Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Paschal Katambi Patrobas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shinyanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii nami niweze kuchangia katika Bajeti hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia afya njema siku hii ya leo, na pia tangu tulipoanza shughuli hizi za Bunge. Aidha, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan ambaye kwa wakati wote ameendelea kuonesha mfano tangu alipoingia katika madaraka. Katika kipindi cha miaka miwili amefanya kazi kubwa sana ambayo Watanzania wote tunaiona na tunaishuhudia katika maeneo mbalimbali. Hata hivyo miongozo yake, maelezo yake katika utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi, kwa kweli sisi sote ni mashuhuda kwamba Mheshimiwa Rais amedhamiria kutuletea maendeleo katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Makamu wa Rais pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Waheshimiwa Mawaziri wangu Mheshimiwa Joyce Ndalichako na Mheshimiwa Mama Mhagama ambao kwa maelekezo yao wamenisaidia sana katika kutekeleza majukumu yangu pamoja na Katibu Mkuu na Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitakushukuru wewe pamoja na Naibu Spika, Wenyeviti wa Bunge, Wenyeviti wa Kamati za Bunge na Wabunge wote kwa kutusaidia sana katika kutekeleza majukumu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda, nianze kwanza kwa kusema naunga hoja mkono na vile vile kwa sababu ya muda, katika yale yote ambayo Waheshimiwa Wabunge wametoa michango, maoni, mapendekezo na ushauri katika maeneo mbalimbali, niombe tu kwamba yaingie katika Kumbukumbu za Bunge (Hansard) katika taarifa yote ambayo nilipaswa kuiwasilisha.

Mheshimiwa Spika, nitaenda kugusia machache. Mengi tunayachukuwa na tunaenda kuyafanyia kazi kadri tulivyoelekezwa na kushauriwa na Waheshimiwa Wabunge. Lipo suala la fedha za ukarabati wa Vyuo vya Watu Wenye Ulemavu na Utangamao. Ofisi ya Waziri Mkuu imefanya jukumu hilo na ilitekeleza na tumeendelea kutekeleza na mpaka sasa tunavyozungumza, kwa mafanikio makubwa Mheshimiwa Rais ametusadia kuweza kufufua vyuo zaidi ya saba ambavyo vilikuwa viko hoi, kwa zaidi ya miaka 10 vilikuwa havifanyi kazi.

Mheshimiwa Spika, tayari Chuo cha Masiwani Tanga kimefunguliwa, kinafanya kazi na wanafunzi ambao ni Wwatu Wenye Ulemavu tayari wameshaanza kupata mafunzo. Chuo cha Luanzari pale Tabora tayari kimeshaanza kufanya kazi, pia Chuo cha Saba Saba Singida, Mtapika Mtwara, na Chuo cha Yombo. Vyote hivi ni kazi kubwa ambayo Mheshimiwa Rais amefanya kwa ajili ya Watu Wenye Ulemavu.

Mheshimiwa Spika, vile vile, katika maeneo hayo, pia katika hoja nyingi ambazo za Waheshimiwa Wabunge zilizoelekeza kwamba tuangalie katika kutoa unafuu kwa watu wenye ulemavu, nawashukuru sana kwa michango yao, lakini pia Mheshimiwa Rais alitoa fedha zaidi ya Shilingi milioni 60 ambazo zimeendelea kutolewa kwenye mwaka wa fedha kuwasaidia watu wenye ulemavu kupata mafuta yale maalum ya ngozi. Vile vile kana kwamba haitoshi Mheshimiwa Rais kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu na kwa maagizo ya Mheshimiwa Rais na maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, tayari tumeshashaandaa mwongozo maalum ambao unawataka kutoa 3% kwa watu wenye ulemavu ya ajira zote ambazo zinatangazwa. Kama mmeona Mheshimiwa Rais ameendelea kutoa ajira na watu wenye ulemavu tumeendelea kuwapa kipaumbele katika kutoa ajira kwa kufuta mwongozo huo unaotutaka katika ajira zote zinazotangazwa 3% angalau iwe ya watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Spika, pia katika upande ya watu wenye ulemavu, kwenye eneo lingine, tumeweza pia kufanikiwa kupitia Mheshimiwa Rais, ameweza kuchukua Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu (SHIVIAWATA) na yeye mwenyewe aliwaalika Ikulu ya Chamwino na zaidi ya hapo akatoa ahadi ya kutoa kiwanja kwa ajili ya kujenga Makao Makuu ya Watu Wenye Ulemavu hapa Dodoma. Mheshimiwa Rais ameshaanza kutekeleza, ametoa kiwanja chenye thamani ya Shilingi milioni 37 kwa ajili wa utekelezaji wa shughuli za watu wenye ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia lilikuwepo suala lingine la kuhusiana Serikali iweke mikakati ya kukusanya maduhuli kufikia lengo ambalo lilikusudiwa. Katika ukusanyaji wa maduhuli, Ofisi ya Waziri Mkuu tunaipata kupitia vibali vya kazi. Hapa tayari mpango umeshafanywa na tumeshaanza mkakati wa kuangalia namna gani tutaongeza ufanisi katika utekelezaji wa jukumu hilo.

