Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Godwin Emmanuel Kunambi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nianze kuungana na Waheshimiwa Wabunge waliotangulia kumpongeza na kumshukuru Mheshimiwa Rais hasa kwa kazi kubwa anayoifanya katika kutuletea maendeleo Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya wananchi wa Mlimba tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa mambo yafuatayo: -

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Mlimba ilikuwa haina hospitali ya wilaya lakini hadi sasa ninapozungumza hospitali ya wilaya inakamilika na tunatarajia mwezi Desemba huduma ianze kutolewa. Vile vile tunamshukuru Mheshimiwa Rais katika miradi ya maji. Tuna Miradi mikubwa ya Maji pale Mlimba Mjini inayokwenda kutoa huduma katika vijiji 11 ambapo Mradi wa Mlimba una thamani ya Shilingi Bilioni 3.7, lakini pia tuna Mradi wa Mbingu - Igima ambao thamani yake ni Shilingi Bilioni 3.6. Jambo hili jambo jema kwa wananchi wa Mlimba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kubwa zaidi, wakati naingia Bungeni hapa kwa mara ya kwanza nilieleza. Changamoto ya kwanza kwa wananchi wa Mlimba ukiwauliza ni barabara, changamoto ya pili kwa wananchi wa Mrimba ukiwauliza ni barabara na changamoto ya tatu kwa wananchi wa Mlimba ni barabara. Mheshimiwa Rais amesikia kilio cha wananchi wa Mlimba na kwa dhati kabisa namshukuru. Leo hii tunapozungumza Mheshimiwa Rais amekwishatoa kibali cha ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami inayoitwa Morogoro – Njombe Border yenye urefu wa kilomita takribani 222. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa awamu hii ya kwanza barabara hii itaanza kujengwa kilometa 100 kwa route mbili, route ya kwanza ni kutoka Ifakara mpaka Mbingu kilometa 67.5 na route ya pili ni kutoka Mbingu mpaka Chita pale Kambi ya Jeshi kilometa 37.5 na hiyo itahitimisha kilometa 100.

Mheshimiwa Spika, awamu ya pili kwa kilomita zilizobaki, Mheshimiwa Rais amepata kupitia mahusiano aliyojenga na Taifa letu na mataifa mengine hasa na taasisi za kifedha duniani. Benki ya Maendeleo ya Afrika imeridhia kufanya usanifu wa mradi wa barabara kipande kilichobaki cha kilomita 122 kutoka Kihansi mpaka pale Madeke, kwa maana ya upande wa Njombe. Katika hili tuna kila sababu ya kujivunia Mheshimiwa Rais na sisi Wanamlimba tunamwahidi ifikapo 2025 tutampa kura zote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nijielekeze kwenye eneo lingine, eneo la elimu na hasa leo hii nitazungumzia suala la elimu ya ufundi. Hapo nyuma elimu ya ufundi ilikuwa inatolea katika taasisi tatu. Taasisi ya kwanza ilikuwa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia, tulikuwa na Vyuo kama Dar es Salaam Institute ot Science and Technology kwa maana ya (DIT), tulikuwa na taasisi pia ya Elimu ya Sayansi na Teknolojia kule Mbeya (Mbeya Institute of Science and Technology) na sasa hivi vyuo hivi viwili vyote vimepoteza hadhi hiyo. Leo hii ukienda Mbeya kuna Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya sio Taasisi ya Elimu ya Sayansi na Taeknolojia. Ukienda Dar esSsalaam kuna Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Dar es Salaam na sio Taasisi ya Elimu ya Sayansi na Teknolojia.

Mheshimiwa Spika, vyuo hivi vimepoteza haiba ya kuzalisha wanafunzi ambao wanakuwa na maarifa na ujuzi na matokeo yake sasa Taifa letu tunakuwa na vyuo vikuu vingi na elimu ya chuo kikuu basically kwa asilimia kubwa inaandaa wanafunzi kwenda kuajiriwa. Hata hivyo, sio tu kuajiriwa inaandaa Managers, lakini elimu ya ufundi inaandaa watu wanaokwenda kuzalisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, rai yangu, ombi langu na ushauri wangu kwa Serikali, ni muhimu sasa itazame upya suala hili na kwa sababu Taifa letu lina changamoto kubwa ya kada ya Mafundi Mchundo. Nieleze jambo hapa, katika safari yangu ya elimu nilibahatika kusoma Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi pale Kibaha, nilisoma elimu ya ufundi miaka miwili na nilisomea ufundi wa magari na mitambo.

Mheshimiwa Spika, vyuo hivi asili yake ni Sweden, Baba wa Taifa alianzisha vyuo hivi mahususi kulifanya Taifa letu liwe na vijana wengi wenye ujuzi lakini vyuo hivi leo hii vimesahaulika kabisa na nikisema nadhani hapa Waheshimiwa Wabunge watakuwa mashahidi, baadhi nikiwambia FDC ni neno jipya kwao leo. Kuna Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi ambavyo viko Kibaha, Ifakara pale kipo Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Ifakara. Sasa vyuo hivi ni muhimu kwa sababu vinatoa ujuzi zaidi ya VETA. Vijana wanasoma elimu ya ujasiriamali, vijana wanasoma elimu ya uchumi na fedha, vijana wanasoma elimu ya uhasibu. Sasa ombi langu na ushauri wangu kwa Serikali ni muhimu sasa ikatazama vyuo hivi, fedha zipelekwe.

