Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Tabasamu Hamisi Hussein Mwagao

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sengerema

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Bajeti hii ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niko katika maeneo mahususi kama matano. Eneo la kwanza ambalo naomba kuelekeza mchango wangu ni miradi inayokuja katika maeneo ya majimbo yetu na miradi inayopelekwa katika halmashauri zetu nchini. Wasimamizi wa miradi hiyo ni Waheshimiwa Madiwani tukiwemo sisi kama sehemu ya Madiwani katika maeneo yale. Lakini pia wasimamizi wengine ni wenyeviti wa serikali za vijiji, na tatu, wapo wenyeviti wa Serikali za Mitaa na vitongoji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa uwiano wa mapato na matumizi; kinachopelekwa kule katika bajeti zetu unakuta halmashauri inapewa bajeti ya bilioni 42, 46. Lakini wanaokwenda kusimamia bajeti ile ni Waheshimiwa Madiwani ambao wanapewa posho ya shilingi 300,000. Wapo watendaji wa kata wana mishahara zaidi ya shilingi 700,000 na kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu uwiano kwamba Mwenyekiti na msimamizi wa shughuli za maendeleo za kata ni Mheshimiwa Diwani. Nilikuwa Diwani wa Kata ya Nyampulukano, Sengerema Mjini, najua matatizo wanayopata Waheshimiwa Madiwani katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamuomba sana Mheshimiwa Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, suala la Waheshimiwa Madiwani kupewa posho na posho zenyewe zinakuja kwa kuchelewa, jambo ambalo haliwezekani, halikubaliki hata kidogo. Taarifa ya CAG, wizi mkubwa unatokea katika halmashauri zetu, wasimamizi wa miradi ile ni Waheshimiwa Madiwani ambao mishahara yao, posho zao haziko katika sehemu ya ajira; haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mafiga matatu tunaachania wapi? Tukienda kutafuta kura tunatafuta kura za Mheshimiwa Rais, tunasema mafiga matatu; tunatafuta kura za Mheshimiwa Mbunge, tunatafuta kura za Mheshimiwa Diwani. Kwenye maslahi tunaachana; haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuwe wakweli; Chama cha Mapinduzi ni chama kikubwa katika Afrika, kina heshima katika Afrika, lakini kinaendesha Serikali ambayo ina matabaka. Kama Mheshimiwa Diwani hataingizwa katika sehemu ya ajira, Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, dada yangu, nakupenda lakini safari hii nakamata shilingi kwa mara ya kwanza. Nimekuwa Mbunge huu mwaka wa pili nakwenda wa tatu, naangalia maslahi ya Madiwani, inashindikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napata shida kule kuendesha halmashauri kama Mbunge. Kila tatizo linakuja kwa Mbunge; Diwani kwanza atasafirije, posho ya Diwani ya kikao, vikao vyenyewe vinahesabika. Diwani akiamka asubuhi ana watu kama nane nyumbani kwake; huyu mtoto anaumwa, mwingine anatakiwa kufanyiwa operation, nilikuwa Diwani, nilikuwa nayaona haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu huyohuyo Diwani ndio akasimamie madarasa. Sasa kama kuna mifuko kule kumi inatakiwa ijengee akiambiwa miwili Mheshimiwa Diwani na wewe utapata shilingi 20,000, kwa nini asikubali? Naomba sana jambo hili ulifanyie kazi tuone namna gani maslahi ya Madiwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maslahi ya wenyeviti wa Serikali za vijiji; mapato yanakusanywa katika halmashauri zetu, ni kutoa mwongozo tu kwamba posho za Waheshimiwa wenyeviti wa Serikali za vijiji zitokane na halmashauri. Wapunguze katika mapato yao, tunapata asilimia 40, hii asilimia 40 iliyopatikana sisi inakwenda katika miradi yetu ya maendeleo. Asilimia 60 inakwenda kutumika kwa watendaji ambao wanaletewa OC, wana mishahara, wanaletewa OC, wana semina, wana kila kitu. Wapunguze kule wapelekewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina vijiji 71 katika Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema. Lakini wenyeviti wangu wa Serikali za vijiji posho watoe kwa Mbunge; hiki kitu hakiwezekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakuja kwa Waheshimiwa wenyeviti na watendaji wa Serikali za Mitaa. Hawa wenyeviti ni kwamba wanapewa mishahara yao ni mihuri, na nilisikia mkuu wa mkoa mmoja anasema anataka kuwanyang’anya mihuri. Hiyo mihuri inasaidia mtu akienda kuuza mfugo wake katika mnada, Mheshimiwa mwenyekiti wa kitongoji ndiyo anapata 5,000; mtu anakwenda kuweka dhamana anapata shilingi 5,000. Hatuwezi kuwa na tabaka la utawala bora watu wengine wanaishi kwa mhuri halafu wanasimamia mapato ya halmashauri; haiwezekani hata siku moja. Hili ni jambo ambalo siwezi kulikubali mimi kama Mbunge wa Chama Cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakwenda kwenye uchaguzi mwaka kesho. Hawa wenyeviti wa Serikali za vijiji ndio wanakwenda kutoa sura ya nchi hii. Tunaanza nao wao kwenda kuwatafutia kura, tunawatafutia kura wakachaguliwe tu hatutafuti malshi yao; inakuaje Waheshimiwa Wabunge? Hili tunataka lije katika majumuisho ya Mheshimiwa Waziri, wanawekwa namna gani hawa watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapato ya halmashauri; mapato haya yako katika server moja katika nchi hii. Kule sisi tunaona kabisa kwamba kwa mfano nina maeneo ya mashine za mpunga zinapakia malori kumi, mtu akichomoa tu kile ki-server kinachokaa katika mashine anaanza kutoa risiti zinatoka na unaona kabisa lori moja pale lina shilingi 600,000, unaona hapa kuna milioni sita. Kwa nini wale wasipewe na wao password wakurugenzi waone? Sisi Wabunge kuna dhambi gani tukipewa password tukaona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu unaona kabisa kwamba leo yamepakia malori kumi ya mbao, lakini unashangaa linalokwenda kulipiwa ni lori moja; haiwezekani. Mapato yaanaza kupigwa kuanzia huko chini. CAG anakuja kukagua kitu ambacho tayari kimeshaibiwa. Kwa nini msitupe password tukaanza kuona sisi hayo mapato? Kuchungulia. Kama tunaweza kuchungulia sisi kwenye statements zetu za benki, unaangalia kwenye mfumo leo tumeuzaje. Leo mtu mmoja tu anaangalia TAMISEMI nchi nzima; upigaji ndio uko kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo unamwamini Mkurugenzi kumpa bilioni 42, unashindwa kumuamini mapato ya shilingi bilioni tatu; inawezekana wapi unashindwa kuwapa wao password wakaangalie kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya utawala, ametoka kuzungumza kaka yangu hapo; naangalia tu kama mikoa hii, Mkoa wa Tabora, tunaangalia Mkoa wa Morogoro, tuangalie Mkoa wa Geita ulivyo mkubwa, tunaangalia kuna wilaya ziko kubwa; Wilaya ya Kahama; Kiteto, Sengerema. Mimi Wilaya ya Sengerema kata zangu nne, kata moja tu ya Nyamatongo Katunguru, ukichukua Katunguru ukachukua na Ngoma B ukachukua na Chifunfu ni sawasawa na eneo moja tu la Jimbo la Nyamagana; kata nne. Ukichukua kata zangu tano, Igalula, Kagunga, Buyagu na Kishinda ni Jimbo la Nyamagana. Halafu leo hii tunavyozungumza hapa… (Kicheko)