Mheshimiwa Spika, tunatarajia kupata magari 17 ambayo yatafanya kazi ya kufanya ukaguzi kwenye maeneo ya kazi ili kuhakikisha kuna kazi za staha, lakini pia kuna afya na usalama mahali pa kazi na hivyo tutaweza kukusanya tozo na ushuru. Sambamba na hilo, katika sheria yetu inayoratibu ajira za wageni ambayo inataka ada zinazotolewa na watu wanaoomba ajira hawa, wamekuwa wakilipa ada na kwa sababu ya uratibu huu, na kwa sababu ya kufungua makampuni na uwekezaji mkubwa kwa Taifa letu, kumepeleka sasa kuweza kusaidia zaidi kwamba tunaweza tukafikia malengo yaliyokusudiwa kwenye kukusanya maduhuli ambayo tunayakusudia.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mikakati ambayo imewekwa pia ni pamoja na kuongeza kupitia Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora ni pamoja na kuongezea uwezo OSHA kwa maana ya kutoa ajira. Kibali cha ajira kimetoka kwa wafanyakazi zaidi ya 18 ambao tunatarajia wataajiriwa na kuweza kuongeza fedha katika uratibu wa shughuli za OSHA katika maeneo kuhakikisha kwamba lile jukumu la Ofisi ya Waziri Mkuu la kuhakikisha kuna kazi za staha nchini linatekelezwa.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja nyingine kama nilivyoeleza ambazo tutazijibu tu; moja ni hii ya kwamba Serikali iongeze bajeti katika program ya kukuza ujuzi. Lengo la Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2015 kwenda 2025 tunakusudia kutoa mafunzo kwa Watanzania zaidi ya 681, na katika kufanya hivyo itakuwa ni kwa kipindi cha miaka mitano. Tayari Wizara ya Fedha imeji-commit kwamba tutaendelea kupata fedha kwa ajili ya kuhakikisha mafunzo haya yanafanyika. Pia kumekuwa na program mbalimbali za ukuzaji ujuzi ambapo kwa mwaka wa fedha 2021/2022 tulipata zaidi ya Shilingi bilioni tisa ambazo zilienda kuwasaidia vijana wengi wa Kitanzania kuweza kupata mafunzo kwenye maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, pia lilikuwepo suala lingine la kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali katika kutoa program hizi za mafunzo. Wapo wadau wa maendeleo ambao tunashirikiana nao; GIZ, International Labour Organization na IOM ili kuona kam tunaweza kushirikiana katika masuala ya kibajeti ili kuweza kuendelea kuboresha na kuhakikisha kwamba tunapata fursa, na pia kuwapa fursa Watanzania wengi katika kupata mafunzo mbalimbali yanayohusiana na kukuza ujuzi na pia kuwaandaa katika kukabiliana na soko la ajira.

