Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuwa mchangiaji wa kwanza katika hoja hii iliyoko katika Bunge letu Tukufu. Kwa dhati kabisa nianze kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa nzuri sana ambayo ameendelea kuifanya kwa Taifa letu. Naamini Waheshimiwa Wabunge wote watakubaliana nami kwamba kwa kipindi hiki kifupi cha miaka miwili, miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yetu katika halmashauri, manispaa, majiji na miji ni kwa kiwango kikubwa sana. Lakini pia nichukue fursa hii kumpongeza Waziri mwenye dhamana ya Wizira ya Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wasaidizi wake Manaibu Waziri na Makatibu na watumishi wote kwa ujumla wao katika kumsaidia Mheshimiwa Rais kazi hii kubwa ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara husika.

Mheshimiwa Spika, mimi nitaanza kuchangia katika eneo zima la barabara za vijijini, kwa maana ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tanzania Rural Urban Road Agency - TARURA). TARURA wanafanya kazi nzuri sana, kazi ambayo katika ile programu ya SDP wana component ya kutengeneza barabara kutoka maeneo ya uzalishaji kuyapeleka katika masoko na magulio. Kazi hiyo wanaifanya vizuri, mafungu yanaenda vizuri na usimamizi ni mzuri, kwa kweli tunaona tofauti kubwa sana tangu tulivyokuwa tunazisimamia hizi barabara kupitia halmashauri; na sasa tangu mamlaka hii imeingia tunaona kwamba kuna ufanisi umeongezeka kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nauliza hapa kwamba mamlaka kama ya DAWASA imepata ithibati ile ya ubora wa Dunia, lakini ninaamini kabisa kwamba sitashangaa siku moja nikiona kwamba TARURA nao wanapata ile International Standard Organisation kwa maana ya ubora wa kazi ambayo wanaifanya, lakini pia sitashangaa Engineer Victor Seff akitunukiwa udaktari wa heshima kwa kazi kubwa ambayo anaifanya kwa namna ambavyo ameifungua Tanzania hasa katika maeneo ya vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika,pamoja na sifa hizo lakini kuna changamoto ndogo ambayo naiona. Changamoto iko katika disbursement ya pesa hasa zinazotokana na Mfuko wa Barabara. TARURA ina vyanzo vikuu vitatu, chanzo cha kwanza ni jimbo cha pili ni tozo na cha tatu ni Mfuko wa Barabara. Sasa fedha za jimbo na za tozo zinaenda kwa wakati lakini fedha hizi zinazotokana na Mfuko wa Barabara zinachelewa, hivyo zinasababisha baadhi ya wakandarasi kuto omba zabuni za barabara ambazo fedha zake zinatokana na barabara. Kwa hiyo nimuombe sana Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla, kwamba tujitahidi kupeleka mafungu ya hizi fedha zinazotokana na mfuko wa barabara kwa wakati

Mheshimiwa Spika, lakini kwakule Lushoto ambako kazi kubwa imefanyika tunachangamoto kubwa mbili. Changamoto ya kwanza ni kwamba TARURA hawana ofisi, ofisi waliyokuwa nayo sasa hivi inavuja kiasi kwamba wakati wa mvua wanaingia na miamvuli ndani ya ofisi, hili si jambo zuri. Sisi tumefanya jitihada kubwa, tumewapa kiwanja jirani kabisa na ofisi ya Mkuu wa Wilaya, ni eneo zuri mno ambalo linafaa kwa ujenzi wa ofisi ya TARURA.

Mheshimiwa Spika, lakini la pili Wilaya ya Lushoto ni wilaya ambayo asilimia 95 ni milima; magari waliyokuwa nayo yamechakaa sana kila siku yanafanyiwa ukarabati. Inafikia hatua ili waweze kutimiza wajibu wao wakati mwingine lazima hata sisi Wabunge tunawaazima magari yetu, hii si sawa. Tunaomba wapatiwe magari ya kuhudumia majimbo yote matatu ya Wilaya ya Lushoto kwa sababu Wilaya ya Lushoto ni milima na mabonde hivyo inahitaji magari ambayo ni madhubuti sana ili waweze kufanya kazi hizi kwa ufanisi mkubwa.

Mheshimiwa Spika, naomba nihame katika eneo hili niende katika eneo la elimu. Tuna changamoto kubwa sana ya watumishi katika Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, na mara kadhaa nikisimama hapa ndani ya Bunge lako nimekuwa nikizungumza jambo hili. Kipekee nipongeze jitihada hizi za Mheshimiwa Rais kutangaza ajira takriban 21,200. Mimi niombe, hizi 200 ambazo zimekaa pale juu zenyewe azielekeze Lushoto; na azielekeze Lushoto kwa sababu hizi zifuatazo.

