Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Venant Daud Protas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igalula

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi kuwa mmoja wa wachangiaji katika ofisi ya Waziri Mkuu katika bajeti ya mwaka 2023/2024.

Kwanza mimi niwaombe Waheshimiwa Mawaziri, mna muda mzuri sana wa kujibu hoja za Wabunge, kwa hiyo tupunguze miongozo. Tumekuja humu kuleta kero na matatizo ya wananchi na ninyi kazi yenu ni kutatua kero na matatizo ya wananchi tunawategemea katika hilo, sasa anaposema Mbunge na nanyi mnanyanyuka mnakuwa mnatuingilia Hansard hazikai sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nianze kwa mchango wangu nategemea mimi sipati mwongozo mpaka namaliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kupongeza Serikali kwa kazi nzuri inayoifanya kwa kuwahakikishia wananchi kuwaletea maendelea. Leo tunapozungumza hapa ukiangalia Serikali zote zilizo pita Serikali ya Awamu ya Sita imevunja rekodi kwa kuleta maendeleo chapu chapu; na sisi viongozi au Wabunge wapya tulioingia mwaka huu tumepata mserereko mkubwa sana, kwa sababu kila kitu tulichokisema kimekwenda. Uiangalia jimbo langu ahadi zote tumemaliza isipokuwa kuna ahadi chache chache tu, na hizo ahadi itabidi niziseme leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kupongeza Serikali, kwanza mimi nishukuru Serikali, tuna mradi mkubwa wa SGR ambapo takriban asilimia 70 au 80 ya Mradi wa Makotopora - Tabora umepita Jimbo la Igalula; hapa ninaombi kidogo kwa Mheshimiwa Waziri Mbalawa. Kuna wananchi ambao reli imewafuata na kuna wanachi ambao wameifuata. Mimi nikuombe, wale wananchi ambao waliifuata reli, wakazi wa kata ya Nsololo na mmoja ambaye ana athirika kwa kubomolewa nyumba yake anataka asilipwe alikuwa mgombea mwenzangu, wa Ubunge wa ACT. Kwa kuwa Mheshimiwa Rais ameweka maridhiano, mimi naomba, kwa sababu wale watu walijenga zaidi ya miaka 20,30 iliyopita basi muwafikirie kuwalipa hata fidia kidogo, basi msiwabomolee na kuwaacha hivyo hivyo. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri Mbalawa katika bajeti hii hao wananchi 20 ambao hawajaingizwa kwenye fidia naomba waingizwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesema hapa Mheshimiwa Rais amefanya kazi nzuri na yenye mfano katika vipindi vyote vya marais. Na mimi nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu; anazunguka nchi hii kwenda kuwatia matumaini wananchi kwa kile kinachofanywa na Serikali; na Mheshimiwa Waziri Mkuu inawezekana kuna muda unapiga kazi mpaka watu wanakuhisi hisi mimi nikuhakikishie piga kazi na sisi kama wawakilishi wa wananchi tuko nyuma yako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sisi wawakilishi wa wananchi; ndio hicho nilichosema wananchi mnatakiwa mtujibu hoja, tunapokuja humu tunawaambia Mawaziri kuna changamoto katika majimbo yetu, Waziri anakuahidi tunakwenda jimboni kwa lengo la kwenda kutatua kero na sio kuongeza kero nyingine. Hii lazima tuikemee. Kumekuwa na Waziri tunakwenda nao kwenye majimbo wanakwenda kutuletea matatizo badala ya kutatua matatizo. Wanakwenda kuahidi vitu ambavyo haviwezi kutekelezeka, mnatuachia kero.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mimi nina ahadi za tangu Mbunge Mfutakamba Jimbo la Igalula hamjapeleka, akaja Musa Ntimizi hamjapeleka, nimekuja mimi mmenipiga fiksi tena, nimekaribia kumaliza muda wangu hamtapeleka. Mimi niwaombe kama kitu hakiwezekani tusiwalaghai wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema hivi kwa sababu Mheshimiwa Jafo alikwenda mwaka 2019 katika Kata ya Igalula akawaambia wananchi; yaani mimi nikienda tu Dar es Salaam hii wodi yenu nitaimaliza nitaleta shilingi milioni 80, mpaka leo milioni 80 haijaenda; mpaka Jafo amehama Wizara sijui nane sijui ngapi, mpaka leo. Sasa wa kumdai ni nani? Ni akina nani wanao ratibu ahadi za viongozi? Sasa ninyi mnakwenda na msafara mkubwa halafu hamfanyi chochote; sasa mna maana gani ya Kwenda? Mheshimiwa Waziri Mkuu nimekusifia hapa lakini na wewe uliacha deni huko. Kuna shilingi milioni 80 katika Kijiji cha Imalakaseko, ulikwenda na jiwe lako la kumbukumbu liko pale, haijaenda tangu mwaka 2017. Ulikuja na msafara, una Katibu na nani, Dereva, nani mpaka leo haijaenda; sasa walienda kufanya nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunaomba ili tuwape hadhi viongozi wetu wa kitaifa wanapokuja kwenye majimbo yetu msituletee matatizo mengine. Sasa wanakuja kutuambia wewe Mbunge tulikwambia upeleke kero yetu.

