Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Kassim Majaliwa Majaliwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ruangwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa fadhila zake ambazo zimetuwezesha kukutana kwenye Kikao hiki cha Sita cha Mkutano wa Kumi na Moja wa Bunge la Kumi na Mbili kwa ajili ya kuhitimisha mjadala kuhusu Hoja ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

Mheshimiwa Spika, mbili, kipekee nakushukuru sana wewe binafsi, pia Mheshimiwa Naibu Spika na Wenyeviti wote wa Bunge kwa kuliongoza kwa umahiri Bunge lako Tukufu wakati wa mjadala kuhusu Hoja ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2023/2024 tangu nilipowasilisha hoja hii.

Mheshimiwa Spika, tatu, natoa shukrani zangu za dhati kwa Wajumbe wa Kamati za Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria chini ya Mwenyekiti Mheshimiwa Dkt. Joseph Kizito Mhagama, Mbunge wa Madaba. Pia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti chini ya Mwenyekiti Mheshimiwa Daniel Baran Sillo, Mbunge wa Babati Vijijini pia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI chini ya Mwenyekiti Mheshimiwa Stanslaus Haroon Nyongo, Mbunge wa Maswa Mashariki na Kamati ya Kudumu ya Bunge, Ustawi na Maendeleo ya Jamii chini ya Mwenyekiti Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum kwa kazi kubwa waliyoifanya ikiwemo kutoa michango yenye tija kwenye hoja ya Waziri Mkuu, nawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nne nitumie fursa hii pia kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mawaziri wa Sekta na Naibu Waziri waliochangia hoja ya Bajeti ya Waziri Mkuu, kadhalika nawashukuru Makatibu Wakuu na Naibu Katibu Mkuu, Wakuu wa Idara, Mashirika, Wakala na Taasisi zote za Serikali kwa ushirikiano wao mkubwa wa kujitoa kwao katika kufanikisha Hoja ya Bajeti ya Waziri Mkuu, Taasisi zake pamoja na Mfuko wa Bunge.

Mheshimiwa Spika, tano, vile vile niwashukuru kwa dhati watumishi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kazi nzuri waliyoifanya na ushirikiano wanaoendelea kunipatia katika kipindi cha maandalizi hadi tunapoelekea kuhitimisha mjadala wa Hoja ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sita, napenda pia kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge, wenzangu wote kwa hoja na michango yenu muhimu yenye nia ya kuimarisha utendaji wa Serikali. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, kuwa michango yenu itakuwa chachu katika kutekeleza kikamilifu wajibu wetu wa Kikatiba na vipaumbele vilivyoainishwa katika Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2023/2024.

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwashukuru wananchi wote kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge 101 wamechangia Hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu wakati wa mjadala huu kati yao Waheshimiwa Wabunge 10 walichangia kwa njia ya maandishi.

Mheshimiwa Spika, natoa shukrani zangu za dhati kwa Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja ya Waziri Mkuu. Aidha, kutokana na ufinyu wa muda naomba uridhie nisiwataje mmoja mmoja kwa majina na badala yake majina yao yaingizwe moja kwa moja kwenye Hansard. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati nikiendelea na mjadala wa Hoja ya Waziri Mkuu. Serikali imetoa majibu ya hoja nyingi zilizowasilishwa na Waheshimiwa Wabunge, kupitia Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri, hata hivyo kutokana na ufinyu wa muda Serikali itatoa majibu yenye ufafanuzi zaidi kuhusu hoja zilizosalia kwa maandishi, lakini vile vile Waheshimiwa Mawaziri, wataendelea kutoa ufafanuzi wa kutosha wa baadhi ya hoja zilizoibuliwa kwenye mjadala huu wakati wakiwasilisha hoja ya bajeti za sekta zao.

Mheshimiwa Spika, pongezi kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tarehe 4 Aprili, 2023 katika Mkutano wake wa Kumi na Moja, Kikao cha Kwanza, Bunge lako Tukufu liliazimia kwa pamoja kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuimarisha demokrasia na kukuza diplomasia ya uchumi hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, nami nitakuwa mchoyo wa fadhila endapo sitaungana na Waheshimiwa Wabunge, wenzangu kumshukuru kwa mara nyingine tena Mheshimiwa Rais, kwa juhudi zake katika kuhakikisha kuwa ustawi wa demokrasia nchini sambamba na kuhimarisha miundombinu ya kiuchumi na kijamii ili kuwaletea maendeleo Watanzania.

Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia falsafa yake ya maridhiano, ustamilivu, mageuzi na mabadiliko ameonyesha wazi na tena kwa vitendo nia yake ya kuifanya Tanzania kuwa moja, salama na bila kundi lolote kuwa nyuma katika kufurahia demokrasia ya kweli hapa nchini. Kwa lugha nyingine amefanikiwa kuendeleza misingi aliyoipokea kutoka kwa watangulizi wake na Waasisi wa Taifa hili ya kukaa pamoja na kushirikiana katika kutafakari, kujadili na kutafuta suluhu ya mambo yanayotuhusu na hivyo kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa.

Mheshimiwa Spika, nasi tukiwa wawakilishi wa wananchi tumefanya jambo la msingi kutumia jukwaa hili adhimu kabisa katika kumuunga mkono Mheshimiwa Rais, katika kuimarisha demokrasia nchini. Niendelee kuwaomba Waheshimiwa Wabunge wenzangu, tuendelee kuenzi mfumo wa kujadiliana, kukosoana na kutumia Bunge hili Tukufu kuibua mijadala kitaifa pamoja na kuikosoa na kuirekebisha Serikali pale inapobidi.

Mheshimiwa Spika, vile vile nikishukuru Kituo cha Demokrasia Nchini (TCD) kwa kuendelea kumuunga mkono Mheshimiwa Rais, katika kuimarisha demokrasia pamoja na kutatua changamoto za maendeleo ya demokrasia hapa nchini. Sambamba na (TCD) inalishukuru sana pia Baraza la Vyama vya Siasa Nchini kwa kuendelea kuhimiza siasa za kistaarabu zinazozingatia sheria na maslahi ya nchi kwa ujumla na kuimarisha uhusiano mzuri baina ya Vyama vya Siasa hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, tangu kuundwa kwake mwaka 2009, Baraza la Vyama vya Siasa limefanya mambo mengi katika kuhakikisha kunakuwa na siasa za kistarabu zinazozingatia sheria na maslahi ya nchi kwa ujumla na kuimarisha uhusiano mzuri baina ya Vyama vya Siasa. Aidha, Baraza limekuwa kiungo muhimu katika kufanikisha kuundwa kwa kikosi kazi cha Mheshimiwa Rais, ili kushauri masuala mbalimbali ya kuboresha demokrasia ya vyama vingi hapa nchini kwetu.

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kutoa rai kwa Baraza la Vyama vya Siasa, kuendelea kufanya kazi kwa karibu na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Serikali Kuu na wadau wengine wa Demokrasia ya Vyama vingi ikiwemo Taasisi zisizokuwa za Serikali na zile za Serikali kama Jeshi la Polisi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar na Bunge. Serikali kwa upande wake itaendelea kushirikiana na Baraza la Vyama vya Siasa na wadau wote muhimu katika kujenga mustakabali mwema wa demokrasia yetu Tanzania.

Mheshimiwa Spika, nianze kuzungumzia huduma za elimu. Nyote mtakubaliana nami kwamba Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kufanya marekebisho ya mazingira kujifunzia na kufundishia kuanzia elimu ya msingi hadi elimu ya juu. Sote tumeshuhudia maboresho makubwa yaliyofanywa katika shule zetu za sekondari, vyuo vya kati na vile vya elimu ya juu hususani katika ujenzi na ukarabati wa miundombinu na upanuzi wa taasisi hizo.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, kwa upande wa sekondari kwa mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imefanikiwa kujenga vyumba vya madarasa elfu ishirini na kuwezesha wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa mkupuo mmoja kwenda shule. Licha ya mafanikio hayo kwa upande wa elimu ya sekondari katika kipindi cha hivi karibuni tumekuwa tukishuhudia uwepo wa changamoto za msongomano wa wanafunzi wa shule za msingi kwa baadhi ya maeneo, mathalani kati ya shule za msingi 17,000,182 zilizosajiliwa shule 10,000,804 sawa na asilimia 62.87 zina msongamano mkubwa wa wanafunzi.

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie mpango wa Serikali kuboresha elimu kwenye shule za msingi. Kufuatia hali hiyo Serikali imeanza kutekeleza mpango wa maboresho makubwa ya elimu msingi. Pamoja na mambo mengine mpango huo unalenga kuondoa changamoto ya msongamano wa wanafunzi kwenye shule za msingi na kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia. Hadi kufikia Machi, 2023, Serikali imetoa shilingi bilioni 230 kwa halmashauri zote nchini kwa ujenzi wa shule mpya za msingi 302, ujenzi wa vyumba vipya vya madarasa 3,338 kwenye shule za msingi zenye msongamano mkubwa wa wanafunzi.

Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine maboresho haya yameenda sambamba na ukarabati wa shule nane za msingi na ujenzi wa nyumba 41 za Walimu. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa watoto wetu wanapata mazingira rafiki ya kujifunzia ili waweze kutimiza zao na falsafa kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, katika hatua nyingine Serikali imetenga shilingi bilioni saba kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vilivyoboreshwa vya mafunzo ya elimu ya awali na mafunzo ya kuwajengea uwezo Walimu wa madarasa ya awali. Kupitia mpango huu madarasa 7,000 ya elimu ya awali yatashehenezwa na vifaa mbalimbali na Walimu zaidi ya 34,000 wa elimu ya awali watajengewa uwezo kuhusu matumizi ya vifaa hivyo pamoja na mbinu bora za ufundishaji.

Mheshimiwa Spika, hatua hizo zinatekelezwa sanjari na mpango wa miaka mitano ya mafunzo endelevu ya Walimu kazini (MEMKWA). Lengo ni kuboresha utendaji wa Walimu darasani na ujifunzaji wa wanafunzi ambapo Walimu wote wa shule za msingi watanufaika na mpango huo.

Mheshimiwa Spika, naomba nianze kutoa majibu ya hoja mbalimbali. Kwa mujibu wa Kanuni ya 118 kipengele cha 13 cha Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Februari, 2023, naomba nitumie nafasi hii kujibu na kufafanua baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge zilizoibuliwa wakati mjadala kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hoja ya kwanza ilikuwa ni Wakurugenzi wa Halmashauri wanazitumia fedha za Mfuko wa Jimbo kinyume cha sheria. Fedha hizi hazitumiki kwa kuzingatia vipaumbele vilivyopitishwa na Kamati ya Mfuko wa Jimbo hasa Maafisa Manunuzi kuzuia ununuzi wa vifaa vilivyopendekezwa na Mheshimiwa Mbunge kununuliwa. Je, Mfuko wa Jimbo ni wa Mbunge au ni wa Mkurugenzi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jibu hapa ni kwamba, moja ya hoja iliyoibuka wakati wa kuchangia Bajeti ya Waziri Mkuu ni kuhusu fedha hizi kutokutumika kwa kuzingatia vipaumbele vilivyopitishwa na Kamati ya Mfuko wa Jimbo hasa kutokana na Maafisa Manunuzi kuzuia ununuzi wa vifaa vilivyopendekezwa kununuliwa.

Mheshimiwa Spika, naomba nilikumbushe Bunge lako Tukufu kwamba, Fedha za Mfuko wa Jimbo zinasimamiwa na Sheria ya Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo, Sura Na.99 na imeeleza kinagaubaga kuwa usimamizi wa fedha za Mbunge wa Jimbo utafanyika kupitia Kamati ya Mfuko wa Jimbo hilo ambayo Mwenyekiti wake ni Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo hilo na Katibu wake ni Afisa Mipango wa Halmashauri husika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa lugha nyingine Mheshimiwa Mbunge, ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Mfuko wa Jimbo inayoratibu miradi na shughuli zitakazoelekezwa kupitia Mfuko huo na pia ndiye mwenye mamlaka ya kuitisha vikao vya Kamati hiyo. Kwa upande wake Kamati inalo jukumu la kupokea, kujadili na kupitisha vipaumbele vya matumizi ya fedha za Mfuko huo wa Jimbo kama ilivyokubaliwa na hakuna kikao ambacho kitakaliwa nje ya Mwenyekiti ambaye ni Mbunge wa Jimbo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ni Afisa Masuuli na anao wajibu wa kusimamia na kuhakikisha kwamba fedha za Mfuko za Jimbo zinaelekezwa kwenye vipaumbele vilivyopitishwa na Kamati ya Mfuko wa Jimbo ambayo Mwenyekiti ni Mbunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kadhalika sheria inataka ununuzi wa bidhaa, kazi na huduma kwa kutumia fedha za mfuko ufanyike kwa kuzingatia Sheria ya Manunuzi, Sura Na.410 na kwa msingi huo nitumie nafasi hii kuwaelekeza Wakurugenzi wote wa Halmashauri kuheshimu na kuzingatia vipaumbele vinavyopitishwa na Kamati ya Mfuko wa Jimbo pamoja na kuhakikisha matumizi ya fedha hizo yanazingatia Sheria ya Mfuko wa Jimbo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile pia ipo Sheria ya Fedha za Umma, Sura ya 348 na Sheria ya Manunuzi, Sura 410. Aidha, nimemwelekeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuhakikisha kuwa Maafisa Manunuzi kwenye Halmashauri hawawi vikwazo katika kufanikisha utekelezaji wa vipaumbele vya matumizi ya Fedha za Mfuko wa Jimbo hususani upatikanaji wa vifaa kwa mujibu wa Sheria ya Manunuzi ya Umma. Pia halmashauri isifanye maamuzi yake nje ya Uenyekiti wa Mbunge ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja ya pili ni Mikopo kwa Makundi Maalum. Kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge kuhusu kiasi kidogo cha fedha za mikopo kinachotolewa kwa Makundi Maalum ya Vijana, Wanawake na Wenye Ulemavu kutokidhi matakwa ya kuyainua makundi hayo kwa kufanya shughuli za uzalishaji au biashara. Aidha, kumekuwa na changamoto kwenye baadhi ya halmashauri kutoa fedha hizo kwa Watumishi wa Halmashauri au wakati mwingine vikundi hewa badala ya walengwa na kusababisha fedha za mikopo hiyo kutorejeshwa.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia malalamiko hayo na maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu matumizi mabaya ya fedha hizo, nazielekeza sasa halmashauri kote nchini kusitisha utoaji wa fedha za mikopo hiyo zitakazotokana na makusanyo ya kuanzia mwezi Aprili hadi Juni mwaka 2023, wakati Serikali inajipanga kwa mfumo mpya wa utoaji wa mikopo hiyo utakaoelekezwa kabla ya mwezi Juni mwaka huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ni Serikali kuwa tayari kuchukua hatua pale majanga yanapotokea kama ilivyoainishwa kwenye sheria kuendana na uhalisia.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeandaa Mpango wa Taifa wa Kujiandaa Kukabiliana na Maafa kwa mwaka 2022 ambao umezingatia viashiria vya maafa nchini, mifumo ya kitaasisi, mahitaji na maendeleo katika shughuli za kujiandaa na kukabiliana na majanga kitaifa. Mpango huu umewezesha utekelezaji wa shughuli za kujiandaa na kukabiliana na maafa kwa kuzingatia taasisi yenye jukumu la msingi na ushirikiano wa sekta na taasisi zisizokuwa za kiserikali kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya mwaka 2022.

Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo Wizara, Idara, Taasisi za Serikali, Tawala za Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa zinahimizwa kushughulikia maafa katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na kujumuisha katika Mipango ya Bajeti zao hatua za kuzuia na kupunguza madhara ya majanga na kujiandaa kukabiliana na maafa kwa mujibu wa sheria husika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ilikuwa ni Serikali iweke mkakati maalumu wa kujumuisha watu wenye ulemavu kwenye program ya Taifa ya Kukuza Ujuzi chini ya program nyingine ili kuhakikisha kuwa fursa kwa wenye ulemavu zinaimarishwa.

Mheshimiwa Spika, jibu hapa ni kwamba Serikali imeandaa mwongozo wa utekelezaji, ujumuishwaji na uimarishwaji wa huduma kwa watu wenye ulemavu wa mwaka 2022 kwa lengo la kuhakikisha ujumuishwaji wa masuala ya watu wenye ulemavu kwenye programu, miradi na mipango mbali mbali ya maendeleo katika sekta zote za uchumi na kijamii.

Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa programu ya Taifa ya kukuza ujuzi, watu wenye ulemavu wamekuwa wakijumuishwa kwa kuhakikisha kuwa matangazo yote ya fursa za mafunzo yanatafsiriwa kwa lugha rafiki na kupelekwa kwenye vyama vya Watu Wenye Ulemavu na kwa Maafisa wa Ustawi wa Jamii na Maafisa wa Maendeleo ya Jamii waliopo katika Halmashauri na Vyombo vya Habari. Mathalani katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023 jumla ya vijana walemavu 1,171 wamenufaika na programu za kukuza ujuzi zinazoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.

Mheshimiwa Spika, sambamba na masuala ya ujuzi, Serikali inahakikisha watu wenye ulemavu wanapewa upendeleo maalum katika masuala ya ajira pamoja na kuimarisha miundombinu mbalimbali na kuifanya kuwa rafiki kwa mahitaji yao. Kwa mfano, katika kutekeleza mpango wa maboresho ya elimu ya msingi kwa mwaka 2022/2023 Serikali inajenga vyumba vya madarasa 41 kwa watu wenye mahitaji maalum.

Mheshimiwa Spika, vilevile chini ya Mpango wa Maendeleo ya Ustawi wa Taifa wa Mapambano dhidi ya UVIKO-19 Serikali yetu imetumia Shilingi Bilioni 3.46 kwa ajili ya ukarabati wa Vyuo Vinne vya Ufundi Stadi na marekebisho ya Rwanzari kule Mkoani Tabora, Sabasaba Mkoani Singida, Mtapika Mkoani Mtwara na Yombo Mkoani Dar es Salaam. Ukarabati huo umewezesha vyuo hivyo kuongeza uwezo wa udahili wanafunzi wenye mahitaji maalum kutoka 407 kabla ya ukarabati na kufikia 800. Aidha fani zilizokuwa zinatolewa awali zimeongezeka kutoka Tatu hadi 10.

