Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Deus Clement Sangu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa hii ili na mimi niweze kutoa mchango wangu kwenye Bajeti hii ya Ofisi ya Rais TAMISEMI. Kwanza kabisa nikupongeze Mheshimiwa Waziri na timu yako hapa ya wachapakazi na mnafanya kazi nzuri katika wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitumie nafasi hii ndani ya Bunge hili kutoa pole kwa wananchi wangu wa Jimbo la Kwela katika Kijiji cha Talanda Kata ya Mileka kwa maafa yaliyotokea, ambapo mafuriko makubwa yamesababisha vifo vya watu saba na zaidi ya kaya 20 zimekosa makazi. Nishukuru Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ametuahidi atatuma timu na dada yangu Jenista uko hapa mtusaidie kwenda kutoa msaada wa kibinadamu kwenye ofisi yako kwa maana ya Kitengo cha Maafa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa aliyoifanya ndani ya Jimbo la Kwela. Nina mirad mikubwa mingi ambayo nikianza kusema hapa nitatumia muda mrefu sana lakini nina forum ambayo tutaendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina mambo machache ya kijimbo na baadaye nitaongea mambo ya jumla ya kitaifa. Jambo la kwanza ambalo nakuja kwenu ni ombi. Katika Jimbo langu la Kwela Mji Mdogo wa Lahela hatuna hospitali kabisa. Tuna jengo ambalo ni Mji wa Makao Makuu ya Wilaya ni mji ambao ndio center kubwa katika ndani ya Jimbo la Kwela lakini hatuna hospitali. Kwa maana ya kwamba tuna kituo ambacho kinamilikiwa na Kanisa Katoliki, wametupangisha pale kwa muda wa miaka 40 na hatuna umiliki wowote kama Serikali. Sasa makao makuu ya wilaya kukosa hospitali na huduma pale kimezidiwa kwa sababu population imekuwa kubwa. Niwaombe, ombi hili nimelileta mara nyingi wizarani mnalijua, naomba tulipe kipaumbele ili kuipa hadhi makao Makuu ya Wilaya, Halmashauri yetu ya Sumbawanga ambayo ni mji mdogo wa Lahela.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu la pili kwenu ndugu zangu Mheshimiwa Waziri naamini ni wasikivu, bajeti yetu ya TARURA ipo inafanya kazi yake nashukuru imeongezeka na hili nampa sifa Mheshimiwa Rais. Lakini kuna barabara maalum, kuna barabara ya kutoka Chombe, Kiandaigonda kwenda mpaka Kaozi ni kilomita 18.8. Barabara hii ni korofi na na barabara muhimu ya kimkakati katika uchumi wa kukuza na kupata mapato ndani ya halmashauri yangu. Ombi langu kwenu, naombeni mfanye hima ili mtusaidie na sisi Halmashauri ya Sumbawanga tuweze kukusanya mapato na tufikie malengo yetu ndani ya halmashauri; mtupatie fedha za dharura kutengeneza barabara hii muhimu. Najua jambo hili liko ndani ya uwezo wenu bajeti ya kwaisa ya TARURA haitoshi muifanyie udharura wake tuweze kuwasaidia wananchi wangu kama hivyo nilivyosema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine muhimu ambalo nawaletea leo ni maboma ya zahanati. Wananchi wangu wamejitahidi, ndani ya vijiji 16 wamejenga zahanati ambazo zimefikia hatua ya mwisho kiasi kwamba tukiwapa fedha kidogo zahanati zile zinaenda kufanya kazi. Kuna Kamsamba, Mtetevu, Tapewa, Kazi, kuna zahanati nyingine ya Mtapenda, zahanati ya Mumba, Zahanati ya Lilolyambula, Zahanati ya Kawila, Zahanati ya Ilambo; ziko zahanati 16 kwa sababu ya muda nitawaletea mzione hapa. Nawaombeni hizi zahanati zinahitaji kupelekewa fedha kidogo zahanati zile zinaanza kufanya kazi na wananchi watapata huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya hapo vituo vya afya. Wananchi wangu wa Kata ya Ilemba, wananchi wangu wa Kata ya Mwive wamepambana wamejenga, wamejitolea zaidi ya miaka 10 kujenga vituo vya afya lakini wamefika mahali nguvu imeisha wanahitaji msaada wa Serikali. Nilishaleta maombi haya hapo wizarani nimesema mara nyingi ndani ya Bunge hili niwaombe sasa na sisi tuweze kufurahia neema ili wananchi wa Ilemba, wananchi wa Mwive wafurahie kupata vituo vya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni uhaba wa watumishi. Na hili naomba mnisikilize Mheshimiwa Waziri. Pale mnawapa ajira zinatoka vijana wanaripoti vizuri mnawaleta