Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ili niweze kuchangia hotuba ambayo imetoka kusomwa hapa ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Spika, naomba nianze na pongezi kwa TARURA. Sisi Wabunge tunaotoka maeneo ya vijijini tunajua umuhimu wa TARURA, pamoja na changamoto nyingine zote lakini tunapenda kuwapongeza namna wanavyofanya kazi, wameweza kuwaunganisha Watanzania kwa kupitia miundombinu.

Mheshimiwa Spika, kuna kata ambazo zilikuwa hazijawahi kupata kabisa kuunganishwa kwa barabara. Ni kwa kipindi hiki baada ya ongezeko la Bajeti TARURA wananchi sasa wameona umuhimu wa chombo hiki cha TARURA. Naomba nitoe ushauri kidogo hapa TARURA. Kwanza, uangaliwe upya ule muundo wake wa TARURA ili waweze kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, tukitaka kupima ubora wa barabara wanazotengeneza TARURA kwa kulinganisha na TANROAD, nafikiri tutakuwa hatuwatendei haki sana watu wa TARURA. Madaraja yale ya vijijini, sasa hivi tunazungumza hapa mafuriko kila kona hasa sisi tunaotoka Mkoa wa Rukwa. Ukiangalia bajeti waliyonayo madaraja mawili tu bajeti inakwisha. Kwa hiyo kama tutasema tupime ubora wake, ni lazima leo tuone tena umuhimu wa chombo hiki tukiongezee bajeti zaidi, sasa tutaweza kuwapima kulingana na kile ambacho wanakipata.

Mheshimiwa Spika, kwa Wilaya yetu ya Nkasi bado tuko gizani, wanapotengeneza hizo barabara tunaomba watuwekee taa za barabarani. Wilaya ya Nkasi ni sawa na wilaya nyingine tunaomba tupate taa za barabarani.

Mheshimiwa Spika, tuna changamoto ya Vivuko. Nimekwishapeleka ofisini kwa Mheshimiwa Waziri mara kadhaa, lakini nasikitika mpaka hapa nazungumza kuna kivuko kinachotoka Kata ya Namanyele kwenda Kata ya Isunta, kwa mara nyingine nimepeleka taarifa ofisini amefariki mwanafunzi wa darasa la saba, tunataka nani afe tena ili tuone uzito wa kutengeneza kivuko hiki? Inaumiza inaumiza sana, tunaomba tupate majibu katika vivuko 23 angalau vivuko saba ambavyo vinaunganisha taasisi ikiwemo upande shule za sekondari na primary tusiue watoto wetu ambao tunategemea kesho wawe viongozi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na ubora wa barabara hizi, ukiangalia vijijini sisi tunalima. Ukija kwenye ile sheria ya tani 10 unategemea sasa huyu mkulima anayelima pale anawezaje kusafirisha mazao yake kwa kuweka hicho kigezo? Kwa hiyo, ni vizuri pia tukaangalia kama kuna namna nyingine ya kuwasaidia wananchi hawa wa vijijini, waone barabara hizi ni baraka na sio balaa tena. Nayasema haya kwa sababu sisi tuna barabara moja ya mkoani ambayo inatoka Mkoa wa Katavi kwenda Rukwa, zile barabara nyingine ambazo magari yanapita lazima tutapitisha kule ambayo ni zaidi ya tani 10. Kwa hiyo niombe kwa namna bora ambayo tunaweza kufanya kama ambavyo wamepokea fedha hizi na kuona baraka ya TARURA iendelee kuwa baraka badala ya kugeuka kuwa balaa.

Mheshimiwa Spika, naomba niongeze tena neno moja la kushauri upande wa TARURA, tuwaongezee wataalam. Tukiwaongezea wataaalam, nafikiri wataboresha zaidi utendaji wao wa kazi.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni mgawanyo wa fedha za miradi inayoendelea. Ukitazama mgawanyo wa fedha hizi unakuta fedha labda za madarasa, fedha za kumalizia vituo vya afya, mtu wa Dar es Salaam na mtu wa Nkasi wakipewa sawa haiwezekani. Sisi tunaotoka kule ukiangalia kwanza eneo lenyewe ambalo vifaa vinakwenda ni gharama zaidi.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, gharama ya vifaa haiwezi kuwa sawa yaani mtu aliyenunua Dar es Salaam haiwezi kuwa sawa na mtu wa Nkansi. Kwa hiyo ukitoa kipimo hicho cha kwamba madarasa yote ni milioni 20, hatuyatendei haki maeneo mengine yakiwemo maeneo ya Nkasi. Kwa hiyo, tuangalie upya namna ya kugawa hizo fedha kulingana na uhalisia wa maeneo yenyewe.

