Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Godbless Jonathan Lema

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Arusha Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Leo nilikuwa nisome hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni; hotuba hiyo kimsingi haikuwa mbaya hata kidogo. Waheshimiwa Wabunge, wenzangu wa Chama cha Mapinduzi tafuteni hiyo hotuba muisome, muitathmini mwone wapi kulikuwa na makosa ya msingi ya kuiondoa Bungeni, kama siyo tu hotuba ile ilikuwa na busara ya kusaidia Jeshi la Polisi na Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ngoja nimwambie rafiki yangu Mheshimiwa Kitwanga, nilimwambia Mheshimiwa Sitta kwenye Bunge hili, kipindi kile Mheshimiwa Lowassa alikuwa yuko CCM. Nilimwambia ukiona Kambi ya Lowassa inakushangilia wewe kuwa Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, maana yake usisherehekee, maana yake ujiulize kwa nini nashangiliwa? Hili jambo linalohusu Mkataba wa Lugumi halikuwa kwa ajili ya kuidhalilisha Serikali, ilikuwa ni kwa ajili ya kuiondolea doa Serikali. IGP anasemwa, Waziri unasemwa, Jeshi lote la Polisi linasemwa na mkataba mchafu wa Lugumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Kitwanga ni rafiki yangu, haya mambo ambayo nimeandika, nimejadiliana naye nyumbani kwake tukiwa tunakula ugali. Nikamwambia mimi ni kipindi cha pili kuingia Bungeni, nazijua siasa za Bunge, nakuomba Mheshimiwa uniambie mimi kama Kambi ya Upinzani naweza nikasaidia mambo gani ambayo Serikali hamwezi kuja nayo direct? Nikamwambia usiponiambia, mimi nitakunyooshea na nitataka majibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeuliza swali ambalo nimeambiwa niliondoe kwamba, hivi Kamati ya Bunge inavyotembea kote huko kutafuta sakata hili la Lugumi, CAG anashindwa kutuambia kama mkataba ule ulikuwa thamani yake ya fedha na vifaa ni okay ama ni no! Anashindwa kujua!
Nikauliza swali lingine ambalo nimeambiwa niliondoe na Kamati; hivi Mheshimiwa Kitwanga wewe ni mbia wa enforce na ni Waziri wa Mambo ya Ndani; na Kampuni hii ya Lugumi iliingia kwenye biashara ukiwa siyo Waziri. Je, kama umekosa taarifa kutoka Jeshi la Polisi ambalo liko chini yako, umekosa pia taarifa kutoka kwenye kampuni ambayo ni mbia, ukijibu haya maswali Bungeni, utaondoa ukakasi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikauliza swali lingine ambalo nimeambiwa niliondoe.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Lema, nakujua wewe ni mzoefu kwenye Bunge, najua uwezo wako. Unatumia njia nyingine kusoma hotuba yako hapo ulipo. Sasa nakusihi, sababu maneno hayo unayosema ndiyo yamekatazwa kuanzia ukurasa wa kumi. (Kicheko/Makofi/Kelele)
Unajua Mheshimiwa Lema, hawa wanapiga vijembe kama mpirani. Referee akipiga filimbi, watu wanalalamika, lakini Serikali, referee anakuwa strict. Jiepushe na maneno yaliyopo kwenye ukurasa wa kumi mpaka wa kumi na nne.
MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajiepusha na hayo maneno, lakini Wabunge wa Chama cha Mapinduzi, nikiangalia Wabunge wote hapa ni wapya kwa asilimia 50.
