Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Issa Jumanne Mtemvu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibamba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye hotuba hii iliyowasillishwa na Mheshimiwa Waziri ya Fungu 56 pamoja na Taasisi zake.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nitumie nafasi hii kwa haraka kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kuaminiwa na Mheshimiwa Rais nami natambua Dada yangu huyu ana uwezo mkubwa na anafanya kazi vizuri sana. Pamoja na timu yake nzima ya Naibu Mawaziri wawili pia kwa Wataalam Kaka yangu Adolph Ndunguru na Wasaidizi wako au Naibu Makatibu wote watatu.

Mheshimiwa Spika, kwa haraka na kwa kipekee sana nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kwa kweli wananchi wa Wilaya ya Ubungo, wananchi wa Jimbo la Kibamba tuna kila sababu ya kumshukuru sana Mheshimiwa Rais. Wengi wamesema hapa nitakuwa mchoyo wa fadhila hizi za kushukuru kama sitasema dakika moja kwenye muda wangu wa kuchangia.

Mheshimiwa Spika, tumeona mambo mengi sana ndani ya Jimbo la Kibamba, ndani ya kipindi chake kidogo tu tayari ametujengea shule Nne za sekondari, ikiwepo shule maalum ambayo kaleta Bilioni Tatu imejenga shule maalumu ya Kidato cha Kwanza hadi Kidato cha Sita ya Wasichana hili ni jambo kubwa sana. Pia juzi tu tayari siku ya Jumatatu inawezekana tukazindua uanzishaji wa ujenzi wa Chuo cha VETA kule pembezoni kabisa ndani ya Jimbo la Kibamba - Kata ya kibamba, jambo kubwa. Mengine mazuri mengi sana tunaendelea kumsemea Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kutokana na hotuba iliyowasilishwa hapa nitajielekeza katika maeneo mawili hivi kama muda utaniruhusu, nilikuwa nina zaidi hata ya mambo mawili.

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza ni hili la asilimia 10 limesemwa na wengi. Jambo hili limenihuzunisha sana na limenihuzunisha kwa sababu ya kuona machozi ya Mheshimiwa Rais kwenye nia njema ambayo kama Taifa tulitamani kuona ile ajenda ya kuwainua wananchi wetu kiuchumi inafikiwa, lakini zimetoka fedha, na nikuambie kwa 2022/2023 zilitengwa bilioni 75 kwa ajili ya eneo hili na hizo ni sehemu tu ya fedha za ndani za miradi ya maendeleo karibu bilioni 394 zikasogea kidogo katika eneo hilo la asilimia 10, bilioni 75 kwa nchi nzima, lakini tunaambiwa na CAG katika mwaka huo tu uliokaguliwa 2021/2022 almost bilioni 88.8. maana yake nini?

Mheshimiwa Spika, maana yake hata zile tunazotengwa za mwaka mzima kwa nchi nzima zinapigwa zote. Ndiyo tafsiri tu ya kihesabu! Kama 2022/2023 tumetenga bilioni 75 lakini 2021/2022 tumetoka kukaguliwa zimepigwa bilioni 88, maana yake asilimia 100 tuliyotengewa imepigwa, hii ni hatari sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, liko jambo hapa kwenye hili, kupigwa tumezoea lakini kuna changamoto kwenye hili. Tunaambiwa vipo vikundi vingine hata havipo, vina fedha nyingi tu. Mimi ninashauri katika eneo hili, kubwa limesemwa na Kamati tumesikia, patakuwa hakuna mahusiano mazuri kati ya Wasimamizi Madiwani lakini na CMT katika maeneo mengi ambayo ukiangalia na analysis imejionesha kwenye Halmashauri nyingi tu ambazo zimeangaliwa au CAG kaziona Tatu zimeaharibu sana.

Mheshimiwa Spika, katika ya milioni 200 karibu milioni 774 ambazo fedha zilitolewa milioni 774 wakajigawia watu wenyewe, miongoni mwa wanakikundi nje ya miradi iliyozingatiwa. Tafsiri yake nini? Unaona Wilaya ya Ubungo ninayotokea mimi milioni 218 zaidi ya asilimia 40, yaani tumeziiba eti! (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nawaona Halmashauri ya Makambako na Geita wanaenda zaidi ya Milioni 172 Makambako, Halmashauri ya Geita Milioni 112, ni nyingi! NI nini hapa nataka kusema? Kanuni zetu na Mheshimiwa Waziri ulizoziweka kwenye kusimamia hii, nikukumbushe tu tunaongozwa na Kanuni ya 24 ya Kanuni za Utoaji na Usimamizi wa Mikopo ya mwaka 2019, tumekubaliana adhabu maana wanaoiba lazima adhabu ziwepo intact, faini ni kati ya shilingi laki mbili na milioni moja au kifungo kati ya miezi 12 na 24.