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: …mimi leo Mbunge nina kata 26; haiwezekani maneno kama haya.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mbunge wa Nyamagana, taarifa.

TAARIFA

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa kaka yangu, Mheshimiwa Tabasam, tunapozungumza ukubwa wa Jimbo na bajeti, siyo ukubwa wa eneo ni wingi wa idadi ya watu waliopo kwenye eneo husika. Kwa hiyo, atambue kwamba anapoizungumza Nyamagana, anazungumzia Jiji la pili kwa ukubwa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Tabasam, unapokea taarifa hiyo?

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei taarifa yake kwa sababu kwanza ninachotaka kukwambia, hiki ninachozungumza mimi ni sehemu ya taarifa ya sensa. Sengerema nina wananchi 500,000…

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: …Ukichukua wananchi wa Jimbo la Buschosa 450,000, ni wilaya ya tatu katika nchi hii kwa idadi ya watu. Haiwezekani kitu kama hiki. Na watu wanaokwenda Nyamagana wanatoka Sengerema.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Tabasam, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mnzava.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Waendelee kunipa hizo taarifa.

TAARIFA

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa mzungumzaji, Mheshimiwa Tabasam, kwamba naungana na anachokisema kwa sababu hata ukiangalia kwa mfano Halmashauri ya Mji wa Korogwe ni ndogo kijiografia lakini kwa sensa ni watu 58,000, Korogwe DC ni kubwa kijiografia lakini kwa sensa ni watu 200,000 na. Lakini mara nyingi migao inatoka sawasawa.

MWENYEKITI: Unapokea taarifa Mheshimiwa Tabasam?

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, imekaa vizuri. (Makofi/Vicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumwambia Mheshimiwa Waziri wa Serikali za Mitaa kwamba idadi ya wanafunzi wa shule ya msingi kwangu ni 116,000, madarasa niliyonayo ni 950. Upungufu wa madarasa katika Halmshauri ya Wilaya ya Sengerema ni 1,600. Nyumba za walimu ninazo 52 tu, upungufu ni nyumba 600 za walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, walimu nilionao hawatoshi kuwafundisha wale wanafunzi. Shule moja ya Chifufu, Shule ya Msingi Bugumbikisa ina wanafunzi 3,700, watoto wa awali 350, wanafunzi 4,000, walimu 22; hawa walimu kweli wako sawa na walimu wa Nyamagana? Shule moja ya Nyamagana ina wanafunzi 2,000 walimu 110; haiwezekani mgao kama huu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyozungumza na wewe tunaomba bajeti ya Serikali za Mitaa igawanywe kwa mujibu wa sensa. Mheshimiwa Rais karuhusu pesa, tumetumia zaidi ya bilioni 400 kwa ajili ya kuhesabu watu na makazi. Tuje kwenye bajeti kwa usawa, hakuna maneno haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatutakubali, safari hii bajeti hii itakuwa ni ngumu. Dada yangu nakupenda sana, umeangushiwa zigo bovu. Amesema Mheshimiwa Shabiby hapa, gari hili ni jipya lakini lina engine ya bajaj. Ninachotaka kukwambia anza kukarabati...

MWENYEKITI: Haya.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunisikiliza, Watanzania msikie haya tuliyoyasema. Safari hii mgao ni kwa bajeti, keki ya nchi hii tuipate wote. Hakuna haya maneno watu wengine wapate keki ya nchi hii, watu wengine tuwe wasindikizaji kwenye nchi hii, hapana. Hapana, hatukubali. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Tabasam.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)