Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon Lucy John Sabu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. LUCY J. SABU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa fursa hii ili nami niweze kuchangia hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Rais TAMISEMI. Kwanza kabisa nichukue nafasi hii kuipongeza Wizara kwa uwasilishaji mzuri wa hotuba ya bajeti; lakini kwa namna ya pekee nimpongeze Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuleta maendeleo kwa wananchi. Sote ni mashuhuda, katika kipindi chake cha miaka hii miwili, tumejionea namna ambavyo anatekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi; hususan katika eneo la elimu, sote ni mashuhuda shule nyingi zimejengwa, zaidi ya Shule 23,000. Pia ujenzi wa shule maalum za za bweni kwa wasichana kuanzia form one hadi form six. Pia vituo vya Afya vimejengwa katika halmashauri zetu.

Mheshimiwa Spika, nitakuwa na mambo matatu. Jambo la kwanza ni kuhusiana na hili suala la mikopo ya asilimia kumi kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu. Sote tulisikia hotuba aliyohitimisha jana Mheshimiwa Waziri Mkuu. Katika maelekezo ambayo aliyatoa ni kwamba usitishaji wa mikopo hiyo ni hadi hapo Serikali itakapojipanga na kuboresha mfumo wa utoaji wa mikopo hiyo.

Mheshimiwa Spika, na mimi nikiwa kama mwakilishi wa vijana nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa kuona jambo hili na umuhimu wake kwa sababu mikopo hii imekuwa ikitunufaisha kwa namna moja ama nyingine hususan kwa vijana ambao wanapomaliza vyuo wanakuwa hawana sehemu ya kuanzia. Hivyo basi mikopo hii imekuwa mkombozi mkubwa sana, na mimi naunga mkono maelekezo ambayo aliyatoa Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na maelekezo ambayo aliyatoa Mheshimiwa Rais. Kwamba ipo haja ya Serikali kuangalia namna ya kuingiza katika mfumo wa kibenki ili kuratibu suala zima la utoaji na urejeshaji wa mikopo.

Mheshimiwa Spika, sote tunatambua kwamba kumekuwa na vikundi hewa vikiendelea na wakati mwingine uwazi kwenye mikopo hii unakuwa hauonekani. Hivyo basi sisi kama vijana tunaunga mkono jambo hili na tuna imani kwamba Serikali inaenda kutengeneza mfumo ambao utasaidia vijana wengi waweze kunufaika. Hii ni kwa sababu kwenye mikopo iliyokuwa ikitolewa na wakati mwingine vikundi vinavyoundwa vijana wanakuwa hawana uelewa mzuri wa project ambayo wanaiendea; lakini na elimu ya biashara pia na upande wa ku-manage fedha ambazo wanafanya katika miradi yao. hivyo Serikali iweze kuangalia jambo hili kwa uzito mkubwa ili vijana wengi waweze kupata na mikopo hii iweze kuwa na tija. Hivyo basi kama itawezekana, kama wengine wataendelea na vikundi ama kutolewa mkopo wa mtu mmoja mmoja ili kila kijana kadri ambavyo atakuwa amejipanga aweze kuona anatumiaje fedha ambazo zinatolewa.

Mheshimiwa Spika, lakini jambo la pili ambalo ningependa kulizungumzia ni taulo za kike shuleni. Kwa muda sasa jambo hili limekuwa halina majawabu kwa sababu kama sote tunavyotambua tumefanya uboreshaji mkubwa katika eneo zima la elimu kwenye shule. Kwa namna ambavyo tunapambana katika kuboresha elimu lakini pia mtoto wa kike ni lazima aangaliwe kwa jicho la kitofauti kwa sababu mabinti wanapoingia katika siku zao wanapata changamoto kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, takwimu za UNICEF zinaonesha asilimia 10 ya watoto duniani wanakosa masomo kutokana na kipindi cha hedhi lakini pia wakiwa kwenye siku zao wanakosa kujiamini. Hivyo, tuiombe Serikali na nimefurahi nimeona upande wa maoni na ushauri wa Kamati wameongelea juu ya jambo hili. Hivyo basi. niiombe Serikali iweze kuona namna bora ya kuratibu jambo hili ili watoto au mabinti wa kike walioko mashuleni waweze kusaidiwa katika eneo hili.

