Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisesa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, utangulizi; na kabla sijaanza kuchangia, niwaombe Waheshimiwa Wabunge na Mheshimiwa Spika tusikubali Bunge hili tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutumika kama sehemu ya kusafisha wahalifu na wabadhirifu wa mali za umma kwani la kuvunda halina ubani. Na hapa nichukue nafasi hii, kuzipongeza sana Mamlaka za Ukaguzi na Uchunguzi kwa kazi nzuri walizofanya katika hesabu zinazoishia mwaka 2021/2022 kwa kuibua wizi, ubadhirifu na ufisadi pamoja na matumizi mabaya ya madaraka katika taasisi mbalimbali za Serikali nchini.
Mheshimiwa Spika, hongera sana kwa CAG, CPA – Charles Kichere na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, CP – Salum Hamduni, hongereni pamoja na maafisa wote wa Ofisi zenu. Uchunguzi na ukaguzi mlioufanya ni kielelezo kikubwa cha uzalendo mlionao kwa Taifa letu, Mungu awabariki sana; na kipekee nimpongeze sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukataa kata kata nchi yetu kugeuzwa shamba la bibi. Na hapa naweka msisitizo Mawaziri na watendaji wote waliohusika wakamatwe na washtakiwe kwa makosa ya uhujumu uchumi.
Mheshimiwa Spika, nimesikiliza hotuba ya bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2023/2024, lakini pia nimesoma Mpango wa Maendeleo na ukomo wa bajeti ya mwaka 2023/2024 pamoja na taarifa ya CAG ya mwaka 2021/2022 ili kuona hatua za utekelezaji wa majukumu na changamoto za Ofisi ya Waziri Mkuu na Serikali kwa ujumla. Baadhi ya masuala ya kiujumla ni kama ifuatavyo: -
(i) Bajeti ya maendeleo kushuka na kufikia 34.1% mwaka wa fedha 2023/2024 ni kinyume na Mpango wa Maendeleo III wa miaka mitano ambapo walau fedha za maendeleo zisipungue chini ya 37.1% ya bajeti nzima. Nini kimesababisha bajeti ya maendeleo kushuka?
(ii) Katiba Mpya, licha ya maelekezo ya muda mrefu ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu kuanza kwa mchakato wa marekebisho ya Katiba na upatikanaji wa Katiba Mpya, hotuba ya Waziri Mkuu na mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2023/2024 hazijaeleza chochote kuhusu maandalizi ya suala hili muhimu. Waziri Mkuu aeleze hatua zilizofikiwa katika mchakato wa Katiba Mpya.
Mheshimiwa Spika, kuhusu changamoto mahsusi ya utekelezaji wa bajeti; mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2023/2024, ukurasa wa 89 kipengele cha 2:4:2 Serikali inakiri kuwepo kwa changamoto mahsusi zinazokwaza utekelezaji wa miradi nanukuu kama ifuatavyo: -
(a) Upungufu wa rasilimali watu hususan wahandisi wa kusimamia utekelezaji wa miradi pamoja na wataalamu wa uendeshaji wa mitambo na vifaa vinavyotumia teknolojia ya kisasa;
(b) Watekelezaji wa miradi kuchelewa kukamilisha taratibu za utoaji wa cheti cha msamaha wa kodi hali inayosababisha kuongezeka kwa gharama za mradi (madai ya riba) na kuchelewa kwa kutekeleza mradi;
(c) Usanifu duni wa mradi hali inayosababisha kuongezeka kwa mawanda, gharama na muda wa utekelezaji wa miradi;
(d) Usimamizi usioridhisha katika utekelezaji wa miradi kwa mujibu wa mikataba na mipango kazi kwa baadhi ya watekelezaji wa miradi;
(e) Kuchelewa kwa malipo ya makandarasi kunakosababishwa na kutowasilishwa kwa nyaraka muhimu za kuwezesha kufanyika kwa malipo kwa wakati hali inayosababisha malimbikizo ya riba na ucheleweshaji wa utekelezaji wa mradi;
(f) Usimamizi na uratibu kwa baadhi ya taasisi kufanyika katika ngazi ya makao makuu bila kushirikisha wasimamizi waliopo katika eneo la mradi hali inayosababisha miradi kuchelewa, kuongeza gharama na kupunguza ufanisi katika malengo ya mradi;
(g) Ushirikishwaji mdogo wa wadau muhimu wa mradi katika kipindi cha maandalizi hali inayosababisha kubadilika kwa mawanda ya kazi wakati wa utekelezaji; na
(h) Kuchelewa kwa malipo ya fidia kwa wananchi wanaopisha miradi.
