Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kipekee namshukuru Mungu kwa muda huu na afya ya kuniwezesha mimi nisimame hapa niweze kuchangia hii hotuba ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuunga hoja mkono na niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge wenzangu wapitishe hii bajeti ya Waziri Mkuu ya shilingi 173,733,110,000 pamoja na ule Mfuko wa Bunge iliyoombwa shilingi 165,627,897,000.

Mheshimiwa Spika, nimeanzia hapo ka sababu ni dhahiri kabisa charity starts from home, sisi tuko hapa kwenye Fungu hili. Baada ya kuwaomba wenzangu na najua itapita bila pingamizi. Nianze sasa kuchangia hotuba ya kurasa 95 ambayo ilimsimamisha Waziri wetu Mkuu takribani masaa mawili akiisoma kwa umahiri mkubwa na baadae tukaenda Pasaka na kuweza kuizungumza huko na wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, wanawake wa Kilimanjaro wamenituma haya yafuatayo: -

Moja, kuhusu nishati safi na salama ya kupikia.

Mheshimiwa Spika, wanawake wamekuwa wakipika wakilia, wakitoka machozi kwa ajili ya moshi, pamoja na hayo katika kukata miti ili ipatikane kuni au mkaa tumeendelea kuharibu mazingira, tabianchi nayo imekuwa ni tatizo. Namuomba Waziri Mkuu atueleze baada ya ule ufunguzi alioufanya Rais wetu Tarehe 01 mwezi Novemba pale katika ule Ukumbi wa Julius Nyerere ni takribani au ni almost miezi Sita, hatujaona jambo lolote.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kushukuru kampuni ya Oryx ambayo imeendelea kutoa mafunzo, tumeona wakigusa kaya mablimbali. Kilimanjaro waliweza kugusa kaya 700, huko Mwanza wakagusa kaya 700 labda na kwingineko kule ambako hatujapata taarifa. Sasa ni lini Serikali hii itatuambia hatua zinazoendelea ili sasa tuweze kuachana na shida hizi za nishati hiyo mbovu.

Mheshimiwa Spika, majirani zetu wameweza kupunguza kodi katika eneo hili ili nishati hii safi na salama iwe affordable, tumeona sasa hivi hakuna watu wanaokoka koka moto tena huko baadhi ya majirani zetu. Tunataka hii ifikiwe kwa sababu hata Ulaya walianza hivyo hivyo kupekicha moto wakawa wanapika kwa kuni. Sasa hivi ukienda unaoneshwa kama museum. Niliona kule Denmark. Sasa sisi tunataka kuachana na hiyo tunaomba sana Serikali itujibu kwa kina ni jinsi gani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hilo niende kwenye Wizara ya Mifugo, nimekuwepo hapa kwa kipindi sasa kama vipindi viwili na hiki cha tatu. Nikiomba Wizara ya Mifugo tusiende tu kuhesabu Mitamba iliyopo kwenye ranchi, sijui mbuzi waliopo kwenye ranchi na vingine, halafu iweje?