Mheshimiwa Spika, nasema hivi kwa sababu natambua katika Serikali ya awamu ya nne ilitoa waraka ambao utatoa pad kwa watoto wa kike mashuleni, lakini waraka huu umekuwa hautekelezwi ipasavyo. Hivyo basi, niiombe Serikali iweze kutenga bajeti mahususi kwa ajili ya mbinti mashuleni ili waweze kuondokana na adha hii ambayo wanakumbana nayo.

Mheshimiwa Spika, nina imani hata tukianzisha viwanda vidogo vidogo kwenye halmashauri zetu ama kwenye ngazi za mkoa kwa ajili ya kutengeneza hizi taulo za kike, tutakuwa tumemlinda mtoto wa kike, lakini pia mtoto wa kike atasoma kwa kujiamini pasipokuwa na changamoto ama adha ya aina yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, natambua kwamba sisi Wabunge tumekuwa tukipeleka pad mashuleni lakini pia kuna baadhi ya wadau mbalimbali wamekuwa waki-support jambo hili lakini bado uhitaji ni mkubwa. Kule vijijini uhitaji ni mkubwa sana kwa sababu baadhi ya watoto wamekuwa wanakata kanga, vitenge ama magazeti wakati mwingine na hii ni hatarishi kwa afya zao. Hivyo basi, tunaomba Wizara ya TAMISEMI waweze kuangalia jambo hili ili kumsaidia mtoto wa kike aweze kuondokana na changamoto hii.

Mheshimiwa Spika, sisi Mkoa wa Simiyu ni kinara katika uzalishaji wa zao la pamba na kulikuwa na mpango wa Serikali wa kuanzisha kiwanda cha vifaatiba na moja ya malighafi ilikuwa ni kutumia pamba ikiwemo kuzalisha taulo za kike. Niombe basi kama jambo hili litakuwa gumu kutekelezwa kwenye halmashauri basi kwa kuwa sisi Mkoa wa Simiyu tunazalisha pamba kwa wingi waweze kutupa jukumu hili ili tutakapokuwa tunazalisha hizi taulo za kike ziweze kuwanufaisha nchi nzima. Vile vile TAMISEMI waweze kutusaidia ili kuharakisha jambo hili liweze kutekelezwa kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama MSD wameweza kutengeneza mipira ya wanaume na kugawa bure, iweje basi jambo hili lishindikane kutekelezwa kwa kutoa pads za watoto wa kike? Hivyo basi, niombe jambo hili waliangalie kwa jicho la kitofauti ili kuweza kumsaidia huyu mtoto wa kike. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu ambalo ningependa kulizungumzia, kwenye halmashauri zetu kuna miradi ya kimkakati ambayo ilianzishwa kwa lengo la kuongeza mapato kwenye halmashauri, lakini pia kupunguza utegemezi katika bajeti ya Serikali Kuu. Katika Wilaya yetu ya Maswa, Mkoani Simiyu kuna Kiwanda cha Chaki kilianzishwa. Hivyo basi, niombe kwa sababu kulikuwa kuna fedha ambayo haijakamilika kutolewa kiasi cha Shilingi Bilioni mbili kwa ajili ya operating cost na umuhimu wa kiwanda hiki ni kutoa ajira kwa vijana 250, vile vile zitaweza kuzalishwa chaki ambazo zitasambazwa nchi nzima, niombe basi Serikali iweze kukamilisha jambo hili na fedha iweze kutolewa ili kiwanda hiki kiweze kuanza mara moja.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nashukuru kwa fursa hii na naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)