Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Jenista Joackim Mhagama

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Peramiho

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kabla sijaendelea ninaomba niunge mkono hoja hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu ambao wameunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Spika, nianze bila kujisahau kumpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo amekuwa akiifanya ndani ya Taifa letu na kwa kweli naungana na Waheshimiwa Wabunge ambao wanatoa wito kwa Watanzania wote kuendelea kumuunga mkono Rais wetu na kuendelea kumtia moyo, kumwombea na kwa kweli kuhakikisha kwamba anatekeleza majukumu yake sawa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi, kama mwanamke na ninaamini wanawake wote wa Tanzania baada ya miaka 60 ya uhuru tumeweka historia ya kuwa na Rais wa kwanza mwanamke. Hatusemi ni Rais wa kwanza mwanamke tu lakini tunasema ni Rais ambaye ana maono makubwa kwa Taifa hili la Tanzania. Kwa hiyo, kwa kweli tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa ajili ya Rais wetu. Tunamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kazi za Rais wetu.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ninaongea hapa kwa kuchangia hoja muhimu ya Bajeti na ni Bajeti yangu ya kwanza toka Mheshimiwa Rais amefanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri nami naomba nimshukuru sana kwa unyenyekevu mkubwa kwa kuendelea kuniamini na kunipa jukumu la kuja kuwa Waziri wa Nchi ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu lakini ninayehudumu katika eneo la Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la Bunge ni eneo ambalo kwa kweli ninajisikia kwamba ninakuja kuwa mtumishi wenu Waheshimiwa Wabunge wenzangu na ninasema mtumishi wenu kwa maana ipi? Kazi yangu nyingine kubwa ni ya uratibu na hapa leo baadhi ya Wabunge wanasema Mheshimiwa Rais alikuja huku, Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuja huku, hiki hakijaenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hizo ni kazi zangu naomba mnitume na nitakuwa mnyamwezi wenu ili ndani ya Serikali tuweze kuongea vizuri pamoja na tunachotaka kwa kweli Waheshimiwa Wabunge mnawawakilisha wananchi. Kwa hiyo, yale ambayo viongozi wetu wakuu wamekuwa wakiyaahidi huko ni wajibu wetu kama Serikali kuyatekeleza na kuhakikisha yanafanyiwa kazi ili ustawi wa wananchi wa Tanzania na Taifa zima viweze kuendelea kwa mbele. Kwa hiyo, ni mtumishi wenu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaomba pia nitumie nafasi hii kumpongeza sana Makamu wa Rais Daktari Mpango kwa kazi kubwa ya kumsaidia Mheshimiwa Rais. Vilevile nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Majaliwa kwa kazi kubwa anayoifanya. Binafsi nina historia ya kufanya kazi pamoja naye, nimefanya kazi na Waziri Mkuu kwa miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Tano; na sasa ninakwenda kwa mwaka mwingine mwaka mmoja Serikali ya Awamu ya Sita na Mheshimiwa Rais amenirudisha tena hapa. Kwa hiyo ninaomba niwahahakikishie yale mnayoyasema wenzangu kuhusu Mheshimiwa Waziri Mkuu ni sahihi, kwa hiyo na yeye tuendelee kumpa nguvu aendelee kumsaidia Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikupongeze wewe, jembe letu Dkt. Tulia Ackson na ninaomba kubwa ili tujenge utaratibu tu ndani ya Taifa hili. Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni.

Mheshimiwa Spika, umeendelea kuliendesha Bunge hili kwa viwango vya kimataifa, umeendelea kuliheshimisha Taifa letu, umeendelea kuwaheshimisha wanawake wa Tanzania, wanaweza. Pia umeendelea kuwaheshimisha wanaume wa Tanzania kwa kukuunga mkono kwa kazi nzuri unazozifanya. Kwa hiyo kwa kweli tunakushukuru sana, tunaona jinsi unavyotekeleza majukumu yako bila upendeleo lakini ukizingatia taratibu, sheria na kanuni zilizowekwa ndani ya Bunge letu. Kwa hiyo nakupongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nampongeza Naibu Spika, tunawapongeza Wenyeviti wetu wa Bunge. Tumeshuhudia hapa Wenyeviti wetu wa Bunge wakiwa wazoevu kweli kweli na wao wakifuata nyayo zako; tunawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli ninaomba binafsi niwapongeze Wenyeviti wote wa Kamati za Bunge kule ambako Wizara yangu imewajibika kwao. Tunaye Mheshimiwa Joseph Mhagama, Makamu wake na Wajumbe wa Kamati yake ya Katiba na Sheria, Mheshimiwa Nyongo, Makamu Mwenyekiti, na Wajumbe wote wa Kamati ya Afya na UKIMWI. Mheshimiwa Fatma Toufiq, Makamu Mwenyekiti wake na Wajumbe wote wa Kamati ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii. Mwisho na si kwa umuhimu Mheshimiwa kaka yangu Sillo Mwenyekiti wa Bajeti, Makamu wake na Wajumbe wote wa Kamati ya Bajeti.