Mheshimiwa Spika, Waziri Mkuu wewe ndio msimamizi mkuu wa shughuli za Serikali na haya yote yanatokea chini ya usimamizi wako, nini kilichoifanya Serikali ishindwe kuchukua hatua stahiki na kuondoa dosari hizo? Kama Wabunge tulitegemea Serikali ingekuwa imetatua changamoto hizo badala ya kulalamika kwa wananchi huku Taifa likiendelea kupata hasara kubwa.
Mheshimiwa Spika, usimamizi wa bajeti na fedha za umma; leo tunajadili hotuba ya bajeti ya mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2023/2024 kukiwa na wizi, rushwa, ubadhirifu na ufisadi wa fedha na rasilimali za umma umetamalaki kila sehemu, fedha nyingi zinazoidhinishwa na Bunge zinaishia mikononi mwa wezi wachache ndani ya Serikali kutokana na mikataba mibovu, usimamizi dhaifu wa mikataba, malipo yasiyo na tija, matumizi na mikopo nje ya bajeti, manunuzi yasiyozingatia sheria, kuongeza bei katika hati za malipo (over invoicing), kutokutekeleza mipango ya manunuzi kama ilivyoidhinishwa na Bunge na kukosekana uwajibikaji Serikalini.
Mheshimiwa Spika, leo ni siku mbaya ambayo tunakwenda kuidhinisha fedha za umma zikagawanwe tena na wachache. Katika kufanya hivyo ni muhimu sana kupitia na kufanya tahmini ya kina juu ya vihatarishi vitakavyopelekea bajeti hii kutotekelezwa ipasavyo, ipo mifano michache kupitia taarifa za utekelezaji na Ripoti ya CAG inayoonesha kuwa kuna vihatarishi vikubwa vinavyoweza kufanya bajeti hii isitekelezeke kwa tija kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kushindwa kutekeleza mpango wa manunuzi; mapitio ya utekelezaji wa mpango wa manunuzi mwaka 2021/2022 imeonesha taasisi 22 zilishindwa kutekeleza mpango wa manunuzi wenye thamani ya kiasi cha shilingi trilioni 3.14 kati ya fedha hizo TANROADS ni shilingi trilioni 2.9 ambazo taasisi hiyo ilishindwa kukamilisha mchakato wa manunuzi kutokana na kuchelewa kupata kibali cha kutangaza zabuni za miradi kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (CAG).
Mheshimiwa Spika, Bunge liliidhinisha fedha hizi katika mwaka wa fedha 2021/2022 kwa ajili ya kwenda kutekeleza miradi mbalimbali kwa maslahi ya Taifa na badala yake fedha hizo hazikutumika na hazijulikani zilipo. Katika mwaka huo wa fedha mapato ya Serikali yalipatikana kwa 97.2% na mikopo ilipatikana kwa 106%; iweje zabuni zisitolewe kwa mwaka mzima, wananchi wanaendelea kuteseka kwa kukosa huduma muhimu ikiwemo barabara, Wabunge wanalia Bungeni, wengine wanapiga magoti Bungeni, wengine wanapiga sarakasi Bungeni kutokana na kukosa fedha za kugharamia miradi ya majimbo yao.
Mheshimiwa Spika, ushauri; CAG na TAKUKURU wafanye uchunguzi na ukaguzi maalum ili kujua sababu zilizopelekea Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, TANROADS na taasisi zingine kukaa na fedha mwaka mzima bila matumizi na pia kujua fedha hizo ziko wapi.
Mheshimiwa Spika, hatua kali za kiutawala na za kisheria zichukuliwe ikiwemo kushtakiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi wa nchi kwa wote waliohusika kwa uzembe na ufisadi huu.
Mheshimiwa Spika, kutokufuata Sheria ya Manunuzi wakati wa kutoa zabuni ya Mradi wa SGR, kwa mujibu wa ripoti ya CAG ya mwaka 2021/2022 inaonesha kuwa gharama ya ujenzi wa SGR Lot. No. 3 na Lot No. 4 ziliongezeka dola za Marekani milioni 1.3 na milioni 1.6 kwa kilometa moja ya SGR baada ya TRC kuacha njia ya ushindani na kutumia njia ya single source na kusababisha hasara ya jumala ya shilingi trilioni 1.7 kwa mchanganuo ufuatao: -
Mheshimiwa Spika, Lot No. 3 Mkataba wa TRC na Kampuni ya Yapi Markenz wa ujenzi wa SGR kipande cha Makutupora – Tabora urefu wa kilometa 368 uliosainiwa Disemba 2021 ambapo TRC iliacha bei ya ushindani ya kiasi cha shilingi bilioni 9 kwa kilometa ya SGR na kutoa zabuni kwa njia ya single source kwa Kampuni ya Yapi Markenz kwa shilingi bilioni 11.97 kwa kilometa ya SGR ambao kumeisababishia Serikali hasara ya zaidi ya shilingi trilioni 1.09.
