hawezi kufanikiwa. Ni wakati mwafaka Serikali mtujie na utaratibu wa kuhakikisha kwamba utakuwepo mgawanyo sawia kwa kadri ya mahitaji ya maeneo na halmashauri zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia lipo tatizo kati ya taasisi za Serikali, pale ambapo taasisi moja inakwenda kutekeleza mradi lakini inakwamishwa na taasisi nyingine kwa sababu taasisi haziongei lugha moja.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA:Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Taarifa.
T A A R I F A
NAIBU WAZIRI,OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA:Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa taarifa Mheshimwa anayechangia kwamba ndani ya Serikali sasa tunao mfumo ambao unaweza kukupa taarifa za watumishi wa Serikali katika kada zote katika mikoa yote na kwa idadi yao na mahali walipo. Kwa hiyo anapozungumza kwamba Serikali haina taarifa hiyo sio jambo sahihi na ningeomba atoe maneno yake hayo katika taarifa yake.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kandege; hiyo ilikuwa ni taarifa au? ulikuwa umeomba taarifa wewe.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mimi naamini alikuwa anachangia na kama hilo ndio ukweli maana yake hatutarajii hawa ambao naambiwa wako Dar es Salaam wanafanya kazi ambayo haihusiani wangeweza kuwa hapo. Tulitarajia kama ndivyo hivyo basi wangepelekwa maeneo ambayo wanatakiwa kwenda kufanya kazi ili productivity yake iweze kuonekana, hiki ndicho tunachokisema. Kwa hiyo kama wanataarifa ambazo hawazifanyii kazi basi hazitusaidii. Ni vizuri ifike pahali ambapo taarifa hizo walizonazo wazifanyie kazi ili haya mapungufu ambayo tunayasema tusiyaseme tena.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uratibu wa shughuli za Serikali. Nilikuwa nimeshaanza kuelezea kwamba taasisi za Serikali haziongei lugha moja. Nitatolea mfano; pale ambapo REA wanataka kupeleka umeme eneo “X” lakini wanakwamishwa kupitisha umeme kwa sababu kuna msitu ambao TFS wanasema hawawezi kupitisha. Tafsiri yake ni nini mradi haufiki kwa wanachi ilhali wananchi wanataka maendeleo yaonekane.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama hiyo haitoshi unaweza ukachukulia mfano mwingine, TARURA wanajenga barabara, wakimaliza kujenga watu wa maji wanakuja kuchimba barabara ambayo imejengwa na TARURA as if hawakujua mradi huu unafanyika lini waka coordinate ili kama ni maji yakatangulia barabara ikafuata, haya ndiyo tunayosema. Kwa hiyo ni vizuri taasisi za Serikali zisomane ziseme lugha moja ili wananchi watuelewe kwamba hiki kinafanywa na Serikali, isije ikaonekana kwamba ndani ya Serikali taasisi zenyewe zinakuwa zinakinzana…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante kengele ya pili.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.