Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kiteto
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi ya kuanza kuchangia TAMISEMI. Kwanza kabisa nimshukuru Mwenyenzi Mungu kwa afya njema aliyotujalia na nimpongeze Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa miradi mingi sana ambayo kwa kweli ameipeleka kwenye majimbo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jimbo la Kiteto pekee yake, miradi ya miaka miwili hii ni karibu bilioni 18. Kwa kweli amegusa karibu kila mahali, VETA sasa tunazungumza inajengwa Kiteto. Tumepata vituo vya afya viwili bilioni 1, Daraja la Sunya karibu milioni 800, shule shikizi madarasa karibu 57, shule za sekondari madarasa 44, mradi wa maji pale Kaloleni, digital x-ray milioni 900 kwa ajili ya kukarabati hospitali ya wilaya. Ambaye sasa sisi tuliomba na hii ni renovation ya Mkurugenzi aliomba kwamba tunajenga jengo la mama na mtoto, jengo la upasuaji na maabara. Sisi tulikataa kukarabati majengo yale na nashukuru TAMISEMI kwa sababu tumeomba na wametuambia, wametupa go ahead. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lniseme TAMISEMI walituambia ili kuweza kujenga majengo hayo sisi tunahitaji karibu bilioni moja na milioni 300 na wao wametupata mia 900 lakini sisi tukasema tutajenga kwa hiyo mia 900. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii pia kumpongeza Mkurugenzi kwa renovation hiyo nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimpongeze Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Angellah, Naibu Waziri Dugange na Ndejembi, Katibu Mkuu, wote na timu nzima hii kwa kazi nzuri ambayo wanajaribu kufanya. Mheshimiwa Waziri kila wakati tukikuandikia, umekua mwepesi sana na timu yako nzuri sana. Nashukuru pia kwa ziara aliyoifanya Naibu Waziri Kiteto kwa kweli timu ya TAMISEMI mmejipanga vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru vile vile kwa pesa tuliozipata kwa ajili ya shule kongwe zile. Shule za Kijungu, Sunya, Ndosidosi, Kibaya na nashukuru kwa sababu tumeona mmetuongezea pesa tena kwa ajili ya shule hizi kongwe. Mheshimiwa Waziri tulikutana, ile idea yako ya kukutana na Wabunge wa Mikoa ilikuwa ni renovation nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na wewe unafahamu tarehe 12 Februari, tulikutana na timu ya Manyara na tukaleta maandishi yetu ya kujaribu kuonyesha miradi. Eneo kubwa ni TARURA, TARURA tulishakubaliana hapa na Ilani ya Chama cha Mapinduzi iko bayana sana, tulisema ni lazima sasa TARURA iongezewe pesa kwa sababu ya mtandao wa barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ilani ya Chama cha Mapinduzi ilisema hivi na tuliahidi kwamba ni vyema sasa tuanze kuangalia ile formula ile kati ya TARURA na TANROADS kwa nia ya kuongezea TARURA pesa. Kwa mfano, kwa Kiteto pekee yake, mtandao wa barabara ni kilometa 1,291. Bajeti tunayoihitaji ni bilioni 11, lakini uhalisia tunapata bilioni mbili na milioni 800 haitoshi na siku ile Mheshimiwa Waziri unafahamu tulisema kama mtatuongezea sisi bilioni tatu walau tuwe tunapata bilioni 5.8 ama sita itatusaidia kuendelea kujenga mtandao huu wa barabara, ili wananchi waliopo vijijini wakapate kusafiri bila shida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ombi langu lipo pale pale, tunategemea kwa kweli hizi pesa ziongezeke. Na kwa kweli nimpongeze Mkurugenzi wa TARURA hata kwa sura simfahamu lakini nimemsumbua kwenye simu, Kiteto ilikua haina gari na sasa tumepata gari. Kwa kweli nampongeza sana. kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri mtuongeze pesa kwa ajili ya TARURA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine Mheshimiwa Waziri, alikuja Katibu Mkuu wa CCM