MHE. GODBLESS J. LEMA: Ama seventy. Wabunge tuliokuwepo Bunge lililopita, hatukuwa hawa ninaowaona hapa. Waheshimiwa Wabunge pamoja na itikadi za vyama vyetu vya siasa, inapokuja kwenye suala la maslahi ya nchi yetu, tuache hizi siasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkisema mambo ya msingi kama haya tusiyaongee, ndiyo sababu uliponiita hapo mbele nilisema basi ngoja na mimi tu nimshukuru mke wangu kwa kuja Dodoma. Kama mambo serious kama haya Kambi inakatazwa kuongea, tunaisaidiaje Serikali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Wizara ya Mambo ya Ndani, unapokuwa na IGP anayesemwa vibaya na hakuna kauli ya Serikali, unafanya Jeshi la Polisi lidharaulike. Unapokuwa na Waziri wa Mambo ya Ndani anatiliwa mashaka kwa mambo ambayo ama ni ya magazeti au mitandao na hakuna majibu, unafanya Wizara idharaulike. Wizara ya Mambo ya Ndani ikidharaulika, ni nchi imedharaulika usalama wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba yangu utakuwa umeipata ambayo ina mambo nimeambiwa nisiyasome. Wewe yajibu tu kimkakati ili uwe na amani. Nakwambia jambo hili halimhusu Lugumi. Lugumi is nothing in this Parliament! Mtu anayetafutwa humu ni wewe.
MHE. GODBLESS J. LEMA: Sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme tu, hii wanataka kutengeneza mlima kutoka kwenye kichuguu. Hii wanaacha pressure iendelee, wanakutafuta wewe. You will tell me my brother, you will tell me! Mimi najua siasa za Bunge humu! Unajiuliza, hii hotuba ina makosa gani? Haina makosa, wanataka pressure iendelee. Wanasema wewe ni rafiki wa karibu wa Magufuli, nawe ndiyo kiherehere mkubwa, kwa hiyo, wanakutafuta wewe! Wanakutafuta!
MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wetu huyu mwema, nikilitumia hivyo kuna shida?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wetu huyu mwema wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni rafiki wa karibu wa Mheshimiwa Kitwanga. Kwa hiyo, nasema kwamba jambo hili siyo jambo dogo, nami maswali niliyokuwa nauliza ambayo nimezuiwa; Waheshimiwa Wabunge, nakatazwa kwenye hotuba yangu hata kuuliza. Jamani leo Mheshimiwa Kangi amenishangaza! Mheshimiwa Kangi anasema, Mheshimiwa Chenge hajawahi kutuhumiwa na scandal ya Rada. Mheshimiwa Kangi!
MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, okay. Naongea nini? Mbunge yeyote ndani ya Bunge hili, zawadi pekee ambayo anaweza akaipa familia yake ama wazazi wake ama nchi yake ni kuthubutu kusimamia ukweli unaolinda Taifa hili. Yeyote! Nawaomba Waheshimiwa Wabunge, bendera zetu zisiwe na nguvu kuliko hadhi ya nchi yetu. Tusaidie hii nchi kwa pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwaambia na nawaambia tena, hatutashinda uchaguzi kwa sababu ninyi ni wabaya, tutashinda uchaguzi siku ambayo watu wataamua tushinde uchaguzi na kuwepo kwa Demokrasia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna mtu amesemwa kwenye Bunge lililopita na kwenye magazeti. Kuna watu walisema mwaka 2015 kwamba kuna siku tutam-miss Kikwete, mimi nimeanza kum-miss Mheshimiwa Kikwete. Hakuna mtu alisemwa kama Rais Kikwete! (Kicheko/Makofi)
MBUNGE FULANI: Kweli kabisa!
MHE. GODBLESS J. LEMA: …lakini hakuwahi kuingilia Mhimili wa Bunge. Hakuwahi kuingilia shughuli za Bunge. Bunge hili lilikuwa linamsema Rais Kikwete kwa namna yoyote ile, Mawaziri akina Mheshimiwa Jenista mlikuwepo, hamkuwahi kuingilia! (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Waheshimiwa Wabunge wenzangu, tuisaidie hii nchi, tuvuke mipaka ya party caucus zetu tusaidieTaifa hili. Kuna mtu mmoja yuko Magereza huko, alipokuwa jela aliulizwa na Wakili wake; aliambiwa, lakini wewe ulikuwa Waziri, wakati mnapitisha hii sheria ya kwamba ukikamatwa na makosa ya ufisadi wa fedha za umma ni lazima ulipe 50 percent kama bail, ulikuwa wapi? Akasema nilikuwa kwenye kikao hicho lakini sikuona jambo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vikao hivi tunavyofanya shughuli za Bunge, tunavyohudumu kama Wabunge, iko siku dhambi tunazozifanya humu zitakuja kuwala watoto wetu na watoto wetu kwa sababu tulishindwa kusimamia ukweli.
MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri…