Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika hoja iliyopo mbele yetu kuhusu hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu aliyoiwasilisha hapa Bungeni. Nianze kwa maneno ya utangulizi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika kwamba nchi yetu imejaliwa au imebarikiwa rasilimali nyingi na za kutosha na tuna utajiri wa kutosha sana. Imekuwa tu ni bahati mbaya rasilimali na utajiri tulionao unatumika vibaya na unatumika kwa wachache na walio wengi hawanufaiki na rasilimali. Ni vema tukatambua na tukakumbushana kwamba hii Nchi ni ya Watanzania wote, hii nchi sio ya watu wachache. Vile vile ukitaka kujua jinsi gani nchi hii inaliwa, ripoti ya CAG imeonesha ubadhirifu mkubwa, matumizi makubwa na mabovu ya rasilimali fedha za Watanzania na ufisadi, upigaji wa dili na kila kitu umeoneshwa katika ripoti hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tukitaka kumsaidia Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ni lazima kwa wale wote ambao wamehusika kwa namna moja ama nyingine tuone neno uwajibikaji kwa vitendo. Bahati mbaya sana neno uwajibikaji halijawahi kutokea ila tumezoea mpaka tuone tumetenguliwa, tumepangiwa kazi nyingine, tumeondolewa lakini haijawahi kama ni mtumishi kama ni kiongozi akawajibika. Kama tunampenda Mama Samia waliohusika kwa namna moja ama nyingine wawajibike katika nafasi zao. Vile vile tunataka rasilimali za Watanzania, fedha za Watanzania ziwafaidishe Watanzania wote kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, unaweza ukashangaa na kujiuliza…
MHE. CATHELINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.
T A A R I F A
MHE. CATHELINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tuzingatie kanuni, muda wa kujadili taarifa ya CAG bado haujafika.
NAIBU SPIKA: Huo ndio ukweli lakini, kwa sababu CAG ame-cite mapungufu aliyoyaona yeye, yanakuja Bungeni, sasa Bunge ndilo lenye kuamua baada ya kuhoji pande zote. Kila Mtu ana haki ya kusikilizwa, sasa kama mnafurahi tu kwenda kuwachanganya wananchi, hii sio sahihi. (Makofi)
Endelea na mchango wako.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Sasa bahati mbaya sana pia badala ya kuisaidia nchi hii tukiwa tunajificha kwenye taratibu na nini nadhani sio sahihi. Ndio maana kama tungekuwa tunataka kweli kumsaidia Rais hata haya mambo tungeyajadili kwa dharura. Ni kiasi kikubwa cha fedha kimeonesha ubadhirifu mkubwa. Anyway, utaratibu upo lakini mwisho wa siku ni lazima tutafakari na kufanya maamuzi kwa maslahi mapana ya nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nifanye reference hapa kwa sababu kufanya reference haikatazwi na ikishaletwa hapa, maana yake it is a public document na ipo kwenye mitandao na iko kila mahali. Saa unaweza ukajiuliza, tunatumia fedha nyingi kuhifadhi vyura Marekani badala ya kumhudumia Mama wa Kitanzania ambaye anaenda kujifungua leo. Inasikitisha yaani nini kipaumbele chetu cha kwanza kwa Mtanzania? Kwa hiyo ni mambo kama haya na mengine mengi sasa wakati ukifika tutajadili kwa undani zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, huo ulikuwa ni utangulizi, sasa nijikite kuchangia kwenye Sekta ya Ardhi. Ardhi ni mtaji, ardhi ni rasilimali muhimu sana na tuna bahati kama nchi tuna ardhi ya kutosha na nzuri ambayo inafaa kwa matumizi mazuri. Ardhi yetu ni lazima ipangwe, ipimwe na kumilikishwa na lazima tutambue kwamba ardhi haiongezeki lakini mahitaji ya ardhi yanaongezeka na watu ambao wanahitaji ardhi wanaongezeka. Sasa ni lazima Serikali iweke mipango mizuri ya kuhakikisha masuala ya upangaji wa ardhi, umilikishaji wa ardhi na matumizi ya ardhi kwa ujumla yanafanyika kwa wakati na yanatiliwa msisitizo wa kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, hali iliyoko sasa hairidhishi na haiendani na uhitaji na bahati mbaya sana takwimu zinaonesha toka tumepata uhuru kati ya vijiji 12,319 ni vijiji 2,600 tu ndivyo ambavyo vimepimwa kwa matumizi bora ya ardhi, toka tumepata uhuru mpaka leo tunapoongea. Sasa ni vizuri sana tukaweka fedha za kutosha kuhakikisha kama tunaweka mkazo wa kupima ardhi yetu ya vijiji tunavipima kweli kweli, kama tunapima kwenye haya maeneo mengine, tunapima. Kwa hiyo, kwa kufanya hivyo maana yake tutapunguza kwa kiwango kikubwa migogoro ya ardhi. Kwa hiyo, tujikite katika kupanga matumizi bora ya ardhi, tusijikite katika kutatua migogoro, tukipanga tutapunguza migogoro.