Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Njalu Daudi Silanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Itilima

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi kukushukuru kunipa nafasi nami niweze kuchangia na nichukue fursa hii. Pia nichukue fursa hii kuishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan. Niwapongeze sana watumishi wa Wizara ya TAMISEMI kwa kazi kubwa na nzuri mnayoifanya kuhakikisha mnatimiza Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2025/2026.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitashauri sehemu ya miradi inayoendelea. Sisi Wabunge tunapokuja kwenye Bunge lako Tukufu tunakuwa na mipango ambayo tumeiandaa kwenye halmashauri zetu. Tumehamasisha wananchi kuhakikisha kwamba tunajenga madarasa, tunajenga zahanati, tunajenga vituo vya afya na tunaambiwa tutakapokamilisha miradi hiyo Serikali kuu itakuja kumalizia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo sasa linatupa changamoto, fedha za Serikali kuu zinapokuja badala ya kumalizia zinakuja na maelekezo ya kuja kuanza miradi mipya. Tayari majukumu yetu kama Wabunge yanakuwa yamepotea kwa sababu ile miradi inakuwa ni chakavu, haitekelezeki, lakini vile vile na miradi mipya tunayoianza ndiyo sasa inayokuja na hoja za CAG hapa inakuwa na gharama kubwa badala ya kwamba yale majengo tuliyoyaanzisha na yale majengo yamesimamiwa na halmashauri. Viongozi watendaji wako pale, ma-engineer wako pale, hatua zote za kitaalam zimefanyika, lakini inapokuja fedha kutoka Serikali Kuu inasema tunaanzisha majengo mapya, tunaanzisha zahanati mpya, hii tunaiacha na hizo ramani zinabadilika tena zinakuja ramani zingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe TAMISEMI iangalie tathmini ya nchi nzima kwenye maboma yote. Zile fedha zinapokuja ziende zikamalizie maendeleo ya wananchi waliyoyaanzisha. Lazima hatutakaa tufike malengo tunayoyatarajia kwa sababu miradi mingi inatakiwa isimamiwe na wananchi, miradi mingi inaenda kuwahudumia wananchi wanaotoka kwenye maeneo husika. Ni vyema tunapofika mahali miradi tukaona inafaa tukaongeza miradi hiyo ili maendeleo yaende.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano na niombe sana Wizara ya TAMISEMI, kwenye wilaya yangu nimejenga zahanati zaidi ya 32. Zahanati 10 zimeshakamilika, lakini bado mipango midogo midogo ya kumalizia, tumewachangisha wananchi mpaka kuchoka. Sasa niiombe TAMISEMI hizi Zahanati za Dasini, Gambasingu, Nkololo, Mwagimwagi,
Nhobola, Kidula, Muhalale, Golambeshi, Laini na Inalo, zina changamoto chache na hizo changamoto sisi kwenye halmashauri tumejibana tumebakiza fedha kwenye jengo la utawala. Waturuhusu zile fedha ziende zikamalizie ili kusudi wananchi waweze kupata huduma ya afya kama Ilani ya Chama cha Mapinduzi inavyotuelekeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, kwenye hizi fedha za BOOST. Niombe, wamefanya kazi nzuri kubwa sana Wizara ya TAMISEMI na wanafanya kazi kubwa kuhakikisha tunapeleka elimu kule vijijini, ni jambo jema. Niombe kwenye yale maboma ambayo yako kwenye mipango mizuri, basi zile fedha waangalie utaratibu wa uwezekano wa kuhakikisha kwamba tunaenda kumalizia miradi mikubwa ambayo italeta impact kubwa kuliko kupeleka shilingi milioni 540, unaenda kujenga shule mpya na kuna shule zingine shikizi zaidi ya shule 30 au 40 kwenye eneo hilo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niiombe tu Wizara wakae kuhakikisha kwamba tunatatua hii changamoto ili wananchi kwenye maeneo yale tuwape morali ya kufanya kazi zile. Vinginevyo tutakuwa tunaelekeza michango yetu, lakini mawazo yetu hayatatekelezeka kwa sababu wanajua hata tukianzisha mradi huu hakuna kitakachofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze TARURA. Kwa kweli wanafanya kazi kubwa na nzuri sana na ndiyo watakaotubeba kwa sababu barabara kila mtu anapita hata kama ni mgeni kutoka nchi ya wapi. Atapita kwenye barabara atasema Tanzania iko safi kwenye barabara. Niwaombe waendelee tu kuongeza nguvu ili kusudi tuendelee