Mheshimiwa Spika, kama haitoshi, eneo la tatu la ufundi ni Vyuo vya VETA na hii namshukuru Mheshimiwa Rais, tumepata fedha Halmashauri ya Wilaya Mlimba kwa maana ya Wilaya ya Kilombero, tumepata fedha za ujenzi wa Chuo cha VETA na Chuo kile kinakwenda kujengwa pale Mlimba, Kata ya Mchombe, Kijiji cha Lukolongo. Kwa hiyo, hii ni fahari kwa wananchi wa Jimbo la Mlimba hususani wa Kata ya Mchombe na Kijiji cha Lukolongo. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ninapokwenda kuhitimisha hoja yangu, ni eneo la mahusiano baina ya Mamlaka za Upangaji na Wizara ya Ardhi kama Msimamizi wa Sekta ya Ardhi.

Mheshimiwa Spika, hapo awali kwa mujibu wa Sheria Namba 8 ya Mwaka 2007 ya Mipango Miji, mamlaka za upangaji ni halmashauri zote nchini na mpaka sasa ipo hivyo. Changamoto inayojitokeza sasa kupitia Waraka wa Utumishi wa Ardhi, Watumishi wa Ardhi walihamishwa kutoka Halmashauri kwenda Wizara ya Ardhi, sasa nini nafasi ya Mkurugenzi wa Halmashauri katika kumsimamia Afisa Ardhi ambaye yuko kwenye Halmashauri yake? Kuna ombwe hapo, ndio maana leo hii migogoro ya ardhi imekithiri nchini.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi yeye ndio mwajiri, yeye ndiye anayepandisha madaraja ya watumishi wa kada ya ardhi. Mkurugenzi wa Halmashauri anaambiwa na niseme kwa dhati, ukiangalia Maafisa Ardhi walioko kwenye halmashauri hawatofautiani na tunaita kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kuna mtu anaitwa Mshauri wa Mgambo, yule pale amekwenda kuhifadhiwa tu na wanashauriana na Mkuu wa Wilaya ila Mkuu wa Wilaya hana Mamlaka ya kumuagiza Mshauri wa Mgambo.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, leo hii nitoe mfano, Mkurugenzi wa Halmashauri amempangia kazi Afisa Ardhi, Kamishna wa Ardhi wa Mkoa naye anamwita, sasa huyu Afisa Ardhi anakwenda wapi? Anamsikiliza Mkurugenzi wa Halmashauri au anakwenda kwenye Mamlaka yake Mkoani?

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

TAARIFA

SPIKA: Mheshimiwa Kunambi kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Angelina Mabula.

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii. Napenda nimpe taarifa msemaji asitake kupotosha. Waraka uliohamisha Watumishi wa Ardhi kwenda Wizarani ndio ule ule uliowataja watu wa TARURA, ndio uliotaja watu wa maji.

Mheshimiwa Spika, la pili, kiutendaji wale watu wako hundred percent kwenye halmashauri kwa sababu Halmashauri ndizo Mamlaka za Upangaji. Sasa hauwezi kuwa Mamlaka ya Upangaji usiwe na sauti na yule mtu. Kwa hiyo, kama analalamikia kwamba ardhi Mkurugenzi anakosa sauti, kwa nini TARURA wanafanya kazi? Kwa nini Wizara ya Maji wanafanya kazi na waraka uliohamisha majukumu ulikuwa ni ule ule mmoja? Wameletwa Wizarani kwa ajili ya ajira na nidhamu na adhabu zozote zinaanzia kwenye halmashauri husika kabla ya Katibu Mkuu kuweza kutoa. Kwa hiyo, hakuna ambacho kimeharibika katika hilo isipokuwa Wakurugenzi wanataka kukwepa majukumu yao kwa kusingizia kwamba hawa watu huwa wako Wizarani.

SPIKA: Mheshimiwa Kunambi unapokea taarifa hiyo?

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, namheshimu sana Mama yangu, lakini sipokei taarifa hiyo. Labda nieleze, ukizungumzia TARURA ni independent, wanajitegemea hawako kwenye Halmashauri, ndio maana wanafanya vizuri, ukizungumzia watu wa Maji RUWASA ni taasisi inayojitegemea, hawako kwenye Halmashauri, sasa ukitoa Mfano wa RUWASA na TARURA hapana.

SPIKA: Dakika moja malizia.

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, naomba nishauri, ili kuboresha ufanisi wa Sekta ya Ardhi nchini, Wizara ya Ardhi ikae na Wizara ya TAMISEMI, warejee huu waraka waone ni namna gani Mkurugenzi wa Halmashauri anakwenda kuwa na mamlaka ya kumwagiza Afisa Ardhi na watu wa mipango miji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)