Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Dr. Dorothy Onesphoro Gwajima

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia kwenye mjadala huu wa Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, kwanza ninawashukuru Wabunge wote ambao wamechangia katika eneo la maendeleo na ustawi wa jamii wakijielekeza kwenye hoja ya mmomonyoko wa maadili unaoathiri mila na tamaduni zetu nchini Tanzania.

Mheshimiwa Spika, naomba kusema kwamba mmomonyoko wa maadili ni jukumu au ni kazi ya taasisi ya familia. Taasisi ya familia ambayo ndiyo chimbuko la watoto inatakiwa kurithisha maadili mema kwa watoto wao. Hivi karibuni kama walivyosema Wabunge wengi kuna kuyumba kwa taasisi hii ya familia ambapo sasa watoto wale hakuna anaewatunza katika malezi na makuzi.

Mheshimiwa Spika, imekuwa taasisi ya familia Baba na Mama na walezi ni rahisi kulea na kutunza na kufuatilia maslahi ya gari wanaloendesha, maslahi ya nyumba waliyoijenga, mali walizonazo kama ni mashamba na vitu vingine kuliko kufuatilia malezi na makuzi ya watoto. Kinachoendelea kwenye familia kwenye suala la mmomonyoko wa maadili, linalochangia maovu mengi sana ukianza ulawiti, ubakaji, kuvuta dawa za kulevya, wizi mpaka tunapata panya road.

Mheshimiwa Spika, nikirudi kwenye suala la ulawiti asilimia 60 ya uovu huu unatokea majumbani. Watoto walawiti wanafundishwa na ndugu zao wa karibu halafu ndiyo wanatoka kwenda kuendeleza mtaani, hofu ya Mungu inakuwa haipo, matokeo yake kila anayekuja na mila yake anapita kokote anapandikiza kwenye kichwa cha hawa watoto lolote lile. Hivyo inabidi taasisi ya familia irudi kwenye misingi yake.

Mheshimiwa Spika, naomba kusema Serikali inafanya nini eneo hili. Serikali imefanya mambo mengi sana na mambo haya tumekuwa tukiyatangaza na kuelimisha katika majukwaa mbalimbali na katika vyombo mbalimbali vya Habari. Kitu cha kwanza kikubwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alichokifanya katika kuangalia mstakabali wa hatma ya Taifa hili kwa miaka mingi ni kuiunda hii Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ili iwekeze nguvu zaidi kuhakikisha masuala ya maendeleo na ustawi wa jamii yanakaa sawa.

Mheshimiwa Spika, ninalishukuru Bunge lako Tukufu pia umeunda Kamati ya Maendeleo na Ustawi wa Jamii ili kuongeza nguvu kushirikiana na Wizara hii na kutoa uongozi katika ajenda zote zilizojadiliwa humu.

Mheshimiwa Spika, naomba pia niseme kwamba Serikali imeendelea na mpango wake wa kutokomeza ukatili kwa wanawake na watoto, ulianza mwaka 2017 umeisha Juni, 2022 sasa tunakwenda kuzindua mwingine wa pili ambako ndani tumeboresha ile mikakati mpaka kwenye Halmashauri zetu kule ajenda hii tumepeleka maelekezo iwe ya kudumu kwenye vikao vyao vyote vya Kijiji, vya Mtaa, vya Kata, kwenye Halmashauri, Kamati zote za Full Council, na Full Council na tutafuatilia kuona utekelezaji wake inajadiliwa vipi.

Mheshimiwa Spika, Sheria Ndogo zitatungwa pamoja na mengine yote taarifa zitawasilishwa sambamba kama tunavyofanya kwenye lishe, tuna mikataba ya utekelezaji masuala ya lishe, hata kwenye masuala ya mmomonyoko wa maadili tutakwenda na sura hiyo ili ku-stimulate haya masuala yaweze kujadiliwa kwa upana wake.

MHE. NICODEMUS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa gwajima kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Nicodemas Maganga.

T A A R I F A

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, napenda kumpa taarifa mchangiaji amezungumzia akina Mama na Watoto, hivi wanaume wenyewe huwa hawapati manyanyaso maana wenyewe hajawazungumzia Mheshimiwa Waziri (Makofi/Kicheko)

SPIKA: Mheshimiwa Waziri taarifa hiyo kutoka kwa Mheshimiwa Maganga unaipokea?

WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, ninaipokea naomba kutoa ufafanuzi.

Mheshimiwa Spika, katika suala hili la ukatili wa kijinsia na kwa watoto kwenye jinsia tunamaanisha jinsia ya ‘ME’ na ‘KE’ kwa hiyo hata kwenye madawati yetu ya jinsia, kama baba amekatiliwa akiripoti pale anahudumiwa kama ambavyo mama atahudumiwa lakini wanaume wamekuwa hawaji wanaona aibu, inabidi huu utamaduni tuubadilishe, wakishaona aibu wanakaa nayo moyoni la kwanza, la pili, la tatu wanachukua kisu wanaumiza au wanaua au wanafanya chochote kile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nilindie dakika zangu mbili.

SPIKA: Mheshimiwa ukipewa taarifa, ni sehemu ya mchango wako. Kwa hiyo, hapa hulindiwi muda wako. Siyo muda wangu unaotumika, ni wakwako. Ahsante sana.(Makofi)

WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSI, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, niendelee?

SPIKA: Dakika moja, malizia mchango wako.

WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSI, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, tuna program ya malezi na makuzo kama Serikali ambayo imeanza 2021 mpaka 2025. Inajielekeza kwenye malezi na makuzi ya watoto sambamba na wazazi, watapata semina jinsi ya kulea watoto wao. Tuna program ya kuwekeza kwenye afya na maendeleo ya vijana balehe kuanzia miaka 10 mpaka 19. Hii nayo ni mwendelezo wa Taifa kusuka mifumo ya malezi na makuzi kwa vijana wake. Pia tuna community centered approach ambapo kampeni za jamii zitafanyika huko huko waliko ili kuhamasisha kaya pamoja na familia ziendelee kufuatilia na kuelimika na kujua juu ya masuala haya.

Mheshimiwa Spika, tuna mambo mengi…

SPIKA: Ahsante sana. Sasa hii hoja ni ya Waziri Mkuu. Kwa hiyo, natarajia ulikusudia kuunga mkono hoja? Siyo!

WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSI, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, hakika naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)