Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ROSE V. BUSIGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia Wizara hii ya TAMISEMI. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa namna ambavyo ameweza kutupatia zawadi ya uhai, lakini nikushukuru sana wewe kwa kunipa nafasi hii adhimu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, binafsi nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, Mama yetu kipenzi kwa namna ambavyo ameendelea kufanya kazi kwa kujituma na naomba tu nizungumze kutoka kwenye vilindi vya moyo wangu kwamba, niwarudishe kidogo nyuma Watanzania wote, ikumbukwe tu Mama alipokea nafasi hii katika mazingira magumu sana, binafsi nilijiuliza hivi itakuwaje na Watanzania wote walijiuliza hivi itakuwaje? Majibu sisi wenyewe tunayaona kwa macho yetu, tunaona Mama ambavyo anaendelea kuchapa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile naomba nilieleze Bunge hili Tukufu, kuna miradi ya kimikakati ambayo tayari ilikuwa imekwishaanzishwa na Mtangulizi wake na sisi kama Wanageita tuna kauli yetu tunasema hakuna kilichosimama. Uzuri Mkuu wangu wa Mkoa yupo na anaendelea kusisitiza, sisi kama Wanageita hakuna kilichosimama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nieleze tu kwamba mimi binafsi niko kwenye Kamati ya Miundombinu, nimetembea mwenyewe kwa macho yangu bila kusimuliwa na mtu, kwa macho yangu Mradi wa SGR Mama alikabidhiwa ukiwa na kilomita za mraba 700, lakini sasa hivi ni zaidi ya kilomita 2000 nani kama Rais Samia? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. Binafsi nakumbuka nilichangia hapa Bungeni, nikaomba suala la watendaji wa kata wapewe posho lakini wapewe pikipiki, jamani mimi mwenyewe dada ya Kairuki alinipa mwaliko nilienda kukabidhi pikipiki 916. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kipindi kidogo tu, Dada yangu Kairuki ambapo ametoka kupewa sasa donge nono na Mama tayari amekwishakamilisha. Hiyo speed aliyonayo Dada Kairuki nimwombe aendelee na speed hiyo hiyo na kila Mbunge hapa anaenda anamweleza tatizo lake anamsikiliza, Mheshimiwa Kairuki asigeuke nyuma, achape raba aendelee. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba univumilie kidogo, nilisema kwamba leo nikipata nafasi hii lazima niitendee haki. Nikaenda mbele zaidi, sisi watendaji wa Kata tulikuwa tunapita tunachangisha michango ya madarasa. Rais huyu huyu aliweza kutoa fedha za madarasa 23,000. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, watendaji wamefanya kazi katika mazingira mazuri hata likizo walipata, walikuwa hawapati likizo kwa sababu ya kwenda kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa. Namshukuru sana Rais wangu kwa namna ambavyo anaendelea kuona sekta hii ya elimu, lakini nimwombe sana Waziri wangu Mheshimiwa Kairuki, kuna madarasa ambayo wananchi wamejenga kwa fedha zao za mfukoni, kwenye bajeti hii tunaomba maboma ambayo yako hatua ya upauaji, Serikali waweze kutenga fedha ili kwenda kuzichukua zile nguvu za wananchi waamini Serikali yao iko kazini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mfano sisi Mkoa wa Geita, tuna maboma 1,016; ya msingi 713 na ya sekondari 303. Mheshimiwa Kairuki akishuka pale Geita akaja akatembea kidogo na Mkuu wangu wa Mkoa ananisikiliza, atakupokea na utayaona yale maboma.
Mheshimiwa Spika, niende mbele zaidi, narudi kwenye afya. Kule kwetu Geita tuna Hospitali ya Chato ya Kanda, ukifika pale ni kama umefika Dar es Salaam ndogo. Hata hivyo, namwomba Mheshimiwa Kairuki atupe watumishi. Kabla ya hospitali ile tulikuwa tunaenda Mwanza sasa hivi tutakuwa tunaishia Chato.
Mheshimiwa Spika, kuna vituo vya afya, hivyo hivyo na vyenyewe wananchi walijichangisha fedha zao za mifukoni mwao, lakini mpaka sasa hivi vituo vile vya afya vipo. Kwa ridhaa yako nitaje hata vitatu au vinne ili ujue kwamba ninavijua. Kuna Kituo cha Afya cha Buhela, Chikobe, Ng’homolwa, Kafita na Nyijondo. Naomba sana sana kwa ridhaa yako Dada yangu Mheshimiwa Kairuki afike kwenye vituo vya afya na fedha ambazo zimetengwa kati ya hivi vituo nilivyovitaja na vinginevyo aone haja ya kunisaidia hata kwa vituo viwili au vitatu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimezungumza sana, lakini nisiposema hili nitakuwa sijawatendea haki Waheshimiwa Madiwani. Waheshimiwa Madiwani wanafanya kazi nyingi sana na katika ziara yangu niliyoifanya Mwezi Machi Waheshimiwa Madiwani waliniomba sana, kwa heshima hiyo wakasema Mheshimiwa Mbunge wewe ulienda kuwasemea Watendaji wa Kata, tunaomba tena ukaliseme na hili, ikimpendeza Mheshimiwa Kairuki Dada yangu awasaidie na wao kidogo kaposho kao kale kaongezeke kidogo, wanatusaidia kazi, sisi tuko Bungeni sasa hivi lakini Madiwani wetu wanaendelea kufanya kazi kule. Kwa hiyo, kwa heshima hiyo hiyo Mheshimiwa Waziri anavyoendelea kuchapa raba na aendelee kuchapa mpaka kwa Madiwani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho, nimalize kwa kusema tuna daraja letu la Busisi na lenyewe mambo yanaendelea. Hata hivyo, Mheshimiwa Kairuki, watendaji wa Kata kipindi alipokuwa yupo kaka yangu Bashungwa waliahidiwa watakutana na Mama waje kidogo waangalie Ikulu jinsi inavyojengeka. Kwa heshima hiyo hiyo ya Dada yangu Mheshimiwa Kairuki, namwamini hana choyo, namwomba Watendaji wa Kata waje watembee Ikulu nami niwepo nawaongoza. Waje watembee Ikulu, waone jinsi Rais wao anavyoendelea kuchapa kazi, anavyoendelea kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nimesikia kengele yangu, naomba niunge mkono hoja. (Makofi)