Mheshimiwa Spika, na huko kwenye Kamati ya Bajeti, Ofisi ya Waziri Mkuu imepitisha Bajeti ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; na hapa kabla sijasahau ninaomba nimshukuru sana Daktari Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kipaumbele na kutizama mahitaji ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili liweze kufanya kazi zake vizuri katika kuisimamia Serikali yetu. Kwa hiyo tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais na tunaishukuru sana Kamati ya Bajeti kuendelea kuishauri Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa pacha wangu hapa amenipongeza, na mimi naomba nimpongeze na nimshukuru sana. Ninaomba kumuahidi ushirikiano wa kutosha yeye na Naibu Waziri lakini na timu nzima ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa upande wake. Kwa namna ya pekee nikushukuru sana kaka yangu George Simbachawene, naamini kabisa yale ambayo nimeyakuta umeanza kuyatekeleza kwenye ofisi hii na mimi nitaendelea kuyasimamia na kazi iende mbele na iendelee. Pia nimpongeze Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Mheshimiwa Ummy ambaye kwa kweli tunajivunia, sasa yuko maternity leave kuonyesha akina mama wana uwezo wa kufanya kazi hizo zote, kwa hiyo nampongeza sana kwa kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini Katibu wa Bunge, vilevile Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu na watumishi wote na wakuu wa taasisi zote ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge. Kwa namna ya pekee niwashukuru sana wadau wakubwa wa Ofisi yetu, vyama vya siasa nchini, ninawashukuru sana kwa kazi nzuri, ushirikiano, na kila siku wameendelea kutushauri.

Mheshimiwa Spika, hoja zilizoletwa ni nyingi lakini tutazijibu zile ambazo tunaweza kuzijibu hapa, hoja nyingine zitajibiwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu mwenye hoja na hoja zingine tutaziwasilisha kwako kwa maandishi.

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza, nimesema hapa ninampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini ninaomba niyaseme kwa ufupi yote ambayo nafikiri ni ya muhimu na baadaye nitaanza kuyachambua moja baada ya nyingine kama muda utaniruhusu.

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza ninaomba Wabunge wote tuinuke na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa namna yoyote tunayoweza kwa maamuzi na maono yake ya falsafa yake ya 4R ambayo ameanza nayo ndani ya nchi hii. Tumeshuhudia kwa kutumia falsafa hiyo Taifa letu limeingia kwenye maridhiano na kutafuta suluhu katika kila jambo, tunampongeza sana Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kwa kutumia falsafa hiyo tumeweza kujenga Taifa hili likiwa na ustahimilivu; na kila mmoja amekuwa ni mstahimilivu kwa mwenzake, kuanzia vyama vya siasa lakini hata Watanzania kwa namna moja ama nyingine, Mheshimiwa Dkt. Samia tunakupongeza sana kwa falsafa hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeshuhudia Mheshimiwa Rais wetu amekuja pia na falsafa ya reform, kuleta mabadiliko. Katika falsafa hii tumeshuhudia mabadiliko makubwa ya kiuongozi, kidemokrasia na ya kiuchumi ndani ya Taifa letu na mahusiano ya kimataifa, hongera sana Dkt. Samia Suluhu Hassan. Tumeona falsafa hii inataka kutujenga upya; kwa hiyo kila Mtanzania aonje kwamba ni muumini wa jambo hili.

