Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Miraji Jumanne Mtaturu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hoja ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ambayo iko Mezani kwa ajili ya Bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024.

Mheshimiwa Spika, nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa taarifa aliyotusomea hapa Bungeni, taarifa ambayo imesheheni mipango mizuri ya Serikali kwa mwaka wa fedha unaokuja. Ninaamini kabisa mipango hii ambayo imeelezwa hapa ikitekelezwa vizuri tutakwenda kubadilisha kabisa maisha ya Watanzania na kuweza kusogeza mbele gurudumu la maendeleo, ikiwemo utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo tuliahidi tutakwenda kuleta maendeleo kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla sijakwenda kuchangia hoja ambayo iko Mezani, nianze kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya kwa ajili ya Watanzania. Kazi kubwa anayoifanya katika muda wa mwaka wa fedha huu tunaomaliza sisi watu wa Singida Mashariki kwa maana ya Wilaya ya Ikungi, tumeona fedha nyingi zimeshuka katika halmashauri yetu. Na hii haijawaki kutokea, tumeweza kupata fedha nje ya bajeti iliyopangwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi tulipokea zaidi ya bilioni 12 katika muda wa mwaka huu wa fedha. Imetekeleza miradi mingi sana. Miradi ambayo hatutaisahau ni miradi ya barabara. Barabara zetu ndiyo uhai wa wananchi wetu katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Spika, barabara zaidi ya kilometa 157 ambazo zilikuwa hazipitiki kabisa zimetengenezwa na kuimarishwa ikiwemo kuwekwa madaraja. Kwetu sisi tuliona tusiposema haya tutakuwa hatumtendei haki na tutakuwa hatuitendei haki Serikali yetu. Tunashukuru sana kwa namna ambavyo Rais ametuletea fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye eneo la barabara kwa mara ya kwanza tunakwenda kupata barabara za lami katika Mji wetu wa Ikungi. Tumepata kilometa mbili ambazo zinaendelea kujengwa na wakandarasi na kuna mpango wa kuweka taa za barabarani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaamini kabisa Mji wa Ikungi sasa utakwenda kuwa na mwanga katika saa za usiku na itasaidia hata wafanyabiashara wadogowadogo kufanya shughuli zao hata kipindi cha usiku kuweza kuhudumia watu wanaopita katika eneo hili. Kwenye hili tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais na tunaendelea kumuombea kila la heri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na kama haitoshi, kwenye eneo la elimu tumeeleza sana, lakini tumepata zaidi ya madarasa 109 ambayo yameweza kutumika, na ni zaidi ya bilioni nne na milioni 900 imetumika. Kwetu sisi ni mabadiliko makubwa sana ya kimaendeleo na tunaamini kwamba tutakwenda kuboresha elimu ya watoto wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tutaeleza mengi, lakini tutaeleza upande wa REA; REA imeendelea kusambaza umeme katika maeneo yetu. Tarafa ya Mungaa ambayo nilikuwa nailalamikia leo kila kijiji kimepelekewa nguzo. Tunategemea ndani ya muda mfupi vijiji vyote vitakuwa vimepata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye hili niendelee kuomba, kama ambavyo tumeambiwa REA hii Awamu ya Tatu itakwenda kupeleka kwenye vitongoji, basi kuna vitongoji ambavyo havijapata umeme. Tuweze kuangalia katika bajeti hii inayokuja. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa maeneo yote hayo, sina haja ya kurudia yote, lakini tunasema tunashukuru, na waungwana wanasema kushukuru ni kuomba tena. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo nianze sasa kuchangia bajeti ambayo iko mbele yetu ya Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, na ameeleza zaidi katika eneo la barabara kuu ambazo zinaunganisha mikoa yetu.

