Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Simon Songe Lusengekile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia Hotuba ya Waziri wa TAMISEMI. Kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anazofanya hasa katika utoaji wa fedha kwenye majimbo yetu. Tunamshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimshukuru sana Waziri wa TAMISEMI pamoja na wasaidizi wake na watumishi kwa ujumla katika Wizara ya TAMISEMI kwa kazi kubwa wanazofanya. Sisi tunapata faraja sana kwa kazi wanazofanya. Pia kipekee niipongeze na kuishukuru sana Timu ya Simba kwa kazi kubwa iliyofanya jana. Kwa kweli ilifanya kazi kubwa kwa ajili ya nchi na nchi imetulia kwa kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ina maana gani? Labda Mheshimiwa Waziri Jenista aiandike hii. Tuliwafunga Horoya goli saba na jana wamefungwa Yanga goli mbili jumla tisa. Maana yake nini? Magoli manne ni ya uongozi wa Mama kuelekea 2025, zawadi na magoli mengine matano ni zawadi ya Mama 2025 – 2030, ndiyo maana ya yale magoli. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Simon kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Rashid Abdallah Rashid.

T A A R I F A

MHE. RASHID ABDALLAH RASHID: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe mchangiaji taarifa kwamba asije kulalamika na muda. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Simon.

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa sababu ya Yanga ndiyo maana kasema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kwenye kuchangia. Pamoja na mambo mazuri ambayo yamefanywa na Serikali, pamoja na fedha ambayo tumepokea kwenye majimbo yetu sasa kuna mambo ambayo pia tunaomba kuiomba Serikali iweze kuyafaya ili tuweze kuwa na tija zaidi kwenye maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie eneo la afya. Katika Jimbo la Busega tuna vituo vya afya ambavyo vilipandishwa hadhi kutoka kwenye zahanati; Kituo cha Afya Kiloleli na Kituo cha Afya Lukungu kwa maana ya Lamadi. Vituo vya afya hivi bahati nzuri sana vilipandishwa na Dkt. Dugange akiwa RMO wa Mkoa wa Simiyu, anavijua vizuri, lakini mpaka sasa hivi havina wodi yoyote. Kwa mfano Lukungu tuna theatre pale, haifanyi kazi kwa sababu hamna wodi. Ukimfanyia mtu operation hamna pa kumpeleka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sasa Wizara ilione hili, vituo vya afya hivi viwili kwa maana ya Kiloleli pamoja na Lukungu kule Lamadi, viwekewe miundombinu ya majengo ili vianze sasa kufanya kazi kama vituo vya afya na kama vilivyopandishwa hadhi na Dkt. Dugange akiwa RMO kule Simiyu. Kwa hiyo anavifahamu vizuri kwa sababu yeye ndiye alivipandisha hadhi kutoka kwenye zahanati kwenda kwenye vituo vya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana tuyachukue haya kuwasaidia wananchi wa Kiloleli ili wapate majengo ya wodi kwa maana ya wodi ya wanaume, wodi ya watoto na wodi zingine pamoja na kule Lukungu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo naomba nichangie eneo la TARURA. Najua kazi kubwa imefanywa na TARURA. Kazi kubwa tumefanya kwenye miundombinu ya barabara. Naomba nami nipige kura ya ndiyo kama Mheshimiwa Waziri atakubali, Engineer Seif awe mfanyakazi bora TARURA mwaka huu Mei, kwa sababu kwa kweli anatutia moyo sana kwenye majimbo yetu. Anafanya kazi kubwa, ukimpigia simu anapokea, ana-respond na fedha zinakuja kwa wakati na wakandarasi wanafanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niwaombe Mheshimiwa Waziri na ndugu yangu Seif, pale Busega tuna Daraja la Lutubiga kwenda Mwasamba, daraja ambalo