Jimbo la Kiteto, ametuahidi kilometa 1 ya lami na taa za barabarani na maombi tumeshaleta. Taa za barabarani pale mjini ni karibu milioni 250 tu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri tunaendelea kumbushia, ambulance kwa ajili ya Engusero aliahidi Mheshimiwa Rais, Sunya gari lao lilipata ajali na hospitali ya wilaya. Kwa hiyo, kwenye zile ambulance mnazogawa Kiteto utupendelee. Kiteto ni kubwa kila siku nasema hapa, square kilometa 1,700. Mheshimiwa Waziri ukituongezea itatusaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la walimu wanaojitolea; Mheshimiwa Waziri tunashukuru mmetangaza ajira, fuatilia tunataka walimu hawa wanaojitolea wapewe kipaumbele kwenye ajira. Kila mtu anapojitolea nia yake, kwanza ni suala kizalendo, kujitolea. Kwa hiyo, kwenye nafasi hizo kwa kweli uwachukue na inasadikika nchi hii sasa wapo walimu wanaojitolea karibu 70,000/80,000 hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wakianzisha mjadala wa kuwachukua hata kama ni kubadilisha sheria, kwamba vigezo ni merit, yes lakini mtu anayejitolea na yeye hicho ni kigezo ambacho ni muhimu sana, hawa watu wanafanya kazi nzuri sana. Kwa hiyo tunategemea kwamba tutaona vijana wengi wa Kiteto wanaojitolea wakipata ajira kwenye nafasi ambazo wametangaza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Madiwani. Madiwani wetu wanafanya kazi kubwa sana. Wanasimamia miradi na nataka niseme kuna link kati ya fedha hizi zinazopotea labda na kwa sababu Madiwani hawako full time. Labda tuangalie huko mbele baadaye maslahi ikiongezeka na posho na stahiki kwa ajili ya Madiwani labda usimamizi utakuwa wa bora sana na pengine hizi fedha zinazopotea potea, haitatokea. Hebu waangaliwe sana Madiwani wanafanya kazi kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, liko suala la maboma ama miradi ile ambayo inafanywa na wananchi. Kiteto, wananchi wa Kiteto ni wachapa kazi sana. Kuna miradi mingi sana, kwa mfano zahanati tu peke yake karibu miradi 14 ipo kwenye lenta, wananchi wale wamefanya kazi kubwa sana. Kwa mfano, Zambia, Mbigiri, Mbeli, Taigo, Chapakazi, Engusero, Sidan, Logoet, Chekanao, Olduvai na mengine mengi. Zahanati zao ziko kwenye lenta. Tulikaa hapa mwaka jana, tukasema tujenge vituo vya tarafa, Kiteto bado nadai vituo vitatu vya tarafa. Tarafa ya Makame, Dosidosi na Kibaya. Tulisema tukipeleka huduma hizi kwenye tarafa itasaidia sasa zahanati tunazozijenga walau tutakuwa tumepeleka huduma karibu na wananchi. Kwa hiyo, kwa kweli tusikubali hili Bunge liishe hatajamalizana na habari ya vituo vya tarafa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli Mheshimiwa Waziri akatafute fedha. Hili halina mjadala hata kidogo, nataka vituo vitatu vya tarafa na tulishapitisha hapa. Haiwezekani watu wengine wanaendelea kujenga za kata wakati sisi wengine tunazungumza habari ya tarafa hapa and I am serious, very serious about this, kwa kweli. This is not negotiable, tumeshakubaliana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya majengo haya, Kiteto hospitali yetu ikipata tena majengo ya maternity, dharura (emergency), RCH na jengo la X-Ray ile mpya ambayo tunaitumia sasa, itasaidia kuweka Wilaya ya Kiteto kwenye hadhi ya Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la watumishi. Kuna Mkurugenzi yuko pale Same. Unajua siyo kila wakati lazima tukutane hapa tuna-complain kuhusu…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Olelekaita, muda wako umekwisha.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkurugenzi wangu anachapa kazi sana abaki na aendelee kumaliza majengo haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ahsanteni sana na naunga mkono hoja.