Mheshimiwa Spika, hivi ni sawa Serikali ikahesabu halafu huku kuna nguvu kazi, kuna akinamama wa Kilimanjaro ambao hawana hata ng’ombe wa kufuga, hawana kuku, hawana mbuzi, wanakaa tu, na wengine wanasubiri Serikali iwawezeshe, lakini wana migomba ya kulishia, wana majani ya kulisha na kila aina ya chakula cha mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali sasa itumie hatua ile ile aliyoitumia Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuleta mitamba bora, wakati huo nchi jirani zikiwa tatu zikiitwa East Africa walipokea. Kwetu baada ya zile mbegu za awali au ile mitamba ya awali kumalizika kutoka Denmark, maziwa yakapungua, lakini tunanunua maziwa kutoka Kenya, tunanunua maziwa kutoka Uganda, tunanunua kutoka South Africa. Sasa tunakwenda wapi? Iliisha ile awamu moja, hizi awamu nyingine zinaonaje? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeona hilo niliseme. Nachukua nafasi hii kupongeza sana wale wanawake wa Uswaa, wale wanawake wa Lawati ambao ni wazalishaji maziwa. Naomba mwendelee kununua maziwa kutoka Kilimanjaro. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maziwa haya au tungepata vifaranga, ndiyo lishe bora. Juzi juzi tulikuwa na sensa ya watu na makazi, lakini taarifa zinasema kwamba bado sisi tuna udumavu, bado maeneo fulani yana viribatumbo, hiyo yote ni lishe mbovu. Endapo watu wetu wangeweza wakazalisha chakula kizuri, wakazalisha mayai, kila mtoto akala yai moja asubuhi kabla hajaenda shule, hivi vitu vinavyozungumzwa visingekuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wanawake wa Kilimanjaro wamefaidika kwa ile asilimia 10 (4:4:2) na wanaomba sasa kilichowafanya wakakimbilia sana ni ile kutokuwa na asilimia ya riba. Waliokuwa wamejikusanya kwenye vikoba vyao ikiwa kama njia moja ya kujikomboa walienda wakaweza kukopeshwa kidogo kidogo. Ni kweli kuna changamoto, lakini hapo tunapoenda kurekebisha bado wanaomba ile riba isiwepo, hilo ni ombi lao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mafuta ya kula yamekuwa ni tatizo katika nchi hii. Kamati ya Bajeti tuliwahi kutembelea bandarini tukaona ma-container kwa ma-container ya mafuta ya kula yakitoka nje. Siku za nyuma Manyara walikuwa wanalima alizeti, Arusha walikuwa wanalima alizeti, Kilimanjaro walikuwa wanalima alizeti, mpaka lilipotokea tatizo la ile kutu kwenye majani. Sasa kwenye hotuba ya Waziri Mkuu, katika mikoa ambayo itapendelewa kupelekewa kulima alizeti, hii mikoa mitatu niliyoitaja haikutajwa tena. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sasa, walioko hapa kwa ajili ya Waziri Mkuu, akiwemo huyo Katibu Mkuu na timu yake, waone kama lilitokea tatizo mahali, kule lilikotokea lirekebishwe na huko kupya pia kuendelezwe. Mafuta ya alizeti ni mafuta safi na salama na ni rahisi kulima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapo hapo kwenye Wizara ya Kilimo wamenituma nihoji, hivi hao waliopatiwa block farms wamechaguliwa vipi? Mbona hawawaoni wana-Kilimanjaro waliopatiwa hizo block farms? Labda na mikoa mingine pia inajiuliza, watu wetu mbona hawakupatiwa? Kwa hiyo, naomba itolewe elimu ili watu wajue, hawa wanaopelekwa kwenye block farms wamepatikana vipi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wale wanaokwenda jeshini tunajua, wakimaliza form six kuna wanaokwenda, lakini wale wengine wa darasa la saba wanapitishwa kwa Mkuu wa Mkoa, wanakwenda, Kamati zinakaa wanapatikana. Sasa swali linakuja, hawa wa block farms wamepatikana vipi? Tunaomba sana tujue ni jinsi gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna mazao yenye thamani kubwa ikiwepo kahawa. Hapa tunaambiwa TaKRI inatoa mbegu kirahisi, bure actually, lakini mbegu hizo hatuzioni sasa zikileta impact kwenye kukuza mapato ya zao la kahawa. Tumeona, ukisema zao la kahawa limeongezeka Kilimanjaro ni zile estates, yaani yale mashamba makubwa ya wageni ambayo wamekodishiwa, lakini ukienda kwenye shamba moja moja la mkulima wa Kilimanjaro ni hoi bin taabani, hakuna kahawa. Nami hapa naomba sana Wizara ya Kilimo, pamoja na kugawa pikipiki kwa wagani na kadhalika, wapite sasa kwenye yale mashamba moja moja, sisi tunaita vihamba; waanzie huko Moshi, waende Same, waende Mwanga, waende Rombo, waende kote Kilimanjaro tuone wamesaidikaje katika kutumia vitu hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nawaomba hawa wa kilimo waweze kutoa elimu kwa drip irrigation, yaani ile ya matone, ndiyo rahisi na pia inatumia maji kidogo. Tuking’ang’ania tu furrow irrigation, ile ya mifereji, hatuna tena mifereji inayotiririsha maji kwa wingi. Kamati Wizara ya Kilimo itatusaidia tukawa na mahali pamoja pa chanzo cha maji, tukaweza kupata hiyo drip irrigation itasaidia mashamba yote.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa pia nataka kuwaomba ili waweze kutenga eneo kama pale KIA kwa ajili ya kongani za biashara. Watu ni wengi Kilimanjaro kutokana na sensa, lakini lile eneo pale KIA likitumika kwa Arusha, kwa Kilimanjaro yenyewe, wakawa na vile viwanda vidogo, vinaweza kutoa ajira kwa wengi kwa sababu wameweza sana kuwaelimisha watu. Kwa hapa naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu alivyoona VETA hizi zijengwe kila Wilaya na sasa zinajengwa, nami nashukuru kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme wazi, katika jambo ambalo linawafanya mabinti wapende kwenda shule, wanajua watakwenda sasa kutoka Standard One mpaka Form Six. Hili ni jambo la Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Wasome bure; na binti ambaye anadanganywa akaolewe kabla ya umri asikubali. Hizo ndoa za utotoni wewe binti unaweza kusema hapana, kimbilia kwenye maeneo ambayo yanataka vijana wasome, wakomae. Usiende ukabeba ujauzito wakati ambapo viungo vyako havijawa tayari.

