Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Prof. Shukrani Elisha Manya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. PROF. SHUKRANI E. MANYA: Mheshimiwa Spika, nami nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia hoja ya hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwanza kabisa nipende kuipongeza Serikali kwa jinsi ilivyoandaa bajeti nzuri ambayo kweli kama itakavyokwenda kutekeleza kwa jinsi ilivyoandaliwa basi inakwenda kuleta tija na maendeleo makubwa katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, nitaongelea hoja tatu kama muda wangu utaniruhusu. Hoja ya kwanza ambayo napenda kuiongea katika Bajeti hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu ni kupongeza jitihada za Serikali katika kukuza matumizi ya lugha ya Kiswahili. Katika ukurasa wa 90 wa hotuba hii inasema kwamba; “Kiswahili kimetafsiriwa katika lugha rahisi katika vyombo vinavyo toa haki kwa maana ya Sheria ya nchi lakini pia Kiswahili kimeendela kufundishwa katika vyuo vikuu vya nje ya nchi.”

Mheshimiwa Spika, hili si jambo jepesi; na wote tunakumbuka kwamba Kiswahili kimeendelea kuwa nembo ya umoja wetu kama Watanzania lakini pia kimekuwa ndio msingi wa ustawi wetu kwa sababu sisi ni watu ambao tumetawayika sana kwa makabila na lugha zetu, lakini Kiswahili kimeweza kutuleta pamoja.

Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada hizi kubwa za Serikali mimi ninavyoangalia ni kama vile umahiri katika lugha yetu ya Kiswahili na hasa katika lugha andishi unazidi kushuka; na hii ni kwa sababu utagundua kwamba matumizi ya nahau, semi, misemo, methali katika watumiaji wa Kiswahili yanazidi kushuka.

Mheshimiwa Spika, niruhusu nitoe mfano mwepesi; ukiwaita vijana wa darasa la nne ambao tunaamini kwamba ndio wameweza kujua kusoma na kuandika halafu uwaambie hivi; ninaomba muniandikie jina la Mwenyezi Mungu Subhanahu Wa Ta’ala baadhi yao wataliandika hilo jina kwa herufi kubwa, lakini wengine wataliandika jina hilo hilo lakini kwa herufi ndogo, na sisi wote tunajua kwamba jina ambalo ni kuu kiasi hicho linapaswa kuandikwa kwa herufi kubwa na ni makosa sana katika vitabu vya dini kulishusha hadhi ukaliandika kwa herufi ndogo.

Mheshimiwa Spika, lakini msingi wa hoja yangu ni nini? Ni kwa sababu hawakujengwa kuelewa tofauti baina ya mambo haya; na sasa sisi tunataka kukipeleka Kiswahili chetu kama bidhaa kwa watu wa nje, sasa tunapelekaje Kiswahili kama bidhaa kwa watu wa nje kama sisi msingi wetu hapa ndani si mzuri?

Mheshimiwa Spika,kule kwetu Ukerewe iwapo unachochea viazi; maana viazi ni chakula kikuu kule kwetu; ukianza na moto mdogo mdogo baadae vile viazi hata ukichochea sana havitaiva kabisa. Maana yangu ni kwamba, kama msingi wa lugha ya Kiswahili utajengwa vibaya hapa chini katika shule za awali, maana yake tusitegemee maajabu huku juu.

Mheshimiwa Spika, na Waingereza walifanikiwa sana kukifanya kingereza kikawa ndiyo lugha takriban ya ulimwengu mzima. Sisi pia tunayo nafasi sasa. Yawezekana hii ndiyo nafasi yetu kama Watanzania kuifanya lugha yetu iweze kuwa ni lugha ya bara zima lakini pia iweze kuwa ni lugha ya mataifa mengine. Sisi ndio chimbuko, sisi ndio chanzo cha lugha hii ya Kiswahili. Kwa nini wenzetu majirani wafanye jitihada hatimae watupite?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi nataka kusema, kwamba tunahitaji kujenga msingi imara wa matumizi ya lugha ya Kiswahili katika ngazi zote kuanzia zile za awali; na ikiwezekana, na ikiwezekana tutumie nguvu kubwa kuwaomba wafundishaji wa Kiswahili wapigwe msasa ili watujengee watoto ambao wanaweza wakaongea kwa umahiri na wanaweza wakaandika kwa umahiri.

Mheshimiwa Spika, mchango wangu huu usichukuliwe kama mjadala wa nini lugha ya kufundisha hasa katika Vyuo Vikuu, hapana. Mimi huwa si muumini wa mjadala huu, mimi ni muumuni wa kwamba kama mazingira yanaturuhusu tuwe mahiri katika lugha ya Kiswahili ambayo ni lugha yetu ya Taifa; lakini pia tuwe mahiri katika lugha ya kingereza ambayo ni lugha ya biashara.

Mheshimiwa Spika, na unapokuwa mahiri katika matumizi ya lugha unakuwa na ujasiri. Yaani huwezi kwenda mahali umeitwa ukaongee ukatoe muhadhara, ujasiri utakuja kwa sababu ya huo umahiri. Kwa hiyo hoja yangu hapa ni kwamba, tunayo nafasi kama taifa la kubidhaisha Kiswahili chetu na kwa jinsi hiyo tuichukue kwa jitihada unganishi. Kama ni vyuo, kama ni watunga Sera, kama ni wafundishaji basi tulishughulikie jambo hili ili hatimaye na sisi tuweze kupenyeza lugha yetu kuwa lugha ya kimataifa lakini iliyojengewa msingi imara.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ningependa kulichangia ni katika ukurasa wa 29 wa Bajeti ya Waziri Mkuu. Katika ukurasa huo tunapongeza jitihada za Serikali ambazo zimeelekezwa katika kuongeza bajeti ya kilimo, kupanua eneo la umwagiliaji na kuweka ruzuku katika mbolea na upatikanaji wa mbegu bora kama mahitaji muhimu ya kufanya kilimo chetu kiweze kuwa na tija.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kuna jambo hapa ambalo huwa linasahauliwa na jambo hili ambalo linasahauliwa ni la mkulima yule mdogo mdogo. Hapa ndani ya Bunge utakuta kuna Wizara yenyewe inajinasibu na ni jambo zuri kwamba tunataka tumtue mama ndoo kichwani, jambo ambalo linapongezwa sana kwa sababu ni kweli Wizara ya Maji wamefanya jambo kubwa sana, lakini huyu mkulima mdogo nilitamani hata kama sio katika bajeti hii, tuje na slogan, tuje na usemi wa kwamba ni lini tutamtua mkulima mdogo wa nchi hii jembe la mkono?

Mheshimiwa Spika, lile jembe linafanya tu mikono inakuwa sugu, halina tija, yaani mtu analima hekari nyingi sana, anatumia muda mrefu sana na kula yake inakuwa ni ngumu na hawezi kupata maendeleo kupitia jembe hili la mkono. Kwa hiyo, mchango wangu ni kwamba kama haiwezekani katika bajeti hii, lakini tuje na Mkakati ambao utamtua mkulima mdogo wa nchi hii jembe la mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja yangu ya tatu, naamini muda wangu unaruhusu ni matumizi ya mifumo ya TEHAMA. Serikali imefanikiwa sana na hasa ilipoanzisha mfumo ule wa GEPG katika makusanyo ya fedha za Serikali. Pia lengo lingine la kuwa na mifumo hii pamoja na kurahisisha kutoa huduma, lilipaswa kuwa ni kupunguza ubadhirifu kupitia mifumo hii. Sasa katika Ukurasa wa 70 katika hotuba ya Bajeti ya Waziri Mkuu wanasema kuhusu habari za rushwa, kesi za rushwa zilizoendeshwa mwaka 2022 ni 696 na 248 ziliamuliwa na 142 walikutwa na hatia”.

Mheshimiwa Spika, sasa katika utendaji wa Serikali Afisa Masuuli yeye check yake ni yule Mkaguzi wa Ndani, lakini pia Afisa Masuuli hawezi kuamua kutoa fedha katika akaunti ya benki bila kuwa na Mhasibu. Hivi kwa nini rushwa inaendelea kutawala? Kwa nini ubadhirifu unaendelea kuwepo? Je, ni kwa sababu hatua zinazochukuliwa ni kidogo? Je, hawa watu wanatoa wapi ujasiri? Kwa nini hawana hofu? Je, hatua zinapochukuliwa zinahusisha watu watatu au idara tatu ya Afisa Masuuli mwenyewe, ya yule Mkaguzi wa Ndani na yule Mhasibu wake wote wanashirikiana katika jambo hili.

Mheshimiwa Spika, tungetamani kuiomba Serikali, mifumo ya TEHAMA inayoanzishwa iweze kuwa na lengo la makusudi la kuhakikisha kwamba kila mtu anapata mrejesho ili kudhibiti ubadhirifu wa mali ya umma.

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwamba, wakati mwingine mifumo hii ya TEHAMA inakuwa ndio sababu ya hasara kwa wananchi. Mfano mdogo kabisa, mfumo unakuwa uko down pale Bandari, kwa mfano, mtu anayetoa gari, halafu siku zikipita hasara inakuja kwa mwananchi wakati mfumo ulikuwa ni hasara ya Serikali. Hebu watusaidie mifumo iweze kuwa sababu ya kurahisisha, lakini pia kutoa huduma ambayo ni njema ambayo haimpi hasara yule ambaye ni mwananchi wa kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kusema hivyo, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)