Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Mary Francis Masanja

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia hotuba hii ya bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ya mwaka 2023/2024.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo ameendelea kutupa maelekezo lakini kutekeleza shughuli mbalimbali za Serikali ikiwemo utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo kwa kusema ukweli tumeiona jinsi ambavyo inaenda kwa kasi.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kuongelea suala la Maliasili Mheshimiwa Rais amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba Maliasili tunazilinda, tunazitunza pia tunaendeleza masuala mazima ya utalii. Kwenye upande wa sekta ya Maliasili na Utalii tumekuwa na changamoto nyingi sana hususani za Wanyama wakali na waharibifu na hili limeweza kujitokeza hata kwenye hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ambapo tuna maeneo mengi yenye changamoto za Wanyama wakali na waharibifu pia kumekuwepo na vyakula mazao yanaliwa na wanyama wakali na kwa bahati mbaya kabisa inapelekea mpaka vifo vinatokea.

Mheshimiwa Spika, Serikali inayongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan inajitahidi sana kupunguza athari hizi ikiwemo kuanzisha vituo mbalimbali vya kudhibiti wanyama wakali na waharibifu, hili tunaendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu mwaka wa fedha ulioisha aliweza kutoa fedha na tumeweza kujenga vituo takribani 16 tukavielekeza katika maeneo hususani yenye changamoto hizi.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo mwaka huu wa fedha tunatarajia pia kujenga vituo 13 na tutaelekeza hukohuko kwenye maeneo ambayo yana changamoto hizi. Niwaombe wananchi kwamba tumeanzisha pia programu ya kufundisha vijana ambao tunawaita VJS walioko kwenye maeneo yetu hayahaya tunayoishi, lengo ni kuhakikisha kwamba jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi zitambue namna ya kujikinga na wanyama wakali na waharifu. Tayari tumeshaanza na kila kituo, vile vituo ambavyo tumeshavijenga tayari tumepeleka vijana wanne wanne kila kituo ambao wanatoka katika maeneo husika. Hii inasaidia kwa sababu tumeanzisha utoaji wa ajira katika maeneo hayo lengo ni kudhibiti hao wanyama wakali na waharibifu.

Mheshimiwa Spika, ninaendelea kutoa ahadi kwa wananchi na Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali ipo na inaendelea kulifanyia kazi suala hili kwa nguvu zote na Mheshimiwa Rais analiangalia kwa ukaribu sana, hata mtakumbuka mwaka jana alifanya ziara katika Mkoa wa Simiyu, ahadi yake ilikuwa ni kuajiri askari takribani 600. Tayari tumeshaanza kupata vibali vya kuajiri.

Mheshimiwa Spika, hivi ninavyoongea kuna Askari 271 tayari tumeshapokea vibali vyao ambao watasambazwa katika maeneo yenye changamoto. Kwa hiyo, ninaendelea kuwatoa wasiwasi Waheshimiwa Wabunge kwamba changamoto hii tunaendelea kuiangalia kwa karibu sana na tunaendelea kufikisha huduma kwa wananchi ili tuweze kuokoa maisha ya Watanzania pia na mazao ambayo yameendelea kupata kadhia hii.

Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba ardhi haitoshi na mahitaji ya ardhi ni makubwa, kila mtu anatamani sana kuongezewa maeneo. Tutakumbuka kwamba Mheshimiwa Rais aliruhusu kusamehe vijiji takribani 920 na baadhi ya vijiji hivyo vingi vilikuwa vimesajiliwa ndani ya hifadhi. Tunaposema tunaachia hivi vijiji kwa upande mwingine tunakaribisha changamoto ya wanyama wakali na waharibifu. Niendelee kuwaomba wananchi pale ambapo Kijiji kiliachiwa kikasajiliwa ndani ya hifadhi lakini tunakutana na changamoto hizi, basi tushirikiane pamoja kudhibiti hawa wanyama wakali na waharibifu.

Mheshimiwa Spika, kile tunachotaka sekta ya maliasili na utalii ni kuangalia maeneo mahsusi ambayo ni shoroba za wanyama wakali na waharibifu ambao wanahama kutoka eneo moja kwenda eneo jingine basi tuachie maeneo hayo ili kuruhusu mzunguko wa wanyama kiikolojia waweze ku- move kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Sekunde thelathini malizia mchango wako.

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kulikuwa pia na hoja iliyojitokeza katika Jimbo la Biharamulo ambalo ilielezewa na Mheshimiwa Engineer Ezra Chiwelesa. Kwanza ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwamba kumekuwepo na tuhuma ambazo zinaidhalilisha Serikali, kwamba kuna watumishi ambao wamekuwa wakipokea kiasi kidogo wanaruhusu wananchi wanaenda kulima katika maeneo ya hifadhi. Ninaahidi kwamba hili tutaenda kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, pia nataka nitoe taarifa tu kwamba tarehe 24 Oktoba, 2022 tulikamata baadhi ya wakulima ambao walikuwa wamechangishana fedha na wakataka kumrubuni Mhifadhi wa Biharamulo, taarifa hizi ziko TAKUKURU ninavyoongea na hawa watuhumiwa walifikishwa Mahakamani. Tunachoomba ni ushirikiano, anayetoa rushwa
na anayepokea wote wako matatani. Kwa hiyo, kama wananchi wanashiriki kutoa rushwa ili waende kulima kwenye maeneo yale, sheria zitachukua mkondo wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho kumekuwa na changamoto ya wakulima ambao wanaingia kisirisiri wanalima, tunapoenda kuyazuia yale maeneo tayari wanakuwa wamefika kwenye hatua ya kuvuna, tunaporuhusu sasa kwamba mkimaliza kuvuna sasa msiingie tena, wanaweka kwenye makoti yao mbegu tena ambayo hiyo mbegu anapovuna anapanda tena kule halafu anakuja analalamika kwamba kwa nini tumezuia haya mazao,

Mheshimiwa Spika, kupitia Bunge lako Tukufu hili naomba...

SPIKA: Sawa Mheshimiwa, nilishakuongeza sekunde thelathini naona umejiongeza dakika nyingi zaidi. Haya malizia sentensi yako.

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, tunaomba wakulima tunapozuia basi wasiingie hifadhini kwa sababu haya maeo tunayalinda kwa maslahi ya taifa letu.

Mheshimiwa Spika, naunga hoja. Nashukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)