Mheshimiwa Spika, nitoe wito kwa Watanzania wote, tuunge mkono falsafa ya Dkt. Samia ya 4R katika kuhakikisha Taifa letu linasonga mbele na hasa wale wote ambao ni wadau wakubwa wa demokrasia na siasa katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, ninaomba nikuhakikishie kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, katika kipindi hiki kifupi tulipata maoni ya kutosha sana kutoka Waheshimiwa Wabunge kuona ni namna gani pamoja na jukumu la kimuundo la Ofisi ya Waziri Mkuu kufanya kazi ya kuratibu shughuli za Serikali.

Mheshimiwa Spika, lakini kulikuwa na jambo hapo katikati ambalo lilikuwa halijakaa sawa, nalo ni jambo la ufanyaji wa tathmini na ufatiliaji wa shughuli za Serikali kila siku hapa nchini. Ninaomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kupitia bajeti yetu ya mwaka huu maamuzi ya Serikali, kwa maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tayari sasa imeanzishwa idara maalum chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu itashughulika na suala zima na tathmini na ufatiliaji wa masuala na sekta zote ndani ya Serikali katika utendaji kazi wa kila siku. Kwa hiyo naomba tumpongeze sana Mheshimiwa Rais, na pia tumpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi nzuri.

Mheshimiwa Spika, vilevile katika kipindi hiki nasema ni kwa nini tunaendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais na Waheshimiwa Wabunge wamechangia hapa ndani, ilikuwa ni namna gani tunajipanga kukabiliana na maafa kwa namna moja au nyingine, ikiwemo magonjwa haya ya mlipuko ambayo yamekuwa yakijitokeza. Naomba niwahakikishie kwenye bajeti ya mwaka huu ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu tumeanzisha kitengo maalum cha dawati moja la afya katika kushughulikia uratibu wa sekta zote pale yanapotokea magonjwa ya mlipuko ili tuweze kukabiliana nayo na kuangalia usalama wa wananchi wa Tanzania. Kwa hiyo jambo hili pia limefanyiwa kazi vizuri.

Mheshimiwa Spika, tumefanya kazi nzuri pia na Waheshimiwa Wabunge wamechangia kwenye eneo zima la lishe, tumeshaanza kujitengenezea uratibu na kujiratibu ndani ya Serikali hasa katika kuitizama Sera ya Lishe. Nilimsikia hapa mdogo wangu Neema amezungumza sana jambo hili ni jambo la mtambuka, na naomba nimwakikishie mdogo wangu Mheshimiwa Mbunge Neema, Wizara ya Afya pamoja na Ofisi ya Waziri Wakuu sasa tunaanza mkakati rasmi wa kuhakikisha Sera hiyo ya Lishe inafanyiwa kazi na tunakuwa nayo.

Mheshimiwa Spika, vilevile sio Sera ya Lishe tuna sera nyingine muhimu ambazo tuliagizwa, kwa mfano Sera ya UKIMWI na Sera ya Dawa za Kulevya; hayo yote tumeyapa kipaumbele kama Wabunge walivyotushauri kwenye bajeti yetu.

Mheshimiwa Spika, kwenye eneo lingine ambalo tumefanya kazi nzuri ni mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya nchini. Sasa hivi tumeanza kuona kwamba changamoto za kimaadili zinachukua taswira na sura tofauti. Ningeomba tu nitoe wito kwa wananchi wa Tanzania na Waheshimiwa Wabunge, tunaposhughulika na changamoto za kimaadili hizo nyingine tusisahau bado tuna tatizo la UKIMWI na pia tuna tatizo la matumizi ya dawa za kulevya ambazo pia zinaletea uvunjivu mkubwa wa maadili.

Mheshimiwa Spika, kwa nafasi ya pekee niwapongeze sana mamlaka iliyopewa dhamana ya kupambana na dawa za kulevya hapa nchini. Na kama Waheshimiwa Wabunge walivyosema na Kamati ilivyotushauri kwa sababu wameendelea kufanya kazi ya kutosha kwenye maeneo yote manne ya kimkakati katika kupambana na matumizi ya dawa za kulevya.

Mheshimiwa Spika, eneo la kwanza ni eneo la supply reduction, kwa maana nyingine kupunguza uingizaji wa dawa za kulevya. Hapo wamefanikiwa kufanya operation mbalimbali za kukamata hao ambao wanatuingizia dawa hapa nchini. Tayari watuhumiwa 7,113 tumewakamata; ni kazi nzuri iliyofanywa na mamlaka yetu.

