Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Eng. Ezra John Chiwelesa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Biharamulo Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hotuba hii ya bajeti ya Waziri Mkuu. Kwanza kabisa nachukua nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa fedha nyingi sana ambazo zimeletwa katika Wilaya yetu ya Biharamulo, lakini pia ziara mbili alizozifanya mwaka jana 2022 mwezi wa Sita na mwezi wa Kumi katika Wilaya yetu ya Biharamulo na akapata nafasi ya kuongea na wananchi katika maeneo ya Biharamulo Mjini na Nyakanazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita kwenye mambo mawili siku ya leo. Jambo la kwanza ni mipango bora ya matumizi ya ardhi, ili kuondoa migogoro kati ya wafugaji na hifadhi zetu za Taifa, halikadhalika wafugaji na wakulima; na wakulima na hifadhi. Jambo la pili, nataka niongelee habari au njia bora ya kuzuia wizi au ubadhirifu kwenye miradi ya umma au miradi yetu inayotekelezwa na Serikali. Ni mambo mawili nataka niyaongelee kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na suala la mipango bora ya matumizi ya ardhi; kwa muda mrefu sana wakulima wa nchi hii au wafugaji wa nchi hii wamekuwa kama watu ambao hawana sehemu ya kukaa. Sasa tulizoea ugomvi kati ya wafugaji na wakulima, lakini leo hii tunashuhudia ugomvi kati ya wafugaji na Serikali yao kupitia TANAPA au kupitia TFS.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunaotoka maeneo haya yenye hifadhi wafugaji wa nchi hii wanapata tabu sana. Wafugaji wengi sana wamefilisiwa. Kila ng’ombe anapokamatwa anatozwa shilingi 100,000 kwenye yale maeneo. Mimi si-support watu kuingiza ng’ombe mle, lakini wafugaji hawa wamedhalilika na wamefilisiwa kwa sababu Serikali haijawawekea mpango bora wa kujua wanafugia wapi? Hii ndio shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunaotoka maeneo kama ya Biharamulo, kwa sehemu kubwa; mimi naongea na wananchi wangu na wananipigia simu; na mara nyingi nimekuwa nawauliza, kwa nini mnaendelea kuweka ng’ombe huko wanakamatwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, makundi makubwa ya ng’ombe kutoka nchi jirani yamewekwa kwenye Hifadhi ya Burigi. Sasa wananchi wetu wanapoingiza ng’ombe mle, wanakamatwa, lakini ng’ombe wa wageni wako mle. Hii ni aibu na udhalilishaji wa wafugaji wa nchi hii. Ninachoomba, kama Bunge ni lazima tupate hatua nzuri ya kuwasaidia wafugaji wa nchi hii. Hatuwa-support kuingiza mifugo kwenye hifadhi, lakini tuje na mpango bora wa kuwasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri wewe ni Mwenyekiti wa Kamati yangu ambayo ninatoka na Kamati ya Mifugo iko chini yako. Tulipata ripoti kutoka kwa Waziri wa Mifugo, a very good report kwamba wanao mpango wa kuleta majani kutoka nje ya nchi waanze kuotesha kwa ajili ya kuwasaidia wafugaji wa nchi hii, lakini wanasaidia wafugaji wangapi? Anayejua ng’ombe wa Biharamulo ni wangapi? Ng’ombe Mufindi ni wangapi? Hatujafanya sensa ya kujua idadi ya mifugo kwenye nchi hii. Sasa naomba hili jambo lifanyike, tujue idadi ya ng’ombe kila eneo na Serikali itusaidie kutenga maeneo kwa ajili ya wafugaji. Halikadhalika, hata ng’ombe ambao tunasema, ni nani anayeweza kuwa-identify?

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tumeanza mnada wa kuuza ng’ombe live. Huko ng’ombe wanakopelekwa, ng’ombe wetu hawana alama wala hawana identification. Tulijaribu kuongelea issue ya alama hapa ya kuwawekea sijui imepotelea wapi? Matokeo yake tutaenda kwenye mnada wa dunia unapeleka ng’ombe kule, wenzetu tunawajua, hata maparachichi yalivyokuwa yanakuwa mabovu kule watasema yametoka Tanzania. Kesho utapeleka ng’ombe pale anaonekana ana ugonjwa katoka sehemu nyingine, kwa sababu hawana alama, watasukumia, watasema ametoka Tanzania. Kwa hiyo, kesho na keshokutwa, hata kizuri ambacho tunakifanya kwenye soko kitaharibika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba hilo tusaidiwe, ng’ombe wafanyiwe identification, pia maeneo yatengwe, na hayo majani yatakapokuja, watu tuwe tunajua, tunapata majosho mangapi kwenye maeneo yetu? Tunapata mabwawa mangapi ya kunyweshea ng’ombe? Halikadhalika, hata hayo majani yaje yaoteshwe. Wafugaji wako tayari kutoa hata pesa kuliko kuhangaika na makundi ya ng’ombe watoke Biharamulo wayapeleke Sumbawanga. Wako tayari kutoa pesa hata hayo majani yakioteshwa ili waweze kuyapata kwenye maeneo yao. Kwa hiyo, nilikuwa naomba hilo liangaliwe kwa ajili ya kulinda wafugaji na kulinda hii mifugo tunayoiuza nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 18/09/2021 Mheshimiwa Waziri Mkuu alitembelea Biharamulo, akafanya mkutano pale kwangu Nyakanazi. Nakumbuka kwenye mkutano ule wananchi wa Nyakanazi walimwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu eneo la kulima. Kuna Swamp pale kwenye eneo la TFS, wakawa wameomba na Waziri Mkuu akatoa maelekezo kwamba, Waziri wa Maliasili, aliyekuwepo wakati ule aje, nami nikamjulisha, lakini as I am speaking today, hakuna Waziri aliyekanyaga Biharamulo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba, kuheshimu maelekezo aliyotoa Waziri Mkuu tarehe 18/09/2021, naomba Waziri wa Maliasili na Utalii afike Biharamulo, aongee na wananchi wale wa Nyakanazi awaambie lile eneo linapatikana au halipatikani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kibaya sana, kitu kibaya mno, Maaskari wa TFS walioko maeneo ya Nyakanazi kwenye ule msitu wetu pale, wamekuwa wanawalaghai wananchi wa Biharamulo, wanawalipa pesa, wanaenda wanalima kwenye hifadhi, muda wa kufanya mavuno unapofika, wale Maaskari wanawakamata wale wananchi na yale mavuno wanayachukua. Huo ni udhulumishi na udhalilishaji wa ajabu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kabla ya kumaliza bajeti hii, Waziri Mkuu atakapokuwa ana-wind up tupate majibu.

