Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Hawa Mchafu Chakoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hotuba ya Bajeti ya Wizara ya TAMISEMI. Awali ya yote nipende sana kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunisimamisha mbele ya Bunge lake tukufu, pia napenda kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, Angellah Kairuki na Manaibu wake Dkt. Festo Dugange pamoja na Deo Ndejembi kwa kazi nzuri wanayoifanya na kwa uwasilishaji wao wa hotuba hii yenye kurasa takribani 286, napenda kuwapongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa ni miongoni mwa Mawaziri ambao wanatoa ushirikiano, wanapokea simu na wanajibu meseji pindi unapowapa changamoto za watu wetu huko Majimboni, kwa hiyo napenda kuwapongeza sana na muendelee kumsaidia Mheshimiwa Rais kwa kasi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa kwanza nitakwenda kwa kuanza kumpongeza Dkt. Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya nchini Tanzania. Nimesoma bajeti mbili zilizopita za Rais Samia kwa upande wa miradi ya maendeleo kwa Mkoa wetu wa Pwani namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwani Halmashauri zote Tisa za Mkoa wa Pwani zimepata miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na miradi ya sekta za afya. Kwa upande wa Mkoa wa Pwani tumepata Hospitali mpya za Wilaya Tatu na siyo Tatu niseme Nne ikiwepo Hospitali ya Wilaya ya Kibiti, Kibaha DC, Kibaha Mji pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze, kilichokuwa Kituo cha Afya Msoga tumepatiwa fedha nyingi sana na tumejenga majengo na kimeshapandishwa hadhi na sasa na yenyewe imekuwa hospitali ya Wilaya. Kwa kusema hivyo ni kwamba tunazo Hospitali mpya 4 ndani ya Mkoa wetu wa Pwani. Tunayo kila sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kusema hapa ni kwamba Mheshimiwa Rais amesogeza huduma ya afya karibu kabisa na wananchi wake na kimsingi kama ambavyo tunafahamu afya ni jambo muhimu sana kwenye maisha ya binadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ninachotaka kukisisitiza ni kwamba Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametimiza wajibu wake, ametupa Mabilioni lakini ametupa hospitali ya Wilaya. Jukumu na kazi iliyobaki hapa ni kwa Wizara na nitaomba Mheshimiwa Waziri na Naibu Mawaziri wako muweze kunisikiliza. Mheshimiwa Waziri tunayo changamoto kubwa ya upungufu wa Watumishi, haitakuwa na maana na haitakuwa na afya, Rais katoa Mabilioni ya fedha, tumejenga Hospitali ya Wilaya, lakini tunakosa Watumishi, wananchi wetu wanaenda pale wanakosa kupata huduma kwa sababu watoa huduma hawapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya Mkoa wa Pwani tuna watumishi wa kada hii ya afya asilimia 48 tu kwa kusema hivyo tunakuwa na upungufu wa watumishi wa kada ya afya kwa asilimia 52. Nitaomba ili u ende kuliandika na peni yako ya kijani. Katika zile ajira 21,200 zilizotolewa na Mheshimiwa Rais, nitaomba Pwani uiangalie kwa jicho la dharura ili tuweze kupata watumishi wa Kada ya Afya, tuweze kupunguza hii asilimia 52 kwani imekuwa ni kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ambalo Mheshimiwa Waziri naomba uende kuandika kwa peni yako ya kijani ni suala la upungufu wa vifaatiba. Tunashukuru tumepata hospitali Nne za Wilaya lakini tunakosa vifaatiba. Katika hili Mheshimiwa Waziri umelisema katika hotuba yako ukurasa wa 150, kwamba umetenga Bilioni 15 point au niseme Bilioni 16 kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba. Kwa hiyo ombi langu hapa ni lilelile kwa hiyo niangaliwe kwa jicho la huruma, ili tuweze kupatiwa vifaatiba katika Hospitali zetu hizo za Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ambalo Mheshimiwa Waziri na lenyewe nenda kaliandike na kalamu yako ya kijani, ni kuhusiana na suala zima la hospitali kongwe. Kama nilivyotangulia kusema katika Halmashauri zetu Tisa Halmashauri Nne mmetupa Hospitali za Wilaya tunawashukuru sana. Halmashauri Tano zimebaki ni hospitali kongwe ambapo kimsingi majengo yake pamoja na mifumo ya kutolea huduma imekuwa chakavu sana inahitahi ukarabati, amezungumza kwenye hotuba yake kwenye ukurasa wa 149 kwamba umetenga Shilingi Bilioni 27.9 kwa ajili ya ukarabati wa hospitali kongwe. Nikuombe sana usizisahau Halmashauri za Mkoa wa Pwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, jambo la nne ninaloomba ukaliandike kwa peni ya kijani, ni vizuri sana kukawa kuna mawasialiano kati ya zahanati, kituo cha afya na hospitali ya Wilaya. Ndani ya Mkoa wa Pwani tunao upungufu wa magari ya wagonjwa, kwa hiyo nimetoa mambo haya manne ambayo nimekuomba na kukusisitiza yaandikwe kwa peni ya kijani kwa sababu nitaomba uyahifadhi na uyafanyie kazi pindi tunapokuja hapa mwakani kwa ajili ya Bajeti.

MWENYEKITI: Ahsante sana, Mheshimiwa Hawa Mchafu kwa mchango wako.

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru ahsante naunga mkono hoja. (Makofi)