Mheshimiwa Spika, Lot No. 4 Mkataba wa TRC na Kampuni ya Yapi Markenz wa ujenzi wa SGR kipande cha Tabora – Isaka urefu wa kilometa 165 uliosainiwa Julai, 2022 ambapo TRC iliacha bei ya ushindani ya kiasi cha shilingi bilioni tisa kwa kilometa ya SGR na kutoa zabuni kwa njia ya single source kwa Kampuni ya Yapi Markenz kwa shilingi bilioni 12.69 kwa kilometa ya SGR ambao kumeisababishia Serikali hasara ya zaidi ya shilingi bilioni 608.8.
Mheshimiwa Spika, licha ya PPRA na Bodi ya Zabuni ya TRC kukataa sharti la kutumia mzabuni mmoja, lakini TRC ilitoa zabuni hiyo kwa njia ya single source kwa Kampuni ya Yapi Markenz. Maamuzi haya yalitokana na maelekezo ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa barua yenye Kumb. Na. PST/GEN/2021/01/55. Ili kukidhi matakwa ya kupata mkopo kutoka Benki ya Standard Charted na kusababisha hasara kwa Serikali ya shilingi trilioni 1.7.
Mheshimiwa Spika, TRC ilimkataa mzabuni wa shilingi bilioni 616.4 na kumpa mzabuni wa shilingi trilioni 1.119 kwa ajili ya ununuzi wa vichwa vya treni vya umeme na makochi bila sababu za msingi na kuisababishia Serikali hasara ya shilingi bilioni 503 hii ni kwa mujibu wa ripoti ya CAG ya mwaka 2021/2022.
Mheshimiwa Spika, dosari alizoziona CAG katika Lot No. 3 na Lot No. 4 zipo pia katika Lot No. 6, Mkataba wa TRC na Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) wa ujenzi wa SGR kipande cha Tabora – Kigoma yenye urefu wa kilometa 506 ambapo TRC iliacha bei ya ushindani ya kiasi cha shilingi bilioni 9.1 kwa kilometa ya SGR na kutoa zabuni kwa njia ya single source kwa Kampuni ya CCECC kwa shilingi bilioni 12.5 kwa kilometa ya SGR hii ni zaidi ya bilioni 3.4 kwa kilometa ya SGR katika mkataba uliosainiwa mwaka 2022, gharama hiyo imeongezeka wakati idadi ya vifaa na ukubwa wa miundombinu umepunguzwa na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya trilioni 1.7.
Mheshimiwa Spika, malipo ya ununuzi wa vichwa vya treni na makochi na ujenzi wa SGR Lot. No. 3, Lot. No. 4 na Lot No. 6 ambapo TRC iliacha bei ya ushindani na kutumia njia ya single source na kusababisha upotevu wa fedha kiasi cha takribani shilingi trilioni 4 huku sheria na kanuni za manunuzi ya umma zikiwa zimevunjwa. Ufisadi huu wa fedha za umma umepata baraka zote za Waziri wa Fedha, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na TRC na bahati mbaya bado wako kwenye Ofisi za Serikali.
Mheshimiwa Spika, kama Mbunge hapa Bungeni nilihoji Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi sababu za kukiuka sheria ya manunuzi na kutoa zabuni bila ushindani na kuisababishia hasara Serikali, lakini Wizara haikuweza kutoa majibu yanayojitosheleza (Hansard za Bunge zipo). Leo CAG ameweka wazi suala hili pamoja na PPRA na Bodi ya Zabuni ya TRC kutoa ushauri wa zabuni kutolewa kwa mujibu wa sheria, lakini Waziri wa Fedha na Mipango na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi waliridhia zabuni hizo kutolewa kinyume cha sheria ya manunuzi ya umma Na. 7 mwaka 2011 na marekebisho yake ya mwaka 2016 pamoja na Kanuni zake za mwaka 2013 na marekebisho yake ya mwaka 2016 kwa sababu wanazozijua wao na kuliingizia Taifa hasara ya takribani shilingi trilioni 4. Huu ni uhujumu uchumi wa nchi kwa mujibu wa Sheria ya Uhujumu Uchumi (The Economic and Organized Crime and Control Act).