Mheshimiwa Spika kama utakavyoona Serikali imeendela kutoa fursa za upendeleo maalum kwa watu wenye mahitaji maalum, katika kuingia kwenye programu ya Taifa ya kukuza ujuzi, chini ya programu nyingine ili kuwawezesha kujikwamua kiuchumi na kujiletea maendeleo.

Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ni juu ya hoja kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), itakumbukwa kuwa Tarehe 29 Machi, 2023 Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) aliwasilisha kwa Mheshimiwa Rais, Taarifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2022. Uwasilishwaji huo ni takwa la Kikatiba kwa mujibu wa Ibara ya 143 kipendele cha (4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Sheria ya Ukaguzi wa Umma, Sura Na. 418.

Mheshimiwa Spika, taarifa hiyo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali iliainisha baadhi ya maeneo ambayo yalikuwa na viashiria vya usimamizi usioridhisha wa mali na fedha za umma. Maeneo hayo ni pamoja na matumizi mabaya ya mikopo ya Halmashauri, kasoro za utekelezaji wa miradi na baadhi ya mifumo kutosomana.

Mheshimiwa Spika, wakati wa mjadala wa hoja ya Waziri Mkuu ya mapitio ya utekelezaji wa kazi za Serikali ya mwaka 2022/2023 na mwelekeo wa kazi zake kwa mwaka 2023/2024. Waheshimiwa Wabunge wenzangu sambamba na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya hawakuweza kuficha hisia zao kuhusu mwenendo usioridhisha wa uwajibikaji kwa baadhi ya Viongozi na Watendaji ndani ya Serikali, kama ilivyoonesha katika taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali.

Mheshimiwa Spika, Tarehe 06 Aprili 2023, taarifa hiyo ya Mdhibiti na Mkaguzi na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali iliwasilishwa hapa Bugeni ikiwa ni utekelezaji wa takwa la Kikatiba linaloielekeza Serikali kuwasilisha Bungeni taarifa hiyo ndani ya siku Saba za kazi kuanzia siku ya Kikao cha Kwanza cha Bunge tangu kuwasilishwa kwake kwa Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Spika, binafsi ninatambua hisia za Waheshimiwa Wabunge pamoja na wananchi kwa ujumla, kuhusu ubadhilifu wa mali na fedha za umma uliobainishwa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Aidha, sote tulishuhudia hisia na namna Mheshimiwa Rais alivyoonesha kutoridhishwa na ubadhilifu uliobainishwa katika taarifa hiyo.

Mheshimiwa Spika, kufuatia hali hiyo na wakati huu ambapo Bunge lako tukufu linaendelea na taratibu zake za kufanyia kazi hoja zilizowasilishwa katika taarifa hiyo, nitumie fursa hii kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba baada ya ripoti hiyo kuwasilishwa Bungeni, tayari Serikali kwa upande wake imeanza kuifanyia kazi mara moja.

Mheshimiwa Spika, miongoni mwa hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ni kuhakikisha kuwa Maafisa Masuuli wote wanaandaa majibu ya hoja kama inavyoelekezwa katika Sheria na Kanuni za Ukaguzi wa Umma na kusisitizwa na Mheshimiwa Rais. Aidha, nitumie fursa hii kuiwakumbusha Maafisa Masuuli wote kuzingatia maelekezo ya Mhehsimiwa Rais ya kuhakikisha kwamba wanapitia kwa kina taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, kujibu na kuchukua hatua za haraka juu ya hoja zote zilizoibuliwa kwenye maeneo yao.

Mheshimiwa Spika, vilevile naahidi kuwa pamoja na hatua zilizochukuliwa na Serikali, taarifa ya kina katika maeneo yaliyobainishwa kuwa na hoja katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali itawasilishwa katika Bunge lako tukufu kwa kuzingatia Kanuni husika. Aidha, nilihakikishie Bunge na wananchi kuwa Serikali ya Awamu ya Sita haitamfumbia macho yeyote atakaebainika katika ripoti hiyo kuwa amehusika katika matumizi mabaya ya fedha na mali za umma na kuwa hatua kali zitaendelea kuchukuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja nyingine iliyojadiliwa mbele yetu ni changamoto ya mmomonyoko wa maadili na vitendo vinavyokwenda kinyume ya mila, desturi na tamaduni za Mtanzania.