Mheshimiwa Spika, pia lipo suala lingine la fursa za ajira nje ya nchi. Hili tumeshaanza kulifanya. Kama tulivyoeleza pia kwenye hoja za Kamati na Waheshimiwa Wabunge kupitia Wakala wa Ajira Nchini (TAESA) ambapo tayari tumeshasajili na kupitia kamishna wa kazi. Tumeshasajili Wakala wa Ajira ambao wanatafuta ajira ndani na nje ya nchi na kwa kufanya hivyo, tayari tumeingia bilateral agreement na nchi zaidi ya nane ambayo tunaingia nao katika majadiliano ili kuweza kuona namna gani tunaweza kupata fursa zaidi za kuwasaidia Watanzania wengi kuajiriwa nje ya nchi na kutengeneza utaratibu maalum wa kuwasajili wale walio nje ya nchi waliopata ajira ili tuweze remittance ambayo ni sehemu ya mapato pia katika Serikali.

Mheshimiwa Spika, pia kwa kumalizia, lipo suala ambalo Waheshimiwa Wabunge walilizungumzia kuhusiana na kuweka kumbukumbu za hawa watu walioajiriwa nje ya nchi. Tayari tumeshaandaa mfumo maalum wa kieletroniki wa wao kuweza kujisajili na pia tunawasajili wale ambao wanatafutiwa na wakala mbalimbali wa ajira ili kuweza kuwa na kanzidata ambayo itatusaidia katika kuwaratibu na pia kusimamia haki zao huko wanapofanya kazi nje ya nchi. Vile vile kazi zote ambazo ni za nje ya nchi tunataka tuziratibu vizuri ili kuepusha Watanzania wengi kwenda kudhalilishwa ama kuumizwa ama kutendewa matendo yasiyofaa wakiwa nje ya nchi. Hilo ni jukumu ambalo tumeshaanza kulifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kuhusiana na maendeleo ya vijana; hapa katika kuboresha kulingana na michango ya Waheshimiwa Wabunge na Kamati, tayari tumeshadilisha miongozo. Mwongozo wa utoaji wa mikopo ule wa asilimia 10 katika Halmashauri, sasa kijana mmoja anaweza kupata mkopo na ni kuanzia Shilingi milioni 10 mpaka milioni 50. Vile vile kwa watu wenye ulemavu, mikopo hii nayo pia inatolewa kwa mapato ghafi ya Halmashauri na tayari mabadiliko ambayo tumeshayafanya huko, ni kuhakikisha pia watu wenye ulemavu kulingana na changamoto zao, ilikuwa ngumu kufanya kazi wakiwa watano, lakini sasa tumefanya mabadiliko, hata mtu mmoja pia anaweza kupewa mkopo kwenye ngazi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kwenye eneo hilo, Mfuko wa Maendeleo ya Vijana tunazidi kuuboresha sasa tuweze kuona ni namna gani tutawafikia vijana wengi zaidi kuweza kuwasaidia: Kwanza, kuwapa mafunzo kama yale ambayo wanamaliza walio wahitimu wa vyuo vikuu, kuwatambua waliko, kutambua kada mbalimbali ambazo wamezisomea, kuwasajili TAESA na kuwapeleka kwa waajiri ili wakapate mafunzo ya utayari wa kufanya kazi kwa maana ya internship. Tayari tumeshapeleka vijana zaidi ya 6,000 kwenye maeneo mbalimbali na wanachangiwa fedha kidogo na Serikali zaidi ya Shilingi 150,000 kwa mwezi kwa ajili ya kuwaandaa.

Mheshimiwa Spika, lakini vile vile nikimalizia kwa sababu ya muda, mambo ni mengi na kwa sababu hoja hizi tayari ziko hapa ziweze kuingia kwenye Hansard, Mheshimiwa Rais ameendelea kuweka mpango wa kuwaangalia vijana katika maeneo mbalimbali. Fedha za Bodi ya Mikopo, hizo nazo ni fedha ambayo ni sehemu ya kuwasaidia vijana, kuwaratibu. Zaidi ya Shilingi bilioni 570 ziliongezwa, pia fedha za Halmashauri, zote hizi zinawasaidia hao vijana ambao tumekusudia kuwasaidia…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Haya, ahsante sana.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, pamoja na kupeleka mafunzo ya utaifa, uzalendo lakini pia maadili na kuweza kusaidia Taifa kuweza kuwaandaa vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa ya hivi sasa na hata ya baadaye.

Mheshimiwa Spika, ahsante, mengine Waheshimiwa Mawaziri watanisaidia katika kuweza kuyajumuisha.

MHeshimiwa Spika, nakushukuru sana.