linahitaji shilingi milioni 900. Tunaomba sana huruma ya Mheshimiwa Waziri tupate shilingi milioni 900 kwenye bajeti ya maendeleo ili tuweze kuwatengenezea daraja wananchi wanaotoka Lutubiga kwenda Mwasamba, kwa sababu imefikia sehemu sasa wanafunzi hawawezi kuvuka pale, imebidi tuwaombee kwenda kusoma kwenye kata nyingine ya jirani kwa sababu kile kijiji hakina mawasiliano na kijiji kingine cha Mwasamba. Kwa hiyo, tunaomba sana tupate shilingi milioni 900 za dharura ili tuweze kuwasaidia watoto wanapotoka Lutubiga kuelekea kule Mwasamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu ambalo nataka nichangie, ni habari ya 20% za maendeleo kwenye mapato ya ndani kwenye halmashauri 56. Fedha hizi ambazo ni 20% katika mwaka wa fedha unaokuja ambao leo tunauzungumza hapa. Wamepanga 20% kwa baadhi ya halmashauri ambazo ziko 56 ikiwemo Busega, Bariadi DC, Bahi, Siha pamoja na zingine lakini jumla ziko 56. 10% ndiyo tunazopeleka kwenye maendeleo na 10% nyingine ni kwa ajili ya makundi maalum kwa maana vijana, wanawake pamoja na watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana, hii 40% ilikuwa ni msaada sana kwenye halmashauri zetu kwa ajili ya mikakati na maendeleo ambayo tulikuwa tunafanya kupitia mapato ya ndani. Tunaomba waturudishie hizi fedha ili tuweze kufanya miradi ya kimkakati kwenye halmashauri zetu. Hii 10% haitatosha kufanya kazi za kimkakati kwenye halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano Busega ni zaidi ya shilingi milioni 300 ambazo zimetolewa kwa ajili kupelekwa kwenye matumizi ya kawaida. Nimshawishi sana Mheshimiwa Waziri, hizi halmashauri tuzirudishie hizi fedha ili ziweze kufanya maendeleo. Kwa mfano, una shilingi milioni moja, sasa kwenye maendeleo tunaenda kupeleka shilingi laki moja. Kwa kweli kwa halmashauri zetu hizi haiwezekani na hizi ndiyo siasa zetu na hizi ndiyo zinazosaidia kazi za dharura kwenye majimbo yetu. Ikitokea kazi ya dharura fedha hizi ndiyo tunatumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, sisi kuna maboma mengi ambayo wananchi wamejenga, tukiwa na fedha hizi itatusaidia kupeleka kwenye miradi ya wananchi ambayo wananchi wetu wameanzisha. Kuna sehemu nyingine pia tunafikiria hata kuanzisha masoko ya kimkakati kutoka kwenye halmashauri. Fedha hizi wakitusaidia zitatusaidia kuweza kufanya kazi za kimkakati kwenye halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tumeona halmashauri hizi hazina fedha tuwaongezee OC ili waweze kupata fedha za kufanyia kazi za matumizi ya kawaida, lakini hizi fedha za maendeleo tunaomba zirudi 40%, 10% iende kwenye makundi maalum na 30% ibaki kwenye miradi ya kimkakati ili tuweze kufanya kazi kupitia majimbo yetu na kupitia fedha hizi. Tumwombe sana Mheshimiwa Waziri, atafakari tena pamoja na wasaidizi wake. Ikibidi kama inafaa waweze kuturudishia hizi fedha na kama wakiona haifai basi waturudishie za Busega ili tuweze kufanya kazi za kimkakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo ambalo pia limekuwa likizungumzwa hapa. Maboma ya wananchi na miradi ya kimkakati ambayo imeanzwa na wananchi. Wananchi wetu wana maboma mengi ambayo wameyaanzisha. Kwa mfano Busega tuna maboma 69 ya madarasa, tuna maboma 10 ya nyumba za Walimu. Wananchi wametoa fedha, wananchi wamejibana wameanzisha miradi hii, lakini bado iko kwenye maboma. Tumekuwa tukipata fedha tunapeleka kuanza miradi mipya. Tunaomba sasa TAMISEMI iangalie ifanye sensa nchi nzima ili kusudi tupate tupewe zaidi kwa ajili ya fedha za mkakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. (Makofi)