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ulinde muda wangu. Maana nadhani Mawaziri wanayo nafasi ya kujibu hoja zetu.

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba tu nimpe Taarifa Mheshimiwa Mbunge wa Biharamulo kwamba, Wizara ya Maliasili na Utalii na Utalii imekasimiwa madaraka na Serikali kusimamia maeneo yote yaliyohifadhiwa. Kazi kubwa kwetu ni kulinda na kuyahifadhi hayo maeneo. Linapofika suala la kuomba eneo, tunawaomba wananchi wanaandaa vikao, wanakuja wanaleta-proposal yao, tunaiangalia kama itawezekana. Kwa sababu, tunapolinda tunaangalia mambo mengi, kuna masuala ya shoroba, kuna masuala ya maeneo ya mtawanyiko, kuna mandhari ambazo tunazitunza kwa ajili ya faida ya wananchi wao wenyewe walioko katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, unapoomba usitarajie wakati wowote utapata. Ni pale ambapo tutaona: Je, kuna umuhimu wa kulitoa hilo eneo ama la?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, maeneo tunayoyahifadhi sisi ni kwa ajili ya faida ya wananchi wenyewe pamoja na Watanzania wote na siyo ya maliasili na watumishi wake peke yake.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Engineer Ezra unapokea Taarifa?

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa siipokei. Mimi nawakilisha wananchi wa Biharamulo, ningeomba nisikilizwe hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sipingani na Serikali, na sijasema wananchi waingize ng’ombe au wafanye kazi kwenye hifadhi. Nilichokisema hapa, kitendo cha askari kuwaambia wananchi wakalime kwenye hifadhi, wakampa pesa akawaruhusu wakalima, kesho wakati anaenda kuvuna wakamkamata, that is insubordination kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi hawana maeneo. Tunapoomba maeneo kwa Serikali hapa, Waziri umekaa hapa, watakuletea taarifa walioko kule site. Aliyeko site kama anafanya bishara ya kuwakodisha wananchi pale, anawadhulumu ardhi, kesho utamwuliza akupe ushirikiano? Hicho ndicho ninachokitaka. Sitaki wananchi wakalime mle bila kibali, lakini ninachotaka, wananchi watendewe haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeomba ardhi, Mheshimiwa Rais tarehe 16 akiwa Nyakanazi nilisimama nikaomba, tumeshawasilisha, Mkoa wa Kagera umeleta, Serikali inafanyia mchakacho, lakini kipindi inafanya mchakato wananchi hawa wasiumizwe na watu wenye uchu kwa kuwadanganya halafu baadaye wanawadhulumu ardhi yao. Hicho ndicho ninachokisema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ameniwahi, sijasema wananchi wakafanye…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ezra, unaweza kukaa pale tu nikiruhusu taarifa. Taarifa hizi zinakula muda wako. Kwa hiyo, endelea kuchangia mpaka itakaponipendeza. (Kicheko)

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Anyway, sasa hilo la hifadhi nadhani limesikika, limeeleweka, naomba mlifanyie kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya pili, naomba unilinde muda wangu maana nimekalishwa mara nyingi hapa. Sehemu ya pili, nilikuwa nataka kuongelea njia bora ya kuzuia wizi na ubadhirifu katika miradi ya umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe ni shahidi, tumesema tusiongelee habari ya Ripoti ya CAG hapa kwa sababu muda bado, lakini ukweli ni kwamba, wananchi wa nchi hii kinachoendelea kila mmoja anakijua. Kwenye vijiwe, kwenye mitandao na kila maeneo, kila mmoja anajua yaliyofanyika na kila mmoja anajua yanayoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wangu nilitaka niseme jambo moja, kidogo nina uzoefu kwenye hii miradi. Kinachofanyika hapa kwenye Ripoti ya CAG…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Naomba uhitimishe Mheshimiwa Ezra, dakika zako zimeisha.

MHE. ENG. EZRA J CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kengele ya kwanza.

MWENYEKITI: Haya, nakuongeza dakika moja nyingine.

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, haitanitosha, naomba nihitimishe.