Mheshimiwa Spika, utakumbuka pia kuwa baada ya kuchangia suala hili hapa Bungeni mara kwa mara na kukosa majibu fasaha kuhusu ukiukwaji mkubwa wa sheria, niliamua kumuandikia barua Katibu Mkuu Kiongozi yenye Kumb. Na. MB/KSS2023/21 ya tarehe 13 Machi, 2023 ambapo na wewe nilikupa nakala nikionesha ukiukwaji mkubwa wa sheria na hasara kwa Taifa.
Mheshimiwa Spika, hivyo badala ya kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya mradi huu hatua za haraka zifuatazo zichukuliwe: -
Mheshimiwa Spika, kwanza; hatua kali za kiutawala na kisheria zichuliwe ikiwemo kukamatwa na kufunguliwa makosa ya uhujumu uchumi wa nchi kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mkurugenzi Mkuu wa TRC na wengine wanaohusika.
Mheshimiwa Spika, pili; kuvunja mikataba au kufanya makubaliano mapya kwa mikataba ya Lot 3, Lot 4 na Lot 6 ili kuondoa dosari zote zinazosababisha Serikali hasara.
Mheshimiwa Spika, kuhusu matumizi na mikopo nje ya bajeti; kama Mbunge nimeuliza mara kwa mara hapa Bungeni Serikali kukopa nje ya bajeti, lakini Waziri wa Fedha alishindwa kutoa majibu ya kina kueleza imekopa kiasi gani nje ya bajeti, amekopa mikopo ya ziada kwa shughuli gani na sababu za kulikwepa Bunge ni zipi (Hansard ya Bunge inajieleza). Leo CAG ameweka wazi ukweli uliokuwa unafichwa. Kama fedha hizi zilikopwa kwa nia njema na kwa maslahi ya Taifa kwa nini zipokelewe na kutumika kwa siri? Huku ni kupoka madaraka ya Bunge na kuna harufu ya ufisadi wa kutisha.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya CAG 2021/2022 Serikali Kuu jedwali na 17 linaonesha kuwa Serikali imekopa nje ya bajeti iliyoidhinishwa na Bunge na bila ridhaa ya Bunge kiasi cha shilingi trilioni 1.285. Waziri wa Fedha alikopa fedha hizi kwa ajili ya shughuli gani na kwa ridhaa ya nani? Fedha na kazi zilizopangwa katika bajeti 2021/2022 zilipitishwa na kuidhinishwa na Bunge tena kwa kupigiwa kura ya ndiyo, fedha za ziada alizokopa Waziri wa Fedha ni kwa ajili ya shughuli gani na kwa ridhaa ya nani?
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Mikopo (Government Loans, Guarantees and Grants Act) ambapo mamlaka ya kukopa mikopo amepewa Waziri wa Fedha kwa niaba ya Serikali na atafanya hivyo kwa kuzingatia ukomo uliowekwa na Bunge kupitia bajeti iliyoidhinishwa na endapo katika utekelezaji wa bajeti kutakuwa na mahitaji mapya atapata kibali cha Bunge.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 ilipotokea ongezeko la mikopo la shilingi trilioni 1.31 kutoka IMF kwa ajili ya kutekeleza mpango wa kukabiliana na hali ya uchumi baada ya kupungua kwa ugonjwa wa Covid-19 bajeti ilifanyiwa marekebisho kupitia Bunge kutoka trilioni 36.68 hadi trilioni 37.99. Hapa Waziri wa Fedha alizingatia matakwa ya sheria ya mikopo inavyotaka ambapo Bunge liliridhia kwa kauli moja na hakukuwepo malalamiko.
Mheshimiwa Spika, swali kubwa wanalojiuliza Watanzania kwa nini ongezeko la mikopo ya ziada la kiasi cha shilingi trilioni 1.285 aliyokopa Waziri wa Fedha haikuwekwa wazi na hakupata ridhaa ya Bunge? Fedha hizi Bunge ni vigumu kuzisimamia kwani halijui ziko wapi na kwa matumizi gani hali inayoweza kusababisha matumizi mabaya na ufisadi. Maamuzi ya Waziri wa Fedha yamekwenda kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sheria ya Bajeti, Sheria ya Fedha na Sheria ya Mikopo lakini pia ni matumizi mabaya ya Ofisi kwenye Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
Mheshimiwa Spika, ushauri; CAG na TAKUKURU wafanye uchunguzi na ukaguzi maalum ili kubaini sababu zilizomsukuma Waziri wa Fedha kukopa na kutumia fedha za mikopo nje ya bajeti iliyopitishwa na Bunge pamoja na uhalali wa matumizi yaliyofanywa.