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunaona Kamati ya Mawaziri inazunguka nchi nzima, ile ni gharama, wanatumia fedha, wanatumia gharama kubwa, lakini kama tungewekeza katika kupanga tungepunguza haya mengine ambayo yanajitokeza leo. Kama haitoshi kati ya mwaka 2013 mpaka mwaka 2022, Serikali ilipanga kurasimisha maeneo 2,348,000 ili wapatiwe hati, lakini mpaka leo mwaka 2022 ni takribani miaka nane, ni maeneo 171,210 ndio peke yake yamerasimishwa na yakapewa hati. Miaka 8 tumeweza kurasimisha kwa asilimia saba tu. Sasa tutegemee ni kwa kiwango gani tutafikia kurasimisha kwa kiwango kikubwa ardhi yetu? Ardhi yetu ndiyo mtaji wetu, ardhi yetu ndiyo rasilimali yetu Watanzania. Kwa hiyo, ni lazima pawepo na msisitizo wa kuhakikisha ardhi hii ya Watanzania inapimwa kwa kadri ya mahitaji na kulingana na soko lilivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama haitoshi mwaka 2012, Serikali ilitarajia kutoa hati miliki 1,638,000, lakini kwa mwaka huo tu waliweza kufanikiwa kutoa hati 643,000. Sasa kama nilivyoeleza kwa kutumia ardhi hii tu Serikali ingeweza kupata mapato ya kutosha sana. Kwa hizi hati ambazo zimetolewa 643,000 ukichukua kiwango cha juu kabisa ukasema kila mwenye hati alipe angalau Sh.120,000 ya kodi kwa mwaka, maana yake Serikali ingepata mapato ya Shilingi Bilioni 77.2 kwa hati hizo chache tu. Vipi kama tukiweza kupima ardhi nzima ya Tanzania tukatoa hati, wenye hati wakailipa kodi kwa wakati? Kwa hakika Serikali ingeweza kupata mapato ya kutosha na yale mahitaji ya msingi ya Watanzania yangeweza kuwafikia kwa wakati na lakini kuhakikisha tunadhibiti ufisadi na mianya yote ya upigaji. Maana yake tungeweza kutengeneza namna bora ya kupata mapato halafu tukatengeneza na namna nyingine ya kupiga mapato haya bila kuwafikia watanzania kwa ujumla. Kwa hiyo haya ni muhimu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kama haitoshi, kuna maeneo makubwa ambayo yanaitwa kwa majina tofauti tofauti. Mfano sisi kule Kaskazini, tunaita mashamba makubwa ya Wawekezaji, kuna mashamba ya settlers, maeneo mbalimbali nchi nzima. Hao wamekuwa wakimiliki ardhi kwa muda mrefu wana lease ya miaka 99, wengine wamelimiliki toka wakati wa ukoloni mpaka leo, lakini wapo wengine ambao wanabadilisha matumizi ya ardhi hii bila kufuata utaratibu. Wako wengine ambao wametekeleza mashamba haya, wako wengine yaani inakuwa ni marufuku kuingia kwenye haya mashamba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano maeneo ya kaskazini, maeneo ya Meru kule, Maeneo ya Karatu, haya mashamba wanaomiliki wameacha mapori, wanyama wanajihifadhi humo, wananchi wanateseka katika nchi yao wakiwa wanaenda, mfano mmoja, kwenye shamba mojawapo katika Wilaya ya Karatu, mwekezaji ameacha pori, hilo pori wananchi wanapita kwenda kupeleka watoto shuleni. Juzi kati hapa mama ameuawa na mbogo akiwa anampeleka mtoto shuleni asubuhi, lakini eneo limeachwa ni pori linahifadhi. Halmashauri haiwezi kufanya kitu, Mwekezaji anasema ni mali yake ndiye ameamua hivyo kwa sababu ana hati. Haiwezekani lazima ifike mahali tuwaonee huruma Watanzania, lazima ifike mahali haya mashamba ambayo kwa namna moja ama nyingine hayajaendelezwa yafutiwe umiliki Watanzania wagawiwe ardhi hii waweze kuyaendeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema watu wanaongezeka, mahitaji yanaongezeka, ardhi ni ile ile haiongezeki. Kwa hiyo, tuweke msisitizo katika kupima, kupanga na hatimaye kumilikisha kwa maslahi mapana ya Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ya mwisho, suala la utawala bora. Suala la utawala bora hasa kwenye halmashauri zetu na kwenye wilaya zetu kuna changamoto kubwa…
NAIBU SPIKA: Waheshimiwa tungepunguza mazungumzo, tupunguze mazungumzo.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, tunategemea kuona utawala bora ni utawala unaofuata sheria, lakini kwenye maeneo yetu, utaratibu na jinsi ambavyo sheria na kanuni inataka, ni kuwepo na Mikutano Mikuu ya vijiji, kuwepo na usomaji wa taarifa ya mapato na matumizi, huo utamaduni uliishakufa na uliishapotea hakuna. Baadhi ya Wenyeviti wa Vijiji, Watendaji wetu wa Kata na Watendaji wetu wa Vijiji kule wamekuwa Miungu watu, yaani wao ndio wanafanya kila kitu, wao ndio watatengeneza michango, watakusanya wao, watapangia matumizi wao, watawatoza faini wananchi, watawaweka kwenye lockup zao wanazozijua. Hatuwezi kuwa na nchi ya namna hii…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: kengele ya pili.
MHE. CECILIA D. PARESSO: …tunataka utawala wa Sheria na utawala bora ufuatwe…
NAIBU SPIKA: Kengele ya pili, ahsante.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.