Mheshimiwa Spika, sisi watu wa Singida bado tuna changamoto ya kuunganisha barabara katika mkoa. Tunayo changamoto ya kutoka Tanga kuja Singida, lakini bado tuna changamoto ya kutoka pale Mkiwa (Itigi) mpaka kwenda kule Mbeya. Tunayo maeneo hayo mawili bado hatujaunganishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini tunayo furaha kwamba tuliwekwa kwenye bajeti inayoisha mwaka huu tuliambiwa tutajengewa kilometa 2,100. Barabara zilizotajwa ni pamoja na Mkiwa – Itigi – Makongorosi – Mbeya. Barabara hii bado hatujapata mkandarasi. Lakini bado kuna barabara ya Singida – Kwamtoro kwenda mpaka kule Kibrashi, Tanga, bado hatujaanza ujenzi wa barabara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, barabara hizi zitakapokamilika zitakwenda kuongeza uchumi wa wananchi wetu, zitakwenda kuongeza thamani ya miradi ambayo tunaitengeneza. Mfano barabara hii ya Tanga kutoka Handeni kuja mpaka Singida itakwenda kuihuisha Bandari ya Tanga ambayo tumewekeza fedha nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninaomba sana tuhakikishe kwamba barabara hii mkandarasi anaingia. Tuliambiwa tutatumia mfumo wa EPC+F, mpaka leo tunavyoongea wako kwenye negotiation, hawajamaliza hatua za manunuzi. Wamalize mchakato wananchi wanasubiri barabara hizi kwa hamu kwa sababu Serikali ilishawaahidi katika mwaka wa fedha tunaokwenda kuumaliza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye eneo hili la watumishi, na nieleze la watumishi kwa maana nilikuwa nalenga kwenye fedha zinazoletwa. Tunaomba sana wananchi kwa maana ya wale waliopata nafasi ya kuwa watumishi wa Umma waitendee haki nchi. Fedha zinaletwa nyingi katika maeneo yetu; wawe wazalendo ili fedha hizi ziwe na thamani. Kwa sababu kabla hujaamua kufanya ufisadi kwenye miradi hakikisha wewe kijiji unachotoka kimemaliza matatizo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tungekuwa tunaangalia umaskini uliopo kwenye vijiji vyetu tunapotoka ninaamini hakuna mtumishi wa Umma ambaye angefuja fedha za Serikali. Niwaombe sana tuwe wazalendo, tuitendee haki nchi yetu kuhakikisha kwamba tunakwenda vizuri katika kujenga Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye eneo la ajira pamoja na wastaafu; naishukuru sana Serikali, tumefanya kazi nzuri ya kuendelea kuajiri, na tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. Na juzi hapa tumetangaziwa tena ajira nyingine 21,000. Ni jambo zuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo hili ninataka niombe; tumekuwa na wahitimu wa mwaka 2015, 2016 mpaka 2020, tumekuwa tukitangaza nafasi hawapati. Watu hawa wameshakaa mtaani vya kutosha. Zimetangazwa hizi ajira za sasa hivi, tunaomba sana wapewe kipaumbele, waweze kuajiriwa ili wasiondoke kwenye muda ule wa utumishi.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu wakicheleweshwa leo katika miaka mitano ijayo watakuwa hawaajiriki na itakuwa haina sababu ya kuwasomesha kwa fedha nyingi. Na wengine wamekopa kwenye mfuko wa elimu ya juu, maana yake watashindwa kulipa fedha hizi. Eneo hili tukifanya vizuri tutakuwa tumewatendea haki vijana wetu ambao wanatafuta ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye eneo hili la wastaafu ninataka niunganishe; tumekuwa na malalamiko ya baadhi ya wastaafu. Wanalalamika wanapomaliza utumishi wao wamefanya kazi nzuri lakini wengine wamekuwa wakilalamika hawalipwi fedha zao kwa wakati. Hili eneo limekuwa likilalamikiwa na sisi Wabunge tumekuwa tukipata malalamiko hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna mzee wangu mmoja ambaye barua yake ninayo hapa, ameniletea kama Mbunge wake. Anaitwa Simon Alberto Makia, ni mzee wangu kutoka pale Siuyu, Singida. Niombe sana nitaikabidhi hii barua yake, amekuwa akilalamika anasubiri kupewa fedha zake ambazo amestaafu.

Mheshimiwa Spika, leo hii tunavyoongea amekuwa akija mpaka Bungeni hapa nje akifanya juhudi za kumuona Mheshimiwa Waziri aweze kumwambia kilio chake. Nitaomba sana kama Mbunge wake nikabidhi na ninaomba sana wa aina hii waweze kutendewa haki kwani wamefanya kazi nzuri katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nimalizie kwenye eneo la utawala, lakini kabla ya eneo hilo, niishukuru sana Serikali kwa kutupatia chakula cha kupunguza makali cha bei nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, chakula mwaka huu kimetusaidia sana watu wa Ikungi, tumeweza kupunguziwa makali ya njaa ambayo ilikuwepo. Hatukuvuna vizuri msimu uliopita lakini toka mwezi Novemba tumekuwa tukiletewa chakula cha bei nafuu. Wananchi wetu wamefarijika, wanaishukuru Serikali na wanamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa upendo wake na huruma yake. Ninaamini kabisa mwaka huu hali ni nzuri, tumeona mazao na huenda Mungu akajalia tukavuna vizuri. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais pamoja na Serikali.

Mheshimiwa Spika, nimalizie eneo la utawala; sisi Wilaya ya Ikungi tunayo majimbo mawili ya kiutawala lakini majimbo haya yamepewa majina ambayo ukiangalia haraka haraka ukimtajia mtu hajui kwanza jimbo liko wapi. Ninaamini kabisa sisi hatuombi eneo jipya tunachoomba ni jina tu libadilike. Tunayo Singida Mashariki na Singida Magharibi; ombi letu, na kwenye RCC tulishaleta, tunaomba tupate majina halisi ya maeneo husika. Kwa mfano tukipewa jina laJimbo la Ikungi angalau linaweza kuleta maana nzuri.

Mheshimiwa Spika, lakini ukiletewa Jimbo la Puma au Jimbo la Sepuka maana yake unakuwa umeshaweka identity ya eneo husika. Ninaamini kabisa hili jambo si kubwa, na pacha wangu ananipigia makofi maana yake anakubaliana, ili tuhakikishe kwamba tunapata identity halisi ya majimbo haya na wananchi wajue Wabunge wao tunapotaja Jimbo la Ikungi, Jimbo la Sepuka maana yake ni Wabunge wanaotokana na Wilaya ya Ikungi.

Mheshimiwa Spika,baada ya maneno hayo kwa heshima kabisa ninaomba kuunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri Mkuu lakini naomba tupitishe bajeti hii ili Waziri Mkuu afanye kazi nzuri anayoendelea nayo. Naunga mkono hoja, ahsante sana.