Mheshimiwa Spika, hatua kali za kiutawala na kisheria zichukuliwe kwa Waziri wa Fedha na wahusika wengine wote ikiwemo kushtakiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi wa nchi ambao umepelekea kuliingiza Taifa kwenye hasara na mzigo mkubwa wa madeni.
Mheshimiwa Spika, kushindwa kusimamia mikataba kikamilifu (JHNPP – 2115); kama Mbunge nilihoji mara kwa mara suala hili hapa Bungeni kuhusu Kampuni ya Arab Contractors kutakiwa kulipa faini ya ucheleweshaji na CSR lakini Waziri wa Nishati muda wote amekuwa mtetezi wa mkandarasi Arab Contractors na kumkingia kifua asilipe malipo hayo halali kwa mujibu wa mkataba (Hansard za Bunge zipo).
Mheshimiwa Spika, CAG ameuweka wazi ukweli wa jambo hili kuwa TANESCO wameshindwa kutoza faini ya fidia ya ucheleweshaji kwa mwaka kiasi cha shilingi bilioni 327.93 sawa na kiasi cha shilingi bilioni 655.86 kwa miaka miwili. Pia wameshindwa kutoza CSR ya kiasi cha shilingi bilioni 270.67 kwa mujibu wa mkataba wa mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Nyerere (JNHPP – 2115) na kusababishia jumla ya upotevu wa fedha kiasi cha shilingi bilioni 926.53.
Mheshimiwa Spika, kwa nini Waziri wa Nishati amekuwa akitumia nguvu nyingi kiasi hicho kumkwepesha mkandarasi kulipa faini iliyowekwa kwa mujibu wa mkataba? Mkataba unakaribia kufika mwisho na fedha anazodai Kampuni ya Arab Contractors zimepungua, je, ni wakati gani Serikali itaanza kukata madai hayo? Huu ni uhujumu uchumi lakini pia ni matumizi mabaya ya ofisi ya umma kwa mujibu wa Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
Mheshimiwa Spika, ushauri; hatua kali za kiutawala na za kisheria zichukuliwe ikiwemo kukamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi wa nchi kwa Waziri wa Nishati, Mkurugenzi wa TANESCO na wahusika wengine kwa kuisababishia Serikali hasara ya shilingi bilioni 926.53.
Mheshimiwa Spika, Serikali ianze kukata malipo ya faini ya fidia ya ucheleweshaji na mchango wa CSR kwa kila hati ya malipo inayowasilishwa na kulipwa na kuhakikisha kuwa fedha zote za umma zinazodaiwa zimelipwa kabla ya mkataba kumalizika.
Mheshimiwa Spika, suala la TANESCO kushindwa kuidai IPTL; kwa mujibu wa taarifa ya CAG ya mwaka 2021/2022, TANESCO kushindwa kudai malipo ya shilingi bilioni 342 kutoka Kampuni ya IPTL baada ya Serikali kushinda kesi Machi, 2021 fedha hizi zinatakiwa kupatikana ili kulipa deni Benki ya Standard Chartered, Hong Kong dola za Marekani milioni 148.4 pamoja na riba kama ilivyoamuriwa na Kituo cha Kimataifa cha Kutatua Migogoro ya Uwekezaji. Kitendo cha kushindwa kukusanya fedha hizi kutafanya Serikali ilipe mkopo pamoja na riba kwa Benki ya Standard Chartered Hong Kong. Nini kilichofanya Wizara ya Nishati, Wizara ya Fedha na TANESCO washindwe kudai IPTL madai hayo halali kwa amri ya Mahakama?
Mheshimiwa Spika, CAG hakuona hatua yoyote iliyochukuliwa na Wizara ya Nishati na TANESCO tangu hukumu hiyo itolewe Machi, 2021 na hivyo kuleta sintofahamu kubwa lakini ilikuwa rahisi kwa Wizara kulipa malipo ya kiasi cha shilingi bilioni 350 katika Kampuni ya Symbion Power LCC.
Mheshimiwa Spika, ushauri; hatua kali za kiutawala na za kisheria zichukuliwe ikiwemo kukamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi wa nchi kwa Waziri wa Nishati, Mkurugenzi wa TANESCO na wote waliohusika na kuisababishia Serikali hasara ya shilingi bilioni 342.