Mheshimiwa Spika, vilevile wameweza kufanya kaguzi 149 katika maeneo mbalimbali yanayofanya biashara ya kemikali bashirifu. Tumegundua sasa hivi kadiri tunavyoendelea kudhibiti uingizaji wa dawa za kulevya hawa wafanyaji biashara wa dawa za kulevya wanatafuta aina za dawa mbadala na kuendelea kuangamiza kizazi cha Taifa letu. Kwa hiyo tumeendelea kufanya ukaguzi kuhakikisha hata kemikali bashirifu haziwezi kutumika kuwa ni alternative ya matumizi ya dawa za kulevya nchini.

Mheshimiwa Spika, tumefanya maboresho ya sheria, na hapa ninaomba niinue sauti yangu kuishukuru sana Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika eneo ambalo limesaidia kupunguza madhara makubwa ya vijana wetu kwenye matumizi ya dawa za kulevya ni utungwaji wa sheria kali, sheria ngumu, ambayo kwa kweli imesaidia sana kupunguza madhara haya. Ninaomba Waheshimiwa Wabunge, tukiona sheria hii tuliyoiboresha bado haikidhi vigezo vya kupambana na matumizi ya dawa za kulevya mtukubalie tulete tena humu ndani ya Bunge tuendelee kuibadilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki kifupi tumeweza pia kuteketeza mashamba ya bangi ekari 1,133, ili kuhakikisha kwamba tunakuwa salama. Tumefanya kazi nzuri kwenye demand reduction, uelewa na utoaji wa elimu kuhusu matumizi ya dawa za kulevya.

Mheshimiwa Spika, vilevile tumefanya kazi nzuri kwenye masuala ya harm reduction, yaani kupunguza madhara na eneo hili tumeendelea na tiba ya methodin, na pia tumeendelea na huduma za Multiclinics na bajeti hii tutaongeza ujenzi wa multi-clinics nyingine tatu.

Mheshimiwa Spika, tumefikiri sasa tuanze kuwa na rehabilitation center ambazo zinamwondoa mtu kwenye matumizi ya dawa zinamwingiza katika kujifunza ujuzi ili akitoka pale akajiajiri na akafanye kazi vizuri.

Mheshimiwa Spika, tunawashukuru sana Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi wameweza kuchukua vijana 245 kwenye program ya kukuza ujuzi, hawa ambao wamekuwa wakitumia dawa za kulevya na wameacha matumizi na wamefundishwa ujuzi.

Mheshimiwa Spika, lakini tunaendelea kufanya ushirikiano wa kinchi, kikanda na kimataifa ili kuhakikisha jambo hili mtambuka tunalifanyia kazi. Tumefanya kazi nzuri kwenye Tume ya Kudhibiti UKIMWI tumeshafanya mapitio na tathmini ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nne wa Kudhibiti UKIMWI, na tayari tumeshaanda mkakati wa tano wa kudhibiti UKIMWI. Na hapa naomba tukumbushane; mnakumbuka mkakati uliopita ulibainisha kwamba changamoto kubwa ilikuwa ni wanaume hawataki UKIMWI na kutumia dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI. Kwa hiyo tunataka kuona utafiti utakaofanyika na ambao umeendelea kufanyika safari hii utatusaidiaje kupambanua changamoto hizo.

Mheshimiwa Spika, changamoto nyingine ilikuwa ni maambukizi makubwa kwa vijana. Kwa hiyo katika mkakati wa tano tutaongeza nguvu zaidi kuhakikisha vijana na nguvu kazi ya Taifa iweze kuwa salama.

Mheshimiwa Spika, maeneo mengine ambayo tuliambiwa na Waheshimiwa Wabunge na hasa Kamati kwa mfano ni matumizi ya Ofisi ya Msajili wa Vyama tunayoijenga. Ninaomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kuwa ofisi hiyo itakuwa na tija. Hapo ndipo tutakuwa ni kitovu kikubwa cha mahusiano na ushirikiano wa Baraza la Vyama vya Siasa Nchini kushauriana na kujenga muafaka katika kuendesha siasa kwenye Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, ofisi hiyo pia ina uwezo wa kutumika kama ni kituo cha kutoa elimu vilevile hata kuwa kitega uchumi kuongeza mapato kwa ajili ya Baraza la Vyama vya Siasa.

