Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Tumaini Bryceson Magessa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii, vilevile namshukuru sana Mwenyezi Mungu kutujalia tena leo kukutana hapa na kutupa nafasi ya kuweza kuzungumza hapa Bungeni.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya ndani ya nchi hii, vilevile kazi kubwa ambayo wananchi wa busanda wanaiona inaendelea kwenye maeneo yetu. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa hilo, pia nampongeza Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, manaibu wake wawili, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa TAMISEMI kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya kwenye maeneo yetu.

Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi hizi nijikite kwenye maeneo matatu, kwanza Elimu ya Shule ya Msingi ambayo hata mwaka jana niliizungumzia. Tumeingia kama Taifa kwenye mmomonyoko wa maadili ambao kila mmoja sasa hivi anapiga kelele sitaki nirudie tena, lakini mahali fulani kwa sababu misingi yetu haikuwa imara ndiyo sababu tuna mashaka na kile kinachoendelea.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tuna kazi kubwa ya kutengeneza msingi ili huu msingi ukiwepo basi tusipate kuyumbayumba kama kuna vitu vinaingia vipya na hapa lazima tunaanza kwenye familia zetu ambako siyo Wizara hii lakini tunakwenda kwenye Shule za Msingi ambako tunapeleka watoto wetu.

Mheshimiwa Spika, Wabunge wote watakuwa ni mashahidi kwamba Shule za Msingi nyingi zimechakaa na uchakavu wake TAMISEMI kwa ubunifu wamekuja na miradi mingi BOOST, LANES, SRWSS kuhakikisha kwamba tunaweza kuboresha shule za msingi, lakini kiukweli uchakavu ni mkubwa sana na pesa inayokwenda hiyo ni kidogo kurudisha Shule za Msingi kwenye hali yake ya kawaida. Hivi watakuwa na kumbukumbu nzuri tu kwamba hata mdororo ile drop out itakuwa ni kubwa. Watoto wengi sasa hawako- interested sana kwenda kwa sababu wanajua mazingira ya nyumbani yanaweza kuwa ni mazuri kuliko Shule ya Msingi anayokwenda.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunategemea sasa waongeze pesa kuhakikisha kwamba shule za msingi zimeboreshwa na zikiboreshwa kama ilivyo sekondari, bahati nzuri ni kwamba sekondari zimeboreshwa, baada ya kuboresha sekondari sasa ni rahisi kujua kwamba Shule ya Msingi hii siyo bora kwa sababu sekondari ina vioo na Shule ya Msingi inaonekana wazi kwamba hii siyo bora, kwa hiyo kuna kazi kubwa ya kufanya ya kuboresha shule za msingi na tujenge msingi kwa kuweka content ambazo watoto wetu hawatayumba kama maadili yatakuwa yameyumbishwa na dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama wasemaji wa kwanza walivyosema juu ya shule za msingi, tuna maboma mengi yaliyojengwa na wananchi kwa nguvu za wananchi yanatakiwa kumaliziwa haya. Ni changamoto kubwa inapokuja kujenga madarasa mapya wakati kuna madarasa hayajaezekwa yako matano shuleni pale. Wananchi wanajiuliza hawa wameona nini waje wajenge mapya haya ya kwetu wayaache? Kwa hiyo, ni ombi langu TAMISEMI waangalie uwezekano wa kuyamalizia hayo maboma ambayo yamekwisha anzishwa na wananchi.

Mheshimiwa Spika, kwenye maeneo yangu kwa uchakavu huu tu nina mifano michache, nina shule kwa mfano ya primary ya Lurama kwenye Kata ya Bukondo, ukifika tu unajua ukweli hii shule ni chakavu, shule ya Lubanda kwenye Kata ya Busanda ukifika tu unajua shule hii ni chakavu, shule ya Lukumbo katika Kata ya Butundwe ukifika tu unajua shule ni chakavu, hii ni mifano michache tu lakini ziko nyingi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ni ombi langu kwamba, pesa hizi tunazozitoa ziwe ni za kutosha ili kasi ya kurekebisha shule zetu za msingi ionekane kwenye maeneo yetu. Kwa mfano, kuna miradi ya BOOST ambayo ilibajetiwa nafikiri mwaka jana, ukiuliza kule Halmashauri wanakuambia pesa haijafika hadi leo! Sasa kama haijafika maana yake tutakuwa tumewaambia wananchi mwezi wa Nane kwamba kuna BOOST inakuja kurekebisha shule za msingi na pesa haijafika, kwa hiyo kinachoonekana ni Mbunge amesema uwongo nafikiri ndiyo ukweli wenyewe huo, ama Mbunge kasema uongo kwenye eneo lake. Kwa hiyo, niombe sana hizo pesa za BOOST zilizosemwa ziende kufanya kazi ile ili tuwezwe kuhakikisha kwamba yale tuliyoyasema ni sahihi.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni TARURA. Kwenye TARURA hapa kuna kazi kubwa wamefanya inaonekana kazi yao, lakini nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuongeza fedha kwenye Mfuko huu wa TARURA tumeendelea kujenga barabara zetu. Changamoto ambayo nataka kuisema hapa, Mfuko wa TARURA hauna fedha ya dharura, kwa hiyo inapotokea kwa mfano sasa hivi mvua zinanyesha kwenye maeneo mengi, barabara ikiharibika huyu Meneja au Injinia wa TARURA wa Wilaya hana uwezo wa kwenda kufanya kitu chochote atakuambia tusubiri bajeti inayokuja.