Mheshimiwa Spika, Serikali iitake IPTL kwa haraka kulipa fedha kiasi cha dola za Marekani milioni 148.4 pamoja na riba kama Mahakama ilivyoamuru.
Mheshimiwa Spika, kuhusu malipo ya tozo za riba bila sababu za msingi; malipo ya tozo na riba kutokana na kuchelewesha malipo ya wazabuni, wakandarasi, bima na mifuko ya jamii katika Serikali Kuu, mashirika ya umma na Serikali za Mitaa na kuipelekea Serikali hasara ya kiasi cha shilingi bilioni 418.5. ucheleweshaji huu ni kinyume cha sheria na pengine unafanywa kwa maslahi binafsi na Wizara ya Fedha na taasisi zingine za Serikali. Fedha hizi zingeweza kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo badala ya kulipa faini. Wahusika wote wachukuliwe hatua.
Mheshimiwa Spika, matumizi ya fedha za umma nje ya bajeti; taarifa ya CAG 2021/2022 inaonesha kuwa matumizi ya fedha za umma nje ya bajeti iliyoidhinishwa katika maeneo mbalimbali ya Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Serikali za Mitaa ambapo kwa ukokotoaji wangu ni kiasi cha shilingi bilioni 502.87 ambapo kati ya hizo shilingi bilioni 104.21 ni za TANESCO hii ni kinyume na sheria ya bajeti na sheria ya manunuzi; hatua zichukuliwe kwa wahusika.
Mheshimiwa Spika, fedha kupelekwa moja kwa moja TARURA; taarifa ya CAG ya mwaka 2021/2022 inaonesha Wizara ya Fedha kupeleka moja kwa moja TARURA fedha za ongezeko la tozo ya mafuta kiasi cha shilingi 100 kwa lita ya dizeli na petroli badala ya kupeleka kwenye Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB) kama sheria zinavyosema kiasi cha shilingi bilioni 330.33 huu ni ukiukwaji mkubwa wa sheria ya ushuru wa barabara na mafuta Sura ya 220. Sababu za kuikwepa Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB) hazifahamiki na pengine fedha hizi zimetumika vibaya.
Mheshimiwa Spika, ushauri; TAKUKURU ifanye uchunguzi ili kubaini sababu za Wizara ya Fedha kukiuka sheria na kama fedha hizo zimefika na kutumika kihalali TARURA.
Mheshimiwa Spika, hatua za kiutawala na kisheria zichukuliwe kwa wahusika wote.
Mheshimiwa Spika, ucheleweshaji wa maamuzi katika Mahakama za Rufani za Kodi; Mahakama za Rufani za Kodi za TRAB, TRAT na CAT kuchelewa kutoa uamuzi katika mashauri ya malimbikizo ya kodi hali inayopelekea kushindwa kukusanya mapato ya Serikali katika mwaka husika na kukosesha Serikali mapato. Mara nyingi CAG amekuwa akijibiwa sababu za ucheleweshaji ni upungufu wa rasilimali fedha na watu. Hizi sababu sio za msingi kwani eneo nyeti kama hili kuacha kupewa kipaumbele na kutumika kama kichaka cha kukwepa kulipa kodi. Ripoti ya CAG ya mwaka 2021/2022 mashauri ya malimbilikizo ya kodi yamefikia kiasi cha shilingi trilioni 4.84.
Mheshimiwa Spika, ucheleweshaji wa maamuzi unaonekana kwenye malimbikizo ya kodi pekee, lakini upande wa mashauri ya kesi za manunuzi chini ya Mamlaka ya Rufani za Manunuzi ya Umma (Public Procurement Appeals Authority – PPAA) maamuzi yamekuwa yakifanyika kwa wakati na kusifiwa na wadau.
Mheshimiwa Spika, ushauri; Bunge liunde Kamati Teule kuchunguza chanzo cha ucheleweshaji huo na kupendekeza hatua za kuchukua.
Mheshimiwa Spika, malimbikizo ya kodi yasiyo na kesi Mahakamani; taarifa ya CAG ya mwaka wa fedha 2020/2021 ilionesha TRA kushindwa kukusanya malimbikizo ya kodi yasiyo na kesi mahakamani kiasi cha shilingi trilioni 7.54 bila sababu za msingi, kitendo cha TRA kushindwa kukusanya kodi hizi kwa wakati kuikosesha Serikali mapato ambapo CAG alilalamikia kasi ndogo ya ukusanyaji wa malimbikizo hayo ambayo ilikuwa ni 10% tu. Taarifa ya CAG ya mwaka 2021/2022 haijatoa taarifa ya hatua iliyofikiwa katika ukusanyaji wa malimbikizo hayo lakini pia haijaeleza malimbikizo ya kodi ya mwaka husika.