Mheshimiwa Spika, pia tumeombwa tuhakikishe tunajenga Kiwanda cha Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali, tunaishukuru Serikali imetoa fedha bajeti iliyopita na bajeti hii tumepata fedha. Hapa ninaomba kutoa wito kwa taasisi zote za Serikali kutofanya machapisho ya document zozote za Serikali nje, na badala yake sasa zipelekwe kwenye kiwanda chetu cha Serikali cha Mpiga Chapa. Hilo ni jambo muhimu na ninaamini ni lazima tulisimamie sana.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge, wametushauri Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali sasa awe Wakala; ninaomba kuwadhibitishia mchakato umeanza na ndani ya mwaka wa fedha wa 2023/2024 tutakamilisha na tunamfanya huyu atakuwa ni wakala ili aweze kushindana kwenye soko la ushindani kama wengine wanavyofanya ndani ya Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ilikuwa ni kuhakikisha tunakuwa na miradi ya maendeleo na hasa kwenye mamlaka ya kudhibiti dawa za kulevya nchini. Kama nilivyosema mwanzo, mwaka huu tumepata fedha ya maendeleo, tuna bilioni sita fedha za nje na biliioni mbili fedha za ndani. Nimesema hapo mwanzo kwamba kazi yetu ni kujenga Multiclinics vilevile tutajenga rehabilitation center hapa Dodoma ya mfano, ambayo itawaondoa waraibu kwenye kutumia dawa, inawapeleka katika kujifunza ujuzi waweze kujiajiri na kuacha tabia hizo za matumizi ya dawa za kulevya.

Mheshimiwa Spika, ATF tuliulizwa hapa mfuko wa UKIMWI, kwamba Serikali imejipangaje; tumefanya kazi nzuri Serikali imeweza kutoa fedha ya ziada kabisa tumepata bilioni moja milioni mia nane themanini. Pia Serikali itaendelea kutenga fedha. Tulichokifanya ni kuwaambia TACAIDS kupitia sheria lakini kupitia mameneja ambaye ameajiriwa kuongeza mapato ya mfuko atengeneze mpango mkakati wa kuhakikisha mfuko unatuna na pia tunajenga uwezo wa ndani wa kupambana na UKIMWI badala ya kuendelea kuwa tegemezi. Kwa hiyo jambo hilo pia tumelifanyia kazi ya kutosha.

Mheshimiwa Spika, tumekubaliana ndani ya Serikali wale wasichana ambao wamekuwa wakifanya kazi ambazo si za staha tutashughulika nao pia kuona ni namna gani tunawaondoa huko na tunawafundisha ujuzi ili waweze kujiajiri na kuweza kujitegemea.

Mheshimiwa Spika, la mwisho labda na si kwa umuhimu, nimepokea maombi ya Mheshimiwa Miraji Mtaturu, ameomba hapa kuangalia majina ya majimbo katika eneo analotoka. Ibara ya 74(6)(c) na Ibara ya 75 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, imeipa jukumu Tume ya Uchaguzi kuratibu, kutathmini na kujenga mipaka ya majimbo nchini. Kwa hiyo tulikuwa tunaomba tu itakapofika muda Mheshimiwa Kingu na Mheshimiwa Mtaturu basi mtuletee mapendekezo ya majina ya hayo majimbo, na hasa kama hayatakuwa na gharama ya kuyagawa na kuyapanga upya basi tunaweza kuangalia tu jina liweze kulingana na sifa na stahiki ya matakwa ya wananchi. Kwa hiyo tutapokea na tutakapopokea basi tutaweza kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda ninaomba niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yenu na ninaomba niwaahidi kwa niaba ya watumishi wote kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu tutaendelea kufanya kazi pamoja na nyie, tutaendelea kuratibu shughuli za Serikali, tutaendelea kusikiliza kero za wananchi na kuzifanyia kazi na tutaendelea kufatilia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Spika, nakushuru sana, narudia tena kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja ahsanteni sana kwa kunisikiliza. (Makofi)