Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Anna Richard Lupembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ninaomba nishukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuchangia Wizara yetu ya TAMISEMI. Naomba nimshukuru Mungu ambaye ameendelea kutupa uzima na uhai leo tuko hapa tukichangia kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichukue fursa hii kwanza kabisa kumshukuru Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ambayo anaifanya kwa ajili ya Watanzania. Amefanya kazi kubwa, hivi leo kwa kipindi hiki kifupi katika Jimbo langu nimepokea Bilioni 6.2 kazi kubwa sana, sana, sana. Ninaomba nimpongeze Spika wetu Dkt. Tulia, amefanya kazi kubwa tumeiona kwa macho, maendeleo ndani ya Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni maendeleo makubwa kuna mabadiliko makubwa. Hongera sana Dkt. Tulia, kwa kazi kubwa ambayo unaifanya katika Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimpongeze Waziri pamoja na Naibu Mawaziri kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya kusimamia miradi mbalimbali na maendeleo ya jumla katika Wizara yetu ya TAMISEMI, pia ninaomba nimpongeze kwa kipekee Mkuu wangu wa Mkoa Mwamvua Mlindoko, kwa kazi kubwa anayoifanya ndani ya Mkoa wetu wa Katavi. Anasimamia miradi, anafuatilia, anahakikisha maendeleo yanasonga mbele katika Mkoa wetu wa Katavi, anastahili pongezi Mkuu wetu wa Mkoa wa Katavi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaenda TARURA, ninaomba nichukue fursa hii ya kumpongeza Chief anayesimamia TARURA. Anastahili tuzo, anastahili tuzo Mheshimiwa Waziri, tunaomba umpe tuzo. Chief wa TARURA kwa kazi kubwa nzuri anayoifanya. Leo hii katika maeneo yetu, Majimbo yetu, barabara zinapitika, madaraja yalikuwa hayapitiki watoto walikuwa wanapata shida hawawezi kuvuka kipindi hiki cha masika lakini leo lhii madaraja yamejengwa wananchi wanavuka, watoto wa shule wanavuka, anastahili pongezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoomba leo hii TARURA waongezewe pesa kwa sababu wanafanya kazi kubwa na vilevile TARURA wana mtandao mkubwa wa barabara kuhakikisha vijiji vyetu na vitongoji vyetu uchumi wa wananchi unakua, kwa sababu tumeona kwa kipindi hiki barabara zimefunguka, wananchi wetu wamepata uchumi mkubwa, mazao yote yamebaki shambani, wafanyabiashara wanawafuata wakulima katika maeneo yao sasa tunaomba TARURA waongezewe pesa na vilevile madaraja yaendelee kujengwa na wapangiwe bajeti kwa ajili ya matengenezo. TARURA hawana bajeti ya matengenezo, lazima wapangiwe bajeti ya matengenezo ili barabara ziweze kuboreshwa siku hadi siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano sasa hivi barabara mvua zinanyesha, barabra nyingi zinaharibika, hawana fungu, tunaomba TARURA wapewe fungu la matengenezo ili barabara zetu ziweze kupitika mwaka mzima bila tatizo la aina yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakuja upande wa elimu ya msingi. Nimepongeza, ninaomba niishukuru Serikali kwa kazi kubwa ambayo inaendelea kuhakikisha kuboresha na leo hii tumepata pesa kwa ajili ya kujenga shule mpya, ninaomba nishukuru kwa kupewa pesa hizo, nimepewa pesa kuhakikisha zile shule zote shikizi ambazo tulizijenga wakati uliopita, vyoo vyao vijengwe, tumepokea hizo pesa, ninaomba nishukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima sasa tujiwekeze, walimu walio katika maeneo ya mazingira magumu kama vijijini hawana nyumba, lazima sasa hivi tuweke mikakati kuhakikisha tunawajengea nyumba ili waweze kukaa katika maeneo husika. Tatizo walimu hawakai kwa sababu hawana sehemu ya kuishi katika maeneo yetu ya vijiji. Ninaomba sana, sasa tujiwekeze kuhakikisha tunajenga nyumba ili walimu waweze kukaa katika maeneo safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajua Serikali imefanya kazi kubwa kupitia vituo vya afya, zahanati zote hizo tumepokea pesa, lakini ninaomba kwenye Jimbo langu, Kituo cha Afya cha Ugala niliahidiwa milioni 800 lakini mpaka sasa hivi nina Milioni 500, Kituo cha Afya cha Itenka niliahidiwa Milioni 800, mpaka sasa hivi nina Milioni 500, ina maana kuwa bado ninadai kuna maeneo ambayo majengo hayajakamilika ninaomba Serikali kupitia Waziri wetu wa TAMISEMI, ni msikivu pamoja na Naibu Mawaziri, tunaomba basi mtumalizie hizo pesa tuweze kumaliza vituo vya afya viweze kukamilika ili wananchi wa Jimbo la Nsimbo waweze kupata huduma safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipongeze tumeshaanza kupata vifaatiba vimeshaanza kuwasili na dawa katika Zahanati tulizozijenga na vile ile nilikuwa ninaomba, kuna Zahanati ambayo maboma wananchi wamejenga, zile Zahanati naomba pesa kwa ajili ya umaliziaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi kubwa imefanyika na Serikali ya Mama Samia, kazi kubwa lazima apongezwe Mama huyu amefanya kazi kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi kubwa inafanywa na Watendaji wa Vijiji lakini ninaomba nishukuru kwa ajira ambazo sasa hivi tumepata ajira 13,000 lakini Watendaji bado hatuna, ninaomba tufanye ajira ya Watendaji. Watendaji wa Mijini kule Vijijini hawapo, tunaomba sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninaiomba Serikali tunaendelea kuomba kila siku Wenyeviti wa Vijiji tunawapelekea miradi mikubwa wanashika hela nyingi, hebu tuwatazame huko Wenyeviti wa Vijiji, tuwawekee posho at least wapate ari ya kufanya kazi. Tunapeleka miradi mikubwa lakini posho yao haijulikani. Ninaomba Wenyeviti wetu sasa hivi wanapokea miradi mikubwa, tunaomba watazamwe kwa jicho la huruma, wapewe chochote ili waweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)