Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Ndaisaba George Ruhoro

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuwa mchangiaji wa kwanza kuanzisha shughuli hii asubuhi hii, ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambae ameendelea kuonesha mapenzi makubwa kwa Watanzania kupitia kuachilia fedha ziende zikatekeleze miradi ya maendeleo. Wabunge watakubalina nami kwamba wao ni mashuhuda wa upendo mkubwa wa Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu Hassan ambae anasukuma fedha nyingi kwenye Majimbo kwa ajiali ya kutatua changamoto nyingi za Watanzania. Nami na wananchi wangu wa Jimbo la Ngara tunamshukuru sana Dkt. Samia Suluhu Hassan, juzi ameidhinisha 2,700,000,000 kwa ajili ya kwenda kujenga Chuo cha Ufundi - Ngara. Tunamshukuru sana Dkt. Samia Suluhu Hasssan na tunaendelea kumuunga mkono.

Mhehsimiwa Mwenyekiti, vilevile nimshukuru Waziri Mkuu, kwa kazi kubwa anayoifanya pia na kuwasilisha hotuba nzuri sana hapa Bungeni ambayo imejaa matumaini kwa Watanzania, kwa kweli ukisoma hotuba ile ya Waziri Mkuu inatuonesha inatupeleka kwenye Tanzania tunayoitaka. Ninamshukuru tena Waziri Mkuu na Waziri wa Kilimo kwa jambo lile la Kahawa, wananchi na wakulima wa Kagera na wale wa Wilaya ya Ngara kwa miaka zaidi ya 50 iliyopita tulikuwa hatujawahi kupata bei ya nzuri ya Kahawa. Katika msimu iliopita kwa mara ya kwanza tumeuza kilo moja shilingi 3,700 mpaka shilingi 2,000. Ni matarajio yetu kwamba msimu unaokuja Mheshimiwa Waziri Mkuu na Waziri wa Kilimo wataendeleza hatua ambazo zilichukuliwa kwenye msimu uliopita ili wananchi wa Jimbo la Ngara na wale wa Mkoa wa Kagera tuendelee kufurahia matunda mazuri ya Serikali yetu kwa kuendelea kuuza Kahawa kwa bei nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nielekeze sasa mchango wangu kwenye eneo la sekta ya madini. Katika hotuba ya Waziri Mkuu alielezea malengo na dira na mwelekeo wa sekta ya madini hapa nchini. Alielezea kwamba kwa upande wa makusanyo ambayo Wizara ya Madini ilikuwa imelenga kwenye mwaka wa fedha uliopita, walikuwa wamepanga kukusanya bilioni 479.51 na wakafanikiwa kukusanya bilioni 409.66 ambayo ni sawa na asilimia 85 ya target yote ambayo Wizara ilikuwa imejiwekea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kumweleza Waziri Mkuu na Mawaziri wengine hasa Waziri wa Madini kwamba kuna mambo kadha wa kadha kwenye sekta ya madini ambayo yanakwamisha juhudi za Serikali ili kuweza kufikia makusanyo ambayo yanatarajiwa, yamkini pengine makusanyo yangefika mpaka trillioni moja endapo vitu ninavyokwenda kuvizungumza vingefanyiwa kazi na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza ambalo napenda kuchangia na naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu alichukulie kwa umuhimu wa aina yake ni eneo la kodi la mapato asilimia 30. Wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu, leseni wanazopewa ni zile leseni za kuwaruhusu kufanya utafiti na kuchimba madini kwa wakati mmoja, hii ina maana kwamba anachimba shimo hapa anakwenda anachimba shimo pale, fedha anazozipata hapa anazirudisha tena kwenye utafiti, TRA wao wanachokiangalia ni mchimbaji huyu kwenye akaunti yake zimeingia Bilioni ngapi, wanaomba nyaraka za viambatanisho, anapotoa nyaraka ambazo siyo risiti za EFD wanazi-reject na wana–subject kwenye kodi ya mapato ya asilimia 30. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kodi hiyo haipo, wachimbaji wadogo hawana na hawataipata na sana sana Serikali itakwenda kuwafilisi kupitia TRA, kwa sababu, shughuli zao zile ni za kusaga mawe, kuchimba mashimo, kusogeza vifusi, na kusomba maji. Shughuli zote zinafanywa na Watanzania wa chini ambao hata TIN Number hawana, hata line za simu kwa kuwa hawana vitambulisho vya NIDA wanatumia za ndugu zao. Kwa hiyo, matokeo yake ni kwamba, ni watu ambao wako kwenye informal sector kuweza kupata risiti, haiwezekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuishauri Serikali katika eneo hili. TRA waachane na kodi ya asilimia 30 (Corporate Tax), waache kuwalazimisha wachimbaji wadogo kufunga mahesabu kwa sababu, hawawezi kufunga mahesabu kwa nature ya biashara zao. Naomba Serikali baada ya kukata mrahaba asilimia sita, baada ya kukata ada ya ukaguzi asilimia moja, baada ya kukata Service Levy, Serikali ikate asilimia moja kama kodi ya mapato kutoka kwenye mauzo ya dhahabu on point of sale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ni sawasawa na ule mchezo wa Biko au Bingo au ule mchezo wa Tatu Mzuka, kwamba, unapocheza Bahati Nasibu ukawa umeshinda pale, Serikali pale pale inachukua kodi yake.