Mheshimiwa Spika, wamesema waliotangulia kwamba kwa sasa hivi wanapata ile hali ya kukua (maturity) kwenye miaka tisa. Sasa fikiria mtoto wa miaka tisa anakwenda kulea nyumba, haiwezekani. Nawaomba sana vijana mwende shule, mtulie darasani, msome kwa makini mpaka mfikie hiyo level ambayo Serikali yenu imejitolea na imewapa baraka mpaka Form Six. Ajali inaweza ikatokea njiani, lakini ajali ikitokea njiani pia wasichana wamepata tena chance nyingine ya kwenda kuingia shuleni kwa kufikiriwa hii ajali ilitokeaje.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwaombe sana mabinti wetu na niwaase, hakuna jambo zuri kama shule na elimu haina mwisho. Hata mkiona hapa, kama mimi mama yenu nimesimama hapa na mpaka sasa niko darasani, ukiniuliza nasoma nini? Napenda nifahamu zaidi, hakuna mwisho wa shule. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimesema hivyo na nikakumbuka, ninatumwa kila wakati salamu zako na hata leo asubuhi. Nadhani wanaonituma wamefurahi sana kwamba, umetuliza hali ya hewa. Wanasema kiambie kile kichwa kinachokalia kiti pale Bungeni, sisi tunamwelewa sana. Kijana wa boda aliyenipa usafiri leo ameniambia, amesikia kuna watu wanakuchokoza huko Mbeya, wako tayari kutoka Dodoma kwenda kunyamazisha hiyo hali ya hewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nisingesema hili kesho akinichukua angeniambia. Mama una uhuru wa kusema, kwa nini hukututolea salamu?

Mheshimiwa Spika, pokea salamu zako, Watanzania wanakuelewa, ukizungumza wanakusikiliza. Naomba tu kwa wale wote waliopata nafasi, ambao ni jenda ya Ke, mwendelee kama hivyo. Tunawaelewa wote; Mawaziri wetu tunawaelewa, viongozi wetu ma-RAS, Wakurugenzi, Wakuu wa Wilaya, tunaomba sana tuendelee na mwendelee kumsaidia Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kuona kwamba, jambo hili jema linakwenda na kila kitu kinaenda kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, nilikuwa naomba tu, leo...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Kengele imegonga Mheshimiwa. Sekunde 30.

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, nimeona ajira zilizotoka, elimu itolewe kwamba Mbunge hawezi kwenda kuomba ajira kwa maandishi. Naomba mwaelezee, ahsante.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)