Mheshimiwa Spika, wakati tunaendelea na mjadala wa hoja hii ya bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu, Waheshimiwa Wabunge wengi walionesha kukerwa na uwepo wa matukio mbalimbali yanayokinzana na tamaduni, mila na desturi zetu. Matukio na matendo haya yamekuwa yakihatarisha uimara wa ustawi wa familia zetu na msatakabali wa Taifa kwa ujumla. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa nchi yetu inazo sheria kali tu na sheria zetu zote zinasimamia kila eneo, pia zinakataza bayana vitendo hivyo na zimeweka adhabu mbalimbali kwa makosa ya namna hiyo na yale ya udhalilishaji kwa watoto ikiwemo ulawiti. Pia sheria zinazokataza kuweka kwenye mtandao maudhui yanayochochea mahusiano ya jinsi hiyo au maonesho ya sanaa yanayochochea vitendo vinavyoashiria mmomonyoko wa maadili yetu.

Mheshimiwa Spika, baadhi ya sheria hizo ni pamoja na Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura Namba 16 ya Sheria ya Tanzania, ambayo inatamka bayana kwamba vitendo vya mapenzi ya jinsia moja au kinyume na maumbile iwe kwa faragha au kwa makubaliano ni kosa la jinai. Sheria hiyo pia inakataza udhalilishaji wa watoto kwenye matendo yanayofanana na hayo, pamoja na kuweka adhabu kwa kosa la kujaribu kufanya vitendo vilivyokatazwa chini ya sheria husika.

Mheshimiwa Spika, Mbili; Kanuni za Maudhui ya Mtandaoni chini ya Tangazo la Serikali Na. 538 la mwaka 2020, linakataza kuweka mtandaoni maudhui yenye kuonesha mahusiano ya jinsia moja sambamba na adhabu zake. Tatu; ipo Sheria ya Makosa ya Kimtandao Sura Namba 22, inazuia kutangaza au kusababisha machapisho ya ngono au matusi kupitia mfumo wa kompyuta au mfumo mwingine wowote wa kiteknolojia na Kanuni nyingnine ni Kanuni ya Baraza la Sanaa la Taifa za mwaka 2018 zinaweka masharti kwamba hakuna kazi ya sanaa itakayopelekwa sokoni kwa walaji kabla ya kupewa kibali cha kuthibitisha kuwa maudhui yamezingatia maadili.

Mheshimiwa Spika, aidha Baraza katika kuhakiki maadili na maudhui linajiridhisha kuwa kazi ya sanaa haishawishi wala kuhamasiha vitendo vya ngono, ushoga, usagaji au matumizi ya dawa za kulevya wakati wote sanaa hiyo inapowasilishwa kwa jamii.

Mheshimiwa Spika, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali imepokea hoja na michango mbalimbali iliyowasilishwa na itaielekeza Tume ya Marekebisho ya Sheria kuzipitia sheria hizo, kuzifanyia utafiti wa kina na utafiti wa kitaalam ili kubaini mapungufu yaliyojitokeza katika utekelezaji na kufanya maboresho yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, aidha nitoe wito kwa Taasisi zote zilizo na wajibu wa kusimamia Sheria, Kanuni na Taratibu tulizojiwekea kama vile Jeshi la Polisi, BASATA, TCRA, kutosita kuchukua hatua kali kwa yeyote atakaebainika anavunja sheria hii inayogusa maeneo haya ya kukiuka mila, desturi na utamaduni wetu na kukiuka misingi ya taratibu zetu tulizojiwekea.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hoja na hisia za Wabunge kuhusu matendo haya, watoto wetu pia wamekuwa ni miongoni mwa wahanga wakuu, kutokana na hali hiyo Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha kuwa watoto wanalindwa dhidi ya vitendo vya ukatili.

Mheshimiwa Spika, mathalani, kutokana na matukio ya unyanyasaji wa watoto yaliyoripotiwa hivi karibuni Serikali imechukua hatua Madhubuti, zikiwemio kutoa waraka kwa wamiliki wote wa shule nchini unaoelekeza kuwa kuanzia tarehe 1 Machi, 2023, kuanza utaratibu wa uwepo wa wahudumu wa jinsia ya kike na wa jinsia ya kiume kwenye magari yanayobeba wanafunzi kuelekea na kutoka majumbani mwao.