kuboresha barabara zetu, madaraja yetu na wilaya zetu zikutane wilaya kwa wilaya. Niombe kwa Mkurugenzi wa TARURA atusaidie sana, kuna maombi ambayo tumepeleka lakini ni ahadi za Mheshimiwa, Viongozi Wakuu waliopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Mto Gamaloha ambao unaunganisha Kata ya Nkuyu, Mwaswale na Laini. Niombe sana kwenye mpango wa maendeleo na yenyewe iwepo. Vile vile kuna Mto Sanjo tunakutana na Wilaya ya Meatu, nako niombe sana Wizara ichukue hili jambo iweze kutusaidia wananchi wa kutoka Meatu na kutoka Itilima waweze kuunganika kufanya kazi za maendeleo katika maeneo hayo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Mto unaitwa Ntagosa unaungana na Ipililo, wilaya mama katika Mkoa wetu wa Simiyu. Niombe sana Wizara ichukue nafasi hiyo kuhakikisha kwamba inatusaidia kwenye maeneo hayo. Jambo hili likifanikiwa tutakuwa tunafanya kazi kubwa na nzuri zaidi kuhakikisha kwamba tunapeleka maendeleo kwa wananchi wetu. Vile vile tutaendelea kutoa hamasa kwenye maeneo haya kwamba Serikali sasa inafanya kazi yake kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, niombe, tuna miradi mikubwa ya maendeleo yetu ambayo tunaifanya, lakini kubwa zaidi tunaomba kupata watumishi. Serikali watuambie na tulishawahi kusema humu ndani kwamba kama tunajenga hizi zahanati tunajenga shule na yote inalenga maendeleo ya wananchi, kwa nini hatupati watumishi wa kwenda kuhudumia zile kada? Tunaamini sasa hivi wameshatoa nafasi hizi, tuombe, kuna vijana wengi wamemaliza vyuo muda mrefu tangu 2018, 2019, 2020, lakini cha ajabu tunasubiria sasa hivi kitakachokuja kutokea unaweza ukakuta wa 2022 ndiyo anachukuliwa, wa 2016, 2017, 2018 anakuwa hayupo. Wanatupa wakati mgumu kwenye majimbo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuiombe Wizara inayohusika ihakikishe kwamba sasa jambo hili la utumishi linatatuliwa la sivyo watueleze Serikali, kwa sababu tunajenga miradi inasimama kwa kukosa wale wahudumu wanaohusika. Watuambie kama uwezekano haupo tujipange sisi kwenye halmashauri zetu tujue jinsi gani ya kutoa huduma kwenye maeneo haya na wakifanya hivyo Mheshimiwa Waziri atakuwa anafanya kazi kubwa na nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua kazi ya Wizara ni nzuri wanayoifanya na kule na sisi tunawaunga mkono kwa 100%, kwa sababu tunaamini yale ambayo tumeyaahidi na wao wanatusaidia hawalali usiku na mchana kuhakikisha wanachapa kazi ya kuhakikisha wanawahudumia Watanzania. Sasa tuwaombe wachukue mawazo yetu waende wakayafanyie kazi ili tufike hatma ambayo tunaitarajia na kama Ilani ya Chama cha Mapinduzi inavyotuelekeza kwamba tutakamalisha yale yote ambayo sisi tumekuwa tukiyafanya ndani ya muda wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho niombe nina miji yangu michache ambayo inakuwa kwa kasi sana. Mji wa Lugulu naomba nitengenezewe barabara za mitaa kwenye maeneo hayo, Mji wa Migato barabara kwenye maeneo ya mitaa, Mji wa Laini na Mji wa Mwamapaa na Suzula yote maeneo haya ni ya kiuchumi. Niombe sana Serikali iyachukue na kuyafanyia kazi na kuendelea kuboresha barabara zilizoko vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hii miradi inayofanyika halmashauri za miji na manispaa, lakini miradi hii haiji kwenye halmashauri zilizoko vijijini. Sasa Serikali ichukue wanapokutana kwenye mipango ya kuratibu wajue wanaporatibu mipango maendeleo yale makubwa watu wanaotoka vijijini ndiyo wanaokwenda mjini kukaa pale kwenye halmashauri na kwenye manispaa. Sasa na kule kijijini ili mazao yatoke vijijini kwenda mjini ni vizuri barabara ziboreshwe. Kwa hiyo kwenye miradi inayokuja ni muhimu sana wakahakikisha wanaangalia mazingira yale ili kusudi jamii inayoishi kwenye halmashauri za vijijini na yenyewe ijitambue kwamba kuna umuhimu wa kukaa kule.

Tunapoirundika kwenye manispaa na kwenye halmashauri za miji, tayari tunanyima haki kwenye halmashauri zilizoko vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haya machache, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)