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. VENANT D. PROTAS: Nani tena huyo?

MWENYEKITI: Mheshimiwa Venance kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Maganga.

T A A R I F A

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nataka nimpe taarifa Mheshimiwa, kwamba mchango wake ni mzuri sana, kweli anaongea vya ukweli kabisa. Ni kweli, unaweza ukapata wageni lakini baadaye wakakuletea matatizo makubwa. Kwa hiyo naomba Serikali ichukue mchango wake maana yapo majimbo mengi viongozi wakiwemo mawaziri wameingia kwenye majimbo yetu na kutuachia ahadi na hazitekelezeki.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Maganga, ahsante. Mheshimiwa Venant taarifa unaipokea?

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ninaipokea, ndiyo haya matatizo ambayo tunayazungumza. Halafu mbaya zaidi mnampiga fiksi mpaka kiongozi wa Kitaifa. Mheshimiwa Rais alikuja ziara mwaka jana katika Mkoa wetu wa Tabora, alisimama katika Kata ya Kigwa. Mimi mwakilishi wao nikamwambia Mheshimiwa Rais tuna changamoto ya umaliziaji wa maji ya Ziwa Victoria katika kata ya Gowekwe, Igalula na Nsololo na Kigwa akamsimamisha Mheshimiwa Waziri wa Maji. Waziri akaniambia Mheshimiwa Rais hilo limeisha, mwezi wa 12 Maji watayapata hapa; mpaka leo hata dalili hakuna. Sasa wananchi wanachanganyikiwa sasa mpaka Rais anapigwa fiksi sasa sisi ni akina nani, sasa Mwenyekiti…

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Athuman Almas Maige.

T A A R I F A

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, hili analoliongelea pacha wangu wa Igalula nami nililiongelea. Marais watatu wana ahadi ya kituo cha afya Uyuwi, Tabora Kaskazini, mpaka leo mwaka wa tano.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Venant, taariifa hiyo unaipokea.

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea hiyo taarifa. Kwa hiyo CAG anapokagua fedha kupotea hata hizi ahadi akague. Awakague viongozi ambao wanachimba mashimo kwa wananchi ili sasa tuwe na Serikali ambayo ni yenye matumaini kwa wananchi na si Serikali yenye mashaka kwa wananchi. Kwa hiyo mimi nilitaka nichangie katika hoja hiyo ahadi za viongozi zifuatiliwe.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Venant, ahsante muda wako umeisha.

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kengele ya kwanza, au imeisha hiyo?

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umeisha.

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, haya, naunga mkono hoja.(Makofi)