Mheshimiwa Spika, Mbili; kusimamia ukaguzi wa mara kwa mara kwenye mabasi ya shule ili kuhakikisha kwamba utekelezaji wa agizo hilo na uwepo wa wahudumu wa jinsia ya kike na kiume kwenye magari hayo unazingatiwa. Tatu; kuthibiti nyimbo na video zisizo na maadali kuchezwa au kuoneshwa kwenye magari ya wanafunzi yanapofanya safari zake. (Makofi)

Mhehsimiwa Spika, pamoja na hatua hizo tumeendelea kuimarisha mifumo ya ushirikishwaji jamii ili kurahisishwa upatikanaji wa taarifa pindi jamii inapobaini uwepo wa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na ukiukwaji wa mila, desturi na tamaduni zetu na kuchukua hatua mbalimbali za kisheria kwa wale wanaobainika kuvunja sheria hizo za nchi.

Mheshimiwa Spika, mtakubaliana nami kuwa suala la malezi ya watoto na utunzaji wa mila, desturi na tamaduni zetu ni jukumu la kila mmoja hivyo sote tunao wajibu wa kuhakikisha kwamba tunakuwa na kizazi salama chenye kuzingatia sheria, mila, desturi na tamaduni. Tamaduni hizi ni zile ambazo tunaziheshimu ambazo pia zinaleta utu na kuimarisha mshikamano wa Kitaifa.

Mheshimiwa Spika, nami nitumie fursa hii kuwaasa Watanzania wenzangu kuendelea kuienzi misingi yetu ya mila, tamaduni na desturi zetu nzuri na kuendelea kuzingatia sheria za nchi. Aidha, nitumie Bunge lako tukufu kuwasihi wafuatao: -

Wazazi na walezi; imarisheni uhusiano na urafiki wa watoto wetu ili kupata taarifa za viashiria wa uwepo wa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto. Jengeni utamaduni wa kutenga muda wa kuwasilikiza watoto ili kujua kinachoendelea katika maisha yao ya nyumbani, mtaani na shuleni vilevile na kuchukua hatua stahiki ikiwemo za kisheria pale inapotokea kuna ukiukwaji wa misingi yetu ya maadili ya malezi ya watoto wetu.

Viongozi wa dini; endeleeni kuwakumbusha waumuni wetu kuzingatia maadili na kushiriki kikamilifu katika kuwalea watoto wetu kiroho, kuwahimiza kuwa waadilifu na kuepuka vitendo visivyokubalika katika jamii. Tumeshuhudia karipio lenu kupitia mikutano yenu, endeleeni kukaripia jamii yetu ili kila mmoja azingatie maadili yetu ya Kitaifa. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge wenzangu; endeleeni kuiunga mkono Serikali katika suala la ulinzi wa mtoto wa Kitanzania na usimamizi wa maadili yetu, sote kwa nafasi zetu tuendelee kuhimiza jamii na kuwa mfano katika kutekeleza sheria tulizozitunga wenyewe, kutunza mila, desturi na tamaduni zetu.

Wito kwa Wizara za kisekta; kusimamia kikamilifu sheria tuliojiwekea Kanuni tulizoziweka na miongozo tulionayo pamoja na kuchukua hatua kali za kisheria kwa wale watakaobainika kufanya vitendo kinyume cha sheria na maadili ya Taifa letu.

Asasi za Kiraia; kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa vibali vyao vya usajili kwa Taasisi zitakazobainika kwenda kinyume na malengo ya usajili ikiwemo kuhamasisha mmomonyoko wa maadili na vitendo vinavyokinzana na mila za nchi hii, utamaduni wa nchi hii na desturi zetu tutachukua hatua kali za kisheria dhidi ya Taasisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikiwa naelekea kuhitimisha hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu, naomba uniruhusu nitumie jukwaa hili kuzungumzia kwa uchache kabisa kuhusu masuala mawili kama ifuatavyo: -

