Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, nawapongeza kwa maandalizi ya hotuba iliyojaa ufafanuzi wa sekta mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha yafuatayo; kwanza kazi na ajira, kupitia kilimo tunaweza kupanua wigo wa ajira, lakini pia tunaweza kujitosheleza kwa baadhi ya bidhaa ambazo kutokana na kilimo tutazizalisha na tukapunguza matumizi ya fedha za kigeni katika kuagiza bidhaa kama mafuta ya kula. Ushauri wangu wa mara zote, kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na Wizara ya Ulinzi na JKT, tuwekeni nguvu kama Taifa katika kuzalisha mbegu ambazo tutazalisha mafuta ya kula.

Mheshimiwa Spika, napongeza jitihada za Mheshimiwa Waziri Mkuu zinazoendelea kule Kigoma za kilimo cha michikichi. Ninaamini tukiwawezesha JKT tutavuka, lazima tufike wakati tuwe na uthubutu, tuwe wakweli wa nafsi, sio sawa kama Taifa kuendelea kutumia zaidi ya USD milioni 300 kuagiza mafuta ya kula, tuone aibu kama Taifa.

Mheshimiwa Spika, hata jitihada za kupunguza VAT kwa waagizaji mafuta ya kula hazijawa na nafuu iliyokusudiwa, zaidi imenufaisha wafanyabiashara waagizaji wa mafuta ya kula, matokeo yake bei ya alizeti imeshuka kwa wakulima wetu na wakati huo huo bei ya mafuta ya kula haina ahueni yoyote.

Mheshimiwa Spika, tukiwekeza katika JKT sio tu kwamba tutaokoa fedha za kigeni lakini pia tutauza mafuta katika nchi jirani za DRC, Malawi, Zambia na hata Burundi na Rwanda. Nchi hizi zinategemea mafuta ya kula kutoka Malaysia, tukizalisha tunalo soko la ndani, lakini pia soko hata ndani ya EAC na baadhi ya nchi za SADC.

Kule Chita, nashauri Serikali ikajifunze kilimo cha mpunga chini ya JKT, ni aibu sisi kutoa vibali na kuagiza michele tani 90,000; haya ni mambo tunapaswa kuyakataa kwa vitendo, hizi programu za Block Farming zingehusisha vijana waliopata mafunzo JKT na usimamizi ungefanywa kwa ushirikiano wa ofisi hizi tatu, Kilimo, Kazi na Ajira na JKT.

Mheshimiwa Spika, pili, usalama wa mbegu na mbegu bora; pia ninashauri tuwe na mpango maalum wa kuhakikisha Taifa linajitosheleza kwa mbegu bora na salama. Mfumo uliopo kwa hakika sio salama katika suala la usalama wa chakula na usalama wa Taifa. Nashauri pia tuhusishe vyombo vyetu hasa JKT.