Mheshimiwa Spika, nataka nizungumzie jambo kidogo hapo. Pamoja na miradi inayoendelea, ni kweli wataalam wetu wanasimamia miradi hiyo. Ukiangalia tu miradi ya kipindi cha COVID, yale madarasa ubora wake sijui ni kwa sababu ya speed au kwa sababu ya jina nilizungumza na mwaka jana hapa. Kuna haja hata kama tunawatumia Walimu wetu kwa sababu ya uhaba wa watalaam, tusiwahukumu kwa makosa yale ambayo hayaendani na taaluma zao. Tupeleke wataalam wa kutosha ili tuwahukumu kwa sababu hizo nafasi ni za kwao na wamesomea mambo hayo.

Mheshimiwa Spika, naomba nijikite kwenye Sera ya Afya. Mkoa wetu wa Rukwa ni miongoni mwa mikoa ambayo bado hatujabahatika sana sera hii kutekelezwa kikamilifu. Nianze tu kwenye jimbo langu. Jimbo la Nkasi Kaskazini lina kata 17, katika kata 17 ni vituo viwili tu kwa maana ya kata mbili kati ya kata 17. Kwa hiyo, tunaomba sera hii ikamilike kikamilifu. Nimesikia kauli mbalimbali zinazungumzwa, mara tunaanza kujenga kwa tarafa, hii sera imebadilishwa lini kutoka kwenye kila kata kituo cha afya, zahanati kila kijiji na mpaka waje tena kwenye tarafa? Kama sera imebadilishwa tujulishwe kwamba kwa sasa sio tena kila kata kituo cha afya badala yake ni tarafa kituo kimoja.

Mheshimiwa Spika, natambua kwamba kuna ujenzi unaendelea Kituo cha Afya Kabwe, nashukuru kwa jambo hilo, lakini ukiangalia umbali wa wanachi wanaotoka Kata ya Korongwe waje Kata ya Kabwe bado tutakuwa hatujakwenda kwenye hiyo sera yenyewe ya namna ya kuwasaidia Watanzania, lakini huduma zitolewe kulingana na hadhi. Kama ni kituo cha afya kitoe huduma kulingana na hadhi ya kituo cha afya, lakini kama tutajenga jengo hakuna vifaatiba, hakuna watumishi, lengo letu sio majengo, tunategemea tupate huduma na kusogeza huduma kwa wananchi. Tukifanya hivyo tutapunguza sasa idadi ya watu wanaokwenda hospitali za wilaya na mkoa kwa sababu huduma kule chini zitakuwa zinatolewa.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, vijiji viko 64 ni vijiji 20 tu vyenye zahanati. Sasa hivyo vijiiji 20 utakuta zahanati moja ina mhudumu mmoja na hiyo zahanati inahudumia zaidi ya vijiji sita. Ndio maana tunasema watu wa mjini kidogo anaweza akatoka pale akaenda eneo lingine, lakini watu wa vijijini aki-move zaidi ya kilomita 90 tumemsaidiaje huyo mwananchi?

Mheshimiwa Spika, kwa sababu waliohitimu upande wa afya wapo, kuna shida gani ya kuwapa ajira? Tuone namna ya kusaidia afya za Watanzania na hiyo itakuwa na maana zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninapozungumzia upande wa afya tukipeleka watumishi, kuna maeneo tumejenga Hospitali za Wilaya kwa ajili ya kuangalia eneo kubwa, kwa hiyo, unaangalia mtumishi ili atoke kwake aende pale ni zaidi ya kilomita Sita, tuombe gari kwa ajili ya watumishi hawa ili watimize wajibu wao, badala ya kuwahukumu kwa kutokwenda kwa wakati na kuwasaidia wananchi kulingana na umbali uliopo anakotoka na anakokwenda kutimiza wajibu wake.

Mheshimiwa Spika, hospitali ya Wilaya ya Nkasi watumishi wanafanya kazi nzuri sana ya kujitolea, hata wananchi wana-appreciate kwa kazi ambayo wanaiona wanavyopokelewa na huduma wanazopewa lakini umbali itakuwa ni changamoto ya watumishi kushindwa kutimiza wajibu wao.

Mheshimiwa Spika, nimalizie…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Sekunde thelathini malizia.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kushauri ajira hizi ambazo zimetoka muangalie sehemu zenye changamoto nyingi ikiwepo Nkasi kwa kutazama kwa upendeleo. Ahsante. (Makofi)