Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Zuena Athumani Bushiri

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nami kunipatia nafasi nichangie hotuba hii ya Bajeti ya Waziri Mkuu. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu, Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya katika Taifa hili na kutuletea fedha nyingi sana kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee Mkoa waa Kilimanjaro. Mkoa wa Kilimanjaro tumepata Shilingi bilioni 620.224 katika miradi 717. Tunampongeza sana Mama, tunaipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Naomba nifafanue miradi hii. Afya tumepata shilingi bilioni 45, elimu tumepata shilingi bilioni 17.21, ujenzi tumepata shilingi bilioni 126, nishati tumepata shilingi bilioni 21.59, maji tumepata shilingi bilioni 358.43, uchumi tumepata shilingi bilioni 17.63, ardhi tumepata shilingi bilioni 11.3, utawala tumepata shilingi bilioni 3.97. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan kwa fedha hizi ambazo tumezipata kwa kuwa haijawahi kutokea, ni jambo la kihistoria. Baada ya pongezi hizi na fedha hizi ambazo tumezipata, nitajikita katika sekta ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefanya kazi kubwa sana katika sekta ya afya, tumejenga zahanati, tumejenga vituo vya afya, tumejenga hospitali za wilaya, za mikoa na za rufaa. Hata hivyo, bado tuna changamoto ambazo hospitali hizi zinaikabili. Kwanza kabisa tuna changamoto ya watumishi, hasa katika ngazi za kata katika zahanati. Ni ukweli usiopingika kwamba tunao watumishi wachache sana hasa katika sehemu za vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna changamoto ya nyumba za watumishi. Unakuta daktari amehamishiwa zahanati fulani, lakini anatumia kilometa kama moja na nusu kutembea kila siku kufika katika kituo chake cha kazi. Naiomba Serikali iliangalie hili kwa kina kirefu, kwa mapana yake ili madaktari hawa waweze kufanya kazi vizuri na kuwahudumia wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende katika Hospitali ya Rufaa ya Mawenzi. Nilisimama tena hapa kuongelea kuhusu Hospitali hii ya Mawenzi ambayo ni Hospitali ya Mkoa. Nashukuru Serikali kwa kuwa imefanya kazi kubwa sana katika jengo la mama na mtoto, linaendelea vizuri na kazi inaendelea. Pia, naishukuru Serikali kwa Shilingi bilioni 1.5 ambayo wametupatia kwa ajili ya ujenzi wa wodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba Hospitali hii ya Mawenzi ni hospitali ambayo imejengwa kipindi cha mkoloni, majengo yake yamechoka sana na hayana hadhi ya kuitwa Hospitali ya Mkoa. Naiomba Serikali ijitahidi kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya wodi zilizoko pale ili angalau ziweze kujengwa zifanane na hadhi ya Hospitali ya Mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine niongelee changamoto iliyopo katika Hospitali ya Mawenzi ambayo ni jengo la kuhifadhia maiti (Mortuary). Kama nilivyotangulia kusema kwamba majengo mengi yalijengwa kipindi cha mkoloni. Jengo hili kwanza ni dogo, lakini pia ni la zamani, hata majokofu yaliopo pale yamechoka. Hospitali ile ya Mawenzi ni ya Mkoa. Tunazo wilaya saba katika Mkoa wa Kilimanjaro, wote wanaitegemea ile hospitali, lakini yanapotokea matatizo ya watu kufariki, nasikitika sana kwa sababu hata hospitali ile inazidiwa kiasi kwamba miili ile ya marehemu itafutiwe nafasi kupelekwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya KCMC, jambo ambalo unakuta sasa nyingine hata kule KCMC kumejaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, naamini ni Serikali Sikivu, iangalie Mkoa wa Kilimajaro na ile Hospitali ya Mawenzi ili iweze kutusaidia sehemu hii ya mortuary. Kwanza tujengewe mortuary kubwa ambayo itakuwa na hadhi ya mkoa na itakayokuwa na majokofu mengi na imara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia baada ya kuchangia kuhusu Hospitali ya Mawenzi kwa maana ya afya, naomba nije katika ukatili dhidi ya watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mwanamke na ninaposema suala la mtoto, niseme wote ni wazazi, Wabunge wenzangu wanaume msije mkasema lakini wanaume sisi; wanawake inatugusa zaidi. Inatugusa kwa ile amini tuliyokula ya kukaa na watoto tumboni miezi tisa na kuwalea mpaka watakapofika hatua ambayo wanajitambua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ukatili wa watoto kwa kweli limekithiri sana hapa nchini. Mimi kama Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kilimanjaro, nilifanya ziara katika Mkoa mzima wa Kilimanjaro nikiambatana na watumishi wa Dawati la Kijinsia katika Wilaya zote. Nasikitika mambo ambayo tulikuwa hatutegemei kwamba yanaweza kufanyika yanafanyika katika Mkoa wa Kilimanjaro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba kama Wabunge wote hatutakuwa na sauti moja, tukashikana, suala hili hatutaweza kulimaliza. Ninasema hivyo kwa sababu gani? Kumekuwa na utamaduni katika baadhi ya maeneo; niiseme Kilimanjaro. Baadhi ya watumishi wamekutana na changamoto ambayo mimi binafsi imeniwia ngumu. Nasema hivyo kwa sababu wanasema, baada ya kukutana na hoja kama hizo watoto wamefanyiwa ukatili, wanapokwenda kufuatilia, unakuta kwamba wale wazazi wanakutana wenyewe, wanayaongea wenyewe na zile kesi kule mahakamani hatimaye zinafutwa. Naiomba Serikali, kesi kama hizi zikipelekwa pale zifanyiwe uharaka ili ziishe haraka ili watu wasipotoshe Ushahidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, samahani kidogo, mimi ni Mpare nimeolewa na Mchaga, ni waume zangu, lakini wana utamaduni ambao mimi binafsi siupendi. Kule Uchagani unapofanya jambo ambalo linakuuma sana au ni zito, kuna jani moja linaitwa sale. Ukiiongea na watumishi wale, dawati la jinsia watakwambia tatizo hilo. Wanapokuta mambo yamekuwa siyo mazuri, linatumika jani la sale kwenda kuomba msamaha ili mambo yaishe. Wakati huo tayari watoto wameshaathirika. Nawaomba ndugu zangu tusitumie vitu vya mila kuharibu vizazi vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisemea hili kwa sababu haiingii akilini uletewe sare wakati mtoto wako amelawitiwa, ni jambo la kusikitisha sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee pia…

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa muda wako umekwisha.

MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naunga mkono hoja.