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ndaisaba, naomba upokee Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Iddi Kassim.

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba unilindie muda wangu.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

T A A R I F A

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa tu mchangiaji. Ukiacha Corporate Tax ambayo ni asilimia 30, sasa hivi TRA wanaenda wanazunguka, wanataka kuweka kodi nyingine asilimia mbili kumwongezea mchimbaji mdogo huyu ambaye hajawezeshwa kupewa mitaji na kupewa maeneo yenye utafiti, ahsante.

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Ndaisaba unapokea Taarifa?

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeipokea vizuri sana. Nakushukuru.

MWENYEKITI: Kengele yako ya kwanza imeshagongwa.

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli muda wangu nimekuomba unilindie. Niongezee hata dakika tano tu.

MWENYEKITI: Mheshimiwa endelea kuchangia, kengele ya pili itapiga sasa hivi.

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Sasa nielekee eneo la pili la VAT. TRA wameendelea kuwabana dealers wote ambao wanafanya biashara ya dhahabu. Wanawataka hawa dealers waweze kulipa VAT kwenye dhahabu wanazonunua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamaanisha kwamba, dealer akiweza kununua dhahabu ya shilingi milioni 100, akishai-subject kwenye VAT anatakiwa kwenda kuuza ile dhahabu shilingi milioni 118. Hii fedha haipo kwa sababu dhahabu, inanunuliwa kwa thamani ya bei ya Soko la Dunia. Hii inamaanisha kwamba, dhahabu inayonunuliwa Tanzania kwa mfumo huo wa VAT, haiuziki mahali popote pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuwaambia TRA, hii fedha kwa dealers haipo na wale dealers wanaowasumbua kule Kahama, Tanga na maeneo mengine kwamba walipe VAT asilimia 18, hawataipata na matokeo yake ni kwamba wachimbaji na dealers wote wataendelea kutorosha dhahabu hapa nchini. Kwa sababu ukinunua dhahabu kwa utaratibu ulivyo hapa Tanzania, huwezi kuiuza mahali popote pale duniani. Naomba niishauri Serikali na TRA, waachane na mambo ya VAT kwenye dhahabu. Warudi kwenye utaratibu ule ambao nimesema wa nipe nikupe, ama nilipe nisepe. Tukutane sokoni, wachukue asilimia moja, iwe inawatosha na Serikali wataona mapato yanavyoongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la mwisho ni eneo la kuchimba madini kwenye hifadhi. Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu Hassan, alishaeleza kwamba, tembo na wanyama wengine huko porini hawali madini. Ukienda kwa mfano kwenye Game Reserve ya Kigosi, mle utakutana na sungura na nyoka tu, hata swala hakuna, wala simba hakuna, lakini pale kuna madini ya dhahabu. STAMICO wamepewa leseni wanatakiwa wachimbe madini yale, lakini ukienda TANAPA ni wagumu utafikiri ukipeleka grader mle linamaliza miti yote linaifyeka wakati unachimba kwenye kaeneo kadogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muda muafaka sasa, naishauri Serikali watengeneze mkakati, watengeneze task force, watengeneze Mwongozo ili uweze kuja na mbinu nzuri za kuweza kuchimba madini kwenye hifadhi, hata yale madini ya Emerald kule Mayoka kwenye Hifadhi ya Manyara, madini yale yachimbwe yaweze kufaidisha Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)