Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Maimuna Ahmad Pathan

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kuongelea Bajeti ya Waziri Mkuu. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupatia uhai wake na pia tunamshukuru sana Rais wetu Mama Samia Suluhu kwa miradi ambayo ametuletea pesa nyingi katika nchi yetu na miradi hiyo inaendelea. Tunampongeza sana na tunamshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya Waziri Mkuu, tumeiona iko vizuri sana. Tunashukuru imekwenda vizuri na waliofanya kazi, kwa kweli wamechakata wamefanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina nyongeza ya mambo ya msingi sana yanayoendelea, lakini hayana matokeo mazuri. Naongea kwa masikitiko makubwa sana na maumivu makubwa sana kutoka moyoni mwangu. Wananchi wa Mkoa wa Lindi Wilaya ya Liwale na Wilaya ya Nachingwea wanavyouawa na wanyama tembo. Ukienda kwenye mashamba ya wananchi wale utatoa machozi, utalia njaa itakayotokea sasa hivi ni kubwa mno. Tuna vijiji vingi ukienda maeneo yanaitwa Nditi, Namapwiya, Ngumichile, Mbute, Nyambi, Mwandila, Matekwe, Majonanga na ukienda Liwale; Kibutuka, Mkutano, Lilombe na Kilangala inasikitisha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ni mbaya wamepelekwa Askari Wanyamapori wachache. Hivi kwa hali ya kawaida kwenye shamba wakiingia tembo hamsini kwa mara moja hawa askari wetu wawili, watatu wataweza kufanya ile kazi kweli? Wataweza kweli? Hali ni mbaya. Mwisho juzi kuamkia jana kuna kijana amefariki ameuawa na tembo mchana kweupe katika maeneo ya Mwinyichile saa tisa mchana, amejitoa nyumbani akasema akaangalie shamba lake kama limebakia mahindi kidogo au alizeti, amefika kule yeye ndiye wamemfanya chakula inasikitisha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulitegemea ingetokea hali ya dharura, ya tahadhari ya haraka ya kupeleka helikopta, lakini tumelizungumzia sana. Haijapelekwa helikopta kufukuza wanyama wale mpaka leo lakini angeuawa ndovu mmoja ingeenda helikopta na maaskari pale kwenda kuwaletea vurugu wananchi, inasikitisha sana hii hali, inasikitisha mno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najiuliza na wananchi wa kule wanajiuliza ndovu na binadamu nani ni muhimu? Inafikia wakati wanasema mtapigiwa kura na ndovu, siyo kwamba wanaongea vile kwa kutulaghai ni hatua na uchungu waliokuwa nao. (Makofi)

MHE. YAHYA A. MHATA: Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Yahya Mhata, taarifa.

TAARIFA

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili la tembo kwa kweli ni la hatari sana. Hata Jimboni kwangu tembo ni tatizo, kwa hiyo namuunga mkono kabisa mzungumzaji. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Maimuna taarifa unaipokea?

MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea taarifa. Hali ni mbaya. (Makofi)

MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa, nimeona kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Pallangyo.

TAARIFA

MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa mzungumzaji pia kwamba kule kwetu Arumeru Mashariki, Kijiji cha Kilinga, tembo wamehamia kwenye nyumba za wananchi. Hali ni mbaya sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Maimuna.

MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, tulitegemea sisi wananchi wa Mkoa wa Lindi hali ya dharura ingetokea, kwa sababu ndovu wanaoingia kwenye shamba moja ni zaidi ya Hamsini, wanapelekwa askari wawili, watatu wanashindwa wanakimbia na wao wanaondoka. Wabunge wenzangu na viongozi mbalimbali wameripoti hicho kitu mara chungu nzima, tulitegemea wangeleta helikopta kufukuza wale wanyama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali iko tofauti. Tunajiuliza wangeuawa ndovu wawili pale pangetulia vile, wananchi wetu wangepona kweli? Inasikitisha sana. Tunaomba…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala lingine, kuna wahanga wananchi wetu wa Wilaya ya Kilwa Masoko na wa Nachingwea kulikuwa na upanuzi wa viwanja vya ndege, walitwaliwa maeneo yao, ni siku nyingi, lakini mpaka sasa hivi hawajawapa pesa zao. Hiyo hali inakatisha tamaa na inarudisha maendeleo. Pia kuna barabara hii ya Masasi – Nachingwea – Liwale. Hii Barabara tangu 2015 kila siku tunaambiwa ipo kwenye upembuzi yakinifu, kila siku tuaambiwa inajengwa, kwani hii keki ya Taifa na sisi pia hatuitaki? Tugawane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba na sisi barabara ile ni ya muhimu ni ya kimkakati ile barabara itengenezwe. Jamani ikinyesha mvua dakika kumi tu, huwezi kupita ile barabara.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Maimuna, endelea na mchango wako.

MHE MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba mtuangalie kwa jicho la huruma. Kuna akinamama, kuna vitu vingi, kilimo kikubwa kule kinaendelea, lakini hatuna barabara, lami hatuijui kule kwetu. Watu wanazaliwa mpaka wanakufa. Tunaomba watusaidie tuwekewe lami barabara ile, kila siku tunapigwa danadana na maelekezo, lakini ilani haitekelezeki, ni kwa nini hii huku tu? Tunaomba watusaidie barabara itengenezwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna migogoro ya wafugaji na wakulima. Hali ni mbaya, kuna watu wanauawa, tuna uhakika na tuna uthibitisho watu wameuawa na wafugaji. Tunaomba watusaidie, hali ni mbaya ni mbaya sana, kwa hiyo hakuna amani, hakujatulia watusaidie wenzao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaomba malambo kwa ajili ya mifugo, Mheshimiwa Dkt. Samia, aliahidi yafufuliwe yatengenezwe tunaomba tusaidiwe kwa Mkoa wa Lindi, hakuna kabisa malambo hali ni mbaya. Pia tunaomba na scheme za umwagiliaji kwa sababu kilimo cha sasa hivi mvua haziaminiki. Mabadiliko ya hali ya hewa ni kila siku, tunaomba tusaidiwe tupate na scheme za umwagiliaji ili vijana wetu waweze kujiajiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mikoa ya Kusini karanga na alizeti zinastawi sana lakini wananchi wa kule wanashindwa kulima vizuri kwa sababu hawana mbegu nzuri. Tunaomba Serikali sikivu ilete mbegu na wataalam kule wa kuweza kuwaelewesha wale ndugu zetu kilimo cha karanga na alizeti. Pale Nachingwea kuna maeneo yalikuwa yanaitwa farm one mpaka farm 17, yale maeneo yalikuwa maeneo mazuri sana kwa ukulima wa karanga. Zilikuwa zinatoka karanga nzuri sana lakini sasa hivi watu wakilima hakuna, tunaomba Serikali yetu sikivu itusaidie tupate mbegu nzuri na tupate na Wagani waweze kuwaelimisha watu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru naunga mkono hoja. (Makofi)