Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Shamsi Vuai Nahodha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. SHAMSI VUAI NAHODHA: Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kuchukua nafasi hii kukushukuru sana kwa kunipa fursa hii adhimu kutoa mchango wangu kuhusu bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, Mwandishi mmoja Tanzania anaitwa Ndugu Godius Rweyongeza, aliandika katika Kitabu chake cha Rasilimali, tatizo si rasilimali fedha zinazopotea bali tatizo ni rasilimali watu tunazozipoteza. Maneno haya yamenifanya nitafakari sana kwa makini kuhusu ripoti za kila mwaka zinazowasilishwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Katika ripoti hizo, mtakubaliana nami makosa yaleyale yanajirudia na pengine yanajirudia kwa sababu hakuna hatua madhubuti zinazochukuliwa.

Mheshimiwa Spika, kwa mawazo yangu kuna matatizo manne makubwa ya msingi na nitayataja ambayo Bunge lako tukufu linapaswa kuyasimamia na kuyafanyia kazi.

Kwanza, nchi yetu haina utaratibu mzuri wa kuandaa Viongozi wake. Mara nyingi watu wa kawaida tu bila ya kupewa mafunzo na maandalizi ya kutosha ya uongozi wanapewa dhamana ya uongozi, halafu matokeo yake tunalalamika Viongozi wanakosa maadili hawana uadilifu, hawana maadili ya uongozi kana kwamba maadili ya uongozi, uadilifu na uzalendo ni vitu tu ambavyo vinakuja bila maandalizi tunazaliwa navyo, hapana!(Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo linalonisikitisha sana, tunapotafuta Wahasibu kwa mfano, tunatafuta watu ambao wana weledi, wana mafunzo ya kutosha, lakini watu ambao tunawapa dhamana wakisimamia Fedha za Taifa, rasilimali, mitaji, rasilimali watu hatuwapi mafunzo yanayohitajika. Kuna wakati Marehemu Baba wa Taifa alianzisha vyuo kwa ajili ya shughuli hiyo ya kuwatayarisha Viongozi wa Taifa hili. Kwa mfano, tulikuwa na Taasisi ya Uongozi ya Mzumbe, taasisi ambayo ilifanya kazi kubwa sana ya kuandaa viongozi mahiri, wenye weledi, wenye maadili, wenye uzalendo na mfano mzuri Hayati Moringe Sokoine, Mzee wetu alikuwa ni mhitimu wa Chuo hiki. Rais wetu wa sasa Madam Samia Suluhu Hassan, Madam Anna Makinda, hawa ni viongozi wanaotokana na chuo hiki. Tunaweza kujua kwa kiasi gani Chuo hiki kilitoa mchango mkubwa sana wa uongozi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile tulikuwa na Chuo cha Kigamboni ambacho kilikuwa kimefanya kazi kubwa sana ya kuanda viongozi wa nchi hii, kwa bahati mbaya sana viongozi waliokuja baada ya Mwalimu Nyerere wamevifuta vyuo hivyo na vyuo hivyo sasa vimefanywa kuwa Vyuo Vikuu vinavyofundisha masomo ya kawaida. Ushauri wangu kwa Serikali, ninaiomba sana Serikali itafakari juu ya jambo hili la kuanzisha tena au kurudisha tena Vyuo vya Uongozi. Bila kuwatayarisha viongozi wetu hatuwezi kuwa na viongozi wenye ueledi, wenye uzalendo na wenye maadili.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo nadhani linachangia katika kuwa na ripoti zisizoridhisha za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Wizara ya Elimu kila mwaka inatoa fedha kwa ajili ya kuwapatia mikopo wanafunzi wanaohitaji elimu ya Chuo Kikuu, kwa bahati mbaya sana wanafunzi hawa wanapewa elimu ambayo haiwasaidii kuwaajiri wala kuajiriwa. Unamkuta mwanafunzi ambae kwa mfano, amemaliza Shahada ya Utawala, amemaliza Shahada ya Utawala anakosa kazi, baadae badala ya kufanya shughuli ya maana utakuta sasa amejielekeza anatafuta ajira kwenye shughuli za utalii, ama anatafuta ajira kwenye shughuli za udereva. Sasa mimi nimekuwa nikijiuliza je, kama Taifa tunadhani haya ni matumizi sahihi ya rasilimali? Badala ya kufanya utafiti tukaangalia kwamba vijana wetu wanahitaji ujuzi wa aina gani tukawapa mafunzo ambayo yataweza kusaidia kujiajiri na kuajiriwa, tunawapa masomo tu ya nadharia ambayo hayawasaidii.