Suala la kwanza ni pongezi kwa timu yetu ya mpira wa miguu ya Fountain Gate kwa kutwaa Ubingwa Mashindano ya Mpira wa Miguu kwa Wanawake wa Shule za Sekondari Barani Afrika. Nikiwa mdau wa michezo nanyi mkiwa wadau wa michezo mmefurahi leo kwamba asubuhi tuliwapokea hapa Bungeni mabingwa wa soka la wanawake wa Shule za Sekondari Barani Afrika kwa mwaka 2023. Shule ya Sekondari ya Fountain Gate iliyoko Jijini Dodoma, ambao wameambatana na wanafunzi wenzao. Mafanikio yao yanaifanya Fountain Gate kuwa mfano wa kuigwa wa shule na vituo mbalimbali katika kuibua na kuendeleza vipaji vya michezo kwa watoto wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii hatuwezi kuzungumzia mafanikio ya soka la wanawake nchini bila kuitaja Fountain Gate. Kwa mfano, katika kikosi cha Timu cha Wanawake wa Serengeti Girls kilichoshiriki katika fainali za Kombe la Dunia za Soka la Wanawake nchini India mwaka 2022 na kuingia hatua ya robo fainali, Timu ya Fountain Gate ilikuwa na wachezaji Saba katika kikosi hicho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo tumekuwa nao hapa Bungeni, mashujaa wetu, mabinti zetu wa Fountain Gate, baada ya kupata mafanikio makubwa na kutwaa ubingwa wa michuano ya CAF kwa shule za Sekondari Barani Afrika na kuwa timu ya kwanza kutoka Tanzania kutwaa kombe lililoandaliwa na CAF. Hongereni sana Fountain Gate. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuipongeza Wizara ya Utamaduni na Michezo kwa kusimamia vema utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Michezo ya Mwaka 1995, ambayo pamoja na mambo mengine inalenga kutengeneza mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kuwekeza katika michezo kwa maslahi ya Taifa. Pia napenda kuipongeza Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kwa kusimamia kikamilifu uendeshaji wa shughuli za michezo shuleni, kutoka shule za msingi na mashindano ya UMITASHUMTA na shule za sekondari kwa mashindano ya UMISETA. Vilevile napongeza Baraza la Michezo Tanzania kwa utendaji mahiri ambao umekuwa chachu ya mafanikio kwenye tasnia ya michezo ikiwemo mpira wa miguu wa wanawake.

Mheshimiwa Spika, uwekezaji uliofanywa na mmiliki wa Fountain Gate wa Jijini Dodoma ni miongoni mwa vielelezo vya mafanikio katika utekelezaji wa sera ya maendeleo ya michezo nchini. Hivyo basi, nitoe wito kwa wadau wa michezo kuiunga mkono Serikali katika kuimarisha miundombinu ya michezo, kuibua na kuendeleza vipaji vya michezo mbalimbali. Aidha, niwapongeze tena mabinti zetu wachezaji mahiri, mashujaa wanafunzi wa Fountain Gate kwa historia waliyoiweka katika soka la Afrika na kulitangaza Taifa letu duniani. Hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukio la pili ni baadhi ya kumbukizi muhimu katika kipindi cha Aprili kwa Taifa letu. Itakumbukwa kuwa tarehe 7 Aprili mwaka huu, tuliadhimisha kumbukumbu ya miaka 51 tangu kitokee kifo cha Muasisi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mzee wetu Hayati Sheikh Abeid Aman Karume. Aidha leo tunaadhimisha mwaka wa 110 tangu kuzaliwa kwa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, jana tarehe 12 Aprili mwaka huu wa 2023 kumeadhimishwa kumbukizi ya miaka 39 tangu kitokee kifo cha Hayati Edward Moringe Sokoine, Waziri Mkuu wa Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, nyote mtakubaliana na mimi kwamba kumbukizi za viongozi hao ni urithi muhimu kwa Taifa kutokana na uzalendo, uwajibikaji na utumishi wao uliotukuka katika Taifa hili, kwa mantiki hiyo, tukiwa Taifa linalothamini na kuenzi utendaji wa Viongozi wetu tunao wajibu siyo tu kuwakumbuka lakini pia kurithisha urithi huo kwa vijana wetu wa sasa na vizazi vijavyo. Kwa kufanya hivyo, tutasaidia vijana wetu na vizazi vijavyo kuyaiga, kuyaenzi na kuyaishi matendo bora yenye tija waliotuachia viongozi hawa na hivyo kuimarisha umoja na mshikamano wa Kitaifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa napoelekea kuhitimisha hoja yangu, niwaombe Waheshimiwa Wabunge wenzangu kuendelea kuiunga mkono Serikali yetu kupitia Bunge hili Tukufu ikiwa ni pamoja na kutoa mapendekezo ya kujenga umoja, kuimarisha mshikamano wa Kitaifa kusaidia Serikali kuwahudumia ipasavyo wananchi wake na kuikosoa pale inapobidi. Aidha, katika maeneo yetu ya uwakilishi tuimarishe ushirikiano na wananchi katika kuhakikisha kwamba miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yetu inaleta tija iliyokusudiwa na kuhakikisha thamani ya fedha ya umma ambayo imetumika kwenye miradi hiyo.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Watanzania wenzangu niwaombe kuendelea kumuunga mkono Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwa ni pamoja na kumuombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee kumjaalia afya njema, maono, hekima na busara katika kuliongoza Taifa hili na kufanikisha azma yake ya kuliletea maenedeleo.

Mheshimiwa Spika, kadhalika niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwamba Serikali kwa upande wetu itaendelea kutoa ushirikiano stahiki kwa wananchi na wadau wote muhimu, katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu yake kwa kuzingatia mustakabali na maslahi mapana ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, naafiki.