Mheshimiwa Spika, eneo hili la malimbikizo ya kodi lisipotazamwa upya na kubaini sababu zinazosababisha TRA ishindwe kukusanya mapato ambayo imeshayafanyia assessment na hakuna pingamizi yoyote itapelekea taasisi hii kuendelea kupoteza uwezo wa kukusanya mapato na eneo hili kutumika kama uchochoro na kichaka cha kukwepa kodi na kuikosesha mapato Serikali.
Mheshimiwa Spika, CAG aweke wazi malimbikizo ya kodi yasiyo na kesi mahakamani yaliyopo kufikia mwaka wa fedha 2021/2022.
Mheshimiwa Spika, ushauri; Bunge liunde Kamati Teule kuchunguza chanzo cha ucheleweshaji huo na kupendekeza hatua za kuchukua.
Mheshimiwa Spika, kufuta madai ya malimbikizo ya kodi; taarifa ya CAG ya mwaka 2020/2021 inaonesha miongoni mwa kesi za rufani zilizoisha ni kesi 45 zenye thamani ya shilingi 5,594,675,387,242.40 ambazo zipo katika mazungumzo kati ya Serikali na kampuni ya madini ambayo ni North Mara Gold Mine, Pangea Minerals Limitied, Bulyanhulu Gold Mine na ABG Exploration, kati ya jumla ya deni la shilingi trilioni 343.5. kesi hii imetolewa kutoka Mahakama za Rufani za kikodi na kurejeshwa kusikilizwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Mheshimiwa Spika, kama Mbunge nimekuwa nikilihoji suala hili mara kwa mara hapa Bungeni kuitaka Serikali kueleza hatua iliyofikia ya kulipwa kiasi cha shilingi trilioni
5.595 za malimbikizo ya kodi kwa makampuni ya madini maarufu makinikia, lakini majibu ya Waziri wa Fedha yalikuwa tofauti na ripoti ya CAG ambapo alidai kuwa madai hayo hayapo na kwamba yalishafutwa na sherehe ya kufuta ilifanyika Ikulu. Ingawa kila nilipomuomba kutoa ushahidi kuhusu uamuzi wa kufutwa madai hayo hakufanya hivyo.
Mheshimiwa Spika, taarifa ya CAG ya mwaka 2021/2022 haijaonesha suala hili limehitimishwa vipi na Serikali, lakini pia malimbikizo ya kodi ya kiasi cha shilingi trilioni 5.595 ambazo zilikuwa kwenye mazungumzo na kiasi cha shilingi trilioni 343.5 ambazo zilirejeshwa TRA hazipo tena kwenye vitabu vya TRA. Nani aliyetoa maamuzi ya kufutwa madai halali ya kiasi cha shilingi trilioni 5.595 na kufutwa kwenye vitabu madai ya kiasi cha shilingi trilioni 360 bila ridhaa ya Bunge.
Mheshimiwa Spika, ushauri; Bunge liunde Kamati Teule kuchunguza sababu za kufutwa madai halali ya malimbikizo ya kodi kiasi cha shilingi trilioni 5.595 na kuondolewa kwa madai ya shilingi trilioni 360 kwenye vitabu vya TRA na kama yamefutwa kwa mujibu wa sheria na kupendekeza hatua za kuchukua.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Mashirika ya Umma yaliyopata faida kupata hasara; Mashirika ya Umma 16 yamepata hasara ya shilingi bilioni 34.5 mwaka 2021/2022 wakati mashirika hayo yalipata faida ya shilingi bilioni 56.57 mwaka 2020/2021 na kupelekea jumla ya hasara shilingi bilioni 91.07 ikiwemo Kampuni ya Mawasiliano (TTCL) ambayo imepata hasara ya shilingi bilioni 15.56 mwaka 2021/2022 wakati mwaka 2020/2021 TTCL ilipata faida ya shilingi milioni 517. Hatua zichukuliwe kwa wahusika wote.
