Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Magu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia Wizara muhimu sana ya TAMISEMI ambayo inawagusa wananchi. Niipongeze Serikali kwa namna ya pekee Serikali ya Awamu ya Sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ya pekee inavyoleta fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali ya kihuduma kwenye halmashauri zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze moja kwa moja kwa TARURA. TARURA kila mmoja hapa anahitaji iongezwe fedha, ni kwa sababu kwamba ili maendeleo ya kiuchumi yaweze kuwepo barabara zinahitajika. Mtu ambaye alikuwa anasafiri masaa manane aweze kusafiri masaa mawili. Mtu ambaye alikuwa anakwenda kupata huduma ya kiafya asafiri kwa haraka ili aweze kufika kwenye huduma za kiafya. Kwa hiyo TARURA ni muhimu sana kwa kweli tukaona namna ambavyo tunaweza kuiongeza fedha ili iweze kuhudumia barabara zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo barabara ambazo kwa kweli zinahitaji madaraja tu kuunganishika, hakuna mawasiliano ambayo yanapatikana bila kuwepo na daraja. Nyuma kule tulikuwa na Mradi wa Bottleneck ambao ulisaidia sana barabara ambazo zilikuwa haziunganiki, kata kwa kata, kijiji kwa kijiji, wilaya kwa wilaya. Kwa hiyo niombe tena, kwa mfano kule kwangu Barabara ya Kahangala, Mwamanga kwenda Kisesa B pale huwezi kwenda mahala popote kama mvua imenyesha; na kuna vijiji vitatu ni kama viko visiwani. Kwa hiyo niombe sana, kwa mfano Inolelo, juzi nilikuwa na mikutano ya hadhara kule, nimemaliza Kijiji cha Kisesa B ikabidi nizunguke Kata ya Nyanguge, Kata ya Kitongo Sima, Kata ya Kahangala ndipo nifike tena kwenye Kijiji cha Inolelo. Kwa kweli ni mateso makubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii tumekwishaiomba siku nyingi TAMISEMI, na tulikaa na Mheshimiwa Waziri Angellah Kairuki nikaiomba hiii Barabara ya Kahangala, Mwamanga, Kisesa B; mwaka huu nipeni fedha ili iweze kutengenezwa na wananchi tuweze kuwasaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siishii hapo, kuna Barabara ya Kisamba Sayata Mkurugenzi wa TARURA, Ndugu Seth, nimeshakuomba mara nyingi kwamba huwezi kufika salama kuelekea Bariadi bila kuwa na daraja pale Kinsalama kuja Sayaka; ninaomba sana mwaka huu. Mheshimiwa Waziri umeanza utaratibu mzuri wa kukaa na Wabunge. Hata tulipokaa na wewe nilikutajia hii barabara. Kwa kweli nakupongeza sana Waziri endelea kuwa na upole huo, sisi tunatoa matatizo yetu ndani tukiwa tuna uhakika kwamba haya yote yatafanyiwa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo Barabara ya Isolo kwenda Isawida kule Itirima. Barabara hii ni ya muhimu sana, inahitaji tu bottleneck kuweza kukamilika ili wananchi wa Itirima, Isolo, Kabila kuja Wilaya ya Magu waweze kusafiri kwa haraka sana. Niombe sana hili jambo liweze kufanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli miji yetu inakuwa, Mji wa Magu unakuwa ni wa siku nyingi tangu mwaka 1974 ni wa umri wangu. Lakini Miji ya Kisesa na Bujora nayo unakuwa, nimekuomba Waziri wa TAMISEMI, tulipokaa pale Msekwa, kwamba angalau nipate kilometa sita za lami zitengeneze Magu Mjini, zitengeneze Bujora na Kisesa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni miji inayokua; ili miji iweze kuendelea tusaidieni. Wenzetu wanapata TaCTIC sisi hatupati; tusaidie Mheshimiwa Waziri hili litakuwa ni mkombozi kwa wananchi wetu. Tumetengeneza barabara za mitaro ni vizuri zikawekewa lami ili kuhakikisha kwamba tunawasaidia wananchi. Niombe sana jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, afya, tunayo majengo maboma 20 tumeezeka kwenye Wilaya ya Magu. Kule Jijimiri ni mbali sana na huduma, kule Isolo ni mbali sana na huduma, kule Ndagalu ni mbali sana na huduma, kule Bwamanga ni mbali sana na huduma, kule Kisamba ni mbali sana na huduma, kule Lutale ni mbali sana na huduma. Ninaomba Mheshimiwa Waziri tupatieni; hizi milioni 50 mnazotupatia kwa zahanati tatu tunashukuru lakini bado hazitoshi kwa sababu mahitaji ni mengi. Ukienda pale Walina wana jengo kubwa sana lakini hatuna fedha za kuweza kulimaliza. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri tukuombe basi zile zahanati tumeziezeka tupatie tu fedha ni milioni 50, ni bilioni moja kwa zahanati 20, tunakamilisha maboma haya Magu na wananchi wanaanza kutindua. Niombe sana jambo hili tuweze kupewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vituo vya afya vya kimkakati. Kule Ng’haya tumeishukuru Serikali milituletea fedha za ukarabati wa zahanati, lakini tukajiongeza Halmashauri ya Wilaya ya Magu tukaleta ombi mkatubalia kuanza kujenga kituo cha afya, tupeni fedha za kumalizia pale Ng’haya ili kituo hicho kikamilike. Sambamba na Kata ya Mwamanga ambayo imezungukwa na mito mingi tusaidie sana Mwamanga nayo tuweze kupata kituo cha afya, pamoja na Lutale tuweze kupata kituo cha afya. Tuangalie pia kukikarabati kituo cha afya cha Nyanguge ili kiweze kukamilika. Ninaomba sana hili kwa Serikali sikivu ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan iweze kutupatia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ajira hizi zilizotoka, ajira za afya na ajira za walimu. Kuna intake ya walimu kuanzia 2016 hawajachaguliwa. Huu mfumo unawasoma akina nani? mfumo ambao hauwasomi watu waliotangulia? wa 2016 hawajachaguliwa, wamechagua 2019, hawa watoto wa maskini ambao wamebaki wanasaidiwa na nani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe na niweze kushauri, kwa kweli kama inawezekana ajira hizi zilenge wilaya, kila wilaya ipewe watu wake ili tuangalie waliotangulia kumaliza na wanaoendelea. Kwa kweli tunawakatisha tamaa wazazi hata kusomesha. Niombe sana kwa kweli, hili linaumiza sana. Sasa hivi kwenye begi langu nimejaza CV za vijana, sina hata pa kuzipeleka. Kwa hiyo ushauri wangu, tutafute namna ya kuwezesha kila wilaya ni nafasi kiasi gani ipelekewe iajiri watu wake ili watoto hawa tuweze kuwasaidia. Niombe sana jambo hili Waheshimiwa Wabunge mliunge mkono, pigeni makofi ili Serikali ijue kwamba leo mmeniunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi nyingi zinaendelea kufanyika, lakini niombe; kuna mapunjo na madai ya watumishi wetu kwenye halmashauri, wanalalamika hawajaweza kupewa mapunjo hayo. Niombe Serikali ione ili kumpa moyo mtumishi huyu anayemsaidia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipwe haki zake, alipwe madeni yake na mapunjo ambayo wanaendelea kushughulika nayo wakati wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo niunge mkono hoja na nikupongeze sana pia kwa kuendesha Bunge kwa standard kama hii, ahsante sana. (Makofi)