Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Dr. Thea Medard Ntara

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nianze moja kwa moja kwa kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita hasa kwa eneo kubwa kabisa la suala la mikopo. Sasa hivi hali imetulia, wanafunzi wametulia, angalau zile Message za mikopo zimepungua. Jambo kubwa sana limefanyika na Serikali hii, lakini bado niombe Serikali hao wanafunzi wa vyuo vya kati, naomba Serikali wajipange safari hii, hatutaki kelele za hao wanafunzi wa vyuo vya kati nikiwa na maana vyuo vya ufundi, maeneo ya afya na maendeleo ya jamii, hata wao waweze kupata mikopo. Tukifanya hivyo tutawasaidia sana watoto wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye suala la maadili. Leo kwa mara ya kwanza nimefurahi sana kuona baadhi ya Wabunge hasa wanaume akiwemo Mheshimiwa Sanga na Saashisha wanalizungumzia suala hili la maadili na hasa katika maeneo ya kuona watoto wetu na hasa wa kiume wanafanyiwa mambo ambayo hayafai.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ifike wakati Serikali ilete Muswada hapa ili kuweza kuwa na sheria kali na sheria kali hizi hatutakuwa sisi wa kwanza. Tunaogopa, mtu akinyongwa tunasema haki za binadamu, lakini huyu mtoto anayelawitiwa hana haki? Tulete sheria niwaombe Wabunge jamani tusimame wote kwa umoja wetu, Serikali walete Muswada hapa wa Sheria hawa watu wanaofanya hivyo wahasiwe au wawekewe dawa wawe wanapata vifafa, yaani mtu akipata kifafa hata zile nguvu zinakuwa hakuna. Nimwombe sana Waziri wa Afya, wao wnajua hayo mambo ya chemicals, watafute dawa hawa watu tuwa-fix, kama hatutaki kuwahasi basi tuwape wadudu wale wa kupata kifafa, waendelee kuanguka na kifafa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa sababu gani Waheshimiwa Wabunge? Hiki kizazi ni cha laana, haya mambo wanayofanya ni laana, tukiendekeza kuwaacha nawaambieni wote hapa tutapata laana. Tuondoe hicho kizazi waondoke kabisa na dawa ya kuwaondoa hawa ni kuwahasi tu wasiendelee na ule mchezo mchafu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunakuwa na huruma na watu ambao hawana huruma na watoto. Leo hii fikiria una mtoto, wengi hapa mna watoto wadogo, sasa fikiria kama ungemkuta yule mtu anamfanyia mtoto wako kitendo hicho wewe ungefanya nini? Ungemshika hapa umpeleke Polisi? Naamini wengi hapa ungemnyonga pale pale, ungemmaliza. Sasa kwa sababu kunyonga wanasema sijui haki za binadamu basi wahasiwe, vyombo viko hapa wanawakamata wanawahasi huko huko kimya kimya au wanaweka wadudu wa kifafa waendelee ili wasiwe katika dunia hii. Hata hivyo, tukiendelea hivyo hawa watoto wanafanyiwa toka wakiwa wadogo, basi kundi la mashoga litaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, wako baadhi ya Viongozi sijui ni wapagani, sijui wana dini gani? Ndani ya Makanisa watu wanatetea ushoga, Serikali wanawaangalia tu, kweli jamani? Clip zinatoka mtu anatetea ushoga, anasema kwani ushoga ni nini? Si mtu unaamua mwenyewe? Serikali iko kimya, huyu wangemchukua kabisa hapo Madhabahuni anakohubiri ushoga wangemchukua wakamfanyia hicho kitu… (Makofi)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

T A A R I F A

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa taarifa mchangiaji kwamba sio sahihi kwamba hakuna hatua zilizochukuliwa. Watu ambao wamefanya hiyo tayari wameshachukuliwa hatua na sheria inachukua mkondo wake na Serikali haitaendelea kuvumilia aina yoyote ya uvunjifu wa sheria za nchi hii. Kwa hiyo naomba nimpe taarifa hiyo.

NAIBU SPIKA: Daktari, taarifa hiyo Waziri mhusika amekupa.

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Masauni mimi nakuheshimu sana, sheria hizo zipo, hizo sheria zipo lakini bado siyo kali, ndiyo maana wanaendelea kufanya hayo madudu, leteni sheria tukifanya kwa watu watano, kwanza ukiwahasi unafikiri watatangaza kwamba mimi wamenihasi? Hawawezi! Leteni hapa tutaweka hiyo sheria, kwa nini mnatetea Mheshimiwa Masauni, hivi kweli hawa watoto tunaowazaa kwa uchungu vile wanafanyiwa hivyo? Hapana, hebu tujipange. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kuhusu ndoa za utotoni. Leo hii mimi huwa nashangaa sana, tunakaa hapa ndani ya Bunge tunasema ndoa za utotoni hazifai, ndoa za utotoni hazifai halafu tunajichanganya wenyewe tunasema eti mtoto akishapevuka anaweza akaolewa wakati wowote.

Mheshimiwa Naibu Spika, watoto wa siku hizi wasichana wanapevuka kati ya miaka tisa na miaka kumi. Fikiria una binti yako ana miaka kumi, eti unaenda kumuoza kwa sababu amepevuka, unaenda kumuoza kwa mwanaume mwenyewe ni giant natamani kutaja hata majina ya mfano, kweli. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba unilinde mtoto ana miaka kumi, kumi na moja, kumi na mbili kumi na tatu, kumi na nne, unaenda kumuoza kwa mwanamme, mtu kama Festo Sanga. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, huo ni mfano, huyu mtoto anapokwenda pale anaenda kuolewa, anaenda kubakwa? Huyu mtoto si atajeruhiwa tu? Zamani watu wanashangaa wanasema zamani…

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, naomba utulivu.

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Napenda kumpa taarifa Mama yangu pale. Mdogo wangu Festo yupo under forty ni mdogo, nadhani ana miaka sijui 32 kwa hiyo huo ni mwili tu usije ukaogopa. (Kicheko)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa endelea.

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Naibu Spika, zamani Mama zetu walikuwa wanaolewa wakimaliza Darasa la Saba. Ni kweli wanaolewa miaka 16, miaka 17, miaka 18 lakini lazima tujue kwamba walikuwa wanamaliza Darasa la Saba au Darasa la Nne hana pa kwenda. Hakuna VETA, hakuna shule za sekondari, leo hii kuna shule za sekondari kibao, kuna VETA, watoto wamalize Darasa la Saba waendelee na masomo. Niwaambie ukweli hata wale wazazi wetu walivyokuwa wanaolewa zamani wakiwa wadogo wengi wao ukiwauliza wanasema mwanangu tulikuwa tunaolewa ni mateso matupu, wala tulikuwa hatufaidi hayo maisha ya ndoa, kwa sababu kibinti kinaolewa kidogo kwa hiyo kinakwenda pale kinanyanyasika, kilichokuwa kinatokea pale ni sexual abuse! Sasa wewe leo unasimama mahali unahutubu unasema eti mtoto akishapevuka akaolewe!

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbunge muda wako umekwisha.

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo ninakushukuru sana. (Makofi)