Sumbawanga. Wakishafika Mkoa wa Rukwa wanaanza kuomba uhamisho na uhamisho huo mnatoa mara moja bila kuzingatia hata kwamba wanatakiwa wakae hata miaka mitano kwa mujibu wa taratibu. Kwa hiyo pale imekuwa ni kama sehemu ya kupatia cheque number. Mtu anachukua cheque number anaondoka anaendelea na maisha mengine. Tumepelekea uhaba wa watumishi ambapo kada ya ualimu tu ina upungufu wa walimu 1187, kada ya afya 867. Hali ni mbaya, tumeshindwa, kuna baadhi ya shule hakuna, nina shule 19 hazina hata mwalimu mmoja wa kike nikuombe sana ni hali ya hatari tunaongelea mambo ya unyanyasi wa kijinsia. Halafu shule nzima hakuna hata mwalimu mmoja wa kike, shule 19, hii ni disaster. Tutakuta mama na mwana wanakuja kulaumiwa mimba za utotoni, ubakaji na mambo mengine mabaya yaliyosemwa ndani ya Bunge hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri haya muyachukue na kwenda kunisaidia tupate ajira hizi mpya zitakapotoka muwape kipaumbele Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la nne ambalo ni muhimu nataka niongelee mambo ya usimamizi madhubuti wa fedha tunazopeleka kwenye miradi. Kuna jambo ambalo ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais ndani ya mkoa wetu tunaenda kupata mradi mkubwa kwenye Manispa yetu ya Sumbawanga Jimbo la Mheshimiwa Aeshi, bilioni 27 zinaenda kujenga barabara na kwenda kujenga soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nataka nitoe tahadhari, tuko kwenye mchakato wa manunuzi sasa hivi, kuna mambo tumeyaona sehemu nyngine, hayafurahishi na yanatia dosari Ofisi ya Rais TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri dada yangu wewe ni mchapakazi, tulifanya ziara pale Dar es Salaam kwenye mradi wa DMDP ambao ulikuwa ni Dola za Kimarekani milioni 330, tumekutana na mambo ya ajabu sana. Tulipokutana pale Ofisi Ndogo ya Bunge tukiwa na timu yako ya Wizara kila mtu ameshika tama anasikitika. Vifurushi vyote, package 19 za miradi ile kuna ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha. Nakupa tu mfano ili mpate picha kwamba miradi hii ya TaCTIC ambayo inaenda kufanyika nchi nzima mmejipangaje, mmejiandaa kuifanya miradi hii au tui-suspend kwa kuwa ubadhirifu unakuwa mkubwa na unakatisha tamaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakupa mfano stendi ile ya Buza mkandarasi walimchelewesha kutofanya kazi kwa siku 289. Hawajamwambia chochote, wako kimya watalamu wako. Baada ya hapo akawaletea madai ya milioni 488 kwamba mmenichelewesha wakalipa bila wasiwasi wowote. Mkandarasi huyo huyo akafanya kazi akamaliza, baadaye wakamchelewesha malipo, alivyoleta certificate wakachelewesha kwa zaidi ya siku 100 akaleta riba ya milioni 879, hasara bilioni moja na kidogo mmeisababishia hasara Serikali. mimi ninalia zahanati 16 kuna mabilioni huku yanaliwa kirahisi tu ndani ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini haitoshi, jambo la kusikitisha kabisa, certificate mpaka leo ninavyoongea, ni jambo tumeliona wiki mbili zilizopita nendeni mka-verify; inawezekanaje mtu analipwa certificate kabla hajamaliza kazi? Kuna miradi iko asilimia 68, asilimia 79, asilimia 80 wameshalipa certificate zote na wengine wako site walishalipwa hela zao, akiamua anaweza akaondoka zake hamna cha kumfanya kitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuko makini, kila mtu anajifanyia jambo anavyotaka. Niwaombe sana mama anahangaika kutafuta fedha ukiukwaji wa taratibu za manunuzi umekidhiri kwenye miradi hii. Tumekuta pale kuna variation mpaka ya asilimia 125, yaani mradi ni ya milioni 720 mtu ameenda kufanya variation wakati imekuwa bilioni 2.3 nashangaa haya mambo yanafanyikaje? Kwa hiyo ukienda kupitia package ili upate somo zuri Mheshimiwa Waziri kapitie package 19 zote za miradi ule wa DMDP utakuta kuna madudu. Uki- sum-up ile cost wewe mwenyewe kichwa kitakuuma utaenda kutafuta maji unywe Panadol, kwa sababu mpaka sasa hivi natafakari jambo hili linasikitisha sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nakushukuru sana naunga mkono hoja. (Makofi)