Mheshimiwa Spika, sasa kama barabara imekatika watoto hawawezi kwenda shule, bajeti inayokuja itakuja lini? Nina mfano mdogo kwenye eneo langu, barabara kutoka Nyakagwe kwenda Butobela ambako ndiko kuna secondary school daraja limekatika, lakini maelezo yake ni kwamba tutaomba kwenye bajeti inayokuja kwa sababu hana uwezo wa kufanya kitu chochote, watoto wasiende shule?

Mheshimiwa Spika, hivyo, tuone tu namna gani tunaweza kuwa na pesa ya dharura kwenye maeneo hayo ili watoto wetu waendelee kupata huduma kwa utaratibu ule ambao unakubalika. Kama inaonekana fedha ni kidogo siyo vibaya kuiga kama TANROADS walivyo wameingiza EPC+F nao waongeze EPC+F na pesa yao iwe ndogo ili tuweze kufanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais alipopita pale kwangu Katoro tuliomba Bilioni 15 kufungua barabara za Katoro, akasema atatoa pesa kidogo kidogo, bahati mbaya sijaziona ninaamini Mheshimiwa Waziri utakuwa umeziandika mahali fulani nisipoziona maana yake nitajua kwamba Mheshimiwa sasa wananchi watakuwa wanasema Mheshimiwa Rais alichokisema siyo sahihi, ningeomba sana ziingie mahali fulani kwa ajili ya kuhakikisha kwamba haya yanawezekana.

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa ni sekta ya afya. Mwaka juzi tulitembezewa karatasi hapa Bungeni kila mmoja aka-suggest vituo vyake vya afya anavyotaka vijengwe. Mimi niandika vitatu hakijatokea hata kimoja sasa nikawa najiuliza huu ni muujiza au ni kitu gani, kwa sababu niliandika vitatu na hakikutokea hata kimoja. Bahati nzuri sana Kata niliyoiandika kwa mfano Kata ya Lwamgasa ni kwa wachimba madini, kuna wananchi takribani 40,000 kwenye Kata ile, wanahitaji kituo cha afya lakini kituo hakikupatikana. Nikaandika Kata ya pili ya Nyakagomba ina wananchi takribani 30,000 kituo hakikupatikana, nikaandika Kata ya Tatu ya Magenge kuna wananchi karibu takribani 17,000 haikupatikana. Ni kweli inawezekana criteria iliyotumika ilitutoa nje kwamba inahitaji Tarafa, lakini hawa wananchi wote tutawahudumiaje?

Mheshimiwa Spika, ni ombi langu sasa Mheshimiwa Waziri uangalie uwezekano wa vituo hivi tuvipate kwa ajili ya kuhudumia wananchi wetu, wananchi 40,000 hawana kituo cha afya tutawahudumiaje wanahamia kwenda kununua dawa kwenye pharmacy, wanapougua tu wanahisi hii yawezekana ni malaria acha nifanye nini, ninunue dawa tu nipone wengine watakuwa wanapoteza maisha kwa mtindo huo. Kwa hiyo, ni ombi langu Mheshimiwa Waziri kwamba hili utalikumbuka na utaweza kulifanya kazi.

Mheshimiwa Spika, kwenye afya nako tuna maboma, nimeona maboma 300 kwenye ukurasa Namba 21 yanaonekana yamejengwa, kule Busanda yapo maboma mengi tu ya zahanati yamejengwa yanahitaji kumaliziwa, niombe sana kwenye bajeti hii Wizara iangalie uwezekano wa kuyamalizia hayo maboma, yako yaliyoezekwa yanahitaji umaliziaji, yako ambayo hayajaezekwa yanahitaji kumaliziwa tu ili wananchi waendelee kupata huduma.

Mheshimiwa Spika, ninaamini kabisa haya niliyoyasema machache kama yakiguswa nitajua hii bajeti kule kwangu watasema ni bajeti ya wananchi. Baada ya maneno haya naunga mkono hoja. (Makofi)