Mheshimiwa Spika, kuhusu mashirika ya umma ambayo yameongeza hasara; mashirika na taasisi zingine za umma 45 CAG alipofanya ukaguzi wa utendaji wa fedha alibaini kuwa hasara katika mashirika hayo imeongezeka kutoka shilingi bilioni 281.76 mwaka 2020/2021 hadi kufikia shilingi bilioni 416.37 mwaka 2021/2022 sawa na ongezeko la shilingi bilioni 134.61 ikiwemo Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ambao hasara yake imeongezeka kutoka shilingi bilioni 109.7 mwaka 2020/2021 hadi shilingi bilioni 204.65 mwaka 2021/2022. Hatua zichukuliwe kwa wahusika wote.
Mheshimiwa Spika, kuhusu matumizi yasiyostahili katika Mashirika ya Umma; CAG alibaini mashirika 21 ambayo yamefanya matumizi yasiyostahili ya jumla shilingi bilioni 77.75 ambayo yalitokana na malipo ya posho kwa watumishi wasiostahili, malipo yasiyokuwa na uthibitisho na vielelezo vya matumizi husika. Ikiwemo Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ambayo ilitumia kiasi cha shilingi bilioni 65.33. Hatua kali zichukuliwe kwa wahusika.
Mheshimiwa Spika, DPP kushindwa kukusanya malipo ya ahadi ya washtakiwa chini ya makubaliano ya mikataba ya kukiri makosa (plea bargain) na hukumu za mahakama kiasi cha shilingi bilioni 179.61 bila sababu za msingi. Hatua zichukuliwe kwa wahusika na Serikali ikusanye fedha hizo haraka.
Mheshimiwa Spika, ubadhirifu wa fedha za umma katika Mamlaka za Serikali za Mitaa; ubadhirifu na upotevu wa fedha za umma uliosababishwa ukiukwaji wa mikataba, matumizi mabaya ya fedha za umma, marejesho ya fedha ya mifuko ya kina mama, vijana na wenye ulemavu, ukiukwaji wa sheria ya manunuzi na upotevu wa mapato, katika Serikali za Mitaa na Sekretarieti za Mikoa Ripoti ya CAG ya mwaka 2021/2022 inaonesha ukiukwaji mkubwa wa Sheria ya Fedha, Sheria ya Manunuzi na Sheria ya Bajeti ambako kumesababisha wizi, ubadhirifu, ufisadi na hasara ambapo kwa ukokotoaji wangu ni kiasi cha shilingi bilioni 637.55. Hatua zichukuliwe kwa wahusika wote.
Mheshimiwa Spika, haya yote yamefanyika Waziri Mkuu yupo, Waziri wa Fedha yupo, Mawaziri wa Wizara husika wapo, Mwanasheria Mkuu yupo, Mlipaji Mkuu wa Serikali, Makatibu Wakuu wapo, PPRA ipo na PPAA ipo hadi kufikia ubadhirifu na upotevu wa fedha za umma kiasi hicho.
Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa mwezi Novemba, 2022 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitoa maazimio kuhusu taarifa ya CAG ya mwaka 2020/2021 kwa watu wote waliotajwa kuhusika na ubadhirifu wachukuliwe hatua, lakini hadi sasa hakuna utekelezaji uliofanyika kuarifiwa Bunge hili.
[MANENO YAMEONDOLEWA KWA MAELEKEZO YA KITI]
Jedwali la Ubadhirifu na Upotevu wa Fedha za Umma
Mheshimiwa Spika, hatua za dharura na za haraka zichukuliwe ili kulinusuru Taifa kupata hasara kubwa na kudidimia kiuchumi na kushindwa kutoa huduma kwa wananchi wake kikamilifu kutokana na ufisadi unaofanywa na baadhi ya Mawaziri na watendaji wengine wa Serikali. Nikipongeze sana chama changu, Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa msimamo thabiti wa kupiga vita wizi, rushwa, ubadhirifu na ufisadi wa fedha na mali za umma.
Mheshimiwa Spika, kipekee pia nipongeze sana maamuzi ya Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi katika kikao chake cha tarehe 1 Aprili, 2023 chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuazimia na kutoa maelekezo ya kuwafuatilia watu wote wanaotumia dhamana za uongozi vibaya na kushindwa kuweka maslahi ya nchi na uzalendo mbele katika nafasi walizoaminiwa kutumikia watu, badala yake wanaweka maslahi binafsi.
Mheshimiwa Spika, aidha Kamati Kuu imeielekeza Serikali kuchukua hatua thabiti kwa wahusika waliobainika kuhusika katika ukiukaji wa sheria na kusababisha ubadhirifu wa mali na rasilimali za nchi. Agizo la Kamati Kuu litekelezwe kikamilifu.
Nawasilisha, Kazi iendelee.