Mheshimiwa Spika, sasa ushauri wangu. Kwa nini Seriakli haifanyi utafiti ikabaini inahitaji watumishi wa idadi gani na ikawapa mafunzo wanafunzi ambao inaweza kuwaajiri na
waliobaki ikawapeleka katika Vyuo vya VETA wakapatiwa mafunzo ya ufundi. Wengine tukawapeleka katika mafunzo ya utalii na ukarimu. Wengine tukawapeleka katika Vyuo vya Sanaa wakajifunza masuala ya utengenezaji filamu na muziki, mambo ambayo yanasaidia sana vijana wengi katika sehemu mbalimbali duniani.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, wenzetu wa India, wenzetu wa Nigeria wenzetu wa Uingereza, wanatengeneza fedha nyingi sana kupitia vijana wao ambao wamepatiwa mafunzo ya kutosha katika sekta ya utengenezaji filamu na muziki. Kwa nini Watanzania hatufanyi jambo hilo?

Mheshimiwa Spika, nikimuangalia kijana wetu Diamond huwa ninasikitika sana, amefikia mahali amejifunza mwenyewe ujuzi wa kutengeneza muziki, sasa vijana kama Diamond hapa Tanzania wako wangapi? Diamond ana uwezo hata wa kumuajiri Daktari, ama kumuajiri Profesa! Kwa nini Serikali yetu haiviimarishi hivi vyuo ambavyo vinatengeneza filamu, vinatengeneza muziki ili tukapata Diamond kama 1,000 hivi na hao watakuwa na mchango mkubwa sana wa Taifa lao.

Mheshimiwa Spika, tatu; hakuna jambo ambalo linanisikitisha sana kama kuona kwamba kazi ya kuwalea vijana wa Taifa letu siku hizi tumeikabidhi kwa dada wa kazi. Zamani tuliozaliwa zamani kidogo, tulilelewa na babu zetu, tulilelewa na bibi zetu na kwa maana hiyo tulifunzwa maadili, tulifunzwa tabia njema, tulifunzwa uzalendo, tulifunzwa heshima kwa watu. Leo tunalalamika kwamba vijana wetu wanakosa maadili lakini tunajiuliza wanalelewa na nani. Unakwenda kwenye kijiji unamchukua dada wa kazi, humjui ana maadili gani, unampa dhamana ya kukulelea watoto wako halafu tunalalamika vijana wetu hawana maadili, hawana uzalendo, hivyo Waheshimiwa Wabunge na Viongozi maadili hayo na uzalendo wao utatokea wapi? (Makofi)

Mhehsimiwa Spika, maoni yangu nafikiri umefika wakati viongozi tujiulize, kwa nini wazazi wa zamani waliweza kuzalisha na kuwalea viongozi kama Marehemu Baba wa Taifa, Edward Moringe Sokoine, Mama Samia Suluhu Hassan na hata sisi! Lakini wengi wetu ambao tunasema tumesoma sana kinyume na wazee wetu ambao hawakusoma, hawajui hata kusoma na kuandika, lakini tunashindwa kutoa vijana ambao wana maadili mema, vijana ambao wana maandalizi ya kutosha, vijana ambao wana sifa za kuwa viongozi.

Mheshimiwa Spika, wala tusimtafute mchawi, tumelalamika hapa kuna mjadala tu toka juzi unaendelea hapa kwamba vijana maadili ya Kitanzania yanaharibika, lakini tumekaa chini tukajiuliza kwanini madili haya yanaharibika? Mimi nafikiri tusimtafute mchawi. Ni kosa letu wenyewe kama wazazi na walezi na kwa maana hiyo basi tubadilike, tubadilishe utaratibu wetu wa malezi, badala ya malezi kuwaachia Dada wa kazi imefika wakati sasa tusimamie malezi hayo sisi kama wazazi, walezi na viongozi. Tukifanya hivyo basi tutapata vijana, wenye maandalizi mema kwa ajili ya kulitumikia Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa niseme...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Dakika moja, kengele ilishagonga Mheshimiwa.

MHE. SHAMSI VUAI NAHODHA: Mheshimiwa Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Bajeti ya Bunge lako Tukufu, katika Kamati yetu tumebaini kwamba taasisi nyingi za Serikali zina mifumo ya kukusanya mapato iliyo dhaifu na ambayo haiwezi kuwasiliana, jambo hili limekuwa likichangia sana katika upotevu wa mapato ya Serikali. Kwa maana hiyo basi tunaishauri Serikali ifanye kila linalowezekana mifumo hii ya kukusanya mapato iimarishwe, iunganishwe ili iweze kuwasiliana ili kudhibiti vitendo mbalimbali vya ubadhilifu.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya nakushukuru kwa kunipa fursa hii.(Makofi)