Mheshimiwa Spika, sisi katika Idara ya Elimu Sekondari mahitaji ya walimu ni walimu 1000, waliopo ni walimu 841 tunaupungufu 159, kidogo hapo kuna uhafadhari. Hata hivyo, mwaka 2022 wamehama walimu 35, 2023 wamehama 25 na bado wanaendelea.

Mheshimiwa Spika, lakini wanahama huku hatujawahi kuona wakihamishwi kutoka maeneo mengine kuja Lushoto, hili ndilo tatizo kubwa. Ukienda kwenye idara ya elimu msingi mahitaji ni 2,250 waliopo ni 1333 upungufu ni 917; 2020 wamehama 34; 2021 wamehama 34 tena; 2022 wmehama 23; 2023 bado sijapata takwimu zake, lakini wanaohamia kuja Lushoto hatuwaoni kila unaye muuliza anakwambia changamoto ni baridi. Sasa mimi nauliza mbona wakipewa viza za kwenda Ulaya hawakatai na Ulaya na kwenyewe kuna baridi?

Mheshimiwa Spika, hizi sababu hatutaki kuzisikia, kwenye ajira hizi mpya zinazotangazwa tunataka tuletewe watumishi ambao wako committed kufanya kazi popote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; na ikikupendeza tuletee ambao wako single, kama ni wanawake wawe hawajaolewa na kama ni wanaume wawe hawajaoa ili wasianze kuleta sababu za kuanza kuhama. Kule wako mabinti wa kisambaa wazuri weupe, watapata wachumba wazuri kule kule.

Mheshimiwa Spika,katika zoezi lile la vyeti fake tumepungukiwa na zaidi ya watumishi 216 ambao walikutwa na tatizo la vyeti; lakini hatuja pata ile compensation ya ile idadi ambayo walipunguzwa. Niombe sana, pamoja na mapungufu haya ninayo yataja basi angalau tupate wale 216 katika mkupuo mmoja ili kuziba lile gape ambalo limetokana na wenye matatizo ya vyeti.

Mheshimiwa Spika,eneo lingine ambalo ningetaka kulisemea pia, wapo walimu ambao wanajitolea katika shule zetu; na katika halmashauri ya Lushoto tunao walimu 97 ambao wanajitolea. Ningependa sana kuomba kwa ridhaa yako Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana, hebu tutafute hawa ambao wanajitolea, hawa wamekaa zaidi ya miaka miwili wanajitolea lakini leo wanakuja kushindanishwa na wengine ambao walikuwa wanafanya shughuli nyingine na inawezekana wakakosa. Nikuombe sana hawa hebu tuwapeni kipa umbele. Hii iwe pia ni zoezi endelevu, Serikali inaweza ikawa na data base ya Watumishi wote na tukawa na utaratibu kwamba kila mwalimu anaye maliza chuo basi apate angalau mwaka mmoja wa kujitolea na hata ikiwezekana muundo wa kuwaajiri ubadilike sasa waajiriwe wale ambao wako katika maeneo ambayo tayari wanajitolea kwa kipindi fulani.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo ningependa kuchangia ni kuhusu afya. Kama ambavyo tuna changamoto ya watumishi katika sekta ya elimu na afya ni vivyo hivyo. Ikama katika halmashauri ya Lushoto ni watumishi 662 ndio wanaohitajika waliopo ni 391 sawa na asilimia 59, upungufu 270 sawa na asilimia 41. Ungufu huo uko katika kada hizi zifuatazo;

i. Madaktari mahitaji ni 29 waliopo ni 11 upungufu ni 18 sawa na asilimia 38,

ii. Madaktari wasaidizi wanao hitajika ni 39 waliopo ni 2 ungufu 37 sawa na asilimia 5,

iii. Maafisa Wauguzi wanaohitajika 24 walipo ni 2 tu upungufu 22 sawa na asilimia 8,

iv. Wauguzi wako 132 wanaohitajika walipo ni 63 upungufu ni 69.

Mheshimiwa Spika, naomba sana, bajeti za miaka miwili, mitatu huko nyuma tumepeleka pesa nyingi sana kwenye miundombinu. Haitakuwa na maana yoyote tutakapokuwa na miundo mbinu lakini ikakosa watumishi.

Mheshimiwa Spika, niombe sana kwa ridhaa yako tuendelee kuhakikisha kwamba maeneo haya yanapata watumishi. Hivi tunapozungumza hivi ni kwamba wakati mwingine si lazima zitokee ajira mpya, hata kufanya restructuring katika muundo mzima wa ajira. Yako maeneo hasa mijini unakuta wamejaa katika maeneo ya miji lakini huku vijijini hakuna wanao hudumia Watanzania. Sasa nchi hii ni yetu sote tungependa kuona regional secretariat zifanye kazi ya ziada kuangalia katika maeneo ya miji lakini na maeneo ya vijijini yawe na usawa wa ikama ya watumishi.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja, nakushukuru sana. (Makofi)