Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa utulivu wake wakati alipokuwa anawasilisha hotuba yake hapa Bungeni asubuhi. Hongera sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia maeneo matatu. Kwanza nitazungumza neno la shukrani; na pili, nitazungumza kidogo maajabu ya Rais Samia, halafu mwisho nitahitimisha na ushauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika shukurani kwa niaba ya wananchi wa Sikonge, naomba niwasilishe shukrani zetu za pekee kabisa na za dhati kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo amekuwa akiyasikia maombi yetu na kututekelezea bila kusita. Ametupatia fedha nyingi kwenye sekta za elimu, afya, maji, umeme, miundombinu ya barabara, kilimo cha umwagiliaji, na kadhalika. Kwa hiyo, kwa kweli hapo tunashukuru sana. Tunaomba Mheshimiwa Waziri utufikishie salamu zetu hizi za shukrani kwa Rais ili atambue kwamba tunathamini sana jinsi ambavyo amekuwa na sisi kwa shida na raha muda wote daima. Ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nieleze kidogo maajabu ya Mheshimiwa Rais. Ajabu la kwanza, tarehe 31/05/2022, saa 3:00 hadi saa 5:00 usiku katika Hoteli ya Serena, ukumbi wa muziki, Mheshimiwa Rais alihudhuria hiyo hafla ambapo miongoni mwa waandaaji alikuwa ni Mheshimiwa Joseph Mbilinyi au Sugu. Hii ilikuwa ni hafla ya muziki wa vijana wa Hip-hop. Hakuna Rais yeyote Tanzania aliyewahi kufanya jambo hilo la kutoka Ikulu usiku kwenda kwenye muziki wa vijana. Watanzania walifurahi, lakini dunia ikashangaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni tarehe 08/03/2023 huko Moshi, Rais Samia Suluhu Hassan alikuwa Mgeni Rasmi kwenye Kongamano la Siku ya Wanawake Duniani ambalo liliandaliwa na Baraza la Wanawake wa CHADEMA au BAWACHA. Tukio kama hilo kwa Mwenyekiti wa chama kinachotawala kwenda kuwa mgeni rasmi kwenye kongamano ambalo limeandaliwa na chama cha upinzani halijawahi kutokea, siyo Tanzania tu, bali ni duniani. Kwa hiyo, hayo ni maajabu ambayo Mheshimiwa Rais ameyatumia kuipa elimu dunia kuhusu falsafa zake za kuiongoza nchi hii ambazo ni maridhiano, kustahimiliana, mabadiliko, pamoja na kujenga nchi upya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Bunge lako Tukufu kwa jinsi ulivyompongeza, inatakiwa tuendelee kumpongeza siku zote kwa jinsi ambavyo ameendelea kuonesha maajabu duniani. Kwa hiyo, nampongeza sana kwa maajabu yake hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maeneo machache ya ushauri. Eneo la kwanza, Mheshimiwa Waziri na Wabunge wote na Manaibu Mawaziri watakumbuka kwamba, tarehe 04 Aprili, 2023 siku tumeanza Bunge la Bajeti hapa niliandika barua ya wazi, nikaainisha ukubwa wa Jimbo la Sikonge, kilometa za mraba 27,873 linazidi mikoa 11; mikoa kamili. Mkoa wa Kilimanjaro kwa jimbo langu unaingia mara mbili kwa eneo la kijiografia. Kwa hiyo, mtawanyiko wa kata na vijiji ulivyo unaweka changamoto ambazo ndugu zetu hawa wa TAMISEMI wanatakiwa watupe kipaumbele maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili niliainisha kwenye barua yangu ile jinsi ambavyo idadi ya watu imeongezeka Sikonge kutoka watu 179,883 mwaka 2012 hadi watu 335,686 ambao ni ongezeko la karibu mara mbili. Katika ongezeko hili asilimia 45 ni watoto ambao wanatakiwa kwenda shuleni. Kwa hiyo, tunahitaji shule mpya zaidi ya 25, tunahitaji madarasa 1,039, tunahitaji madarasa ya kukarabati 90, tunakaribisha maboma 200. Mambo yote haya nimeyaainisha kwenye ile barua yangu ya wazi na Mheshimiwa Waziri ameisoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vipaumbele ambavyo nimevieleza kwenye ile barua yangu ya wazi, naomba sana avikumbuke wakati watakapopata fedha zile ambazo zinakuja nje ya bajeti kwa sababu, haya mengine yapo ndani ya bajeti hii ambayo tutaipitisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, naomba Serikali ikamilishe na ilete Bungeni Muswada wa Sheria ya Elimu, kutekeleza Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 ambayo ilitoa maelekezo kwamba mtoto asome kuanzia Chekechea mpaka Form Four bila kupumzika. Maana yake ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba, hata ile Sheria ya Ndoa ambayo ilikuwa inazungumzwa sana kwenye jamii itakuwa haina maana tena kama tutapitisha hiyo Sheria ya Elimu, kwa sababu mtoto atasoma kuanzia Chekechea mpaka Kidato cha Nne bila kupumzika wala kuishia Darasa la Saba wala kuishia wapi. Kwa hiyo, hiyo ndiyo itakuwa suluhisho la matatizo na mjadala kwenye jamii kuhusu mambo ya ndoa. Maana Sheria ya Elimu haitaruhusu mwanafunzi aolewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, naunga mkono. (Makofi)