Mheshimiwa Spika, hebu ona watu wamepiga Milioni 700 unaenda kumwambia adhabu yake ni kukulipa kati ya Laki Mbili na Milioni Moja tumekuwa wapi? Hii ni changamoto kweli! Au Kifungo cha kati ya miezi 12 na 24 mojawapo, lakini wangapi wamefungwa? Mpaka leo hatuoni. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri nakuamini sana kwenye hili, tuendelee kumsaidia Mheshimiwa Rais nia yake ya kuona watu wanachukuliwa hatua haraka wachukuliwe hatua haraka na sheria zinakuongoza tu, hata kabla hatujakaa mwezi wa Nane na wa Kumi na Moja kwa maana ya Taarifa ya CAG. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la pili, utakumbuka sana mara nyingi huwa nachangia sana Wizara ya Afya na mwaka huu nimeomba lakini sidhani kama nitafanikiwa kuichangia, eneo lenyewe leo nimelijua ni la nani. Mheshimiwa Waziri kazungumzia juu ya K tatu, Kupima, Kupanga na Kurasimisha ardhi, kumbe ni jukumu la msingi la Ofisi ya Rais-TAMISEMI.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Ubungo Jimbo la Kibamba tunalia hapa kila siku, tumefeli kabisa kwenye jambo la urasimishaji, mara nyingi nimechangia hapa nakuonyesha zaidi ya bilioni tatu zimepotea Mheshimiwa Waziri anashuka mara kwa mara Wilayani lakini tumefanikisha mimi na yeye kukubaliana dhamana ya kwake kama Msimamizi wa Sera ni kutoa Hati, lakini jukumu la Kupima, Kupanga na Kuthaminisha ni jukumu hili ambalo lipo chini ya Ofisi ya Rais -TAMISEMI. Bilioni zetu Tatu na zaidi zilishapotea, nimeomba hata Waziri Mkuu aingilie kuzitafuta hizi hela hamna.

Mheshimiwa Spika, nimeshangaa hotuba ya Mheshimiwa Waziri naikuta najua hili janga kalikuta, kuna Bilioni 49.9 kazitamka yeye zimeenda kwenye Halmashauri huko kama revolving kwa jukumu la KKK, na yeye anasema kwenye ripoti amefanikiwa kwa asilimia zaidi ya 90 ya jambo hilo, lakini CAG sasa wakati anamkabidhi Mheshimiwa Rais anazungumza bilioni 29.9 zaidi ya asilimia 59.6 zimepigwa hazijarudishwa mpaka sasa, eneo hilo hilo katika Bilioni 50 zimetoka, nyuma yake tulitoa Bilioni 46 zaidi ya asilimia 50 hela zinapotea.

Mheshimiwa Spika, ni lazima wenyewe tujionee huruma, wananchi kule Kibamba wametoa wenyewe zaidi ya Bilioni Tatu za kwao, Halmashauri nyingine zinapewa na hela hazirudi, tujitahidi kwenda na Kibamba zile hela wale waliopima kupanga au wameshatoa hela zao laki mbili hadi laki tatu tuone jinsi gani ya kuwasaidia wapate hati zao badala ya kuendelea kuwatesa. Niliona hilo niliweke katika sura hiyo.

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu na la mwisho ni jambo la TARURA limesemwa na waliotangulia. Nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, wakati wa reference ya mwaka 2020/2021 tulikuta TARURA inapokea takribani Bilioni 250 hivi, lakini kwa kuingia ule mwaka wa 2021/2022 Mheshimiwa Rais kwa kufikiria kwa kina sana akaona hela haitoshi, Wabunge tukalia hapa akaingiza Shilingi Mia Moja ya tozo ya mafuta ya diesel, petrol na mafuta ya taa ikatuongezea tukafika Bilioni 700. Kwa hiyo, unaweza kumuona Mheshimiwa Rais alituvusha na tukiona kwenye Halmashauri zetu, tumeona kwenye Majimbo yetu mambo mazuri yamefanyika. Kuanzia 2022/2023 ongezeko kutoka pale ni dogo sana lakini hata leo anatamka tena Mheshimiwa Waziri kiasi kilichoongezwa TARURA bado hatuioni ile nia tena ileile iliyoanza, madhara yake ni nini?

Mheshimiwa Spika, mimi na wewe ni mashahidi hata kule kwenye Jimbo lako la Mbeya, population inaongezeka kwa mujibu wa statistics iliyotolewa sasa hivi ya mwaka 2020, vilevile maombi mengi ya barabara za vumbi kuelekea TARURA ni makubwa sana lakini na mtandao wa barabara wa muda mrefu ni 144,000 lakini za vumbi ni zaidi ya kilomita 130,000 hivi, maana yake hali ni mbaya sana! Nini kinaweza kikafanyika?

Mheshimiwa Spika, tukitaka kujenga barabara zote na akili kubwa tukaipeleka kwa wananchi ambao ndiyo tunawawakilisha, maana yake tukapeleke angalau kwa kilomita 130, 000 zilizobaki hazijawahi kushughulikiwa Milioni 500 tukajenga lami, maana yake unaweza ukaenda ukatafuta Trilioni 65 unazitoa wapi, kama kuanzia leo hatuna nia njema ya kupeleka hela nyingi kama alivyofanya Rais mwaka 2022/2023 kwenda kuogeza zaidi ya bilioni 500 pale kupitia shilingi 100 ya mafuta.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nia yangu ni kuona kama Taifa tunapeleka nia njema ya kujenga barabara za vumbi na changarawe zikawe za lami ili maendeleo haya yaende kwa kasi sana, kuliko yale ambayo tunayaona ni ya kimkakati, miradi ya vielelezo ni vizuri lakini wananchi wa pale Kibamba kule ndani ambao hawawezi hata kupata huduma ya afya kwa sababu ya vumbi na udongo, anashindwa kuweza kuelewa ataenda saa ngapi kwenye reli ataenda saa ngapi kwenye maeneo yenye ndege ataenda saa ngapi kwenye maeneo mengine, kwa hiyo tufungamanishe miradi ya kielelezo na miradi inayowagusa wananchi moja kwa moja.

Mheshimiwa Spika, nafikiri nimetendea haki siku uliyonipa na kwa kutumia nafasi hii niunge mkono hoja iliyopo mbele yetu. Nakushukuru sana kwa nafasi. (Makofi)